Kanisa kuwafunza waumini namna ya kuwabana wanasiasa

Wakati Tanzania ikielekea katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2000, Tume ya Haki na Amani iliyo chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) imeazimia kutoa mafunzo kwa waumini wa kanisa hilo na wananchi wengine namna ya kuwachuja wanasiasa wanaowania madaraka ya Serikali kuanzia ngazi ya Mtaa hadi Taifa.

Akiongea katika semina ya siku nne ya kitaifa ya Tume hiyo jijini wiki iliyopita, Katibu wa Tume hiyo Padre Vic Missiaen, alisema kwa hali ilivyo hivi sasa nchini ambapo wananchi wengi wana hali ngumu ya maisha akitokea mtu mbaya wa kuwachochea waingie katika ghasia hatapata kazi ngumu.

Kwa sababu hiyo alisema uangalifu wa hali ya juu usipokuwepo katika jinsi ya kuwachangua viongozi watakaoshughulikia matatizo ya wananchi ifaavyo, haitashangaza kuona Tanzania inaingia katika machafuko kama yale yaliyotokea huko nchini Rwanda.

Padre Missiaen, alisema wananchi wanapaswa kuelimishwa vema ili kuepuka utamaduni wa kuzungumzia majina ya watu badala ya masuala (issues). " Tusizungumzie majina ila tuwaulize; utatufanyia nini kwa tatizo letu hili?" alisema Padre huyo.

Katibu huyo aliwataka wajumbe wa tume hiyo ambao walitoka mikoa mbali mbali nchini wanapotetea haki na amani nchini kujitoa mhanga kusema kweli bila hofu kwa sababu kwa kufanya hivyo watakuwa wanafanya kazi ya Mungu.

"Tusibaki katika hali ya kuogopa kusema... lakini tujifunze namna ya kusema" aliangaliza Padre Missiaen na kuongeza kuwa katika utetezi wa haki jambo la kwanza la muhimu ni kushinda hofu na kuzingatia ukweli wa mambo.

Alieleza kigezo kingine muhimu ambacho ni kuwa macho, kwa maana ya kuyafahamu matatizo ya watu. "Watu wengi mijini wanapenda kuwa vipofu; wana matatizo mengi binafsi hivyo hawataki kuona matatizo ya wengine. Kama kanisa tuone matatizo ya jamii" alisema.

Mkazo mwingine alitaka uwepo katika takwimu badala ya kudakia mambo ya vichochoroni na kuyakubali na vile vile akasisitiza umuhimu wa kujitoa kwa dhati kwani ni heri kuwa na watu wachache waliojitolea kutetea haki na kulinda amani kuliko kundi kubwa la watu wenye kelele zisizo na utekelezaji.

Akifungua semina hiyo iliyoanza jumatatu iliyopita na kumalizika Alhamisi Askofu Paul Ruzoka ambaye ni Mwenyekiti wa Tume hiyo ya Haki na Amani alisema hali duni ya maisha ni moja ya sababu kuu za machafuko katika nchi mbali mbali.

"Tanzania je, ina hakika gani ya kuendelea kuwa kisiwa cha amani?" alihoji Askofu huyo ambaye amekuwa akishughulikia matatizo ya Wakimbizi katika Jimbo la Kigoma.

Alisema katika vita vinavyoendelea katika nchi za Maziwa Makuu hivi sasa baadhi ya Watanzania wamejipenyeza kupigana vita ili wapate posho.

Askofu Ruzoka alisema Kanisa lina wajibu mkubwa wa kulinda na kutetea haki za watu ndio maana Papa Yohane Paulo ll na hata Papa Leo Xlll alipenda kutetea haki za msingi za binadamu.

Naye Mbunge wa Jimbo la Muhambwe Bw. Archardo Ntagazwa, ambaye pia alihudhuria semina hiyo alitoa angalizo kwa watendaji wa Tume ya Haki na Amani kuwa macho katika utendaji wake kwani baadhi ya wanasiasa hususan wa chama tawala wanaweza kudhani kuwa chombo hicho kinatumika kuipa wakati mgumu serikali iliyopo madarakani.

 Wakatoliki huhama dini kutafuta faraja - Luena

MWENYEKITI wa Wanawake Wakatoliki nchini (WAWATA) Bibi Olive Luena, amesema Wakatoliki wengi wamekuwa wakiihama dini yao kutafuta faraja katika madhehebu mapya kutokana na matatizo ya maisha na kukosa faraja hiyo katika kanisa lao.

"Kuna uwazi fulani (vacuum) katika namna ya kushughulikia matatizo ya watu katika kanisa (Katoliki) ambayo yanapelekea watu kuhamia kwenye madhehebu mengine kutafuta faraja, amani au utatuzi wa matatizo yao," alisema Bibi Luena katika mada aliyoiwasilisha katika Semina ya Umisionari katika Sinodi ya Afrika iliyofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Msimbazi jijini.

"Tunahitaji roho ya Pentekoste mpya katika kanisa la Mungu ili kuwaweka huru waliosetwa na shida mbali mbali za kiroho na kimwili kama Kristu alivyofanya na kututuma tukafanye hivyo hivyo," alieleza Bibi Luena na kuongeza kuwa kuongezeka kwa madhehebu ya dini ni changamoto kwa kanisa Katoliki inayohitaji kubadili mbinu za umisionari.

Alisema madhehebu hayo yamekuwa yakiwavuta waumini wa Kanisa Katoliki na ukichunguza kwa undani utagundua kuwa waliovutwa hasa ni watu wenye shida mbali mbali wanawake na vijana ambao pengine wamekosa faraja katika jumuiaya au kanisa lao hasa katika jiji la Dar es Salaam.

Bibi Luena ambaye pia aliongelea hali ya uchumi nchini alisema kinyume cha matarajio ya wengi, Tanzania ni nchi inayorudi nyuma badala ya kusonga mbele.

"Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) zinaonyesha kuongezeka kwa umaskini kiasi kwamba matarajio ya kuishi sasa yameshuka kufikia miaka 50" alisema.

Aliongeza kusema kuwa idadi ya wasiojua kusoma na kuandika imeongezeka na Watanzania wanaoishi katika hali ya umaskini hohehahe imefikia asilimia 50. "Ajira kwa vijana wawe wamesoma au hawakusoma imetoweka kabisa" alisema na kufafanua kuwa wakati wale waliokuwa kwenye ajira wanapunguzwa na kupoteza kabisa matumaini.

Alisema kwa sababu hiyo kanisa halina budi kujizatiti kupambana na umaskini katika jamii kwani hata Kristo aliwajali wenye shida na kuwasaidia. "Kampeni kabambe za kuondoa umaskini zinahitajika" alisema.

 Padre Rwoma ateuliwa Askofu Singida

Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania, Ijumaa iliyopita,umesema Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili amemteua Mheshimiwa Padre Desderius Rwoma kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida.

Askofu Mteule Desderius Rwoma alizaliwa Mei 8,1947 katika kijiji cha Ilogero, Parokia ya Rutabo, Jimbo la Bukoba akiwa mtoto wa Balthazar Bururi na Aurelia Mukansingakwoga, wakiwa wote wawili Wakatoliki.

Katika masomo yake, alijiunga na Seminari ya maandalizi ya Rutabo mwaka 1963-64 na baadaye aliingia Seminari ndogo ya Rubya (1965-68). Kuanzia mwaka 1969-70 alijiunga na masomo ya Falsafa kwenye Seminari Kuu ya Ntungamo, Bukoba na alichukua masomo yake ya Teolojia kwenye Seminari Kuu ya Kipalapala mwaka 1971 hadi 1974.

Alipata daraja la Upadre Julai 28, 1974 kwenye Parokia ya Rutabo. Askofu mteule alifanya kazi za msaidizi wa Paroko Parokia ya Kassambya mwaka 1974. 1975 hadi 1976 alikuwa mwalimu kwenye Seminari ndogo ya Rubya.

Mwaka 1977 alikwenda masomoni kwenye Taasisi ya Kichungaji ya Gaba na mwaka 1978 hadi 1984 alikuwa Makamu wa Gombera na Mkurugenzi wa Kiroho kwenye Seminari ndogo ya Rubya.

Mwaka 1984 hadi 1987 alikuwa mlezi wa Shirika la Masista la Mt. Theresa la Bukoba na mwaka 1987 hadi 1997 alikuwa Gombera wa Seminari ndogo ya Rubya. Mwaka 1997 hadi kuteuliwa kwake, alikuwa ni Naibu wa Askofu wa Jimbo la Bukoba. Askofu Mteule Rwoma ana Stashahada ya Teolojia ya Kiuchungaji.

 Vijana waambiwa ‘thaminini maisha yenu kushinda vishawishi’

Vijana hapa nchini wametakiwa kujikubali wenyewe,kujithamini na kuyathamini maisha yao ili waweze kuepukana na vishawishi vya ulimwengu.

Changamoto hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa wa kikundi cha kuhamasisha vijana kufuata maadili kiitwacho YOUTH ALIVE, Bw. Anthony Norbert wakati wa kutoa mafunzo ya semina ya siku mbili katika shule ya sekondari ya Kigamboni Nevy. Semina hiyo ilikuwa na lengo la kutoa mafunzo ya maadili mema kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Akiongea katika semina hiyo iliyofanyika Jumatano iliyopita, Mwenyekiti wa kikundi hicho alisema vijana wanatakiwa kujijali kwani ulimwengu wa sasa umejaa vishawishi vingi.

Vijana hao pia walitakiwa waache kujihusisha na masuala ya uasherati, kubadili rangi ya miili yao kwa kujichubua na kuuza miili yao, kwani Mwenyezi Mungu alipowaumba alikuwa na lengo na makusudi mazuri.

Hivyo vijana walitakiwa kutojiongezea urembo kwa kuichezea miili yao kwani ni mahekalu ya Mwenyezi Mungu na kwamba Mungu bado anawahitaji kama alivyowaumba.

Akichangia mada hiyo mwanachama wa kikundi hicho Bi Rose Makalla, aliwashauri vijana kuutambua umuhimu wa kuwepo kwao duniani na kwamba Mungu ana makusudi mazuri ya uwepo huo.

Aitha semina hiyo iliwataka vijana kutothamini mambo ya ulimwengu ili kuepuka upotezaji wa muda pia kuwa waangalifu katika kuchagua marafiki na kutokubali marafiki ambao wanawaza kuwapotosha.

"Rafiki mwema ni yule anayekuelekeza mambo mema," alisema mmoja wa washiriki wa semina hiyo na kuwaonya wasichana wasikubali kudanganywa kwa vitu vidogo kama chips, kuku na fedha kwani vinachangia kuharibu maisha yao.

Mmoja wa wanasemina, alilaumu tabia ya wavulana kupenda kuoa wasichana mabikira wakati wao ndiyo huwaharibu usichana na kuwashauri kuacha tabia ya uasherati ili waweze kupata wasichana walio safi katika ndoa zao.

Aidha aliushutumu msimamamo wa baadhi ya taasisi mbalibali zinazojihusisha na masuala ya kutoa ushauri nasaha na kugawa vifaa vya kuzuia na kutoa mimba kwamba ni vishawishi vikubwa kwa vijana kujihusisha zaidi na masuala ya kujamiiana na kuongeza kwamba vifaa kama kondomu vinapogawiwa kwa wanafunzi wa shule za sekondari huamsha hisia za mapenzi kwa vijana hao.

Vifaa vya Kanisa visitumike kufanyia biashara - Askofu

Askofu wa Kanisa Katoliki Tanzania Jimbo la Tanga Antony Banzi amesisitiza kuwa vifaa vya kanisa vinatakiwa vitumiwe kwa ajili ya mawasiliano ya kueneza injili na si kuvifanyia biashara.

Askofu Banzi ambaye ni mwenyekiti wa idara ya mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania yasema hayo katika mkutano wa 24 wa mwaka wa idara hiyo, uliofanyika kwenye ukumbi wa baraza la maaskofu Kurasini Jijini.

Ameyataka majimbo ya kanisa hilo ambayo yamebahatika kupata vifaa kama video kamera, redio na televisheni kutoka kwa wahisani mbalimbali kuwa makini sana na kuvitumia vifaa hivyo kwa ajili ya kueneza injili na si kwa kufanyia shughuli ambazo ziko nje ya suala hilo.

Alisema swala la mawasiliano katika jamii ni muhimu hivyo kuwataka wakurugenzi wa habari na mawasiliano wa majimbo ya Kanisa Katoliki kutumia fursa waliyonayo na vifaa kwa ajili ya manufaa ya Kanisa na jamii nzima kwa ujumla na si kwa manufaa ya watu binafsi.

‘Majimbo yaliyo na vifaa kama vile video kamera wazitumie kurekodi mikanda ambayo itakuwa inatoa mafundisho kwa Kanisa la Mungu na mikanda hiyo isambazwe sehemu mbalimbali hapa nchini ili kila mkristo apate mafundisho ya kiroho’, alisema Askofu Banzi.

Alisema mikanda ya video iliyozagaa mitaani hivi sasa, haiwezi kumjenga mkristo yeyote kiroho.

Kwani imejaa picha zisizopendeza na kuongeza kwamba endapo juhudi za kusambaza mikanda yenye mafundisho ya kiroho zitafanikiwa basi jamii inaweza kunusurika kutoka katika hali mbaya ya mmomonyoko wa maadili ambao unazidi kushamiri na kukua siku hadi siku.

Askofu Banzi alisema kuwa wahisani waliotoa vyombo hivyo kwa ajili ya kueneza injili hivyo kusaidia kuijenga jamii katika maadili mema kwa manufaa ya kanisa.

 Wasio na ajira huchanganyikiwa wasikiapo mahubiri yahusuyo utoaji sadaka -Mratibu

Imeelezwa kuwa mahubiri yanayotolewa katika makanisa mbalimbali kuhusu utoaji wa sadaka yamekuwa yakiwachanganya vijana wengi wasio na ajira kutokana na matatizo ya ukosefu wa fedha ambao ni tatizo kubwa kwao.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa Vijana wa Chama cha Kujisomea Biblia- Tawi la Tanzania (Scripture Union) Bwana Emmaus Bandekile kwenye semina maalumu ya vijana iliyofanyika katika eneo la Mikadi-lililoko Kigamboni ufukweni mwa Bahari ya Hindi Jijini Dar es Salaam.

Ndugu Bandekile alisema pamoja na elimu waliyonayo, vijana wengi walioko makanisani wanakabilina na ugumu wa maisha kutokana na ukosefu wa ajira ambalo ni tatizo la kitaifa na kimataifa.

Amesema kutokana na hali mbaya ya kiuchumi wnayokabiliana nayo, vijana wengi wamekuwa na mawazo mabaya ikiwa ni pamoja kuyakimbia makanisa yao ili kuepuka ‘kero’ za mahubiri yanayohusu utoaji.

‘Kumtolea Mungu ni jambo muhimu katika maisha ya mkristo yeyote, lakini pamoja na mahubiri lingekuwa jambo la busara kwa wahubiri kutoa ushauri nasaa kwa wanowahubiria, jinsi ya kujikwamua kutoka katika hali ya umasikini uliokithiri’, alifafanua mratibu huyo wa vijana.

Aidha Bwana Bandekile alisema kutokana na ugumu wa maisha, makanisani wapo vijana wengi waliokwishapita umri wa kuoa lakini wameshindwa kufanya hivyo wahofia uwezo wao kuzihudumia familia zao vizuri, endapo wanashindwa kukidhi mahitaji yao bila familia hizo.

Ili kukabiliana na matatizo ya ajira nchini Bwana Bandekile aliwashauri vijana kuacha uvivu na badala yake wabuni miradi mbalimbali ambayo itawawezesha kujitegemea wao wenyewe na kuongeza kwamba makanisa yanaweza kuwasaidia kutokana na juhudi watakazozionyesha.

Akizungumzia swala la elimu Bwana Bandekile aliwataka vijana wanaomaliza kidato cha nne na cha sita kujiunga na masomo ya ufundi katika vyuo mbali mbali hapa nchini na kuachana na dhana potofu iliyojengeka miongoni mwao kwamba ni lazima mtu kuendelea na elimu ya juu kila unapohitimu kidato fulani.

‘Tuna matatizo ya kukariri kwamba ulimaliza kidato cha nne basi unasubiri kwenda kidato cha tano, na unapomaliza kidato cha sita unajiunga na chuo kikuu, hii ni dhana potofu na watu wengi wamepoteza muda mwingi wakisubiri nafasi katika shule na vyuo ambazo ni chache sana ikilinganishwa na idadi ya wahitimu’Alisema Bandekile.

Alitaja tatizo jingine kuwa ni vijana wengi kutokuwa wabunifu wa shughuli ambazo zinaweza kuwawezesha kujitegemea na badala ya kuwategemea wazazi wao ambao wengi wao hawana uwezo wa kuwasaidia zaidi ya kuwalisha na kuwapa mahali pa kulalala.

Mratibu huyo wa vijana alieleza kusikitishwa kwake na tabia ya vijana kuchagua kazi pia kukosa uvumilivu, uaminifu na heshima kazini mambo ambayo aliseyataja kama kikwazo kikubwa kinachowakwamisha vijana wengi kupata ajira.

Sambamba na kuwa wabunifu na waaminifu, Ndugu Bandekile aliwashauri vijana hao kuwa wavumilivu pia kutomuweka Mungu kando, ili waweze kufanikiwa katika shughuli zao na masomo yao.

Semina hiyo iliwashirikisha vijana kanisa la KKKT Usharika wa Keko na vijana wa Kanisa la Udugu wa Kikristo.

 CARITAS lapokea msaada wa baiskeli za walemavu

SHIRIKA la Misaada lililo chini ya kanisa katoliki la Caritas limepokea jumla ya Baiskeli 15(Wheel Chairs) kutoka Nchini Marekani kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye tatizo la ulemavu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa wiki kwenye ofisi za Caritas muhudumu wa kitengo cha huduma za jamii Bibi Betty Mwaluli alisema kuwa msaada huo umetoka kwa familia moja inayojulikana kama Janet and Jim Wenninger inayoishi nchini marekani .

Bibi Mwaluli alisema kuwa familia hiyo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye matatizo ya ulemavu zikiwemo nguo na magongo ya kutembelea.

Aidha Bibi Mwalula alifafanua kuwa baiskeli hizo ni kwa ajili ya watu walioonana na Bibi Janeth wakati alipotembelea ofisi ya Caritas mwaka juzi.

Alisema msaada huo umetolewa kufuatia ahadi ya Bi Janet aliyoitoa baada ya kupokea ombi kutoka kwa watu wenye ulemavu.

Wakati huo huo Bibi Mwaluli amewaomba watu wenye mapenzi mema kuonyesha moyo wa kutoa walichonacho kwenye kitengo cha huduma za jamii kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye matatizo mbalimbali .

 Takataka hazijazolewa Sokoni Tandika tangu mwaka juzi

WAFANYABIASHARA wa soko la Tandika Wilayani Temeke wameilalamikia Tume ya Jiji kwa kushindwa kuzoa taka kwenye eneo la soko hilo.

Habari kutoka ndani ya soko hilo zinasema kuwa ni kipindi cha miaka miwili sasa tangu Tume ya Jiji ifike sokoni hapo na kuzoa taka.

Kiongozi lilipotembelea eneo hilo lilishuhudia maji machafu pamoja na takataka nyingine zikiwa zimekundikana kwenye eneo la soko hilo na sehemu iliyoathirika zaidi ni ile ya kuuzia bidhaa za matunda ya jumla.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Katibu soko hilo Bw.Kazi Ngogota alidhibitisha kuwepo kwa hali hiyo ambapo alisema wameishapeleka taarifa Tume ya Jiji lakini hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyokwisha chukuliwa.

Bw.Kazi alisema kuwa mbali na uchafu kulundikana sokoni hapo,soko hilo pia linakabiliwa na tatizo la choo ambapo alisema choo kilichopo hadi hivi sasa hakitumiki kutokana na kujaa na kuongeza kwamba Tume imetoa ahadi ya kukarabati choo hicho.

Tatizo lingine linalo likabili soko hilo ni ukosefu wa umeme na maji tataizo linaloelezewa kuwa sugu na hakuna hatua iliyokwisha chukuliwa.

Hata hivyo Mwandishi wa habari hizi alipokwenda kuonana na uongozi wa Tume ya Jiji kuhusiana na suala hilo Afisa mmoja wa ngazi ya juu ambaye ahakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa hali hiyo ya uchafu inayakabili masoko mengi na kinachochangia hali hiyo wafanyabiashara wenyewe kukataa kulipa ushuru mpya wa shilingi 300 kwa siku.

 TAMWA kujadili sheria za habari

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinatarajia kuandaa kongamano la kujadili mapendekezo na kurekebisha sheria zinazokandamiza uhuru wa habari.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi , Mkurugenzi wa TAMWA, Bi. Leila Sheikh alisema kuwa kongamano hilo litavihusisha vyama mbalimbali nchini ambavyo vitarekebisha sheria hizo zinazokandamiza uhuru wa habari.

Alivitaja vyama hivyo kuwa TGNP, TAWLA, TASWA, AJM, MISA-TAN, JET, BJA, TAJA, TANAP, TAMWA , na vilabu vya waandishi wa habari mikoani.

Kongamano hilo linakuja baada ya uzinduzi wa wiki ya Uhuru wa vyombo vya Habari ulioanza hivi karibuni katika ukumbi wa British Council na kutarajiwa kumalizika Mei 3 mwaka huu katika ukumbi wa Simba grill- Kilimanjaro hoteli kuanzia saa 8: 00 mchana.

Bi. Leila alisema katika kongamano hilo kutakuwepo na ukusanyaji wa maoni kutoka kwa waandishi kuhusu sheria zote zinazohusu habari kutoka mikoa yote.

Aidha alisema kuwa maoni hayo yataandaliwa na kuwekwa kwenye usimamizi mzima wa uchambuzi wa sheria hizo zinazokandamiza uhuru wa mwandishi, uhuru wa mchapishaji na uhuru wa msomaji, ambapo baada ya kufanya hivyo mapendekezo hayo yatapelekwa kwa Waziri Mkuu.

Pia kongamano hilo litaomba serikali kuanzisha shahada ya mafunzo ya uandishi wa habari katika Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam ili kuweza kuinua fani ya uandishi iliyo bora zaidi.

Alisema kuwa waandishi wa habari wanatakiwa kujua sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ili kuacha tabia ya kuandika habari zisizo za ukweli jambo ambalo limekuwa kero kwa jamii.

Waandishi pia walitakiwa kujua na kujadili sheria ya Uandishi , kwani ilidaiwa kuwa ni silaha yao katika kuandika habari na sio vingine.

Hata hivyo alisema kuwa waandishi wa habari walio wengi hawana vitendea kazi , hivyo aliwaomba wamiliki wa magazeti na televisheni kuboresha vitendea kazi wa waandishi wao.

Bi. Leila alipoulizwa tarehe ya kongamano hilo alisema kuwa ni mapema sana kutaja tarehe hiyo lakini wanatarajia kufanya kongamano kwa wiki tatu zijazo.