KABLA YA JANUARI MWAKA 2000

Makanisa yote Afrika kuungwa na Roma kimawasiliano

Na Arnold Victor

KABLA ya kuingia kwa karne ijayo Januari 1, 2000, Parokia zote za Kanisa Katoliki barani Afrika zitakuwa zimeunganishwa katika mtandao maalum wa mawasiliano ya Kompyuta ambao utakuwa na kituo kikuu cha kuuongozea mjini Roma, Italia, imeelezwa.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa mawasiliano kutoka makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani mjini Roma, Padre Jean - Paul Guillet, teknolojia hiyo ambayo ni ngeni kabisa iitwayo Intranet inalenga katika kurahisisha mawasiliano na kubadilishana taarifa kirahisi zaidi katika mfumo wa Kanisa Katoliki duniani kote.

Padre huyo ambaye alitembelea makao makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania wiki hii na kuongea na Wakuu wa Idara mbali mbali na watumiaji wa kompyuta alisema teknolojia hiyo ambayo imeanza kwa mafanikio katika Jamhuri wa Kidemokrasia ya Kongo itawawezesha pia watumiaji kufanya mawasiliano ndani ya majimbo yao bila gharama yoyote, tofauti na ilivyo kwa Internet ambapo mtumiaji hulazimika kujiunganisha katika simu (telephone line) ndipo afanye mawasiliano. Padre Guillet alisema mfumo huo mpya unakuja ili kuziba pengo la udhaifu wa simu za upepo(Radio call) ambazo zimekuwa zikitumika zaidi barani Afrika.

Mkakati wa Teknolojia hiyo mpya ambao ulianza kufanyiwa kazi miaka mitatu iliyopita , tofauti na ile ya mtandao maarufu ujulikanao kama Internet, itawawezesha watumiaji kufanya pia mawasiliano ya ndani (intercommunication) miongoni mwao bila gharama yoyote. Katika mfumo wa Internet lazima mtumiaji aunganishe komputa yake na simu (telephone line) ndipo afanye mawasiliano, jambo ambalo humfanya alipe gharama kubwa, tofauti na Intranet ambayo haihitaji simu.

Padre Guillet aliliambia kiongozi baadaye kuwa parokia ambazo hazina kompyuta zitapatiwa bure kutoka Roma ili kuingia katika mtandao huo.

Kwa Tanzania kituo cha kuongozea mawasiliano hayo (Saver) kitafungwa katika makao makuu ya TEC kwa ajili ya mawasiliano ya ndani ambapo mtu anapotaka kuwasiliana na nje ya nchi atatuma ujumbe wake hapo na kituo hicho kitarusha ujumbe huo hadi Roma ambako kuna kituo kikuu cha kusambazia mawasiliano (Central Saver).

 

TRA yawanasa wakwepa ushuru Mwanza

Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikishirikiana na Jeshi la Polisi nchini imeanza kupata mafanikio katika mkakati wake wa kupambana na wakwepa ushuru, na tayari watu kadhaa wametiwa mbaroni mkoani Mwanza, taarifa ya mamlaka hiyo iliyotolewa jana imesema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na makao makuu ya Mamlaka hiyo jijini na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Walipa Kodi Bw. Augustine Mukandara, watu wawili wametiwa mbaroni mkoani Mwanza hivi karibuni kwa kukwepa kulipa ushuru wa wastani wa Sh. milioni 67.

Waliokamatwa, taarifa hiyo imeeleza kuwa ni Bw. Hamis Sudi wa S.L.P 774 Shinyanga na Bw. Khalid Juma Kaspare wa Mwanza.

Taarifa ya TRA imesema Bw. Sudi alikamatwa vitenge visivyolipiwa ushuru vyenye thamani ya Shilingi zipatazo milioni 126 ambavyo alistahili kuvilipia ushuru wa zaidi ya Sh. milioni 63. Mali hiyo ilikamatwa katika maghala ya mfanyabiashara mmoja mjini Mwanza Agosti 20, mwaka huu.

Naye Bw. Khalid Juma Kaspare ambaye baada ya kunaswa alitozwa faini ya Sh. milioni kumi, alikamatwa akiwa na mali yenye thamani ya Sh. milioni 7 zilizostahili ushuru wa zaidi ya Shilingi milioni 3 na kodi nyingine zenye thamani ya Shilingi kiasi cha milioni moja. Bidhaa hizo zilikamatiwa ufukweni mwa Ziwa Nyamutukuza, wilayani Geita zikiwa zimebebwa na lori aina ya Scania lenye namba za usajili ART 105 Agosti 23, mwaka huu na dereva wa lori hilo Bw. Daud Twala naye pia alitozwa faini ya Shilingi milioni moja.

Taarifa ya TRA imesema hivi sasa inaendesha kampeni ya kudumu ya kuwakoesha wakwepa ushuru wote ambao imebainika wamekita mizizi yao katika maeneo ya mipakani na jirani.

 

Waziri Ameir apewa mapumziko

Na Neema Dawson

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya nchi Mheshimiwa Ali Ameir Mohamed inasadikiwa amekuwa akisumbuliwa na Ugonjwa wa moyo kwa zaidi ya miezi miwili sasa na hivi sasa amepewa mapumziko ya miezi mitatu kuanzia Agosti, mwaka huu.

Taarifa za kuaminika ambazo gazeti hili limezipata zimesema kuwa Waziri Ameir alianza kuumwa kabla ya kuanza kwa Kikao cha Bajeti cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Juni, mwaka huu na baadaye alipelekwa nchini India kwa matibabu ambako alikaa kwa mwezi mmoja kabla ya kurejea nchini hivi karibuni na kupewa mapumziko hayo.

Hata hivyo Waziri Ameir aliweza kuhudhuria kipindi chote cha Bunge kwa mujibu wa Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Bw.Bernard Mchomvu hakuweza kupatikana jana kuelezea hali halisi ya Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Donge, Zanzibar lakini habari za uchunguzi zimeeleza kuwa Waziri Ameir anaendelea vizuri.

Habari zaidi zimeeleza kuwa chama cha Lions Club ndicho kilichogharamia usafiri na matbabu ya Waziri Ameir japo haikuweza kufahamika zaidi mchango wa Serikali, watu au taasisi nyingine yoyote.

Wakati Waziri Ameir akiwa katika mapumziko Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere naye aliondoka hivi karibuni kuelekea nchini Uingereza kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa ambao hakuna taarifa zozote rasmi zilizokwishatolewa kuuelezea japo baadhi ya magazeti yamekuwa yakiutaja kuwa ugonjwa wa Mkanda wa Jeshi au Tambaazi.

Baraza la Walei lajiweka sawa kusherehekea Jubilei Kuu

Na Getruder Madembwe

Katika maandalizi ya Jubilei ya mwaka 2000,Baraza la Walei limeandaa semina, makongamano, mikutano, maandamano, hija, tafakari, na ibada maalum kwa ajili ya kuwatayarisha Walei katika Jubilei hiyo.

Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Idara ya Utume wa Walei Padri Nicholaus Segeja alipokuwa akiongea na KIONGOZI ofisini kwake hivi karibuni.

Padri Segeja alisema alisema kwamba wanatayarisha mambo hayo katika maandalizi ya Jubilei Kuu ya Ukristo mwaka 2000 kulingana na maagizo ya Baba Mtakatifu Yohane Poul II yanayosema " Yapasa mipango yote ielekezwe kwenye lengo kuu la Jubilei" yaani kutia nguvu na kuimarisha imani na ushuhuda wa Wakristo.

Alisema ni lazima kuamsha moyo wa bidii kati ya waamini wote wajisikie hamu ya kweli ya utakatifu na uhitaji wa ndani wa kuongoka na kuanza maisha mapya.

"Tunupotafakari utendaji wetu kuelekea Jubilei Kuu, kituo kidogo cha Walei (Bakanja TEC Laity Center) ambacho kinajengwa Dar es Salaam kinatarajiwa kuwa kitatumika wakati wa maadhimisho ya Jubilei Kuu Januari mwakani"alisema Padri Segeja.

Wajawazito walevi huzaa walemavu wa akili-Mtaalamu

Na Dalphina Rubyema

MKUU wa Kitengo cha Watoto wenye ulemavu wa akili cha Shule ya Uhuru Mchanganyiko jijini Mwalimu Ditrick Mkwale, amewatahadharisha akina mama wajazito kuacha tabia ya "kubugia" pombe kwani ulevi kwa wajawazito ni moja ya sababu zinazopelekea kuzaliwa watoto wenye taahira ya akili.

Ushauri huo ulitolewa na Mkuu huyo wa kitengo hivi karibuni ofisini kwake jijini wakati alipokuwa akiongea na KIONGOZI juu ya sababu za ulemavu wa akili kwa watoto.

Mwalimu Mkwale alisema kuwa watoto wengi wenye ulemavu wa akili wanaosoma shuleni hapo walipata tatizo hilo kutokana na mama zao kuwa walevi wakati walipokuwa wajawazito.

Alitaja sababu nyingine inayochangia hali hiyo kuwa ni mama mjamzito kuugua ugonjwa mkali, ajali, kipigo kikali kutoka kwa mume ama mtu mwingine,kudekaza mtoto kupita kiasi hususan kwa watoto wanaolelewa na bibi au babu zao.

Alisema pia kwamba akina mama wanaozaa wakiwa na umri mkubwa yaani zaidi ya miaka 35 wana nafasi kubwa zaidi ya kuzaa watoto wenye ulemavu wa akili.

Mwalimu alisema kuwa ulemavu huo unasababisha mtoto akose mambo mengi kwa vile akili yake inakuwa chini ya wastani na wakati mwingine anahitaji msaada na uangalizi makini ambao ni nadra kupatikana kwa familia nyingi.

"Mtoto mwenye hali hii kama ni wa kike anashindwa hata kujifanyia usafi wa mwili wake na asilimia 70 ya watoto wenye taahira ya akili wanaweza kushindwa kusoma na kuandika ingawa baadhi wanamudu kazi za ufundi na za mikono.

Alisema pamoja na hayo kila mtoto mwenye ulemavu wa akili ana kiwango chake cha uelewa kwani baadhi hujiweza kuliko wengine.

"Unakuta Mtoto mwingine hajiwezi kabisa,anaweza akajisaidia na kuanza kukichezea kinyesi.

Yeye hajui baya na zuri, hivyo sisi walimu tunapata kazi kubwa ya kuwafundisha watoto kama hawa,"alisema.

Alisema Shule yake iliyoanza kupokea wanafunzi wenye ulemavu wa akili tangu mwaka 1984,hivi sasa ina jumla ya wanafunzi 95 wenye tatizo hilo sambamba na tatizo kubwa la walimu wenye ujuzi wa kuwafundisha watoto hao.

Alisema mambo wanayofundishwa ni usafi wa kujitunza wenyewe, kazi za ufundi, kazi za mikono, kuchora na wale wanaoonyesha uwezo wa kumudu kusoma na kuandika hupelekwa kwenye madarasa ya kawaida.

Tumieni teknolojia kufundisha Neno la Mungu

Na Peter Dominic

WATUMISHI wa kikristo wametakiwa kutumia teknolojia ya kisasa kulitangaza Neno la Mungu na badala ya kuitumia kumwabudu shetani.

Usahauri huo umetolewa na Mhashamu Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro wakati akifungua warsha ya siku tano kwa ajili ya uongozi wa Masista na Mama Wakuu wa Kanisa wa Tanzania ikiwa ni mpango wa kuwaendeleza kielimu, na kimaemdeleo.

"Fanyeni mikutano mara kwa mara ili kubadilishana mawazo na tumieni televisheni na teknolojia nyingine ili msaidie jamii kulielewa Neno la Mungu kutokana na mabadiliko ya dunia" alisema na kuongeza kuwa hakuna mtu ambaye anaweza kusema kuwa ametosheka na Neno la Mungu hata aendelee kiasi gani kiteknolojia.

Akiongea katika warsha hiyo Mhashamu Askofu Mkude, alisema tunapoelekea Milenia ya tatu viongozi wakuu wa kidini wamepewa jukumu kubwa la kuongoza jamii kujua matatizo yao na kuyatatua.

Hata hivyo alionya kuwa mabadiliko ya dunia ya Sayansi na Teknolojia yasitumike kupotosha ukweli wa Neno la Mungu na Ukristo kwa ujumla kwani alisema kuna dini ambazo zimekwishaanzishwa na zinatumia ishara zote za kikristo lakini ni za waabudu Shetani.

 

Waumini wafurika Parokia ya Mt. Petro Dar

Na Neema Dawson

KUTOKANA na waumini kufurika na kujaa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay Jijini, Paroko wa Parokia hiyo Padri Valens Mruma amelazimika kufanya mipango ya kujenga kigango kingine Mikocheni ili keweza kuwasogezea huduma wakazi wa maeneo hayo pamoja na kupunguza msongamano wa waumini kanisani hapo.

Padri Valens alisema hayo alipokuwa akizungumza na KIONGOZI parokiani hapo kuhusiana na maendeleo ya parokia hiyo wiki hii alisema parokia yake imezidiwa na idadi ya waumini hivyo kufikia mahali ambapo waamini wengine hulazimika kusalia nje ya kanisa hilo.

Alisema katika misa moja pekee wanakuwepo kiasi cha waumini 1,500 na kuna ibada tano kwa kila Jumapili.

Alifafanua kuwa kanisa hilo sasa lina waumini wapatao 12,000 wakati uwezo wake ni watu wasiozidi 1000.

Tarime walilia matangazo ya redio

Na Joseph Sabinus, Tarime

WANANCHI mbalimbali Wilayani hapa wameiomba Serikali ibuni mipango madhubuti itakayowezesha matangazo ya redio mbalimbali hapa nchini kuwafikia badala ya kusikiliza redio za nchi za nje pekee ikiwemo nchi jirani ya Kenya.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti wilayani hapa hivi karibuni wananchi hao wa sekta mbalimbali walisema hali ya kukosa matangazo ya redio za nchini inawafanya wasinufaike wala kujua hali halisi ilivyo nchini kwao,kiroho, kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii na badala yake kuishia kuelewa mambo ya nchi jirani yasiyo na umuhimu kwao .

Mchungaji Michael Nyasonga, wa Kanisa la Menonite Tanzania Jimbo la Tarime Mjini, alisema ‘’Ninajua kuweka kituo cha kukuzia matangazo ni gharama kubwa, lakini serikali na watu binafsi wenye uwezo watuhurumie watu wa Tarime, maana ni hatari kusikia na kujua habari za nchi za nje. Hali hii inatuathiri hata watumishi wa Mungu, kwani huwezi kuhubiri mambo ya kanisa tu bila kujua hali ilivyo ndani ya jamii."

Naye mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa hosipitali ya MIF na pia ni Rais wa shirika lisilo la kiserikali la OKOA WATOTO WA TARIME (SACHITA) lenye makao yake makuu mjini hapa Bw. Peter Mwera, alisema kibiashara hali hii inawaathiri kwani hawapati nafasi za kutangaza biashara zao.

‘’Biashara ni ushindani ikiwa ni pamoja na matangazo sasa nifanyeje? niende kutangaza KBC wakati redio yetu ya taifa tunayo? Au unadhani wananchi watapataje mafunzo bora na ushauri juu ya afya zao;siyo wote wanaomudu kununua magazeti hata yenyewe vijijini hayafiki njia iliyo bora ni kuboresha huduma za redio za hapa nchini’’.

Mwalimu Morris Mathias wa shule ya msingi Rebu na mkazi wa kijiji cha Buhemba, nje kidogo ya mji wa Tarime alikuwa na haya ‘’inatuwia vigumu walimu kujua mambo yaliyo nchini kwa wakati muafaka na hivi kufundisha somo la uraia ( Civics) inakuwa kazi ngumu kwa sababu hatupati matangazo ya redio na badala yake tunasikia taarifa mbalimbali toka kwa watu watokao miji mingine zikiwa zimepitwa na wakati. RTD kuna vipindi vingi muhimu kwa walimu na wanafunzi lakini hatuvipati hali hii ni hatari sana’’.

‘’ Wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita mambo mengi muhimu hatukuyasikia ikiwemo midahalo kutokana na ukosefu wa matangazo ya redio na hata wakazi wa vijijini hawakusikia sauti hata moja ya mgombea urais hii ni hatari sana kwani inaweza kusababisha wananchi kumchagua kiongozi asiyewafaa."

‘’Kilimo pia kinahitaji utaalamu na kuelimishwa kwa njia mbalimbali hivyo tunahitaji kuelimishwa kupitia redio zetu ili hata waishio vijijini wanufaike’’ alisema Mzee Robert Mganda mkulima maarufu, mwana siasa na mkatoliki aishie maeneo ya Sabasaba mjini hapa.

Wakazi wa Wilaya ya Tarime kwa kiasi kikubwa hupata matangazo ya redio ya Taifa ya nchi jirani ya Kenya KBC,Sauti ya Ujerumani na BBC ambapo Redio Tanzania Dar Es Salaam ambayo ni redio ya taifa, husikika kwa taabu masaa ya usiku na alfajiri .

 

Makamu wa Rais awataka madaktari kufuata maadili

Na Josephs Sabinus Neema Dawson

MAKAMU wa Rais Dk. Omari Ali Juma amewataka madaktari kote nchini kuepuka mienendo inayachafua maadili ya kazi yao kwa kuvipiga vita vitendo vya matumizi mabaya ya madawa, rushwa na kupambana zaidi na milipuko ya magonjwa na kuwahudumia wagonjwa kwa moyo wa upendo , huruma na kujituma ili kuokoa maisha ya binadamu.

Dk. Omari aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akifungua Mkutano wa 62 wa Chama cha Madaktari Wakristo Tanzania (TCMA) uliofanyika jijini Dar Es Salaam na kuwahusisha madaktari, wauguzi, makatibu wa hospitali na wafanyakazi mbalimbali wa hospitali.

Alisema kazi ya udaktari ni ya wito na hivyo watumishi hao hawastahili kufanya kazi kwa tamaa ya kujinufaisha kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na kutumia taaluma yao kibiashara hali inayosababisha baadhi yao kushiriki utoji mimba mambo ambayo ni kinyume cha maadili na wito wa udaktari.

"Utoaji mimba usiojali matakwa yenye lengo la maisha ya binadamu ni tatizo kubwa ambalo ninyi wenyewe mnalielewa zaidi.Udaktari ni wito; madaktari na wauguzi wanapaswa kufanya kazi kwa moyo wa kuthamini maisha ya binadamu bila kushawishika na tamaa ya kujinufaisha hivyo mnapaswa kupiga vita vitendo vya rushwa."alisema.

Juu ya matumizi mabaya ya madawa yakiwemo ya kulevya, Makamu wa Rais alisema hali hii inachangiwa pia na gharama kubwa za hospitali na ongezeko la wafanyakazi na wenye maduka ya madawa wasio na taaluma ya madawa au udaktari na kubainisha kuwa hali hizo zimechangia tabia ya watu kujinunulia wenyewe na kutumia madawa bila kupata ushauri wa daktari na akawataka madaktari kubuni mbinu za kupambana kukomesha hali hiyo.

Katika mkutano huo wa kujadili uwezekano wa madaktari kutengeneza dawakatika hospitali za hapa nchini,Mwenyekiti wa TCMA Bro.Dk. Ansgar Stufe alisema hali hiyo si kwamba itapunguza tatizo la uingizaji nchini madawa yenye ubora wa chini, bali pia tatizo la usafirishaji wa dawa hizo.

Kanisa la Kristo lawaonya Wakristo wanaoshitakiana

Na Gabriel Mduma, DSJ

KIONGOZI wa madhehebu ya Kanisa la Kristo lililopo Magomeni jijini amewataka Wakristo kutumia Biblia kutatua tofauti zao badala ya kushtakiana mahakamani.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kanisani hapo wiki hii Mwinjilisti Zacharia Shemtuhu, alisema ni aibu kwa Wakristo kupelekana mahakamani kwani ni kitu ambacho kinalidhalillisha kanisa.

Mwinjilisti Shemtuhu, amesema kuwa wakati sasa umefika wa kuwavuta watu wasioamini wamwendee Bwana Yesu kwa kuonyesha mafanikio ya Wakristo,lakini ni vigumu kwa hao wanaotaka kuja kwa Kristo kuvutika iwapo wataona wenyeji wao {Wakrito} hawapatani wenyewe kwa wenyewe.

Alisema kuwa Waislamu wengi wanasoma Biblia kanisani hapo ili kuufahamu ukweli na mara wanapohitimu wapo ambao wanabaki kwenye Ukristo baada ya kuufahamu huo ukweli, hivyo ni vema kanisa likawa na amani ili kuvuta wasioamini kwa Kristo.

"Ni kitu cha aibu, kama utamkaribisha mgeni nyumbani kwako akakuta mna migogoro wewe na mkeo, je, huyo mgeni hata kama alitaka kukaa wiki moja atakaa kweli?". alihoji Mwinjisti Shemtuhu akiwa na maana {wageni} wasioamini wanatakiwa wakute uelewano mwema kwa Wakristo.

Hivyo amewataka Wakristo kufuata katiba zao ili kuondokana na migogoro ya mara kwa mara makanisani lakini wakizingatia kuwa Biblia ndiyo katiba mama.