UWAZI KATIKA KUTANGAZA MALI

Mkapa atakiwa asiridhike na kauli za viongozi wake

lUchunguzi ufanyike juu ya kujirundukia utajiri

Na Seraph Kuandika

 

Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kimemtaka rais Mkapa na serikali yake kutoridhika na sababu zinazotolewa na viongozi wa chama tawala cha CCM na serikali juu ya mahali walikozipata mali wanazomiliki na badala yake uchunguzi wa kina ufanyike kuona kama kuna ukweli wowote kuhusiana na madai ya viongozi hao.

Mwenyekiti wa chama hicho,Bw.Bob Makani aliliambia KIONGOZI ofisini kwake jana kuwa viongozi hao hawana budi kueleza kikamilifu jinsi walivyopata mali na ili serikali iweze kuridhika na maelezo,haina budi kufanya uchunguzi wa kina kwa lengo la kupata ukweli.

Alisema kuwa iwapo Rais na serikali yake hawatachukua hatua za kufanya uchunguzi juu ya suala hilo ni dhahiri kwamba zoezi hilo halitakuwa na maana yoyote zaidi ya kuwadhihaki wananchi.

"Mkapa na serikali yake wanafanya juhudi gani kuchunguza madai ya wakubwa wanakozipata mali wanazozitangaza,"alihoji Bw.Makani. na kuongeza kusema," sio tu wanatangaza mali na serikali inanyamaza.

Mwenyekiti huyo wa Chadema aliongeza kusema kuwa serikali inapaswa kujiridhisha kwanza yenyewe kwa kuona viongozi wanatangaza mali na kwamba wamezipata kihalali badala ya kuwaacha wakiendelea kutangaza juu juu tu bila kuwepo na vigezo muhimu.

Aidha aliongeza kusema kuwa pamoja na umuhimu huo wa kufanya uchunguzi wa kina kufahamu kama mali hizo zimepatikana kihalali,pia kitendo hicho cha kutangaza mali kinadhihirisha wazi jinsi watu wanavyoweza kujilimbikizia mali kwa kutumia nyadhifa zao.

Alitolea mfano wa mkuu wa wilaya ya Geita.Bibi.Halima Khatibu,ambaye alimwelezea kuwa ni mmoja wa viongozi ambao serikali haina budi kumuhoji zaidi juu ya mali alizonazo japokuwa ametaja mahali alikozipata.

Alisema kuwa kwa nafasi aliyonayo ya ukuu wa wilaya ni vigumu sana kwa kuiongozi huyo kuwa na mali nyingi na zenye thamani kubwa ikiwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kuwasomesha watoto wake wawili kwa gharama ya shilingi milioni 12 kwa mwaka.

"Hebu fikiria mtu kama mkuu wa wilaya anazo mali nyingi ikiwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kuwasomesha watoto wake wawili kwa gharama ya shilingi milioni 12 kwa mwaka, hali hii inaonyesha dhahiri jinsi viongozi wanavyojilimbikizia mali kwa kutumia nyadhifa zao," alisema huku akionyesha gazeti la Mzalendo lililokuwa na habari zinazomwelezea mkuu wa wilaya huyo ya Geita akitangaza mali zake.

 

 

Kijana ampandisha kizimbani mjomba wake akimdai mkewe

lAdai kwa nini alimpa talaka mkewe bila idhini yake

Na Neema Dawson

HASSAN Hashimu Mkazi wa Tandika amempandisha Kizimbani Mjomba wake akimdai amrudishie mkewe ambapo inadaiwa kuwa mjomba wake Mauridi Makungu alimpa talaka mke wake Salima Yahaya na kumshawishi aondoke nyumbani kwake bila idhini yake.

Madai hayo yalifikishwa mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya mwanzo Temeke Asia Dege ambapo ilidaiwa na Hassani Hashimu ambaye ni mdai katika kesi hiyo kuwa tangu walivyooana na mkewe Salima wamekaa kwa muda wa miezi Mitatu tu ndipo mojmba wake alipowaingilia katika ndoa yao na kuanza kuwafanyia vitimbwi. Hadi hivi sasa mkewe hamtaki na anaishi bila mke .

Upande wa madai hayo uliendelea kudai kuwa ghafla alimuana mkewe akianza kubadilika na kugoma kumpikia, kumfulia nguo , na zaidi zaidi kugoma kumpa tendo la ndoa hali ambayo ilimtia uchungu sana na alipokuwa akijaribu kumbembeleza mkewe ndipo mkewe alipokuwa akidai apewe talaka yake kwani kuolewa ameshindwa.

Hali hiyo ilinitia wasi wasi hivyo niligoma kumpa talaka mke wangu kwani sikuona sababu ambayo itasababisha tuachane , hali hiyo ya ukorofi wa mke wangu iliendelea kubadilika siku hadi siku hadi ilifikia hatua mke wangu akaamua kubeba vyomba vyangu na kuhamia nyumbani kwa mjomba wangu ambapo sikuridhika nilimfuata huko huko. Alisema Hassani ambaye anadai mke wake.

Aliendelea kuelezea kuwa alishangazwa na kitendo cha mjomba wake kuamua kumuandikia talaka mke wake ambapo mimi niliyemuoa nilikataa kuandika talaka hiyo kwani mke wangu bado ninampenda na siwezi kumuacha na bado ninajua kuwa bado ni mke wangu.

Kutokana na mgogoro uliokuwepo tulifika katika Baraza la Waislamu Tanzania ( BAKWATA) na baada ya mke wangu kudai kuwa hanitaki na tuachane na mimi nilikataa kutoa Talaka kwani bado ninampenda na baraza hilo lilitoa uamuzi kuwa kama mke wangu anataka tuachane basi anunue talaka hiyo.

Hakimu Dege alimuuliza mdai huyo kuwa alimuoa mkewe kwa mahari kiasi gani ? mdai huyo alidai kuwa alimuoa kwa mahari ya sh. 60,000 na aliulizwa kuwa endapo ataiuza talaka hiyo ni kwa gharama gani? Alidai kuwa hayuko tayari kumuacha mkewe itabidi anunue talaka hiyo kwa thamani ya sh. 120,000.

 

Moro wataka BAKWATA ivunjwe

Na Mwandishi Wetu

 SHEIKH Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Alhaj Omari Bafadhli ametaka Baraza Kuu la Waislamu nchini (BAKWATA) livunjwe kutokana na kushindwa kuwasaidia Waislamu.

Kiongozi huyo wa Bakwata aliyasema hayo alipokuwa akihutubia Baraza la Idd lililofanyika kwenye msikiti Mkuu wa Ijumaa uliopo Barabara ya Boma mjini Morogoro mwishoni mwa wiki.

Alisema kwa kipindi chote ambacho Baraza hilo limekuwepo limeshindwa kuwasaidia Waislamu matokeo yake wamewasaliti waislamu na kusema kuwa ni wakati muafaka kwa baraza hilo livunjwe na liundwe jipya ambalo liongozwe na vijana imara wenye elimu.

Sheikh Bafadhili ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya usalama kitaifa alisema endapo BAKWATA itakuwepo bila kufanyiwa marekebisho waislamu hawatapata maendeleo kwa kuwa viongozi wengi hawana mwamko wa maendeleo.

Aidha, aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu kuacha kuilalamikia serikali kwamba inawabagua Waislamu katika kupata elimu ambapo aliwataka Waislamu kuwaandaa watoto wao ili waeze kuwa na elimu ya kutosha.

Alisema pamoja na jumuiya za Kiislamu kuwa na shule zake za sekondari lakini shule nyingi zinazoendeshwa na Waislamu hazina maendeleo mazuri kwa kukosa walimu wenye sifa ambapo aliongeza kuwa shule hizo zinazoongoza kwa kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa.

Kiongozi huyo alisema njia pekee ya kuweza kuondoa pengo la tofauti ya elimu kati ya waumini wa Kiislamu na madhehebu mengine ni kuwaanda vijana katika kupata elimu.

Mbali na hayo sheikh Bafadhili pia aliwataka wananchi wa mkoa wa Morogoro kuzitumia vizuri mvua zinazoanza kunyesha mkoani hapa kwa kulima mazo yanayostahimili ukame pamoja na wananchi hao kudumisha amani na utulivu kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

 

CARITAS yaagiza tani 3,804 za chakula

Na Dalphina Rubyema

 SHIRIKA la Kimataifa linaloshu-ghulika na utoaji wa Misaada la Caritas tawi la Tanzania, limeagiza tani 3,804 za chakula kutoka kwa wafadhili ambao ni nchi wanachama wa shirika hilo kama msaada kwa watu walioathirika na njaa hapa nchini.

Chakula hicho ambacho kinatarajiwa kufika mwishoni mwa mwezi huu na kuanza kusambazwa kwa waathirika mwanzoni mwa Februari mwaka huu, kina thamani ya Dola za Kimarekani 1,348,948 sawa na shilingi 903,795,480.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi hapo jana kwenye ofisi zilizopo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), Katibu Mtendaji wa Caritas Tawi la Tanzania, Bw.Clement Rweramila alisema kuwa uagizaji wa chakula hicho umekuja baada ya Caritas ambayo ipo chini ya TEC kufanya uchunguzi wa kina kwenye Majimbo 24 ya Kanisa Katoliki.

Aliyataja Majimbo hayo kuwa ni Tanga, Same, Arusha, Mbulu, Mbinga, Shinyanga, Kahama, Tabora, Singida, Dodoma, Mahenge, Bukoba, Dar es Salaam, Mtwara, Tunduru-Masasi, Lindi, Iringa, Mbeya, Morogoro, Musoma, Mwanza, Geita na Rulenge.

Bw. Rweramila alisema kuwa katika uchunguzi huo, Caritas ilibaini kuwa watu wapatao 317,024 wameathirika na njaa kali na hawa watu ni wale ambao hawana uwezo wa kulima wala kununua chakula ikiwa ni pamoja na wazee, yatima ,wagonjwa na wajawazito na hao ndio watakaopata msaada wa chakula.

Aliongeza kuwa Msaada huo utaweza kuwatosheleza wahusika kwa muda wa mwezi mmoja na baada ya hapo serikali itakuwa inapata ufumbuzi wa suala hilo, alisema Caritas itaweza kuagiza chakula kwa awamu ya pili baada ya kuona jitihada za serikali.

Plan International kutumia milioni 450/- kusaidia Kilombero

Na Saidi Mmanga

 SHIRIKA la kimataifa lisilikuwa la kiserikali la Plan International limetumia zaidi ya shilingi milioni 450 mwaka 98/99 kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo wilayani kilombero.

Akihojiwa na Kiongozi ofisini kwake mjini Ifakara juzi programu meneja wa Plan International Bibi Josephine Kashe ametaja miradi hiyo kuwa ni ya afya, elimu, hifadhi ya mazingira pamoja na miradi ya maji.

Bibi Kashe katika taarifa yake kwa Kiongozi amefafanua kwamba lengo la shirika hilo ni kuboresha huduma mbali mbali za jamii katika wilaya hiyo ya kilombero.

Amesema kuwa Plan International limekuwa likijihusisha zaidi na ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, usambazaji wa vifaa vya afya vijijini pamoja na ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu na usambazaji wa vifaa vya elimu vijijini..

Bibi Kashe katika taarifa yake hiyo kwa Kiongozi ameeleza kuwa katika kipindi cha cha mwaka wa fedha wa 1999/2000 plan international linatarajia kutumia zaidi ya shilingi milioni 850 kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya huduma za jamii wilayani Kilombero. Shirika la Plan International lilianza shughuli zake wilayani kilombero mwaka 1996 kwa kujihusisha zaidi na utekelezaji wa miradi ya elimu na afya.

Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu uendelezaji wa wataalamu katika sekta ya elimu pamoja na utoaji wa vifaa vya elimu katika shule mbali mbali za msingi.

Ametaja vijiji ambavyo vimekuwa vikinufaika zaidi na msaada huo wa Plan International kuwa ni Kidete, Lumemo, Kibaoni, Michenga katika tarafa ya Ifakara.

Ametaja vijiji vingine ni vya tarafa ya Mangula na Mgeta ambamo pia miredi ya maji itaanza kutekelzwa kwa kushirikiana na serikali za vijiji.

 

Kisarawe wahitaji tani 5000 za chakula kuwasaidia wakazi wa Mzenga na Chole

Na Said Mmanga, Morogoro

 WILAYA ya Kisarawe mkoani Pwani inahitaji tani 5000 za chakula kwa ajili ya wananchi 21,000 wa kata ya Mzenga na Chole wanaokabiliwa na upungufu.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Kapteni James Yamungu alilieleza gazeti hili mjini Morogoro kuwa tarafa hizo zinakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na kuchelewa kwa mvua pamoja na mvua za el nino ambazo ziliharibu mazo ya wakulima.

Amesema wananchi wa kata nyingine za wilaya hiyo za Manerumango na Sungwi hawana tatizo la chakula kwa kuwa wana ziada ya kutosha ya tani 45,000 ya zao la muhogo.

Kepteni Yamungu amesema katika kukabiliana upungufu wa chakula hasa nafaka wamewaagiza wafanya biashara wanaonunua mihogo wilayani humo kupeleka bidhaa nyingine hasa nafaka ili kufidia upungufu wa chakula.

Akieleza zaidi mikakati iliyochukuliwa na wilaya yake katika kukabiliana na upungufu wa chakula kepteni Yamungu alisema wananchi wenye mifugo na vitu vingine wameshauriwa kuviuza ili waweze kujikinga na baada hilo la njaa.

Wakati huo huo Bw. Yamungu alisema wilaya ya Kisarawe imevuka lengo la utengenezaji wa madawati kwa shule zake za msingi ambapo hivi sasa wilaya hiyo ina ziada ya madawati 700

Alisema jambo hilo limefanikiwa ktuokana na wananchi kushirikishwa katika shughuli za maendeleo ambapo hivi sasa kila kata wilayani humo ina jumuia ya maendeleo.

Kepteni Yamungu ameongeza kuwa mbali na jumuiya za maendeleo na kata pia walaya ya kisarawe ina umoja wa maendeleo unaojulikana kwa jina la UMAKI ambao huwaunganisha wananchi wa wilaya ya Kisarawe wanaoishi jijini Dar es Salaam na wale walioko wilayani humo katika kuleta maendeleokatika nyanja mbali mbali kama elimu, afya na uchumi.

 

Zanzibar ikijitegemea muungano utavunjika-Bob Makani

Na Seraph Kuandika

 Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw.Bob Makani amesema kwamba iwapo Zanzibar itafanikiwa katika mpango wake wa kuwa na Bandari yake inayojitegemea, itakuwa ni dalili tosha za kumomonyoka kwa muungano.

Akizungumzana Kiongozi ofisini kwake jana,Bw.Makani alisema kuwa hatua ya Zanzibar kuwa na Bandari yake (Free Port) ni moja ya harakati zinazochukuliwa ili kuhakikisha Zanzibar inaendesha shughuli zake binafsi ,hali ambayo itapunguza nguvu za kuwepo kwa muungano.

Bw.Makani alikuwa akitoa maelezo juu ya athari za kuifanya bandari ya Zanzibar kuwa huru.

Mpango huo ulitangazwa hivi karibuni na rais wa serikali hiyo,Dk. Salmin Amour alipokuwa akihutubia sherehe za kutimiza miaka 35 ya mapinduzi ya zanzibar ,zilizofanyika kwenye uwanja wa Gombani,Pemba.

Mwenyekiti huyo wa Chaderma alisema kuwa kwa kuwa Zanzibar hawataki kumezwa na serikali ya Muungano na wakati huo huo katiba ya muungano inaitambua Zanzibar,hivyo wanaitumia nafasi hiyo kuendeleza masuala yao ambayo ni dhahiri yanaelekea kuvuruga muungano uliopo baina ya Tanganyika na Zanzibar.

"Unajua katiba ya muungano haiitambui Tanganyika bali inaitambua Zanzibar hivyo kutokana na hali hiyo,wenyewe (Zanzibar) wanaitumia nafasi hiyo kuendeleza uzanzibar," alisema mwenyekiti huyo wa taifa wa CHADEMA na kuongeza kwamba kuifanya bandari ya Zanzibar kuwa huru kutachangia pia kushusha mapato ya serikali ya muungano pamoja na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ambayo alidai itapata wakati mgumu sana katika ukusanyaji mapato.

Aliongeza kusema kuwa ili kuweza kuondokana na utata unaoweza kujitokeza kwenye masuala ya muungano,wao kama chadema ndio maana siku zote wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa serikali tatu, ya muungano,Tanganyika na ya Zanzibar.

Alisema kuwa hali hiyo itaiwezesha serikali ya tanganyika kufanya mabo yake ambayo kwa namna moja ama nyingine yatachagia kuleta maendeleo zaidi kwa upande wa Bara am,bapo alisema kuwa miongoni mwa mambo hayo ni kuwa na uwezo wa kujihami na masuala mbalimbali yatakayoweza kutishia uchumi wa Bara.

"Moja ya majibu ya kutatua matatizo ya muungano ni kuwa na serikali tatu hapo itasaidia kwa Tanganyika kujifanyia mambo yake yenyewe hasa ya kujihami na masuala ya uchumi",alisema.

 

Wakulima wa mpunga Mbeya sasa kuwa na soko la uhakika

Na Lucas Mlekeafike Ndanga - Mbeya

 WAKULIMA wa zao la mpunga mkoani Mbeya wataanza kuwa na soko la uhakika wa zao hilo kwa kiasi cha tani 18,000 kila mwaka kuanzia msimu huu wa kilimo.

Pamoja na kuwa na uhakika wa soko la zao hilo kuna matumaini makubwa ya kupanuka kwa biashara na kilimo cha zao hilo kufuatia kuzinduliwa kwa kiwanda cha kusaga nafaka cha Wella Highland Millers Mjini Mbeya.

Mwenyekiti mtendaji wa kampuni hiyo Bw. Ramzan Walji ameiambia Kiongozi hivi karibuni mjini hapa kuwa kufunguliwa kwa kiwanda hicho kutawasaidia wakulima wa zao hili kwa kuwapunguzia adhaa na gharama za usafirishaji wa zao hilo kwa sababu watendaji wa Kampuni hiyo watakuwa wanawafuata wakulima vijijini.

Bw. Walji amesema sambamba na kupunguza gharama za usafirishaji mashine hizo za kukoboa na kusaga zitarahisisha ununuzi kwa walaji kwa kuupakia na kuuweka mchele katika madaraja mbali mbali kuanzia la kwanza mpaka la nne na vifuko vya kilo mbili hadi 50 kulingana na uwezo wao kiuchumi.

"Kuzinduliwa kwa kiwanda hiki kutaleta ajira kwa watu 80 ambao mwaka jana nimeajiri watu 20 na wengine waliosalia 60 nitawaajiri mwaka huu". ameeleza Bw. Walji.

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa kiwanda hicho hivi karibuni mjini hapa,Waziri wa kilimo na ushirika Bw. William Kusila amewataka wamiliki wa kiwanda hicho kukitumia vema kuhakikisha kuwa kinainua kipato cha wakulima wa zao hilo kwa kununua mpunga kwa bei nzuri ili kuinua hali ya maisha yao.

 

AJM yalaani tabia ya waandishi wa Tanzania kukashifiana katika vyombo vyao

Na Burton Brown

 CHAMA cha Waandishi wa Habari na wafanyakazi kwenye vyombo vya habari (AJM) kimelaani vikali tabia ya baadhi ya vyombo vya habari hususani magazeti kutumika katika kuwakashifu waandishi wengine kwa makusudi.

Akizungumza jijini Mwenyekti wa AJM Lawrance Kilimwiko, alisema "tabia hii ni mbaya sana kwa vile inalenga kuididimiza taaluma ya uandishi wa habari hapa nchini hivyo inafaa ikomeshwe"

Kilimwiko alisema ipo haja ya waandishi kuungana pamoja ili kulinda taaluma hii badala ya mtindo wa sasa wa kukashifiana. "As a journalist we must come together to promote the solidarity of this profession". Alisema mwenyekiti huyo, akimaanisha kuwa ni lazima waandishi wa habari wote washirikiane kuinua hadhi ya taaluma hii".

Alisema tabia ya waandishi kukashifiana imesababisha zaidi ya kesi 30 zipo kwenye mahakama kuu ya Tanzania, jambo ambalo litaweza kusababisha baadhi ya magazeti kudaiwa fidia kubwa na hivyo kufa kabisa.

Kilimwiko alisema tabia ya waandishi kukashifiana wenyewe kwa wenyewe siku hizi inasababisha vita baridi viliopo kati ya waandishi wa kujitegemea na wale wenye ajira. "Hili nadhani ni tatizo sugu hivyo linafaa kupatiwa ufumbuzi wa haraka" alisema.

Alisema uandishi kama taaluma nyingine, unafaa uheshimiwe kwa watu kukosoana kwenye baraza la habari la Tanzania ama dani ya menejimenti ya AJM.

Alisema ni mwiko mkubwa kwa waandishi kufichuana siri zetu kama ambavy madaktari wanavyotunza siri za wagonjwa wao.

"Kama madaktari wanatunziana siri, kwa nini waandishi tutukanane hovyo mbele ya jamii" alihoji.

Kilimwiko, aliwataka wahariri wa habari wa vyombo vyoe vya habari nchini kuidhinisha habari za ripota wao zenye nia njema kwa Taifa na watu wote.

Alisema wahariri makini ni wale wanaojua wajibu wa kazi wa kuzichambua habari zenye mantiki tu na sio majungu tu.