Maaskofu wazungumzia kushindwa kwa wapinzani

lWasema CCM inahitaji kuchangamshwa

Na Neville Meena

MAASKOFU na viongozi wa dini nchini wamesema kuwa japo wao si wapinzani wa chama tawala-CCM, lakini si jambo la kufurahisha kuona chama hicho kinabeba ushindi katika kila uchaguzi unaofanyika nchini.

Wakizungumza na KIONGOZI kwa nyakati tofauti, Askofu mstaafu wa KKKT-Dayosisi ya Mashariki na Pwani Elinaza Sendoro, Askofu Basil Sambano wa Kanisa la Kianglikana-Dayosisi ya Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Padri Pius Rutechura wamesema, chama tawala chochote kiwe CCM au kingine kinastahili kupata upinzani wenye nguvu ili kukichangamsha na kukifanya kiwajibike.

Kwa upande wake Askofu mstaafu Sendoro, alisema vurugu ndani ya chama cha NCCR-Mageuzi zilizopelekea aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Augustine Mrema kuhamia TLP, kwa kiasi kikubwa zimedhoofisha nguvu katika kambi ya upinzani hapa nchini hivyo kuwapa CCM ushindi katika chaguzi ndogo za majimbo ya Temeke na Ubungo hivi karibuni.

Alisema inasikitisha kuona vyama vya upinzani vinabakia kuwa wasindikizaji karibu katika kila uchaguzi mdogo unaofanyika na kuongeza kwamba hilo linatokana na vyama hivyo kutokuwa na mbinu za kuwashawishi wananchi ambao wengi wanahitaji maendeleo na huduma muhimu.

"Siyo vibaya Chama Cha Mapinduzi kupata ushindi, ila ikumbukwe kuwa dhumuni la kuanzisha vyama vingi vya siasa ni kutoa changamoto na upinzani wa dhati kwa chama tawala na serikali yake ili waweze kufanya vizuri katika kuwahudumia wananchi", alisema Sendoro ambaye aliwahi kujaribu kusuluhisha mgogoro ndani ya chama cha NCCR-Mageuzi bila mafanikio.

Alisema kwamba hata kama chama chochote cha upinzani kingefanikiwa kutwaa dola asingependelea kuwepo udhaifu katika kambi ya upinzani , hivyo hata CCM inahitaji kupata upinzani wenye nguvu ili kiweze kutekeleza sera zake kwa manufaa ya umma wa Watanzania.

Hata hivyo Askofu Sendoro alisema kwamba wapinzani bado wanyo nafasi nzuri ya kujirekebisha ili waweze kupata mafanikio katika uchaguzi mkuu ujao.

Naye Askofu Basil Sambano wa Kanisa la Kianglikana-Dayosisi ya Dar es Salaam amesema, Chama cha Mapinduzi kwa Watanzania walio wengi ni kama baba aliyezoeleka wakati vyama vya upinzani ni kama baba wa kambo na kwamba hiyo ndiyo sababu kubwa iliyopelekea chama tawala kupata ushindi katika majimbo ya Temeke na Ubungo.

"Vyama vingi vya upinzani havina sura inayoeleweka kwa Watanzania hivyo watu wengi hawaoni umuhimu wa vyama hivyo, ikizingatiwa kuwa mfumo huu bado ni mpya katika jamii yetu na bado haujazoeleka", alisema Askofu Sambano na kuongeza kwamba hicho ni kichocheo kikubwa kilichowafanya watu wengi kuelekeza kura zao kwa chama tawala.

Aidha Askofu huyo alisema kwamba watu wengi wamepoteza imani kwa vyama vya siasa vya upinzani kutokana na migogoroya muda mrefu ndani ya vyama hivyo na kwamba vinahitaji kujijenga upya ili viweze kurudisha imani hiyo.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Pius Rutechura, alisema CCM kimetumia udhaifu na mgawanyiko uliomo ndani ya vyama vya upinzani kujipatia ushindi katika uchaguzi mdogo.

Alisema siku za hivi karibuni vyama hivyo vimekuwa vikitumika kama miradi ya kuwanufaisha watu binafsi hivyo kuzua migogoro ambayo imevifanya vyama hivyo kukosa mtazamo ulio wazi na unaoeleweka kwa wananchi.

"Kama vyama hivi vinahitaji kujenga upinzani wa kweli vinahitaji kujisafisha na kijijenga upya. Hata hivyo muda uliobaki kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani ni mdogo sana kwa vyama hivyo kurudisha imani kwa wananchi, vinginevyo serikali iliyoko madarkani ifanye makosa ambayo yatapelekea wananchi kutoichagua mwakani", alisema Naibu Katibu Mkuu huyo. Katika uchaguzi mdogo wa wabunge uliofanyika wiki iliyopita wagombea wa CCM Bwana Venance Ngula (Ubungo) na Bwana John Kibasso (Temeke) walichaguliwa kuwa wabunge baada ya kuwashinda wagombea wa vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF, TLP, CHADEMA na TPP.

Ajitokeza kuchukua mwanae aliyetelekezwa

Asema mkewe ameolewa na mwanaume mwingine

Na Peter Dominic

Baba wa Mtoto Mariam Gudluck (2) Amejitokeza kumchukua mwanae baada ya kutelekezwa katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Msimbazi Center, jijini hivi karibuni na kuelezea sababu zilizomfanya mwanae kutelekezwa.

Mlezi wa kituo hicho Bi. Lucresia Seria ambaye aliongea kwa niaba ya msemaji wa kituo hicho Sr. Maria Cyrilla, ameliambia gazeti hili wiki hii kuwa mapema mwezi wa sita mwishoni baba wa mtoto huyo aliyemtaja kwa jina la Gudluck alifika katika kituo hicho akiwa katika harakati za kumtafuta mwanae Mariam.

Mlezi huyo amesema Bw. Goodluck alikabidhiwa mtoto huyo baada ya kujieleza kwa kina na kuhadithia kisa cha mkewe kumbwaga mtoto katika kituo hicho cha Msimbazi na kukimbia.Habari juu ya kutelekezwa kwa mtoto huyo ziliandikwa na gazeti hili Juni, mwaka huu zikionyesha picha ya mtoto aliyetelekezwa.

Kwa mujibu wa habari hizo mtoto huyo aliwekwa katika mlango nje ya kituo hicho na baada ya mtu aliyemleta kubonyeza kengele alitokomea na kuwafanya walezi walipofungua kumkuta mtoto huyo akiwa peke yake pamoja na kikaratasi kinachoeleza kuwa mzazi wake ameshindwa kumlea.

Baba huyo aliyatajwa kwa jina la Godluck alisema kuwa alianza kuwa na uhusianao wa kimapenzi na mama wa mwanae Mariam (jina tunalihifadhi)na hatimaye kufanikiwa kupata watoto wawili wa mwisho akiwa na Mariam.

Alisema wazazi wa msichana huyo walimtaka Godluck afunge ndoa na mtoto wao lakini yeye hakuwa tayari kwa vile yeye ni Mkristo na mama Mariam ni Mwislamu.

Hivyo aliomba ndoa yaoa ifungwe bomani, jambo ambalo halikukubaliwa na wazazi wa msichana.

Baada ya tofauti hizo kujitokeza, baba huyo aliomba wagawane watoto ambapo Mariam alibaki kwa mama yake kwa makubalino ya kumpatia matumizi kila itakapohitajika jambo ambalo lilileta muafaka kwa pande zote mbili. Kwa mujibu wa Bw. Godluck mpenzi wake huyo alimpata bwana mwingine na kuolewa.eneo la Manzese, akiwa na mtoto wake Mariam wakati huo yeye akiishi maeneo ya Temeke jijini na mzazi mwenzake huyo alikuwa akifika kwake mara kwa mara kuchukua matumizi ya mtoto.

"Huenda mume mwanzangu ndiye aliyemshawishi mzazi mwenzangu ili wamtelekeze mtoto wangu" alikaririwa akisema.

"Mimi nilikuwa safarini kutokana shughuli zangu za kibiashara na niliporudi nilipewa barua na wapangaji wenzangu, nilipofungua na kusoma ndipo nilipopambana na ujumbe ukielezea kuwa "mtoto wako utamkuta Msimbazi".

Kuhusishwa kwa mume mwenza katika tukio la kumtelekeza mtoto huyo kunatokana na maelezo ya mlinzi wa zamu ambaye alisema kuwa siku ya tukio alimuona mwanaume akiwa amembeba mtoto pamoja na mfuko wa Rambo lakini hakumfuatilia kwa vile hakumtilia mashaka hadi iliogundulika kuwa alikuwa na lengo la kumtelekeza mtoto.

Serikali inajifunza mengi kwa Kanisa-Waziri

Na Neema Dawson, Singida

WAZIRI wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu Mh. Pius Ng’wandu ameliomba Kanisa nchini hapa kuisaidia serikali ili kupambana na kuondoa tatizo sugu la umaskini linalozidi kushamiri na kuwasonga Watanzania wengi.

Akitoa salamu za serikali kwa niaba ya Rais Benjamin Mkapa katika sherehe za kumuweka wakfu na kumsimika Askofu Mteule wa Jimbo Katoliki la Singida Mhashamu Desderius Rwoma zilizofanyika katika Kanisa Kuu la Jimbo hilo mjini hapa, Mh.Ng’wandu alisema kwa muda mrefu sasa serikali imekuwa ikijitahidi kuondoa tatizo la umaskini kwa Watanzania lakini bado hadi sasa juhudi hizo kwa kiwango kikubwa hazijafanikiwa.

Alisema Kanisa halina budi kuisaidia serikali kuihamasisha jamii ili kwa kushirikiana nayo jamii hiyo iweze, kujitegemea na kuondokana na umaskini kwa kutumia juhudi, maarifa na raslimali walizo nazo na akaonesha kushangazwa kwake kwamba ni vipi Kanisa linafanikiwa katika mipango yake lakini serikali inashindwa.

" Kama Kanisa linaweza kupanga kufanya mambo na mipango yake ikaenda vizuri, iweje serikali inashindwa?"alihoji kwa mshangao na kusisitiza kuwa upo umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na kubadilishana mbinu zinazotumika kujiletea maendeleo miongoni mwa serikali na Kanisa.

Waziri alisema katika kipindi hiki cha kuingia karne ya 21 ya sayansi na teknolojia, serikali na Kanisa hazina budi kuimarisha mahusiano na umoja miongoni mwao na akasisitiza kuwa misaada inayotolewa na mataifa wafadhili haina budi kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Alionya kuwa endapo misaada haitatumika kwa malengo na badala yake kuishia katika matumizi ya kibinafsi, ipo hatari ya kuendelea na hali ya kuzidi kuzama katika umaskini zaidi..

‘’Hakuna binadamu anayeweza kutembea mwili ukiwa peke yake na roho peke yake hivyo lazima viwe pamoja hivyo kila mtu anaishi kwa kumtegemea na kumtumikia Mungu katika maisha yake hivyo kiongozi yoyote yule habagui wala haitengi jamii. hakuna haja ya serikali kutoshirikiana na kanisa ‘’

Waziri Ng’wandu alilishukuru Kanisa kwani limekuwa likisaidia kutatua matatizo mbalimbali yanayolikumba taifa ikiwa ni pamoja na kutoa misaada mbalimbali yakiwemo malezi bora kwa jamii na akasema viongozi wa madhehebu ya dini ni wa jamii nzima hivyo malezi yao yanahitajika kwa manufaa ya Watanzania wazingatie maadili na kutumia maarifa na ujuzi walionao kujiendeshea maisha yao. Alifafanua kwa kusema kuwa serikali imekuwa ikijitahidi kuondoa tatizo la umaskini bila kuwa na mafanikio ya haraka hivyo katika sherehe hizo amejifunza na kupata mawazo mazuri kutoka kwa Askofu Mstaafu wa Jimbo la Singida Mhashamu Benard Mabula aliyeeleza kuwa alipochaguliwa March 25, 1972 na kusimikwa Julai 9, 1972 na kuliongoza jimbo hilo kwa miaka 27 jimbo hilo halikuwa na pesa wala nyumba ya kuishi askofu hali iliyomfanya kuigeuza ofisi iliyokuwepo kuwa nyumba yake hadi anakabidhiwa Jimbo likiwa katika hali nzuri.

Mh.Ng’wandu aliusifu ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali na madhehebu ya dini Mkoani hapa na akamtaka Askofu Desderius Rwoma ambaye tangu alipoingia jimboni hapo kuuimarisha zaida ili watu wazidi kujengeka kiroho na kijamii .

‘’ Sasa nimebaini kwa kuona mifano halisi kwa kanisa kuwa inatakiwa muonekano uonekane kwa matendo na si kwa mahubiri, hivyo inapendeza hata machoni pa watu kusimulia matumizi ya misaada yenye maendeleo kwa jamii badala ya kusema maneno yasiyo na utekelezaji wala mafanikio

Sherehe hizo zilizofanyika Julai 11 mwaka huu na zilihudhuriwa na Waziri wa Maji Mh.Musa Nkangaa ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mjini pamoja na Viongozi mbalimbali wa serikali mkoani hapa. Baadhi ya viongozi wengine wa Kanisa nchini waliohudhuria sherehe hizo ni Balozi mpya wa Papa Nchini Tanzania Askofu Mkuu Luigi Pezzuto, Askofu wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Askofu wa Jimbo Kuu la Tabora Mhashamu Mario Mgulunde na maaskofu kutoka katika majimbo mbalimbali.

Ni aibu kupeleka kesi za dini mahakamani - Jaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu

JAJI Mkuu nchini Mh. Francis Nyalali, amesema ni aibu kwa madhehebu ya dini kupeleka migogoro yao mahakamani, kwani haipendezi masuala ya kiroho yakaamuliwa kwa vigezo vya kidunia ambavyo mahakama hutumia.

Jaji Mkuu amesema hata hivyo kwamba kisheria hakuna kosa kupeleka migogoro hiyo kortini japo kuna athari zake.

Ushauri huo wa Jaji Nyalali uko katika kabrasha la mada aliyoitoa hivi karibuni mjini Dodoma katika Mkutano wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).

"Zipo athari za kupelekea migogoro ya kidini Mahakamani.Katika nchi kama Tanzania, ambayo hufuata mfumo wa sheria ambao hupata uhai na miongozo yake kutoka maamuzi ya Mahakama katika kesi zilizotangulia(precedents), maamuzi ya Mahakama katika migogoro ya kidini huweza kuingilia miongozo ya dola au kidunia katika taasisi na jumuiya za kidini badala ya miongozo ya Mwenyezi Mungu," inasema aya moja ya katika mada hiyo ambayo KIONGOZI limepata nakala yake.

Alisema kwa uzoefu wake aina ya migogoro ya kidini inayopelekwa mahakamani ni ile inayohusu shughuli na uendeshaji wa taasisi au jumuiya za dini.

Katika kesi kumi na sita za madhehebu ya Kikristo na Kiislamu alizowahi kuzishughulikia, Jaji Mkuu amesema , saba zinahusika sana na uongozi, sita zinahusika sana na umilikaji wa mali, mbili zinahusika sana na utekelezaji na moja inahusika na itikadi.

Jaji Mkuu alisema wakati mwingine Mahakama imetakiwa kutoa uamuzi juu ya ajira na maslahi ya masheikh, mapadri na wachungaji au uhalali wa hatua zilizochukuliwa kudhibiti nidhamu ya wachungaji, mapadre na masheikh.

"Katika kesi za kiitikadi mahakama zimetakiwa kutoa uamuzi juu ya fujo au ghasia zinazotokana na uhasama wa kiitikadi,"amesema Jaji Nyalali.

Akielezea maoni yake juu ya chimbuko la migogoro ya dini ambayo hupelekwa mahakamani nchini, Jaji Mkuu alisema ni sababu nne. Kwanza kuibuka kwa itikadi kali ya dini; pili kubadilika kwa washika hatamu wa taasisi au jumuia za dini; tatu ni jumuia au taasisi za dini kutokuwa na katiba zinazoeleweka kwa waumini; na nne ni jumuia au taasisi hizo kutokuwa na utaratibu madhubuti unaoeleweka wa kutatua migogoro ndani ya taasisi au jumuia.

Akizungumzia sababu hizo, Mheshimiwa Jaji Mkuu amesema kuibuka kwa itikadi kali ya dini si jambo la kushangaza kwa kuwa ni sehemu ya mwamko mpya wa dini duniani na ni jambo ambalo hutokea katika vipindi mbali mbali vya historia ya ulimwengu.

"Jambo la kuzingatia, kwa maoni yangu, ni kuhakikisha kwamba mwamko huo unasisimua mioyo ya watu bila fujo au ghasia nchini,"alisema.

Jaji Mkuu akishauri juu ya nini kifanyike ili kudhibiti migogoro ya kidini alisema ni vema jumuia au taasisi za dini ziwe na katiba zinazoeleweka kwa waumini na sio kwa viongozi tu kama ilivyo kwa wengi hivi sasa.

Kadhalika alishauri viwepo vyombo teule vya kushughulikia migogoro ya kidini ndani ya jumuia au taasisi za dini na viwe na jukumu la kuchochea na kudumisha moyo wa udugu katika uwanja wa dini na mahusiano miongoni mwa dini tofauti zinazoamini Mungu mmoja.

Askofu Lebulu kuongoza ibada ya pamoja mkoani Arusha

Na Vicent Kawishe, Arusha

WAKATOLIKI katika Jimbo Kuu la Arusha na Wakristo wa madhehebu mengine jumapili hii watafanya ibada ya pamoja kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abedi katika harakati za kuhitimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu na kuukaribisha mwaka mpya ndani ya Karne ya 21.

Hayo yalielezwa hivi karibuni na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Arusha Padre Augustino Temu ambaye yuko katika maandalizi ya shughuli za misa hiyo.

Alisema ibada hiyo itaongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha Mhashamu Josaphat Lebulu na akasema siku hiyo hakutakuwa na ibada nyingine itakayofanyika katika kanisa lolote la Kikatoliki mkoani hapa.

Padre Temu alisema ibada hiyo itakuwa ya kuwaombea watu wote wa taifa hili kuiaga karne ya 20 na kuingia kwa amani katika karne ya 21, na pia ili kuwe na mafanikio zaidi katika shughuli zao zitakazoanza mwanzoni mwa mwaka ujao.

Kufuatia kuwepo kwa maandalizi ya ibada hii, viongozi wa jumuiya ndogo ndogo kwa kipindi cha zaidi ya juma zima sasa, walisimamisha baadhi ya shughuli mbalimbali zikiwemo za maombezi ikiwa ni pamoja na ibada za vikundi katika makanisa yote mkoani hapa ili kuungana pamoja katika kuhitimisha ibada hii ya pekee baada ya miaka 10 iliyopita.

Aidha, imefahamika kuwa watu wengine watakaoshiriki ibada hiyo itakayoanza saa nne asubuhi ni pamoja na mapadre wote toka makanisa ya Kikatoliki mkoani hapa pamoja na vikundi vya kwaya toka makanisa mbalimbali .

Padre Temu amewaalika waamini wa madhehebu mengine ya Kikristo mkoani hapa kushiriki katika kukamilisha maombezi hayo yenye lengo la kuimarisha amani na uhakika kwa maisha bora ya kumtegemea Mungu.

Tanzania kunufaika kwa kilimo cha michikichi

Na Mwandishi Wetu

TANZANIA inatarajia kuingiza shilingi Billion 10.8 kila mwaka kama ushuru kufuatia mauzo ya mafuta ya mawese kutoka katika mashamba ya michikichi yanayotarajiwa kufunguliwa katika wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani mwishoni mwaka huu.

Akizungumza na wakazi wa jiji la Dar es Salaam wapatao 700 waliojiandikisha kuchukua mashamba hayo yaliyoko eneo la Chole. Mratibu wa mradi wa chole Agro-palm Bwana Gilbert Kadanga aliema mafanikio hayo pia yatapunguza uagizaji wa mafuta ya kula kutoka mashariki ya mbali.

"Uzalishaji wa mafuta ya mawese utakaotokana na mavuno ya michikichi wilayani Kisarawe kutapunguza uagizaji wa mafuta ya kula kutoka mashariki ya mbali"Kaganda alisema.

Kwa hivi sasa kiasi kikubwa cha mafuta ya kula wanayotumia Watanzania yanaingizwa kutoka nje kwa vile kwa mafuta yanayotengenezwa hapa nchini hayatoshelezi.

Bwana Kaganda pia amesema wakazi wa jiji la Dar es salaam wapatao 1500 wamejiandikisha kuchukua mashamba hayo katika eneo linalopakana na mbuga ya hifadhi ya Selous.

Mratibu huyo amewahakikishia wakazi hao waliojiandikisha kwenda kulima michikichi wilayani Kisarawe kwamba kila mtu atapatiwa hekta 100 za eneo ambazo 80 kati ya hizo zitapandwa michikichi na zile zilizobaki zitapandwa mazao yeyote kulingana na matakwa ya mwenye eneo.

Akizungumza na wakazi hao Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Kapteni James Yamungu alisema Serikali ya wilaya imetenga jumla ya hekta 3565 ambazo watu wa Dara es salaam wametengewa.

Pia amesema Kisarawe ambayo ni moja ya wilaya maskini Tanzania itajikwamua tu kutokana na kilimo hicho cha michikichi.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umeonyesha kuwa kuna wawekezaji kutoka nje ambao watatoa pembejeo kwa hayo na baadaye kufungua viwanda vya mafuta nchini.

Kupasuka kwa mabomba kero Makuti

Na Mwandishi Wetu

WAKATI baadhi ya maeneo jijini yanakabiliwa na uhaba wa maji, hali hii ni tofauti kwa wakazi wa Magomeni Makuti ambao maji yamekuwa ni kero kufuatia kupasuka kwa mabomba ya maji yanayozunguka eneo hilo.

Hali hiyo imeshuhudiwa na Mwandishi wa habari hizi wakati alipotembelea eneo hilo hivi karibuni ambapo alishuhudia maji yakiwa yanamwagika hovyo hali inayoleta kero kwa wakazi wa eneo hilo.

Hali ni mbaya zaidi kwa wale wanaoishi karibu na daraja linalotenganisha Magomeni Makuti na Mwananyamala Bondeni ambapo mabomba yote ya maji yanayozunguka eneo hilo yamepasuka na kusababisha madimbwi yaliyojaa maji.

Mkazi wa eneo hilo Bibi Fatuma Mohamed (57) alimwambia Mwandishi wa habari hizi kuwa kupasuka kwa mabomba haya ni kwa muda mrefu ambapo alisema yana zaidi ya miezi minne na kuongeza kuwa Tume ya Jiji haijachukuwa hatua yoyote.

"Tumeisha ona ni kero kubwa maana tangu haya mabomba yapasuke ni zaidi ya miezi minne sasa na hakuna hatua iliyokwishachukuliwa na Tume ya Jiji wala DAWASA na na kila mara viongozi mbalimbali wa Jiji wamefika eneo hili na kushuhudia hali halisi ilivyo"amesema mkazi mmoja wa eneo hilo Bibi Fatuma Mohamed.

Naye Bw.Omary Muhando, alimwambia Mwandishi wa habari hizi kuwa Tume ya Jiji haina budi kuchukua hatua madhubuti haraka kukarabati mabomba hayo ambapo alisema maji yakiendelea kutoka kuna hatari ya nyumba zinazozunguka eneo hilo kubomoka kutokana na maji hayo kuwa na kasi kubwa.

Hata hivyo Afisa mmoja wa ngazi ya Juu Tume ya Jiji ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa madai kuwa siyo Msemaji wa Jiji alipohojiwa alisema kuwa tayari ofisi yake imekwishapokea malalamiko hayo na ukarabati utaanza wiki ijayo.

Baadhi ya maeneo ya jiji yanayokabiliwa na uhaba wa maji ni pamoja na Ubungo,Tabata, Mabibo na Buguruni maeneo ambayo hupata maji mara mbili kwa wiki wakati mwingine mara moja ama kutopatikana kabisa.

Kariakoo wadai hawamtambui mjumbe wa Bodi

Na Dalphina Rubyema

WAFANYABIASHARA wa Soko kuu la Kariakoo wamemtaka Waziri Mkuu Bw.Frederick Sumaye kufanya utaratibu mpya wa kubadilisha wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Masoko Kariakoo kwa kile walichokiita kuwa wao hawana wawakilishi kwenye Bodi hiyo.

Akizungumza na KIONGOZI hivi karibuni ofisini kwake,Mwenyekiti wa Kamati ya Wafanyabiashara Sokoni hapo Bw.Ally Msikamo, alisema kuwa Kamati nyingine zina wajumbe wawili wawili kwenye Bodi hiyo ila kamati yake ndiyo haina wawakilishi.

Alisema aliyeteuliwa kuwa mwakilishi wao Bw.Adamu Said siyo mfanyabiashara hivyo hatambuliki kwa wale anaowawakilisha wala hajui matatizo yao.

"Huyu Adam Said siyo mfanyabiashara. Sisi hatumtambui kabisa na hata huko kwenye vikao vya Bodi huwa hatutetei hata kidogo na badala yake huwa anatukandamiza" alisema Bw.Msikamo.

Mwenyeki aliendelea kusema kuwa Kamati yake imekuwa haina wawakilishi kwenye Bodi hiyo tangu mwaka 1995 na tatizo hilo lilikwisha fikishwa kwa Waziri Mkuu.

"Adam alitolewa mwaka 1995 kuwa Mwakilishi wetu sisi tukapinga uteuzi huo na hivyo tukamwandikia barua Waziri Mkuu ya kumpa taarifa hiyo lakini cha kushangaza ni kwamba huyo huyo Adamu Said ameteuliwa tena kuwa Mwakilishi wetu ,hii inaonyesha kwamba huko ofisini kwa Waziri Mkuu kuna mtu anamlinda"alisema Bw.Msikamo.

Alisema waliyomwandikia Waziri Mkuu barua yenye Kunbukumbu Na.

K/WB/SK/106/96 ambayo ilipata jibu lililosema kuwa suala la kuwakilishwa kwenye Bodi ni suala la kisheria ambapo itabidi sheria iliyoanzisha na shirika kuangaliwa kama inaruhusu wajumbe wa Bodi kuteuliwa na Wafanyabiashara..

Jibu hili limo ndani ya barua waliyoandikiwa wafanyabiashara hao ambayo imetoka Ofisi ya Waziri Mkuu ya Novemba 26 mwaka 1996 yenye Kumbukumbu Na. PC/1/C /150/18/45/1996 na imesainiwa na Katibu wa Waziri Mkuu Bw.E.A Pallangyo.

Ujenzi wa Hekalu la Bikira Maria kugharimu Milion 7 Dar

Na Josephs Sabinus

Ujenzi wa "Kihekalu"cha Bikira Maria unaotarajiwa kukamilika mwanzoni mwa Agosti mwaka huu, katika Kanisa Kuu la Parokia ya Msimbazi katika Jimbo Kuu la Dar Es Salaam, utagharimu jumla ya shilingi milioni 7; imefahamika.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake hivi karibuni, Msimamizi wa shughuli za ujenzi huo ambaye pia ni Msaidizi wa Paroko wa Parokia hiyo Padre Mansuetus Brinkhof alisema ujenzi huo ulianza mapema mwezi Juni.

Aliongeza kuwa ujenzi wa kihekalu hicho unaendelea vizuri kutokana na moyo wa waamini wa parokia hiyo wanaochangia fedha toka mifukoni mwao ili kuufanikisha.

Awali, Paroko wa Parokia hiyo Padre Sergi Tarimo aliliambia gazeti hili kuwa waamini wanaojitolea kuchangia kiasi chochote cha pesa huongezewa mara mbili na wafadhili kadhaa wa Ulaya. Hata hivyo alikataa kuwataja wafadhili hao.

"Kama mwamini akichanga sh.50,000/=, mfadhili huyo wa Ulaya anamuunga mkono kwa kumuongezea sh.100,000/= na hivyo mwamini huyo anayepewa stakabadhi anakuwa amechanga jumla ya sh.150,000/=; na kama ametoa sh. 10,000/=, mfadhili humchangia sh. 20,000/= na hivyo kuwa amechanga sh.30,000/=" alisema Padre Tarimo.

Paroko huyo alisema hadi hivi sasa jumla ya shilingi 2,260,461/= zimekwisha changwa na akaongeza kuwa ujenzi huo unaendelea vizuri.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mapadre hao wa Parokia ya Msimbazi waliupongeza ushirikiano na moyo wa upendo wa dhati uliooneshwa na waamini hao na wakawahimiza kuzidi kujitolea zaidi ili kukamilisha shughuli hiyo kwa muda uliopangwa.

Mwandishi wa habari hizi aliwashuhudia mafundi kadhaa wakiendelea na ujenzi wa kihekalu hicho kinachotarajiwa kuzinduliwa Agosti 15 mwaka huu Siku ya Bikira Maria.