Ujima umerudi kwa sura nyingine - Pengo

MFUMO wa Uchumi wa ujima ambapo uzalishaji wa bidhaa unatiliwa maanani bila kujali wazalishaji unajirudia kwa sura nyingine nchini na duniani tofauti na ilivyokuwa miaka ya kabla ya kuporomoka kwa Ukomunisti duniani.

Hayo yalisemwa yalisemwa hivi karibuni na Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo,wakati wa tamasha la Siku ya Mtakatifu Josefu Mfanyakazi lililoandaliwa na Vijana wa Kikristu wa Kanisa Katoliki nchini (VIWAWA) na kufanyika kwenye ukumbi wa Don-Bosco jijini.

Kardinali Pengo ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam,alisema kuwa hivi sasa walio wengi wanajali bidhaa zinazozalishwa kuliko wazalishaji na watu hao alisema wamefikia hatua ya kuthamini mashine na vifaa vingine vya uzalishaji kuliko binadamu.

Alisema wenye uwezo wa Sayansi na Teknolojia wamekuwa wakijali matumizi ya Komputya na Robot katika uzalishaji wa bidhaa badala ya binadamu na kisha kudai kuwa inadadi ya watu ni wengi hivyo lazima uwepo uzazi wa mpango.

"Kompyuta inachukuwa nafasi za kazi za watu 1,000 na hivyo kuwaacha 999wakiwa hawajui wataenda wapi,"alihoji Kardinali Pengo na kuongeza kuwa hapo ndipo linapokuja suala la uzazi wa mpango kwa kisingizio kuwa tupo wengi hivyo ni lazima mbinu yoyote itumike ili kutupunguza.

Akiwahutubia vijana wa Kanisa Katoliki ambao ndio walioandaa tamasha hilo ,Pengo alisema zama za ujima ambapo wazee na watu wengine kama vilema walikuwa wakirundikwa sehemu moja ili kusubiri kifo inajirudia.

Alisema kundi hilo katika jamii lilikuwa likionekana ni la watu wanaokula bure hivyo hawakustahili kuwepo na waliokuwa wanathaminiwa ni wale wenye nguvu za kuzalisha mali tu na wala si vingine.

Alisema hivi sasa kinachofanyika ni kuwa na mashine za kisasa sehemu za kazi hali ambayo inapelekea walio wengi kukosa nafasi za kazi na papo hapo zinasambazwa propaganda kuwa watu ni wengi hivyo lazima uwepo uzazi wa mpango.

"Hawa watu wanataka kutumaliza na namna hiyo naamimi sina jibu la nini la kufanya ila vijana ni lazima mjue kinachofuata katika milenia ijayo"alisema na kufafanua kuwa ni lazima kila mmoja afanye kazi ambayo itahusisha mikono yake.

Alisema kuwa Mtakatifu Yosefu ambaye ndiye Mtakatifu wa VIWAWA,alikuwa ni fundi seremala na alitumia mikono yake, ,hivyo ni vema pia kwa vijana kuchapa kazi kwa kushirikiana katika jamii walizomo na wasikubali kumezwa na mabadiliko yanayokuja.

"Mungu aliumba wanadamu ili waijaze na kuitawala dunia na wala hakuweka ahadi kuwa wanadamu wenyewe ndio wakabidhi ulimwengu kwa Kompyuta na Robot, hivyo amesisitiza umuhimu wa kuwa waangalifu na kuelewa maana ya uzazi wa mpango"alisema.

Alisema Kardinali Pengo kuwa wakati ujao wenye uwezo kifedha ambao ndio hao wanaoshikilia Sayansi na Teknojia ,wanachotaka kufanya ni kuwakimbiza wanadamu katika ulimwengu wao walioahidiwa ili kuvipisha "vitu" ambavyo ni Kompyuta na Robot.

Awali akisoma risala wakati wa tamasha hilo,Katibu wa VIWAWA Jimbo Kuu la Dar es es Salaam,Bw.Petro Kinumbi alisema suala la ajira limekuwa likiwakwaza vijana wengi katika kuchangia shughuli za chama chao.

Alisema hali hiyo inapelekea walio wengi kujiondoa na kujiingiza katika matendo maovu kama uvutaji bangi ,matumizi ya madawa ya kulevya na vitendo vingine ambavyo ni kinyume na maadili ya jamii.

Bw.Kinumbi alisema kuwa wapo katika jitihada za kutafuta wafadhili ili waweze kuendesha shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na alisema wamekuwa wakiendesha semina za mafunzo kwa vijana sehemu mbalimbali.

Tamasha hilo lilijumuisha Vijana kutoka Parokia mbalimbali za Jimbo Kuu la Dar es-Saalam na michezo mbalimbali ilionyeshwa katika tamasha hilo.

 VIPANDIKIZI: sumu kwa ajili ya kuua watu weusi?

Wakati Wizara ya Afya kupitia programu yake ya Nyota ya Kijani na Shirika la hiari la UMATI wanasifia matumizi ya vipandikizi kama dawa na njia nzuri ya kupanga uzazi, utafiti uliofanywa na nchi mbalimbali duniani ikiwemo Marekani umedhihirisha kuwa dawa hiyo ina kiwango kikukbwa cha chachu iitwayo "progestorene" inayoleta madhra makubwa kwa watumiaji wake.

Taarifa iliyotolewa na Chama Cha Kutetea Uhai (Pro-Life) nchini Tanzania wiki hii imesema katika Jimbo la Florida nchini Marekani watu weusi ni asilimia 13.8 ya watu wote lakini asilimia 56 ya watu wote wanaotumia vipandikizi hivyo ni weusi.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa katika kitabu cha Brian Clowes (Phd) kiitwacho "The Facts of Life" (1997,) imeelezwa kuwa matumizi ya vipandikizi husukumiwa watu weusi na maskini ili wavitumie na kwamba ndiyo maana majaribio yake yamekuwa yakifanywa katika nchi maskini ambapo nchini Marekani watumiaji wakuu wa sumu hiyo ni watu weusi.

Chachu ya kawaida "progestorene" hutolewa na mwanamke wakati wa kipindi cha uzazi ili kuandaa mji wa mimba kwa ajili ya kupokea na kumtunza mtoto iwapo tendo la ndoa litafanyika wakati huo.

Dawa hiyo ya bandia ambayo hutengenezwa viwandani hutumiwa na wanawake kama dawa ya kaharibu mazingira ya tumbo la uzazi na kumfanya mtoto mchanga auawe na mama yake akiwa tumboni na kutolewa nje pamoja na damu ya mwezi yaani kutoa mimba (abortion.)

Taasisi ya utafiti juu ya masuala ya Idadi ya Watu Duniani yenye makao yake nchini Marekani, "POPULATION RESEARCH INSTITUTE" imetoa wito wa kusitisha utengenezaji, usambazaji, uuzaji na utumiaji wa dawa hiyo.

Taarifa imeongeza kuwa, akiongea katika mkutano huko Washington,Marekani, Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo Steven Mosher aliita dawa hiyo kuwa ya mauaji kwani ina kiwango kikubwa cha madhara ukilinganisha na dawa nyingine za kupanga uzazi kwani inaleta ulemavu wa kudumu na kuongeza uwezekano wa maambukizo ya virusi vya UKIMWI.

Shirika la Utangazaji la (BBC) katika moja ya vipindi vyake ilionyesha kipindi cha jinsi dawa hiyo inavyotengenezwa bila kuzingatia utaalamu na majaribio yake kufanyika kwa wanawake wa nchi za dunia ya tatu kama Haiti na Bangladesh ambapo wanawake walieleza madhara wayapatayo kiafya na jinsi wanavyodanganywa kwa kuelezwa kuwa dawa hiyo ni salama na haina madhara yoyote.

Halmashauri ya Idadi ya Watu ya New York ndiyo inayomiliki utengenezaji wa dawa hiyo iliyovumbuliwa na Sheldonsegal wa Shirika la Rockefeller Foundation na iliidhinishwa kwa matumizi na Shirika la Chakula na Madawa la Marekani (FDA)mnamo Desemba 10,1990 na hutengenezwa na kampuni ya Wyeth Ayerst ambayo ni kitengo cha Shirika la American Home Productions.

Taarifa hiyo imezidi kuvifafanua vipandikizi kuwa ni dawa inayowekwa kwenye vijiti sita vilivyowekwa sumu ya "progestorene levonorgestrel" ambavyo huwekwa ndani ya ngozi ya sehemu ya juu ya mkono ili kuzuia au kuua mimba kwa miaka mitano.

Idadi ya wanawake milioni moja wa Marekani na milioni mbili na nusu duniani kote wanakadiriwa kuwa wamewekewa vipandikizi ambapo nchini Marekani utumiaji wa vipandikizi humgharimu mtumiaji dola 300 mpaka 600.

Takwimu za Pro-life zinaonyesha kuwa katika majaribio yaliyofanyika tangu mwaka 1972 wanawake katika nchi za Haiti, Brazil, Indonesia, Bangladesh, Jamaica , Chile na Jamhuri ya Dominica. USAID, Shirika la Misaada ya Maendeleo ya kimataifa liligharamia kiasi cha dola milioni 20 kwa ajili ya majaribio hayo.

Hadi mwaka 1998 wanawake wapatao 50,000 waliotumia dawa hiyo huko Marekani wamelishitaki shirika la Wyeth-Ayerst kutokana na madhara waliyoyapata.

Bibi Colglazier (23) alianza kupoteza uwezo wa kuona siku nne na baada ya juma moja alipata upofu kabisa. Naye Bi.Triezenberg (24) alipata matatizo ya kuumwa na kichwa na kuongezeka uzito na unene kwa kiasi kikubwa na kisha kupoteza uwezo wa kuona. Habari zaidi zinasema alipoomba kuondolewa vipandikizi hivyo, havikuoneka.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vipandikizi hutumika kwa misingi ya ubaguzi kwani dawa hii ilifanyiwa majaribio miongoni mwa wanawake weusi na maskini.

Ikitoa mfano taarifa inasema nchini Marekani nchini Marekani matumizi ya vipandikizi yanashauriwa kwa watu weusi pekee wakati watu weupe huzuiwa kuitumia dawa hiyo.

 Kila mwanafunzi kuwa na kompyuta Sekondari ya St. Anthony

ILI kujiandaa vema katika kuingia karne ya ishirini na moja ya sayansi na teknolojia, shule ya sekondari ya Mtakatifu Antoni iliyopo Mbagala jijini Dar -Es _Salaam inatarajia kuzindua mfuko wa elimu utakaoiwezesha kuwa na kompyuta zinazotosheleza idadi ya wanafunzi wote na kuboresha zaidi mazingira ya utoaji wa elimu shuleni hapo.

Wakizungumza kwa pamoja na mwandishi wa habari hizi shuleni hapo katikati mwa juma, Mkuu wa Shule hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Uzinduzi wa Mfuko huo Brother Martin Masabo na msaidizi wake ambaye pia ni Katibu wa kamati hiyo John-Bosco Katatumba walisema mfuko huo unajulikana kama MFUKO WA KUMBUKUMBU YA MAREHEMU PADRE FIDELIS VERSARI (OFM.CAP).

Walisema ili kuuweka hai mfuko huo ambao pia una lengo la kusaidia katika kugharamia wanafunzi wanaosoma shuleni hapo wasiomudu gharama za masomo yao, kila mwanafunzi na wafanyakazi wote wamepewa barua na kadi zenye nafasi 25 kila moja kwa ajili ya kupeleka kwa wazazi, walezi na wafadhili mbalimbali ili kuchangia mfuko huo uliosajiliwa rasmi kiserikali Julai15, mwaka jana.

Mkuu huyo wa shule Bro.Masabo ametoa wito kwa wazazi, walezi, na wafadhili mbalimbali kujitokeza zaidi katika kuchangia mfuko huo na akaongeza kusema kuwa lengo lingine la kuanzishwa kwa mfuko huo unaotarajiwa kuzinduliwa rasmi Juni 7, mwaka huu katika maadhimisho ya miaka mitano ya kifo cha mwanzilishi wa shule hiyo Padre Fidelis Versari ni kuunga mkono juhudi za kuleta maendeleo ya elimu nchini. Kuhimiza moyo wa ubunifu na uongozi bora miongoni mwa vijana wa jamii ya Kitanzania ni kusudi jingine.

Kwa muda wa wiki nzima iliyopita wanafunzi wa shule hii wamekuwa wakionekana mitaani kwa hali ya uchangamfu na bidii wakizunguka na barua zao za michango zenye kumbukumbu namba AF/1041/Vol.11/404 ya Aprili 29, mwaka huu iliyosainiwa na mkuu wa shule hiyo ili kuwatafuta na wafadhili kuwaomba waachangie mfuko huo ambapo wafadhili wanaombwa kuchangia kiasi chochote kuanzia shilingi 500/= na kuendelea.

Ujenzi wa shule ya sekondari ya Mtakatifu Antoni ambayo hutoa mafunzo ya kompyuta kwa wanafunzi wote wa kidato cha kwanza hadi cha sita wapatao 1168 wa dini na kabila zote, ulianza mwaka 1986 hadi 1988 chini ya marehemu Padre Fidelis Versari aliyezaliwa Mei7, 1917huko Macato Saraceno nchini Italia ambapo alibatizwa Juni 9, 1940kama mwanachama wa shirika la St,Franciscan Capuchin Fathers na kufariki dunia Juni 7,1994.

 Kanisa lahitaji misaada kuendesha hospitali

KANISA Katoliki Nchini Tanzania limesema linahitaji misaada zaidi kutoka kwa wafadhili mbalimbali ili kuweza kusaidia kuendesha huduma za kiafya katika hospitali zake zilizo chini ya kanisa hilo.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni Katibu Mtendaji wa Idara ya Afya katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Dk. Alban Hokororo alisema Kanisa Katoliki nchini hapa lina hospitali 40 katika majimbo mbalimbali, hospitali ya Rufaa Bugando ya Mwanza iliyo chini ya Baraza la Maaskofu pamoja na Zahanati zaidi 400.

Dk.Hokororo aliendelea kusema kuwa serikali imeingia mkataba na hospitali teule zilizopo majimboni na kwamba zinapata ruzuku ya asilimia 10 toka serikalini kwa ajili ya kuziendesha na kuboresha huduma za afya.

Alisema kuwa sera za hospitali hizo zilizo chini ya Kanisa Katoliki ni kutoa huduma za afya ili kuweza kuisaidia jamii, na kwamba hospitali hizo haziendeshwi kwa nia ya kupata faida kubwa kwani si za biashara hivyo wagonjwa hutakiwa kuchangia kwa kiasi kidogo na akaongeza kuwa kwa wasio na uwezo wa kuchangia, huduma hiyo hutolewa bure kama msaada.

Akizidi kufafanua juu ya uchangiaji, Dr. Hokororo alisema kiasi kinachopatikana ni kati ya asilimia 20 na 40 kiasi ambacho pamoja na ruzuku toka serikalini hufikia asilimia 50 hivyo kuhitaji asilimia 50 nyingine toka kwa wafadhili ambao hutoa misaada ya aina mbalimbali ili kuboresha huduma za afya katika hospitali hizo.

Aliongeza kuwa ingawa hospitali hizo ziko chini ya Kanisa katoliki uendeshaji wake unaenda sambamba na sera za Wizara ya Afya na sera za Kanisa Katoliki, ambapo Idara yake inahusika kutoa mafunzo pamoja na semina mbalimbali ili kuwaendeleza watu katika kazi zao ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri na utaalam mbalimbali pamoja na kuratibu kazi shughuli majimboni

Hokororo alisema hadi hivi sasa kuna hospitali moja ya Rufaa ambayo ni Bugando iliyopo Mwanza inayoendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, hospitali teule za wilaya ni 12 pamoja na hospitali zinazoendeshwa na majimbo ni 27 na zilizo chini ya mashirika ni mbili.

Mbali na hizo pia alisema kuna zahanati zaidi ya 400 zilizopo nchini na kwamba hadi hivi sasa kuna zahanati kadhaa zinazotarajiwa kufunguliwa katika majimbo mbalimbali.

Vijana waweka nadhiri ya kupinga uasherati

VIJANA wa Kikatoliki wameahidi mbele ya Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kutokushiriki katika tendo la ndoa nje na kabla ya ndoa ili kuepuka uvunjanji wa Amri ya Sita ya Mungu inayokemea vitendo vya uzinzi na uasherati na pia kuepuka ugonjwa hatari wa ukimwi

Vijana hao wa kikundi cha YOUTH ALIVE CLUB walitoa ahadi hiyo wakati wa maadhimisho ya miaka mitano ya kikundi hicho iliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa makao makuu ya Don Bosco Upanga jijini.

Akiongea katika dhifa hiyo Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo aliwaambia vijana na watu wenginewaliohudhuria kuwa kukusanyika kwao kusiwe ni kwa kucheza ngoma na ngonjera tu, bali kuwe ni kwa kuleta manufaa katika kufanya kazi ya Mungu.

Mwadhama Kardinali Pengo aliwahimiza vijana wamuombe Mwenyezi Mungu ili awasaidie waweze kuwa na nguvu za kudumu katika wito na mwisho waweze kuliokoa kanisa na watu wake kwenye majanga.

"Tunajua kuwa tumekusanyika hapa kwa ajili ya wito, hivyo tumuombe Mwenyezi Mungu atupe nguvu za kudumu katika wito, ‘’ alisema na kuongeza kuwa kuongezeka kwa maafa hapa nchini ni changamoto ya wito huo ili watu wafanye kazi ya Mungu ya kulinda na kulitetea kanisa lisisambaratike.

Mfumo wa habari katika nchi za SADC una matatizo lukuki - Profesa Mmari

Mwenyekiti <P>wa Baraza la Habari Profesa Geofrey Mmari amesema mfumo wa upashanaji wa habari katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa Afrika (SADC) unakabiliwa na matazizo lukuki pamoja na kuwepo kwa kanuni pia uhuru wa habari unaotambulika kikatiba katika nchi hizo.

Profesa Mmari alisema hayo hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani yaliyoandaliwa rasmi na Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-TAN) yaliyofanyika kwenye hoteli ya Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.

Alisema serikali nyingi katika jumuiya hiyo hazijihusishi kabisa na uhuru wa vyombo vya habari na kwamba vyombo vya habari vimekuwa vikinyimwa uhuru wa kufanya kazi kwa makusudi kabisa pasipokuwa na sababu za msingi.

Profesa Mmari ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu huria alisema inashangaza kuona hata vyama vya siasa vya upinzani katika nchi hizo ambavyo vingetakiwa kufahamu umuhimu wa habari katika jamii haviheshimu kabisa vyombo vya habari, hivyo kuacha vyombo hivyo kubanwa na sheria zilizowekwa kwa makusudi pia kuendelea usumbufu usio wa lazima kwa waadishi wa habari.

Alifafanua kwamba pamoja na kukua kwa demokrasia katika nchi za SADC uhuru wa habari katika nchi hizo umekuwa haukui na kwamba vyombo vya habari vinakabiliana na mazingira magumu sana ya utoaji na uapatikanaji wa habari katika jamii.

Aidha Profesa Mmari alisisitiza kuwa kwa kuwa demokrasia ya kweli inahitajika katika nchi za SADC basi upo umuhimu wa kuwepo kwa mawasiliano na ushirikiano wa karibu kati ya serikali hizo na vyombo vya habari pia jitihata za kukuza sekta za habari katika nchi wanachama ili kujenga demokrasia ambayo ni muhimu kwa jamii.

Profesa huyo alisema vyombo vya habari vinahitaji kupewa nafasi ili viweze kufanya kazi yake ipasavyo kubwa ya yote likiwa ni kuiwezesha jamii kujenga utamaduni wa amani hasa tunapoelekea karne ya 21 ambayo ni ya sayansi na teknolojia.

Alisema kwamba ili jamii iweze kujenga utamaduni wa amani inahitajika elimu juu ya umuhimu wa amani, demokrasia ya kweli katika jamii na kuinua kiwango cha demokrasia hiyo katika jamii, pia kuishi maisha ya upendo na mshikamano mkubwa.

Aidha alitaja mambo mengine kuwa ni kulinda na kuheshimu haki za binadamu pasipo ubaguzi, kulinda na kuyaheshimu mazingira na kupambana na umasikini pia kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika jamii kwa kila mmoja kupata mahitaji yanayolingana na thamani ya utu alionao.