Waislamu 'wateka kanisa la Mtikila

lWawatimua walinzi na kuweka ulinzi wao

KUNDI la Waislamu wenye msimamo mkali hivi karibuni lilivamia na kuteka jengo ambalo Mchungaji Christopher Mtikila na kanisa lake la Full Salvation walikuwa wakijihifadhi kwa ibada baada ya kutimuliwa kutoka katika majengo ya Shule ya Uhuru, Ilala jijini ambako walikuwa wakisalia kila jumapili kwa miaka kadhaa.

Kundi hilo ambalo kwa mujibu wa Mchungaji Mtikila ambaye pia ni mwanasiasa mwenye msimamo mkali lilifika katika nyumba hiyo namba 58 iliyoko Karikakoo katika Mtaa wa Somali likiwa na mapanga na kuwatimua walinzi waliokuwepo na kisha kuweka ulinzi wao ambao unadumu hata leo.

Gazeti hili lilipofika katika nyumba hiyo mwishoni mwa wiki wakati tukielekea mitamboni lilikuta jengo hilo likiwa limefungwa lakini kukiwa na bango lililobandikwa lenye maneno ya kumtaka Mchungaji Mtikila akae chonjo na walichokiita mali za Wakf za Waislamu.

Mwandishi wa habari hizi alipokwenda kuona hali halisi ilivyo kwenye eneo la nyumba hiyo pamoja na kupata maelezo zaidi kutoka kwa wahusika, alikuta nyumba hiyo ambayo kwa mbele kuna vijana wanaouza vyakula mbalimbali,ikiwa imefungwa na kwenye ukutwa kulibandikwa tangazo lenye kichwa cha habari ‘Mtikila kaa chini’ lililosomeka kama ifuatavyo;

Nyumba ya Wakf ya Mtaa wa Somali ni ya waislamu yoyote atakayejitokeza kuwasaidia Daniel Zakaria na Pius Kipengele kupora nyumba hiyo ajue anatangaza vita na Waisalamu.

Waislamu hawana vita na Wakristo ,tafadhali Mchungaji Mtikila acha kuwasaidiana na wezi ,Mtikila wewe ni mchungaji acha kushirikiana na wezi.

Pia tunaviomba vyombo vya dola na hasa polisi viache kuwalinda Daniel na Pius,visimamie haki .Waislamu ni raia wa nchi nchi hii wanastaili haki maka raia wengine,tunawaomba viongozi wa nchi wamlike wale wote wanaotaka kuvuruga amani na utulivu wa nchi hii.

Waislamu ni watu wa amani ,lakini hawatakubali kuona wanazalilishwa katika nchi yao, wananyang’anywa mali zao tena za Wakf.Mtikila shughulika na mkutano wa katiba ya nchi siyo kuanza kuwa pamoja na matapeli kama kina Daniel.

Waislamu Mtambani DSM.

Kutokana na kanisa la Full Salvation kukosa kanisa la kuabudia,wafuasi wa dini hiyo akiwemo Mchungaji Mtikila walimshauri Bw. Pius Kipengele awape nyumba hiyo ambayo inadaiwa aliinunua kutoka kwa Bw. Daniel Zakaria ambaye ni mrithi wa nyumba hiyo iliyoirithi kutoka kwa mlezi wake aliyekuwa Muislamu ambaye hivi sasa amefariki ili waitumie kama kanisa ambapo ombi hilo lilikubaliwa kwa masharti maalum.

Akiyafafanua masharti hayo,Kiongozi wa Full Salvation,Mchungaji Christopher Mtikila alisema kuwa Bw.Pius alilitaka kanisa hilo litoe kiasi cha sh.600,000 kwa ajili ya ukarabati wa nyumba hiyo ambapo walifikia muafaka kwamba baada ya ukarabati wa nyumba hiyo yenye vyumba sita,chumba cha kuabudia kingetumika bure na vyumba viwili vingetumika kama ofisi kwa kodi ya Sh.50,000 kwa mwezi kila chumba. Vyumba vingine vitatu ilikubaliwa vibaki kwa mwenyewe. Imefahamika kuwa kanisa la Full Salvation lililipa Sh. 600,000 kwa ajili ukarabati wa jengo hilo lakini wakati ukarabati ukiwa njiani Waislamu hao wenye itikadi kali walivamia na kusababisha kila kitu kisimame.

Mchungaji Mtikila aliripoti tukio hilo katika kitu cha polisi cha Msimbazi ambapo watuhumiwa kadhaa walikamatwa lakini wakaachiwa baadaye, jambo ambalo limemfanya Mtikila awashutumu polisi akidai wanafuga majambazi waliojipachika blanketi la Uislamu na hivyo kutishia kuwashitaki wakuu wa polisi endapo hawatachukua hatua haraka.

Mchungaji Mtikila aliongeza kuwa baada ya mlinzi na mfanyakazi wa Bw.Kipengele kufukuzwa,kundi hilo ambalo inadaiwa kuwa lilifanya uvunjaji wa nyumba na kuiba baadhi ya vitu vya Bw.Pius,lilipiga kambi kwenye nyumba hiyo na kuongeza kuwa hadi hivi sasa linaendelea kuweka makazi kwenye eneo hilo.

Hata hivyo Mchungaji Mtikila amemwandikia barua Mkuu wa Jeshi la polisi nchini,Bw.Omary Mahita kumtaarifu hali halisi ilivyo ambapo alidai kuwa Polisi wa Makao makuu wanawakumbatia Waislamu hao aliowaita majambazi.

Sehemu ya barua hiyo ambayo Kiongozi ina inasomeka nakala yake,inasomeka kuwa ‘ndugu Inspector General,tunafanyiwa haya na maafisa wako wanaofahamu fika kwamba dini si kinga mbele ya sheria na siyo "balack Cheque" ya mtu yeyote kutendea wengine udhalimu wa ina yoyte ile,husasan katika jamii yenye kuongozwa kisheria katika misingi ya haki za kibinadamu’.

Nakala za barua hiyo zimesambazwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai,Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste, Jumuia ya Kikristo Tanzania,Baraza la Maaskofu Katoliki ,Waziri wa Sheria na Katiba na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya kulinda mali za Waislamu Sheikh Yahya Hussein alipoulizwa undani wa mgogoro huo alisema haitambui nyumba hiyo inayogombewa kati ya Waislamu na Kanisa la Mtikila.

 

Jihadhari na mikutano ya kilokole - Askofu aonya

lAtaka wapate kibali kabla ya kuhudhuria

Na Modest Msangi, Moshi

ASKOFU wa kanisa katoliki jimbo la Moshi Mhashamu Amedeus Msarikie ambaye pia ni Mwenyekiti wa Idara ya Kichungaji katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC) ameandika barua na kuwaonya waumini wa jimbo la Moshi kutohudhuria mikutano ya kidini ya hadhara ikiwemo ya walokole bila mawasiliano na viongozi wao kwani baadhi ya wahubiri hupotosha maandiko. Mtindo wa kuendesha mikutano ya hadhara ya kidini kwa jina la "mikutano ya injili" umeshamiri siku hizi kama njia rahisi ya kila dhehebu jipya linaloanzishwa kujipatia waumini.

Askofu Msarikie pia amewataka Wakatoliki wa jimbo lake wanaosali au kukesha usiku katika jumuia ndogondogo kuanzia saa 1.00 usiku waache mara moja.

Aliongeza kusema kuwa waumini wanaotaka kufanya hivyo wawashirikishe viongozi wa kanisa kwanza ili wapate ruhusa.

Hayo yamo katika barua ambayo aliagiza isomwe katika parokia zote za jimbo Katoliki la Moshi Jumapili ya pili ya Kwaresima.

Katika barua hiyo, alionya jumuiya ambazo zinaalika wahubiri au watu ambao wanakuja katika vikundi vya namna hiyo kuwa kuanzia sasa ni marufuku.

Aliongeza kusema kuwa kikundi kinachotaka kufanya hivyo basi kiwasiliane na ofisi ya Askofu kushauriana naye kabla ya kufanya hivyo.

Alisisitza kuwa waumini wanapaswa kujiepusha na mageuzi ambayo yataleta fujo katika kanisa aliyosema yanaenezwa na baadhi ya wahubiri wa madhehebu mbali mbali.

"Msiende katika mikutano ya aina hiyo," ilisisitiza barua hiyo.

Aidha Askofu Msarikie pia aliwaonya wasichana wanaochora mikono yao kwa rangi mfano wa moyo uliochomwa na mkuki na kupaka rangi midomoni mwao waache tabia hiyo.

Alisema hali hiyo ni ya uchafu na akawaagiza Mapadre wawanyime Ekaristi Takatifu kwa kuwa ni wachafu.

 

Serikali yatakiwa ichuje zaidi ajira za polisi

Na Neema Dawson

SERIKALI imeshauriwa kuweka utaratibu mpya wa kupata taarifa za wanaoomba kazi ya upolisi kutoka kwa wenyeviti wa serikali za mitaa na mashuleni walikosomea ili kupunguza uwezekano wa Jeshi la Polisi kuajiri wahalifu ambao badala ya kuzuia uhalifu wanauboresha.

Katika kuchangia moja ya mada iliyokuwa inahusu Jeshi la Polisi kuimarisha usalama mijini,Bw, Martini Barua ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa kutoka Kata ya Keko alisema kuwa kutochunguzwa vya kutosha kwa vijana wanaoajiriwa na jeshi la polisi kumesababisha wahalifu wengi kujichomeka katika kazi hiyo nyeti na kutumia madaraka yao vibaya au kinyume na matarajio.

Alitoa mfano kwamba wakati Serikali ikisisitiza wananchi wawe na ushirikiano na polisi ili kupunguza wimbi la uhalifu, kumekuwa na matatizo ambayo yanajitokeza mara kwa mara ya baadhi ya mapolisi wanapopelekewa taarifa vituoni juu ya matukio mbalimbali ya uhalifu na majina ya wahalifu kutoa siri kwa ndugu au kwa wahalifu hao wenyewe na kuwaeleza majina ya waliotoa ripoti vituoni, hali ambayo inahatarisha usalama wa raia wema na kuwafanya waogope.

Bw. Martin aligusia suala la ajira za mapolisi na kusema kuwa zina upungufu mkubwa kwani utaratibu unaotumika kuajiri mapolisi hao haufai kwani baadhi ya wahalifu hutumia vyeti ambavyo si vyao ili mradi tu wameona matangazo magazetini ambayo yanawataka wawe na vyeti vinavyoonyesha kuwa wamemaliza kidato cha nne au cha sita bila kujali sifa zao. Hivyo aliliomba jeshi hilo kuwa endapo watafanya ajira hapo baadaye wawahusishe Wenyeviti wa serikali za mitaa pamoja na walimu wakuu wa shule mbalimbali walikosomea waombaji ili kuhakikisha vyeti vyao ni sahihi kutoka katika shule walizosoma na kwenye mitaa yao wanafahamika kwa tabia na sifa nzuri.

‘’Unadhani kijana ambaye alikuwa anakaa kijiweni na vijana wenzake halafu akafanikiwa kupata cheti cha kununua kwa mtu aliyefaulu vizuri na hatimaye kuwa polisi wa kituo fulani anaweza kwenda kuwakamata wahalifu akipelekewa taarifa na akawa anafahamu kuwa wahalifu hao ni kati ya makundi ya vijana ambao hapo awali walikuwa wanashinda wote vijiweni?" alihoji.

Pia Bw. Barua aligusia suala la mapolisi kuishi uraiani kuwa ni sababu mojawapo ya kuongezeka kwa uhalifu kwani unaweza kukuta majambazi sugu ni watoto wa mwenye nyumba wa askari polisi au wamiliki wa nyumba hizo ambazo wanaishi mapolisi. Alisema katika hali hiyo itakuwa vigumu kwa mapolisi hao kuwakamata kwa kuhofia kufukuzwa na wenye nyumba.

Kamishna msaidizi wa Jeshi la polisi ACP Kosseyi alisema Jeshi la Polisi linaoendelea na mpango wa kuhakikisha polisi wanaoishi uraiani wanarudi makambini na wengi wao wameishafanya hivyo ila jitihada za kuwatafutia nyumba waliosalia zinaendelea.

Kosseyi alishukuru kwa mchango unaohusiana na ajira za polisi na aliwataka wakuu wa upelelezi na wakuu wa vituo ambao walihudhuria warsha hiyo kuhakikisha kuwa wanapambana na mapolisi ambao wanatoa siri za waharifu na kusema kuwa polisi yeyote atakayefahamika amehusika na kuvujisha taarifa za wahalifu atachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.

Pamoja na kukiri kuwepo kwa udhaifu kwa baadhi ya watendaji katika Jeshi la Polisi ACP Kosseyi aliwataka wananchi watoe ushirikiano wao ili kuwafichua askari wanaokiuka miiko yao ya kazi ili wachukuliwe hatua.

 

Ujenzi wa uzio shule ya Kurasini kugharimu milioni 60

Na Mwandishi Wetu

UKOSEFU wa uzio katika shule ya Msingi Kurasini iliyopo Wilayani Temeke unazorotesha kwa kiasi kikubwa kushuka kwa elimu shuleni hapo kwani kumekuwepo na vibaka ambao hupitapita shuleni hapo, hali ambayo inawafanya wanafunzi kutokuwa wasikivu wawapo darasani.

<GFIRST 11.35>Hayo yamesemwa na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bw, Madoshi Manoni alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake.

Mapema mwaka jana Waziri Mkuu Fredrick Sumaye alitoa maagizo kuwa walimu wa shule zote za msingi nchini wanatakiwa wahakikishe kuwa shule zao zina madawati ya kutosha na zijengewe uzio.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bw. Madoshi Manoni alisema kuwa tayari shule yake imetekeleza kwa sehemu agizo kwani shule yake ina jumla ya madawadi 1028 na ina idadi ya vyumba vipatavyo thelathini na tano vya madarasa na wanafunzi wanaosoma shuleni hapo hakuna anayekaa chini hata mmoja. Hata hivyo alisema anatakiwa kuongezea madawati ili yafike 1300 na kuwepo na mengine ya ziada.

"Ukosefu wa uzio katika shule hii ni tatizo kubwa sana ukizingatia shule hii ina wanafunzi wengi sana hivyo kutokuwa na uzio kunawafanya wanafunzi kuzungukazunguka nje hovyo na wakati masomo yakiwa yanaendelea baadhi yao huchungulia nje na kuangalia watu mbalimbali wanaopita, hali ambayo inawafanya watoto kutokuwa wasikivu, hivyo ninafanya jitihada kuweza kukamilisha ujenzi wa uzio shuleni hapo’’alisema Mwalimu Mkuu wa shule hiyo.

Aliendelea kuelezea kuwa hadi hivi sasa wameshapata mfadhili (hakupenda kumtaja jina lake) ambaye amejitolea kuijengea shule hiyo uzio na ameshafika hadi hapo shuleni na kuweka mipaka kuzunguka shule hiyo pamoja na kuchora ramani halisi ya uzio huo na makadirio yaliyofanywa yameonyesha kuwa ujenzi wa uzio huo utagharimu kiasi cha Sh. milioni 60.

Mwalimu Mkuu huyo alieleza tatizo jingine kuwa ni ukosefu wa nyumba za walimu kwani pamoja na kwamba shule ina majengo mawili hayawezi kukidhi haja ya walimu wapatao 99 ambao wa shule hiyo ambao wengi wao wanaishi mbali na shule.

 

Tume ya Jiji yaandaa mpango kuzuia uhalifu

Na Mwandishi Wetu

TUME ya jiji la Dar es Saalam kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la makazi (Habitat) la Nairobi, kupitia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Dar es Salaam imeandaa mpango wa kuendeleza, kuimarisha juhudi za kupunguza uhalifu kwa lengo la kuboresha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira.

Mpango huo utawashirikisha wakazi wa jiji pamoja na taasisi nyingine husika kumi na tatu za kitaifa na kimataifa kwa mujibu wa Bi. Anna Mtani ambaye ni Mratibu wa mpango huo.

Hayo yalielezwa katika Warsha juu ya uhamasishaji wa usalama mijini iliyofanyikia katika ukumbi wa Chuo cha Biashara Temeke.

Bi. Mtani alieleza kuwa moja ya sababu za kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu ni ukosefu wa ajira na hali duni ya maisha inayowakabili vijana wengi hasa waishio mijini hivyo moja ya mipango ambayo Tume ya Jiji imeiandaa ni pamoja na kuanzisha miradi ya ulinzi na mingine yenye lengo la kupunguza uhalifu na kufufua juhudi za ulinzi wa jadi yaani Sungusungu.

Pia alisema kuwa sababu zilizopelekea kuanzishwa mpango huo ni kuongezeka siku hadi siku matukio ya uhalifu yanayoripotiwa katika vyombo vya habari na mengi ambayo hayaripotiwi hata katika vituo vya polisi.

Kwa mujibu wa Bi. Mtani tathimini ya utafiti uliofanywa inaonyesha kuwa uhalifu uliokithiri na kuleta hofu kwa wakazi wa jiji ni pamoja na unyang’anyi na uporaji wa kutumia silaha ambao mara nyingine unasababisha vifo na ulemavu kwa wananchi.

Alisema makatibu kata na wenyeviti wa serikali za mitaa ndio wanaotegemewa sana kufanikisha mpango huo wa uimarishaji wa usalama mijini.

Mratibu wa mpango huo pia alisema kuwa uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa sababu ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa uhalifu mijini ni sababu za kiuchumi, kwani umaskini ambao unachangiwa na mfumo mbaya wa mgawanyo na matumizi ya rasilimali na huduma muhimu za jamii.

Sababu nyingine alizitaja kuwa mishahara isiyokidhi mahitaji muhimu ya watu,vipato vya chini, mfumuko wa bei, elimu duni na isiyo na ajira, makazi duni na ukosefu wa malezi bora.