Tanzania sasa kujiunga na OIC

lMaafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje wasema suala ni zito, liko kwa Waziri Kikwete

lAskofu wa KKKT asema ni hatua ya kuwagawa Watanzania

lKitwana Kondo asema kama ni wazo la CCM hana tatizo

lKatibu Mkuu wa TEC Dakta Kilaini naye apinga

Na Waandishi Wetu

LILE suala lenye utata la mwaka 1992 la Serikali ya Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya kimataifa ya Kiislamu (OIC) hivi sasa limeinuka tena, zamu hii likiwa na nia ya kuiingiza Tanzania yote Bara na Visiwani katika Jumuiya hiyo ambayo moja ya vipengele vya katiba yake ni kuisilimisha dunia nzima.

Ilipobainika mwaka 1992 kwamba Zanzibar ilikuwa na mipango ya kujiunga na jumuiya hiyo ya kiislamu kulizuka mvutano mkubwa ambao ulizaa hoja ya Wabunge wa Tanzania Bara kudai "Tanganyika yao." Waziri Mkuu wa wakati huo John Malecela na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM Marehemu Horace Kolimba walipoteza nafasi zao, kwa shinikizo la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyedai kwamba wakuu hao walikuwa wamemshauri vibaya Rais wa wakati huo Ali Hassan Mwinyi.

Jumatatu Mei 10, mwaka huu gazeti la The East African linalotolewa na kampuni ya moja ya Kenya, liliandika kuwa Tanzania iko katika hatua za kuiingiza Tanzania katika uanachama wa jumuiya hiyo ya Kiislamu ya OIC.

Waandishi wetu walipofika katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje Alhamisi iliyopita ili kupata ufafanuzi wa hatua hiyo, walimkuta Afisa Uhusiano Bw. Simon Ileta, ambaye alisema suala hilo limempita "kimo" hata Katibu Mkuu wa Wizara Balozi Elly Mtango, kwani ni Waziri Jakaya Kikwete tu anayeweza kulitolea ufafanuzi.

Waandishi wetu walipita kwa Msaidizi wa Waziri Bw. Mtawa ambaye baada ya kupata ufafanuzi wa gazeti hilo lilichokuwa likitafutia ufafanuzi, aliwasiliana kwa simu na Mkurugenzi wa Habari wizarani hapo Balozi Patrick Chokala, ambaye pia hakuwa tayari kuzungumza chochote zaidi ya kuwataka waandishi wasubiri kuonana na Waziri Kikwete mwenyewe.

Hata hivyo Balozi Chokala, alisema Waziri yuko katika kikao cha Baraza la Mawaziri siku hiyo ya Alhamisi na kwamba kesho yake Ijumaa angeelekea Zanzibar kushughulikia masuala ya muafaka kati ya CCM na CUF. "Tutawasiliana na Waziri... acheni contact zenu tutawapigia simu pengine baadaye Jumatatu ijayo," alisema Bw. Mtawa baada ya kuwasiliana na Balozi Chokala.

Gazeti hili lilikutana na Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Adam Kombo Alhamisi hiyo hiyo kwa ajili ya ufafanuzi.

Mchungaji Kombo aliionya Serikali kutochukua hatua hiyo "kwani ina hatari ya kutugawa sisi Watanzania ambao nchi yetu haina dini."

Alisema haoni sababu yoyote ya Tanzania kujiunga na jumuiya ya namna hiyo kwani tayari ilishajadiliwa mwaka 1992 na kukaonekana kuna dosari hata kwa Zanzibar peke yake kujiunga.

Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Dk. Method Kilaini alipohojiwa na gazeti hili juzi alisema hatua hiyo haifai kuiunga mkono.

"Hatuna tatizo kama Serikali ya Tanzania ikifanya mahusiano ya kiserikali na nchi yoyote ya Kiislamu. Lakini Tanzania kama nchi haiwezi kuwa mwanachama wa jumuiya ya kidini, iwe ya Kiislamu au ya Kikristo,"alisema Dk. Kilaini.

Waziri mmoja mwandamizi wa Zanzibar Bw. Idi Pandu ambaye ni Muislamu alipoongea na The East African alikaririwa akisema kuwa Tanzania inastahili kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo ya Kiislamu kwa vile ina Waislamu wengi.

Naye Mbunge wa Kigamboni Alhaj Kitwana Kondo, alipotakiwa kutoa maoni yake juzi alisema yeye kwa kuwa ni Mbunge wa chama tawala CCM, hawezi kupingana na maazimio ya uongozi wa juu wa serikali. "Mimi sifahamu lolote juu ya mpango wa serikali kujiunga na OIC, ila ninachoweza kusema ni kwamba inawezekana viongozi wetu wamefanya utafiti na kuona kwamba wananchi wanaweza kufaidika kwa namna fulani,"alisema mbunge huyo.

Mheshimiwa Kondo alisema awali suala la Zanzibar kujiunga na jumuiya hiyo lilizua manung’uniko kwa sababu lilifanyika kinyume cha katiba ya Jamhuri ya Muungano kwa sababu Zanzibar ni sehemu tu ya Muungano na kwamba haikuwa na uwezo wa kujiunga na OIC kama nchi inayojitegemea.

Jitihada za kumpata Sheikh Mkuu Mufti Hemed Bin Juma Bin Hemed kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda.

Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipojiunga na jumuiya hiyo mwaka 1992 kulizuka mvutano mkubwa hata miongoni mwa viongozi wa juu wa Serikali ya Tanzania hata ikafikia mahali ambapo ilidaiwa kwamba Waziri Mkuu wa wakati huo Bw. John Malecela na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM marehemu Horace Kolimba walichukizwa na jambo hilo na hivyo kubariki wazo la kikundi cha Wabunge 55 wa CCM (G 55) kilichotaka iundwe Serikali ya Tanganyika.

Waziri Mkuu na Katibu Mkuu wa CCM walijiwa juu na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa kuruhusu wazo la kudai Serikali ya Tanganyika lijadiliwe Bungeni wakati sera ya CCM iko wazi kwamba ni Serikali moja. Mwalimu Nyerere aliwataka wale wote wanaotaka kujadili suala hilo wajiuzulu kwanza uanachama wao wa CCM na baadaye alihitimisha kwa kuandika kitabu "UONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA" ambapo aliwashutumu vikali Bw. Horace Kolimba na John Malecela. Hatimaye aliyekuwa Rais (Mwinyi) aliwabadilisha nyadhifa zao wakuu hao wawili na Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo Balozi Hassan Diria.

Vitamini ‘A’ yaweza kuzuia maambukizi ya UKIMWI - UNICEF

Na Justine Mwereke

Vidonge vya Vitamin ‘A’ vinaweza kutumika kudhibiti maambukizi ya UKIMWI kwa mtoto kutoka kwa mama wenye virusi vya ugonjwa huo wanapokuwa waja-wazito, imegundulika.

Kulingana na maelezo ya wataalamu, watoto wachanga wanaweza kuambukiza ukimwi kutoka kwa mama zao wakati wakiwa tumboni, wakati wa kuzaliwa na wakati wa kunyonya maziwa ya mama zao.

Ripoti ya Unicef ya mwaka 1998 kuhusu hali ya watoto Duniani inaonyesha kuwa utafiti ambao umekuwa ukifanaywa tangu mwaka 1994 umewawezesha wanasayansi kugundua uwezekeno wa lishe bora kutumika kama njia za kupunguza uambukizaji UKIMWI kwa watoto kupitia kwa mama zao.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo maabukizi hayo yanatishia uhai wa watoto kati ya milioni nne na milioni tano ifikapo karne ijayo hasa katika nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Ripoti hiyo imesema utafiti wa kina kwa mama wenye UKIMWI uliofanyika nchini Malawi mwaka 1994, ulionesha kuwa ni asilimia saba tu ya mama wenye vitamin ‘A’ ya kutosha mwilini waliowaambukiza watoto wao UKIMWI, ikilinganishwa na asilimia 32 ya kina mama wenye upungufu wa vitamini hiyo ambao watoto wao waliambukizwa ugonjwa huo hatari.

Hali hiyo inaonyesha kuwa upo uwezekeno mkubwa kwa kina mama wenye upungufu wa vitamin ‘A’ mwilini kuwaabukiza watoto wao virusi vya ugonjwa huo, mara nne na nusu ya akina mama wenye vitamini hiyo, ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya UNICEF na kuongeza kwamba hata utafiti wa mwaka 1995 uliofanyika nchini Kenya ulibaini wingi wa virusi vya UKIMWI kwenye maziwa ya mama wenye upungufu wa vitamini ‘A’.

Aidha utafiti huo ulionyesha kuwa kina mama wenye virusi vya UKIMWI ambao pia wana upungufu mkubwa wa vitamini ‘A’ uwezo miili yao ni mdogo mara tano zaidi ikilinganishwa na wenye vitamini hiyo ya kutosha, kuweza kuviondoa viumba mwili (cells) vilivyoambukizwa virusi kutoka katika sehemu za uzazi, kigezo ambacho ni muhimu katika maabukizi ya ugonjwa huo kwa njia ya kujamiiana au kwa kupitia kwa mama mjamzito.

Wanasayansi pia walijaribu kudhibiti uambukizaji ukimwi kwa watoto wakiwa tumboni kwa kuwapa kina mama dozi ya dawa ya vidonge inayoitwa ‘Zidovudine’wakati wakiwa waja-wazito.

Njia hiyo imeonyesha kufaa katika kupunguza uambukizaji huo, lakini ni ghali mno kwa watu wengi katika nchi zinazoendelea kuweza kumudu kulipia.

Hata hivyo ripoti hiyo imesema dawa za gharama nafuu za ‘Zidovudine’ kwa matumizi ya vipindi vifupi na vidonge vingine zinafanyiwa majaribio nchini Haiti, Sub-Sahara Afrika na Asia ya kusini-Mashariki.

Vitamini ‘A’ hupatikana kwa njia ya vidonge vya vitamini hivyo na katika vyakula mbalimbali ikiwa ni pamoja na maziwa ya mama, maziwa ya n’gombe, maini, mayai, siagi, karoti, maboga, mboga za majani,

 

BAADA YA POLISI KUTUMWA KUMKAMATA

Mchungaji aanguka chini na kuzimia

Na Freedom Msuya- Mwanga

Mchungaji wa KKKT Dayosisi ya Pare aliyesimamishwa kazi Bibi Joyce Muze alianguka na kuzimia hivi karibuni baada ya kuwaona polisi waliotumwa kumkamata.

Tukio hilo la aina yake lilitokea hivi karibuni nyumbani kwa mchungaji huyo (mwanamke) baada ya polisi kutaka kumkamata kufuatia madai kwamba alifunga kanisa alilokuwa akilihudumia kabla ya kufukuzwa kwake ili Mchungaji mwingine asilitumie na yeye mwenyewe kuendesha ibada nje ya kanisa hilo.

Mchungaji huyo alisimamishwa kazi ya uchungaji pamoja na wenzake sita kufuatia kitendo chao kuasi

Dayosisi ya Pare na kutangaza kuanzisha dayosisi ya mpya ya Mwanga ambayo inapingwa vikali na Uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) hali ambayo imeleta mgawanyiko katika dayosisi hiyo ya Pare.

Baadhi ya Wachungaji ambao wamefukuzwa kazi wamekuwa wakiendelea kutoa huduma mbalimbali za kichungaji kama vile kubatiza, kufunga ndoa, kuzika na mengineyo licha ya kuwa nafasi zao zimeshachukuliwa na wachungaji wengine.

Mchungaji Muze ambaye alipangwa katika Parishi ya Mamba kabla ya kufukuzwa kwake anatuhumiwa pia kwa kuwashawishi waumini wa Parishi hiyo kufunga Kanisa hilo kitendo kilichosababisha Mchungaji aliyepangiwa parishi hiyo Herbet Msangi kuendesha ibada nje ya kanisa:

Baada ya kuzinduka katika tukio hilo la Mei 2, mwaka huu na kuhojiwa na polisi, Mchungaji Muze inadaiwa alikiri kufunga kanisa hilo lakini kutokana na afya yake kuwa mbaya aliachiwa huru na kutakiwa kuripoti kituoni Mwanga kesho yake yaani Mei 3, 1999.

Hii ni mara ya pili kwa mchungaji huyo kukamatwa, kwani alishakamatwa kwa mara nyingine na kufunguliwa kesi mahakamani kufuatia tuhuma ya kumwita Askofu wa Dayosisi ya Pare Mheshimiwa Msangi kuwa ni Firauni.

Naye Mchungaji Hubert Msangi wa Parishi hiyo anayetambuliwa na dayosisi hiyo ya Pare alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu kufungwa kwa kanisa na kuendesha ibada nje, alisema kwamba ataendelea na kazi kama kawaida bila kusita kwani ni wajibu wake kuitikia wito popote anapotumwa kwa ajili ya kulisha kondoo wa Bwana.

Mgogoro wa madai ya dayosisi ya Mwanga ulilipuka kwa nguvu mwishoni mwa mwaka jana na matukio kadhaa yasiyopendeza likiwemo la baadhi ya waumini kuvamia madhabahu na kutaka kumvua Mchungaji wao joho, jambo ambalo limepelekea watu kadhaa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kuzusha ghasia kanisani na kuhatarisha amani.

TUKUTA kufanya upya usajili wa waagizaji chakula

Na Dalphina Rubyema

Tume ya Kudhibiti Vyakula ya Taifa (TUKUTA) itafanya upya usajili wa waagizaji wa vyakula nchini, baada ya kugundua kuwa kuna ukiukwaji wa sheria unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara ikiwa ni pamoja na kuingiza vyakula visivyokuwa na alama ya wazalishaji "label", kuthibitishwa ubora wala tarehe ya kuisha muda wa matumizi yake.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa TUKUTA, Bw.Fabian Magoma wakati wa mkutano wa wenye maduka ya kuuza vyakula jijini uliofanyika hivi karibuni ofisini kwake Ocean Road Jijini Dar es Salaam.

Bw.Magome alisema asilimia 90 ya watu wanaofanya biashara ya vyakula hawana usajili hali inayosabisha kuingiza nchini vyakula visivyokuwa na label na hivyo kusabisha kukwama kwa zoezi la kutambua aina ya vyakula vinavyoagizwa na wafanyabiashara hao na kuhatarisha afya za wanachi.

Bwana Magome aliendelea kusema kuwa lengo la kuweka label kwenye chakula ni kuonyesha aina ya chakula kilichoagizwa na kwamba hiyo ni kwa mujibu wa sheria ndogo ya label ya chakula ya mwaka 1989.

Alisema kuwa sheria hiyo ina masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na kuonyesha jina la biashara, jina halisi la chakula, ujazo na kwamba kama siyo halisi basi lazima label hiyo ieleze na pia kutakiwa kuonyesha tarehe ya kutengenezwa chakula pamoja na ile ya kuisha muda wa matumizi yake. Alitaja masharti mengine kuwa ni lazima label ya chakula ionyeshe rangi na dawa za kuhifadhia,vikolezo bandia,viini vilivyo changanywa katika chakula hicho, jina na anuani halali ya mtengenezaji na kusisitiza kuwa taarifa hizo zote ni lazima ziandikwe kwa maandishi yanayosomeka na kueleweka ama kwa lugha ya Kiingereza au Kiswahili.

Bwana Magome aliwataka wafanyabiashara hao kupitisha vyakula vinavyoagizwa katika vituo vilivyoidhinishwa na sheria ambavyo ni Tanga, Dar es salaam ,Lindi, Mtwara, Himo mkoani Kilimanjaro, Namanga, Musoma, Mtukula, Bukoba, Mwanza, Kigoma, Tunduma na Itungi na kuongeza kwamba vyakula vyote vinachoingizwa nchini ni lazima viambatane na uthibitisho wa afya "Health Certificate".

Alisema soda za kopo zenye label zilizoandikwa kwa lugha ya kiarabu ambazo bado zinaendelea kutumika hapa nchini , zinangia nchini kinyume cha sheria.

Waunga mkono Kanisa la Malawi kupinga maonyesho ya picha zisizofaa

Josephs Sabinus na Dalphina Rubyema

MAKANISA mbalimbali nchini yameunga mkono hatua ya Makanisa nchini Malawi kuungana katika kupinga sinema ambazo zinazoonyesha picha ambazo ni kinyume cha maadili ya nchi hiyo, picha ambazo huonyeshwa sehemu mbalimbali nchini humo.

Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, viongozi wa makanisa ya Anglikani, Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) waliunga mkono hatua hiyo na wakasema kwamba tatizo linaloikumba nchi ya Malawi halina tofauti na la hapa nchini ambapo filamu zinazoenda kinyume na maadili huonyeshwa sehemu mbalimbali vikiwemo vituo vya Televisheni.

Katibu Mkuu Msaidizi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nchini ,Padri Pius Rutechura alisema kuwa kitendo cha makanisa ya Malawi kuungana ili kupinga sinema hizo ni wazo zuri na la kishujaa katika kutetea na kulinda maadili ndani ya jamii na akasema kuwa hapa nchini inakuwa vigumu Kanisa kujua watu wanaoingiza sinema hizi na hata kama kanisa litaingilia kati inawezekana vyombo vya dola visiunge mkono.

Alisema Kanisa Katoliki linaelewa kwamba baadhi ya filamu na vitabu vinavyotoka nje ya nchi vinaenda kinyume na maadili ya jamii ya Kitanzania na akaongeza kuwa maadamu vitu hivi vipo,kanisa litazidi kuitahadhalisha jamii ili kuwa makini na sinema hizo zinazochangia kwa kiasi kikubwa kumomonyoka kwa maadili ndani ya jamii ya kitanzania.

Aidha Padri Rutechura alifafanua kwamba nyingine zimekuwa zikionyeshwa hadharani na mbele ya watoto lakini hazina maadili, mafunzo wala ujumbe wowote wa kudumu na akatoa mfano wa sinema za Holly Wood ambapo waigizaji wake ni kutoka nchini Marekani.

Alisema tatizo kubwa linalochangia suala hili ni Watanzania walio wengi kujenga kasumba kwamba kila jambo linaloingia kutoka nchi za Ulaya ni zuri kitu ambacho alisema siyo kweli.

Padri huyo aliishauri serikali kuweka sheria itakayozuia uingizaji wa picha na vifaa ambavyo vinaoonekana kuvunja maadili ya jamii na iweke adhabu kali kwa mtu au kundi litakaloonekana kuvunja sheria hiyo.

Naye Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Anglikana, Padri Dk.Frank Kajembe alisema kimaadili kanisa hilo haliruhusu mambo hayo na kwamba linahubiri watu washike amri kumi za Mungu na Kanisa linazidi kuyalaani mambo haya ya sinema za namna hiyo.

"Kanisa letu linalaani vitendo vyovyote vinavyoenda kinyume na maadili ya jamii ya Kitanzania na hivi sasa serikali inaoneka kulifumbia macho suala hili maana sinema za kutisha zinazidi kuonyeshwa katika Televisheni mbalimbali za hapa nchini"alisema Dk.Kajembe.

Naye Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)-Dayosisi ya Mashariki na Pwani Mchungaji Adamu Kombo amesema uamuzi wa makanisa nchini Malawi hauna budi kuigwa na nchi zote zenye lengo na mwelekeo wa kudumisha maadili katika jamii zao.

"Ingawa Tanzania hatuna chombo cha kuzuia sinema hizo, hatukubaliani nazo na hii ni changamoto kwetu tuwe na chombo kama hiki", alisema na kuongeza kwamba tunaharibu utamaduni na kuleta uchafu wa kiroho na kimaisha na hii yote labda ni kwakuwa serikali imetoa uhuru mkubwa.

Mchungaji Kombo alitoa wito kwa vikundi vyote vya dini vya Kikristo na vya Kiislamu kuungana ili kuwa na chombo kimoja chenye nguvu za kuzuia uvunjaji wa maadili kunachochangiwa na sinema pia majarida yasiyo na maadili mema.

Februari 11, mwaka huu Tume ya huduma ya makanisa nchini Malawi ilizindua kampeni kubwa ya kukagua sinema zinzopotosha na zisizo na maadili kwa jamii na vyombo vingine vya namna hiyo ili kuilinda jamii hiyo isizidi kupotelewa na maadili ambapo shirika moja la Haki za Binadamula Denmark (Danish human Rights) lenye makao yake makuu huko Lilongwe lilitoa Dola za Kimarekani zipatazo10,000 kwa ajili ya kampeinihiyo.

Mpango huo unafuatia kuoza kwa maadili kulikoelezwa kuwa kunachochewa na kutokuwepo mpango wa kuchuja sinema na majarida mbalimbali yanayoingizwa nchini humo na ulilenga katika kuwalinda vijana wasizidi kuathirika na utamaduni mchafu wa nchi za kigeni.

Siasa makanisani zinaleta vurugu - Mtheolojia

Na Neema Dawson

IMEELEZWA kuwa kuchanganya dini na siasa katika makanisa kunachangia kwa kiasi kikubwa kuzuka kwa migogoro miongoni mwa waumini na vikundi mbalimbali pia kumomonyoka kwa maadili katika makanisa mengi.

Hayo yalisemwa na Mtheolojia Bi. Cecilia Kwikima wakati wa sherehe za akina mama wa Kianglikana zilizofanyika katika kanisa la Mtakatifu Albano jijini Dar es Salaam.

Bi Cecilia aliwataka waumini kuacha kuingiza siasa katika taratibu za kikanisani na kuwataka kuenenda sambamba na maandiko matakatifu ambayo yako katika Biblia takataifu.

Bi Cecilia ambaye ni mwanafunzi wa theolojia mwaka wa tatu katika Chuo cha Theolojia cha Kianglikana kilichoko Bugruni mjini Dar es Salaam, alisema wahubiri wanaosimama mathabauni wanatakiwa kutoa mifano ya kibiblia zaidi badala ya kurejea sera mbalimbali za vyama vya siasa na kuongeza kwamba kila jambo lina wakati na mahali pake.

Aidha alionya watu kuacha tabia ya kutumikia Mungu na siasa na kuwashauri kuchagua moja kati ya hayo kwani mchanganyo huo unaweza kusababisha migogoro mingi na mikubwa pia kujenga chuki miongoni mwa waumini na vikundi mbalimbali vya dini.

Mtheolojia huyo aliwahimiza viongozi wa makanisa kutilia mkazo zaidi mafundisho ya kiroho kwa waumini wao, hasa wakati huu ambao jamii inakabiliwa na matatizo ya kushuka kwa maadili.

Wachumba kujamiiana kabla ya ndoa ni uasherati - Paroko

Na Getruder Madembwe

Vijana ambao wamo katika uchumba wametakiwa kutofanya tendo la ndoa kabla ya kufunga ndoa zao kwani uchumba unaweza kuvunjika wakati wowote na kuwaacha wakiwa na sifa mbaya ya uasherati.

Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Padri Deogratias Mbiku wa Parokia ya Chuo Kikuu sehemu ya mlimani, wakati akitoa mada juu ya Uchumba na Ndoa kwenye ukumbi wa Nkrumah chuoni hapo.

Padri Mbiku ambaye pia ni mlezi wa Chuo Kikuu alisema kuwa kuonyeshana upendo baina ya wachumba sio lazima kujuana kimwili badala yake ni kuombeana kwa Mungu ili malengo yao yaweze kufanikiwa.

"Upendo wa kweli ni wa kumtakia mwingine mema na siyo mabaya , kujuana kimwili kabla ya ndoa ni dhambi na uchumba si ndoa kwani unaweza kuvunjika wakati wowote hivyo wachumba waombeane kwa Mungu na kulinda uchumba wao uwe safi,"alisema hayo Padri Mbiku.

Aliwataka vijana ambao hawajapata wachumba kuomba nguvu za Roho Mtakatifu ziwe msaada na uongozi mwema katika kuchagua mchumba toka kwa Kristo Mwokozi.

Pia aliwataka vijana kutumia muda wa uchumba kujadili mambo muhimu juu ya maisha yao ya baadaye na maendeleo ya familia wanayotarajia kuwa kuitunza.

Semina hiyo iliwashirikisha wanafunzi kutoka chuo kikuu, watu kutoka taasisi ya elimu ya juu na wanafunzi wa sekondari.

Makanisa kutoa elimu ya uchaguzi

Na Dalphina Rubyema

WAKATI uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge unakaribia kufanyika,Kikundi cha Majadiliano ambacho kinaunganisha Makanisa mbalimbali ya Kikristo kinachoshughulika na masuala ya kisiasa na kiuchumi hapa nchini cha Tanzania Ecumenical Dialogue Group (TEDG) kitaanza uhamasishaji wa wananchi na vyama vya siasa pamoja na viongozi waliopo madarakani juu ya uchaguzi huo utakaofanyika mwaka kesho na zoezi hilo litaanza hivi karibuni.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi hivi karibuni,Mwenyekiti wa TEDG na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk. Method Kilaini alisema uamzi huo umefikiwa baada ya TEDG kukutana na Makanisa mbalimba ya Kikristo ya nchini Ujerumani katika mkutano wa siku sita uliofanyika mjini Bonn, Ujerumani.

Padri Kilaini alisema kuwa mkutano huo ulioanza Mei hadi 8 mwaka huu ulijumuisha ujumbe wa watu watano kutoka TEDG ambapo pamoja na makanisa mbalimbali ya nchini Ujerumani ,mashirika mbalimbali ya nchini humo likiwemo la EZE pia yalishiriki mkutano huo.

Mbali na yeye,aliwataja washiriki wengine alioongozana nao kuwa ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Dk.Wilson Mtebe ,Mratibu wa TEDG,Bibi Jesca Mkucha na wajumbe wengine wawili ambao ni Marry Mgila na Bibi Ndemba Mbise.

Akitoa ufafanuzi zaidi juu ya TEDG,Mwenyekiti alisema kuwa Kikundi chake kilichoanzishwa mwaka 1992 kinafanya kazi kwa kushirikiana na makanisa mbalimbali ya nchini Ujerumani na hufanya kazi zake katika ngazi ya Jimbo,Kanda na Taifa ambapo madhumuni yake ni kujenga jamii yenye kuelewa mambo yanayoendelea katika Ulimwengu kiuchumi na kisiasa.Akielezea uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Padri Kilaini alisema kabla ya uchaguzi huo TEDG ilitoa mafunzo katika Kanda sita, mafunzo yaliyohusu uelimishaji wa wananchi juu ya uchaguzi ambapo watu 8760 walielimishwa.

Aliongeza kuwa hata baada a uchaguzi huo TEDG ilifanya warsha ndogo ya kupata taarifa kutoka sehemu mbalimbali nchini inayoeleza jinsi uchaguzi ulivyofanyika.

Mbali na suala hili la uhamasishaji,mkutano huo pia ulifanya tathmini pamoja na kupanga mikakati ya kusaidiana na kujulisha watu jinsi ulimwengu unavyokwenda ,kiuchumi na kisiasa. Hata hivyo hakutaja kiasi cha pesa kitakachotumika katika kipindi hiki cha uhamasishaji.