NCCR-MAGEUZI BADO SI SHWARI

Wazidi kugawanyika kuhusu Bunda

lWampinga Makongoro wadai ni mgombea wa mtu binafsi

Na Mwandishi Wetu

 MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya NCCR - Mageuzi, Bw.Charles Makongoro Nyerere, anatazamiwa kuwa na wakati mgumu katika harakati zake za kuwania Ubunge wa jimbo la Bunda mkoani Mara, baada ya chama chake Makao Makuu mjini Dar es Salaam, kuamua kwa kauli moja kwamba kitakwenda kumpigia kampeni mgombea wa chama cha UDP kinachoongozwa na Mbunge wa Magu, Bw. John Cheyo "Mapesa".

Habari za uhakika zilizopatikana kutoka ndani ya chama cha NCCR-Mageuzi, zimethibitisha kuwa uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha dharura kilichofanyika ofisini kwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Bw. Augustine Lyatonga Mrema, Jumanne wiki hii.

Kwa mujibu wa habari hizo, hatua hiyo ilifuatia taarifa rasmi zilizotolewa na Bw. Mrema kwaWajumbe waliohudhuria ambapo alieleza kuwa uteuzi wa mgombea Ubunge wa chama hicho katika jimbo hilo ulivyofanyika kwa mizengwe.

Bw. Mrema ambaye alitakiwa kutoa ufafanuzi huo kutokana na taarifa mbalimbali zilizokuwa zikitolewa kupitia vyombo vya habari, alisema mgombea halali aliyestahili kukiwakilisha chama

hicho katika uchaguzi huo mdogo ni Bw. Victor Kubini ambaye alishinda kwenye kura za maoni kama inavyoelezwa kwenye Katiba ya NCCR - Mageuzi, lakini akadai kuwa zilifanyika njama za kumuengua kwenye nafasi hiyo kutokana na sababu zisizofahamika.

Baada ya Bw.Mrema kusema hayo,wajumbe wa kikao hicho walimlazimisha atoe tamko rasmi kwamba chama hicho hakina mgombea kwenye uchaguzi huo hasa kutokana na kile walichodai kuwa mgombea aliyepitishwa Bw.Makongoro Nyerere amwpitishwa na mtu binafsi,waliyemtaja kuwa ni Bw.Marando.

Kana kwamba haitoshi, Wajumbe wa kikao hicho waliazimia kuwa NCCR - Mageuzi ishiriki katika

kampeni za uchaguzi huo, lakini "impigie debe" mgombea wa UDP endapo atakuwa Bw. Kubini kwa vile alitazamiwa kujiunga na chama hicho kama hatua ya kupinga kwake kitendo alichofanyiwa na Bw. Marando kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa NCCR - Mageuzi wa mkoa wa Mara.

Katika hali hiyo, kikao hicho kilikubaliana kwa pamoja kwamba Bw. Kubini apewe baraka zote na

kisha aungwe mkono, na kwamba ufanyike utaratibu wa kupeleka wahamasishaji wa chama katika

kampeni za Bunda ambao watatumia majukwaa ya mgombeaUbunge wa UDP kwa ajili ya kumpinga

Kapteni Makongoro na mgombea wa CCM, Kanali Laban Makunenge.

Miongoni mwa Wajumbe walioshiriki katika kikao hicho ni Naibu Katibu Mwenezi wa Taifa, Bw. Thomas Ngawaiya, Mwenyekiti wa NCCR - Mageuzi wa mkoa wa Mara, Bw. Mustapha Wandwi, Katibu Mkuu wa Kitengo cha Wazee, Bw. Karawa Mushi, Katibu Mkuu wa Kitengo cha Kina Mama, Bibi Getruda Pwillah, Katibu wa NCCR - Mageuzi wa mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Octavian Matikila,

Katibu Mwenezi wa chama hicho wa mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Charles Charles pamoja na Afisa Utawala wa Makao Makuu ya chama hicho, Bw. John Komba.

Kapteni Makongoro aliondoka Dar es Salaam Jumanne wiki hii kwenda Bunda kurejesha fomu zake kwa Msimamizi wa uchaguzi huo baada ya kuwekewa saini na Mwenyekiti wa Taifa wa Kitengo cha Kina Mama, Bibi Kibibi Senyagwa bila maelekezo yoyote kutoka kwa Bw. Mrema.

 

CUF wataka neno "ujamaa" liondolewe ndani ya Katiba

Na Seraph Kuandika

 Wakati mjadala juu ya mabadiliko ya katiba ya nchi ukiendelea nchini kupitia waraka maalum wa serikali namba moja wa mwaka 1998, chama cha wananchi (CUF) ,kimesema kimegundua jambo la kuwalaghai wananchi lililoingizwa kwenye waraka huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Bunge,Baraza la Wawakilishi na Sheria wa chama hicho,Bw.Shaban Shomari Ngozi,imesema kuwa katika utafiti wao ,wamegundua kuwa serikali kwa kutaka kwake kung'ang'ania itikadi za ujamaa na kujitegemea,imeamua kuingiza neno "Ujamaa"kwenye waraka huo huku ikidai kuwa hata katiba ya India inayo neno hilo,jambo ambalo CUF inadai sio kweli.

Chama hicho kimesema katika taarifa yake hiyo kuwa dhamira ya serikali ya chama tawala cha CCM kuwapotosha wananchi imo kwenye ukurasa wa 36 na 37 wa waraka huo ambapo katika hoja yake ya 15 inayoeleza kuwepo kwa maneno "Ujamaa na kujitegemea" kwenye katiba kwa kutolea mfano kuwa neno "ujamaa" pia limo kwenye katiba ya India.

Hata hivyo chama hicho cha CUF kimesema kuwa katika utafiti wake,kimegundua kuwa katiba ya India haina neno kama hilo la "Kisocialist"(Ujamaa) bali kinachofanywa na serikali ni kutaka kuwapotosha wananchi juu ya suala zima la mabadiliko ya katiba ya nchi.

Chama hicho kimesema kuwa Bunge la India baada ya kutafakari kwa makini na kuona kuwa nchi yenye vyama vingi haiwezi kuwa na itikadi moja,iliamua kuliondoa neno hilo kwa kupitisha badiliko la Katiba Na.41 la sheria ya mwaka 1976 ambalo lilianza kutumika Januari tatu mwaka 1977.

Kutokana na hali hiyo,chama hicho kimeitaka serikali iliondoe neno hilo katika Katiba ya nchi na bila ya

kufanya hivyo,ni dhahiri kwamba serikali ya CCM haina nia ya kuleta mabadiliko ya haki na kweli ya kikatiba,hali itakayofanya asilimia kubwa ya watanzania waishio vijijini wasipate ukombozi wa kweli.

"Kufutwa kwa neno hili katika katiba kutasaidia Taifa kuondokana na ukiritimba wa kuhodhi uchumi mikononi mwa viongozi wachache wa chama cha CCM na kujijengea heshima na uaminifu miongoni mwa mataifa kuwa ni Taifa lenye kuthamini haki za binadamu,"imesema sehemu ya taarifa ya chama hicho.

Wakati huo huo wakuu wa vyama vya siasa vya upinzani nchini wameshauriwa kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na viongozi wa mataifa ya nje kwa lengo la kuviimarisha zaidi vyama hivyo katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kisiasa na kiuchumi.

Akizungumza na KIONGOZI ,mmoja wa wanasiasa wa kambi ya upinzani,Bw.Salum Chitanda ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi mkoa wa Lindi, alisema kuwa mawasiliano ya aina hiyo baina ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa nchini na viongozi wa nchi za nje (marais),utasaidia kwa kiasi kikubwa kuleta changamoto ya kimaendeleo ndani ya vyama hivyo.

Alisema kuwa mawasiliano hayo ndio yatakayosaidia kujenga ushirikiano katika mambo mbalimbali na kwamba hata viongozi wa nchi za nje wanapokuja nchini watakuwa na wasaa wa kukutana nao na kubadilishana mawazo yenye lengo la kuboresha demokrasia na maendeleo ya kiuchumi ndani ya vyama hivyo vya siasa .

Alisema kuwa tabia ya viongozi wa vyama hivyo vya siasa vya upinzani kutokuwa na ushirikiano na viongozi wa mataifa ya nje ndiko kunakosababisha viongozi hao wanapofanya ziara zao hapa nchini wasiwafikirie kabisa viongozi wa vyama hivyo.

 

Pengo awachachamalia wanaovunja ahadi za utawa

Na Dalphina Rubyema

 MWADHAMa Kardinali Polycarp Pengo amesema kuwa yupo tayari kuwashitaki kwa Mungu wale mapadri,watawa,Masisita na Mashemasi wanaoisaliti ahadi ya Useja.

Mwadhama Pengo ambaye ni Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar-Es-Salaam alitoa kauli hiyo mwanzoni mwa wiki wakati wa kuwapatia daraja la Ushemasi mashemasi 30 kutoka majimbo 14 nchini na jimbo moja la Kenya, ibada iliyofanyika katika Seminari Kuu ya Segerea Jijini.

"Nitakuwa tayari kuwashitaki wale wote walioweka ahadi ya useja ambao wanaisaliti ahadi hiyo na zaidi nitakuwa shahidi mbele ya Mungu kuwa nyie Mashemasi mlitoa ahadi hii mbele yangu"alisema Kardinali Pengo na kuongeza "Ingawa mimi siyo yule anayestahili kuchagua ni yupi anafaa kwenda kwenye ufalme wa Mungu na yupi anafaa kwenda toharani".

Useja ni kutokuishi na mume au mke au kuwa na ahadi ya useja ni kukataa kumtwaa mke au mume kwa namna yoyote ile.

Alisema kuwa ulimwengu wa leo hauthamini Useja kitu ambacho alisema kuwa wale wanaoenda kinyume na ahadi hiyo wanashitaka kubwa la kujibu kwa Baba aliye mbinguni.

Mbali na hilo,Kardinali Pengo alitoa wito kwa Mashemasi hao wapya kuwa wasitumie ukabila na Utaifakuisaliti dini ya Kikristo.

"Tumia Ukabila na Utaifa mlionao kuitangaza injili ya Mungu ,nyie ni wenyeji wa ulimwengu mzima ,fanya kama Saulo alivyokuwa Mhebrania lakini vile vile Mrumi"alisema Kardinali Pengo kauli iliyowavutia maelfu ya waumini walikuwepo katika ibada hiyo.

Kardinali Pengo aliongeza kuwa pamoja na Mashemasi hao kupata daraja hilo lakini hana uhakika wangapi watafikia daraja la Upadri kwa kusema kuwa wapo wengine wengi ambao hufikia hatua ya ushemasi lakini hushindwa kufikia daraja la Upadri.

"Pengine hapa baadhi yenu mnajua fika kwamba hamna nia ya kufikia daraja la upadri,mnaona tu ushemasi unatosha,kama kuna mmoja wenu mwenye nia kama hiyo nafasi bado ipo wazi unaweza ukatoka ila nisinge furahia hilo,ninachowaombea ni baraka za Mwenyezi Mungu awangazie ili nyote muweze kufikia daraja la upadri"alisema Kardinali Pengo.

Majimbo yaliyopata bahati ya kutoa Mshemasi ni Arusha, Bukoba, Geita, Dodoma, Morogoro, Same, Rulenge, Shirika la OCS, Moshi, Mbulu, Dar-Es-Saalam, Tanga, Singida , Musoma na Jimbo la Kakamega kutoka nchini Kenya.

Jimbo la kwanza kutoa Mashemasi wengi ni jimbo la Dodoma ambalo lilitoa mashemasi watano likifuatiwa na jimbo la Bukoba, Moshi na Mbulu ambapo kila jimbo lilitoa mashemasi watatu.

Majina ya Mashemasi hao na majina yao yakiwa katika mabano ni Albert Lubuva, Daniel Kijaji, Raphael Malijite, Paulo Nyange,Pius Matonyi (Dodoma), Fautini Kamugisha, Florence Rutaihwa, Johanes Rweyemamu (Bukoba), Pastori Mafikiri,Peter Neglo Mushi na Jovinali Asante Mungu (Moshi).

Wengine ni Emanuel Masangu, Elias Maligwe, Paul Mahe (Mbulu), Charles Saguti (Tanga), Desidel Rugemalila, Sixtus Kimario (Dar-Es-Salaam), Sabinus Molemi (Musoma ),Panfilius Kitondo,Revelian Miompae(Lulenge)Fredelick Mtokambali, Gerevas Taito(Arusha), Liston Lukoo (morogoro), Anthony Chilwa (Singida),Vicenti Sanga na Anthony Mochenditsi (Kakamega).

Ibada hiyo iliyofuatiwa na sherehe kubwa, iliwajumuisha watu mbalimbali akiwemo Askofu wa Jimbo la Mahenge,Mwashamu Agapiti Ndolobo na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC),Padri Method Kilaini na Msaidizi wake Padri Pius Rutechula

Walemavu wataka serikali moja ya Muungano

Na Said Mmanga - Morogoro.

SHIRIKISHO la vyama vya walemavu mkoa wa Morogoro limependekeza kuwepo na serikali moja ya muungano badala ya muundo wa sasa wa serikali mbili.

Mapendekezo hayo yametolewa na wawakilishi wa vyama mbali mbali vya walemavu mkoani Morogoro katika warsha ya siku moja ya kujadili waraka namba moja wa serikali, yaani white paper iliyofanyika kwenye ukumbi wa Social Educational Centre mjini Morogoro.

Wamesema muundo wa Muungano uliopo sasa bado unalegalega hasa kwa kuwepo na serikali mbli yaani serikali ya mapinduzi Zanzibar na serikali ya muungano jambo ambalo wamesema linawanyonya watu wa Tanganyika.

Wakijadili waraka huo wamesema kuwepo kwa serikali moja ndiyo suluhisho la kupata muungano wa kweli badala ya serikali mbili au tatu kwani kufanya hivyo kutaondoa malalamiko ya upande mmoja kuona unanyimwa haki. Aidha, shirikisho hilo limepinga kuwepo kwa wagombea binafsi wa nafasi ya uraisi ambapo wamependekeza mfumo wa sasa wa wagomeba kutoka kwenye vyama vya siasa uendelee.

Washiriki hao pia wamependekeza kuwepo na utaratibu wa kuwaondoa madarakani wabunge wasiotimiza matakwa ya wapiga kura wao ambapo pia wamependekeza mawaziri wasichaguliwe miongoni mwa wabunge kwani kufanya hivyo kutarahisisha utendaji kazi badala ya sasa.

Wamesema kutokana na mawaziri kuchaguliwa kutoka miongoni mwa wabunge inakuwa ni vigumu kwa wananchikuibana serikali kwa kuwa wabunge ambao ni mawaziri wanalazimika kuitetea serikali badala ya wananchi waliowapeleka bungeni.

Wakijadili kipengele cha rais kuendelea na uwezo wa kuwaweka watu kizuizini walisema kipengele hicho kiendelee kwa kuwa kinampa rais uwezo wa kudhibiti watu wasioitakia mema nchi. Hata hivy mjadala huo ulishindwa kukidhi haja kwa kiasi kikubwa kwa kuwa baadhi ya walemavu walilazimika kupata mawasiliano kwa taabu hasa viziwi kutokana na kutokuwepo kwa mtaalamu wa lugha ya ishara.

 

Ngulume atakiwa kuingilia kati mgogoro wa wafugaji na wakulima

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

 WANANCHI wa Lugala kata ya Mazimbu mkoani Morogorowamemuomba mkuu wa wilaya ya Morogoro mjini bibi Hawa Ngulume aingilie kati mgogoro kati ya wakulima na wafugaji wa eneo hilo.

Katika barua yao kwenda mkuu wa wilaya ambayo kiongozi imepata nakala yake wananchi hao wamesema tatizo la mifugo limekuwa kero kubwa kwa wakulima wa maeneo ya Lugala, Chamwino na Mazimbu na hivyo kuomuomba kiongozi huyo awasaidie kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji.

Wamesema kutokana na wafugaji hasa wa kabila la wamasai kuchunga mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima wamelazimika kuvuna mazo yao yakiwa mabichi kwa kuhofu yasiliwe na ng'ombe pamoja na mbuzi na hivyo kusababisha uhaba wa chakula kwa wananchi hasa wakulima.

Kufuatia wafugaji kuchunga mifugo yao kwenye mashamba wananchi hao wa Lugala wamesema kuwa athari zimeanza kujitokeza ikiwa ni pamoja na eneo hilo kuwa nusu jangwa na sababu ni idadi kubwa ya mifugo katika eneo hilo.

Barua hiyo ambayo nakala yake imepelekwa kwa kamanda wa polisi wa mkoa wa Morogoro, wananchi hao wamesema kwa sasa wanaishi kwa hofu kwa kuwa wakijaribu kuwafukuza ng'ombe mashambani ugomvi mkubwa huzuka kati ya wakulima na wafugaji.

Aidha, wananchi hao wa Lugala wamemuomba bibi Hawa Mgulume atembelee eneo hilo ili aweze kujionea hali ilivyo katika eneo hilo.

Wakati huo huo baraza la halmashauri ya wilaya ya Morogoro vijijini limeitaka serikali kukomesha rushwa katika vituo vya afya ili kupunguza vifo vya mama na watoto wilayani humo.

Wito huo umetolewa na madiwani hao wakati walipokuwa wakijadili mkakati wa uboreshaji wa mpango wa uhai, ulinzi na maendeleo ya mama na mtoto wilayani humo waseme kuzorota kwa mpango huo kumechangiwa na watendaji wa Zahabati na vituo vya kuomba rushwa kwa wagonjwa na mama wajawazito.

Aidha, madiwani hao wameishauri serikali kuwa makini katika kusimamia huduma za afya na kutahadharisha kuwa masuala ya afya yasiendeshwe kisiasa kwani kufanya hivyo ni kuzorotesha huduma.