‘Siasa bila
dini ni uendawazimu’
Na Lilian Nyenza
Kanisa
halitaacha kutoa mwongozo kwa watu wake hata kwa mambo ya kisiasa ukiwamo
uchaguzi kwa kuwa, siasa bila dini ni sawa na uendawazimu.
Aidha, imedaiwa kuwa tabia ya
kuwalaghai vijana kuwa ni taifa la kesho, ndiyo inayowadumaza kiakili na
kuwafanya watumiwe na wanasiasa kufanya fujo, badala ya kujitokeza kuongoza kwa
kufuata taratibu za nchi.
Mkurugenzi
wa chama cha kifamilia cha Undugu
Association Tanzania, Padri Baptiste Mapunda, alitoa kauli hiyo katika
sherehe za kuuaga mwaka 2004 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2005, zilizofanyika
katika ukumbi wa Parokia ya Mt. Yosefu,
Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo wa UNDUGU ASSOCIATION TANZANIA
alisema kuwa, Tanzania imeanza kuonesha dalili mbaya za machafuko kutokana na
baadhi ya watu wakiwamo wanasiasa kuweka mbele ubinafsi.
“Tukikaa
kimya huku mambo yanaharibika katika jamii; eti tuwaachie wanasiasa wafanye
watakavyo, tutakuwa hatutendi wajibu wetu na hivyo, Kanisa halitaacha kusema
ukweli kwa maslahi ya umma hata kama unamkera mtu. Hii ni kwa kuwa tunajua wazi
kuwa siasa bila dini, ni uendawazimu ambao mtu hajui akifanyacho kwa kuwa akili
yake haijatimia kiroho.” alisema.
Aliitaka
jamiii ya Kitanzania ijifunze thamani ya amani na siasa safi kutokana na hali
ya amani na usalama katika nchi jirani za Rwanda na Burundi ambayo ni hatari na
inasikitisha.
Alisema
vita na mauaji yanayoendelea katika nchi hizo, yanasababishwa na uroho wa
madaraka wa watu wachache ambao hawajali utu wa wengine.
Aliongeza
kuwa, “Siku zote tunapaswa kukumbuka kuwa, amani na mapendo ambayo Mungu
ametujalia, tunapaswa kuyaenzi sisi sote kwa kuwa siasa bila dini, ni sawa na
uendawazimu.”
Padri
Mapunda aliiasa jamii kuendelea kumuomba Mungu ili azidi kuwajalia amani,upendo
na utulivu uliopo sasa, kuwa uwepo hata baada ya Uchaguzi Mkuu kupita.
Amewataka
Waamini kuwaombea viongozi wanyanyasaji kama Herode, wabadilike na hivyo,
kuongoza nchi kwa haki na akawasihi Watanzania kuyashinda maovu kwa kutenda
yaliyo mema.
Hata
hivyo, Padri Mapunda amewatahadharisha vijana kujiepusha kutumiwa na baadhi ya
viongozi wa siasa, kwa nia ya kufanya fujo katika uchaguzi.
“Vijana
mara nyingi wamekuwa wepesi wa kurubuniwa na vijizawadi vidogo vidogo, ili
wafanye kile wanachokitaka wanasiasa wabinafsi. Sasa mimi nasema mkae chini na
mlitafakari hilo kwa makini. Mtakao angamia ni ninyi na si wao,”
alitahadharisha.
Alisema
vijana ni Taifa la leo na Taifa bila vijana limekufa, hivyo aliwasihi
kuwaheshimu wazazi na walezi ili wapate kuishi maisha marefu na yenye heri
duniani, kama walivyojaliwa kuuona mwaka huu mpya.
Naye
Mwenyekiti wa Umoja huo, Bw. Benjamini Komba alisema, lengo la Shirika la
Undugu, ni kuiunganisha jamii, ikiwa ni pamoja na kuimarisha Ukristo katika
kupata hamasa katika kazi ya umisionari, ili ijengeke roho ya umisionari wa kweli nchini Tanzania.
Bw.
Komba alisema kuwa, Shirika limekuwa na mchango mkubwa kwa jamii, kwa kuwa ni
chombo cha kuelimisha jamii na kuendeleza mawasiliano na wamisionari wa Afrika
ambao wapo ndani na nje ya nchi kwa lengo la kusukuma mbele kurudumu la Injili
katika Taifa hili.
Umoja
huo haujishughulishi na mambo ya siasa na hauna ubaguzi wa dini, rangi, imani
wala itikadi.
Katika
sherehe hizo, Wanaundugu na watu wengine walialikwa na kuhudhuria pamoja
na familia zao.
WARIOBA: Spika, Jaji Mkuu waondolewe
l Asema Wanawake watatu wamenyimwa Uwaziri Mkuu
l Tume ya
Uchaguzi yamtia hofu
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI
Mkuu wa zamani wa Tanzania, Jaji Joseph Warioba amelishauri Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuwaondoa Spika wa Bunge hilo pamoja na Jaji Mkuu wa
Tanzania kushika moja ya nafasi nyeti ya nchi.
Nafasi ambayo Jaji Warioba
alishauri isishikwe na viongozi hao ni ile ya kukaimu nafasi ya urais, pindi
Rais ama Makamu wake wanapokuwa nje ya nchi kikazi ama wawapo katika mazingira
yanayoweza kuwafanya washindwe kutimiza majukumu yao, ikiwemo ugonjwa ama hata
kifo.
Akihojiwa na gazeti moja la
kila wiki hapa nchini hivi karibuni, Jaji Warioba alisema haikuwa sahihi
kuwafanya Spika wa Bunge na Jaji Mkuu kukaimu nafasi hiyo na kumwengua mtu
muhimu kama Waziri Mkuu na kwamba, anaunga mkono Mabadiliko ya 14 ya Katiba
yanayopendekeza kuwaondoa watu hao kushika nafasi hiyo.
Alisema
kutokana na mazingira ya sasa, sio jambo la busara kumpa nafasi mtu kama Jaji
Mkuu kushika nafasi za kiutawala. Hakufafanua.
Aidha, alisema ingawa baadhi
ya nchi Spika huwa wa pili ama wa tatu kwa itifaki ya uongozi, kwa mfumo wa
Tanzania ni vema Waziri Mkuu akashika nafasi ya tatu baada ya Makamu wa Rais.
“Makamu wa Rais na Waziri
Mkuu ni wasaidizi wa Rais wa moja kwa moja na wanaweza kutekeleza shughuli za
Rais vizuri zaidi na kwa urahisi,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe nchini
katika mahojiano hayo.
Pamoja na kukubaliana na
Marekebisho ya 14 ya Katiba hususan Ibara ya 37, Jaji Warioba alipingana na
Kifungu cha 51 (2) ambacho kinataka Waziri Mkuu atokane na Wabunge wa
kuchaguliwa kutoka majimbo ya uchaguzi, akidai kwamba kimesababisha mawaziri
wanawake watatu katika Serikali ya Rais Mkapa ambao uwezo wao wa kushika nafasi
ya Uwaziri Mkuu umeonekana bayana kutoteuliwa.
“Katiba imewanyima sifa ya
kufikia nafasi ya Waziri Mkuu kwa kuwa wamechaguliwa kwa utaratibu maalum,”
alisema na kuongeza kuwa, hawa ni wale ambao ubunge wao hautokani na
kuchaguliwa majimboni.
“Kwa hiyo, napendekeza kuwa
sharti la sasa kuhusu uteuzi wa Waziri Mkuu liondolewe, na mbunge yeyote awe na
nafasi ya kushika nafasi hiyo,” alisema Jaji Warioba.
Kwa upande mwingine, Jaji
Warioba ameonesha hofu ya waziwazi kuhusiana na kuundwa kwa kile kitakachoitwa
“Tume Huru ya Uchaguzi” itakayowajumuisha wajumbe watano kutoka vyama vya siasa
na akasema, kufanya hivyo ni kuvunja misingi ya demokrasia na uhuru wa kweli wa
Tume hiyo.
“Mabadiliko ya Ibara ya 74
yanaleta wasiwasi. Ibara Mpya ya 74 (16) inaonesha kuwa Tume ya Uchaguzi
itakuwa na wajumbe wanasiasa ambao watawakilisha vyama vya siasa. Badiliko hili
linavunja msingi wa kuwa na Tume huru. Hii ni taasisi ya umma na inatakiwa iwe
huru kabisa bila kuegemea upande wowote,” alisema Jaji Warioba na kuongeza
kuwa, ndio maana chini ya Ibara ya 74 (14 na 15), watu wote wanaohusika na
uchaguzi ikiwa ni pamoja na wajumbe wa
Tume, wanazuiwa kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa.
Aliongeza
kuwa, kuchagua wajumbe wa Tume kutoka vyama vya siasa kutaleta matatizo makubwa
kwa vile vyama vya siasa ni vingi na haitawezekana vyama vyote vikubaliane
kumchagua mjumbe mmoja kuingia katika Tume.
Alionya
kuwa, nchi zenye Tume ya Uchaguzi iliyoundwa kisiasa zimepata matatizo kwenye
uchaguzi kwa sababu ziliendesha shughuli zake kisiasa na kuitolea mfano Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar ambayo mwaka juzi ilionesha dalili hizo wakati wa uchaguzi
mdogo uliofanyika visiwani humo.
“Wajumbe wa CUF
hawakukubaliana na hoja ya kuwazuia wagombea waliowekewa pingamizi na
NCCR-Mageuzi. Ingekuwaje kama waliopingwa wangekuwa ni wagombea wa CCM?”
aliuliza mwanasiasa huyo.
Jaji Warioba
aliitaka Serikali kulinda uhuru wa Tume kwa kufanya mabadilko na kuteuwa
wajumbe wake nje ya vyama vya siasa ili kuifanya iaminike na wananchi na hivyo
kuondoa matatizo yanayoweza kutokea wakati wa uchaguzi.
Amani ina utata –
Kardinali
ASKOFU
Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,
ametahadharisha juu ya utata wa amani uliopo nchini na akasema jamii
isipochukua hatua mbadala kuukabili, ikubali kulaumiwa na vizazi vijavyo.
Kardinali Pengo aliyasema hayo
katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoandaliwa na Wanawake Wakatoliki Tanzania
(WAWATA), Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam na kufanyika katika Kanisa
Kuu la Mtakatifu Yosefu jijini Dar es Salaam.
Kardinali Pengo
alisema amani inayodaiwa kuwapo nchini ina utata kwa kuwa imeanza kutishiwa
kutokana na matukio mbalimbali ya uvunjaji wa amani vikiwemo vitisho vya mauaji
hivyo, akaitaka jamii kutobweteka na kuhadaika ili nusuru taifa lisiangamie.
Alisema “dawa” ya kuepukana na
janga hili la kutoweka amani linaloitishia Tanzania, ni kila raia mwenye sifa
kujiandikisha na kupiga kura ili kumchagua kiongozi anayefaa vinginevyo, ipo
hatari wasioongozwa na Mungu wakawachagulia watu kiongozi asiyefaa.
“Inatisha sana maana kama katika
hatua za kujiandikisha tu, watu wanauana, basi ni wazi tuna kila sababu ya
kumuomba zaidi Mungu alinde amani yetu…,” alisema.
Katika kudumisha amani nchini,
Kardinali Pengo aliwaambia wana WAWATA akisema, “Tusichoke kuomba kabla na
baada ya uchaguzi… Tusihadaike na amani iliyopo na badala yake, tumkimbilie
Mungu katika kipindi hiki.”
Alionya dhidi ya tabia ya baadhi
ya watu kukwepa na kuzembea kujiandikisha na kupiga kura akisema, “Tusibaki
kusali tu kanisani wakati wengine wanakwenda kupiga kura…Hii ni hatari kwani
tukifanya hivyo tunawapa nafasi wasiofanya tafakari kama hii ya Neno la Mungu,
kuchagua viongozi wasiofaa na sisi tukabaki kulalalmika.”
Baada ya ibada hiyo iliyofanyika
Jumamosi iliyopita, WAWATA jimboni Dar es Salaam, waliwatembelea wagonjwa wa
saratani katika Hospitali ya Ocean Road na kuwapa misaada ya vitu
mbalimbali vyenye thamani ya takriban shilingi 3,500,000/=
Msaada huo ulihusisha, dawa za
meno, kanga, maziwa ya kopo, kandambili, miswaki na taulo.
Uongozi wa Hospitali hiyo
uliwashukuru WAWATA jimboni kwa moyo wao wa huruma na upendo kwa wagonjwa na
wenye shida mbalimbali.
Tanzania
iko katika vuguvugu la kuelekea katika UchaguziMkuu wa Rais, Wabunge , Madiwani
na Wawakilishi, unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Kumekuwapo
na matukio kadhaa yanayotishia amani ya nchi katika vituo kadhaa vya
kuandikisha wapiga kura hususan katika baaadhi ya maeneo ya Tanzania Visiwani.
Hali hiyo pamoja na
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vijiji uliofanyika Novemba mwaka jana,
umesababisha vifo vya watu takriban watatu jambo ambalo limeleta hofu kubwa kwa
Watanzania wengi.
Serikali
inaangamiza upinzani - Prof.
l
‘Ruzuku ingekuwa chanzo cha migogoro, CCM ingekufa’
Na Mwandishi Wetu
KITENDO cha Serikali kutoa ruzuku kwa vyama vya siasa vyenye
wawakilishi bungeni pekee, kimeelezewa kuwa ni mpango wa kuangamiza mfumo wa
vyama vingi nchini.
Mwanzilishi
wa Chama cha siasa cha Demokrasia MAKINI, Profesa Leonard Shayo
alisema jijini Dar es Salaam kuwa, utoaji wa ruzuku kwa ubaguzi unafanya sera
ya siasa ya vyama vingi nchini kuwa ya kinafiki na inayotishia kuviangamiza
vyama vichanga.
Shayo
ambaye ni Profesa wa Idara ya Hisabati na Komputa ya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaamu, alisema ni jambo la kushangaza kuona ‘Baba anamzaa mtoto lakini
unapofika wakati wa chakula anamuweka pembeni.’
“Serikali
ndiye baba wa vyama vyote na ilikubali mfumo wa vyama vingi, sasa inakuwaje
ishindwe kutoa ruzuku kwa vyama vyote vyenye usajili wa kudumu?” alihoji.
Alisema
uamuzi wa kutoa ruzuku kwa uwiano wa jumla ya wabunge, unaonesha dhahiri kuwa
unafanywa na serikali kwa nia ya kukipendelea chama kilichoshika madaraka kwa
kuwa kina wabunge wengi.
Profesa
Shayo alisema anashangaa kuona hata baadhi ya vyama vya upinzani eti navyo
vikakubaliana na suala hilo, bila kuangalia athari zake huko mbeleni.
“Ni mbinu tu ilitumika kuvibana vyama vingi
na kitendo cha vyama vingine kukubali kucheza mchezo wa siasa bila kuwa na
uwanja wa siasa kinaashiria uwezekano mkubwa wa kuwepo viongozi wa vyama
waliopandikizwa kuviendesha, ”alisema Profesa Shayo.
Alisema
vyama vya kweli vya siasa, ni lazima viendeshwe na nguvu za wananchi katika
utaratibu wa kulipwa ruzuku na kwamba, michango kwa vyama, inaweza kutolewa ama
na wanachama wa chama husika au vyama vya siasa vyenyewe.
Alisema
kukosekana kwa ruzuku kumepunguza jukumu la vyama vya siasa katika kuwaelimisha
wananchi na kutangaza sera, jambo ambalo si tu lingewapa mwanga wa kutambua ni
kipi chama kizuri, bali pia wangeweza kutambua waanzilishi wababaishaji na wale
wasio wababaishaji.
Hata
hivyo, amekanusha madai kwamba suala la migogoro ndani ya vyama linasababishwa
na ruzuku inayotolewa na serikali.
Aidha,
Profesa Shayo amewaasa wananchi kuwa makini na vyama vyenye migogoro na
kubainisha kuwa, wanapaswa kuangalia na kuichambua migogoro hiyo ili kujua kuwa,
inasababishwa na nini kabla hawajatoa maamuzi.
Alisema
huenda kuna njama zinazofanywa na baadhi ya watu, katika kuzua migogoro wakiwa
na nia ya kuvidhoofisha vyama vya upinzani.
“Migogoro
hii ichunguzwe kwa makini, inawezekana kabisa kwa kiongozi wa chama cha siasa
akawa kibaraka aliyepandikizwa kwa lengo la kudhoofisha chama chake na upinzani
kwa jumla, kwa maslahi ya aliyempandikiza,” alitahadharisha.
Akaongeza
kuwa, “Kama kugombania ruzuku kungekuwa ndiko chanzo cha migogoro, basi
migogoro mingi ingejitokeza ndani ya Chama Tawala ambacho ndicho chenye ruzuku
kubwa pamoja na raslimali nyingi.”
Amemshauri
Rais Mkapa kuwa, pamoja na kufanikisha mambo mbalimbali ya kimaendeleo katika
nchi hii, pia hana budi kulisimamia na kuliangalia upya suala hilo.
Alisema
hali hiyo itasaidia kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu kipate ruzuku
ambayo katika kipindi hiki kinachoelekea katika Uchaguzi Mkuu ili kitajikimu
katika kampeni.
“Ni
ndoto kutegemea chama kichanga kama cha Demokrasia MAKINI kueneza
sera zake kwa wananchi kwa kutegemea nguvu za wanachama peke yake,” alisema
Prof.Shayo.
Aliongeza
kuwa, “Watanzania wengi ni maskini kiasi kwamba wanashindwa hata kulipia kadi
zao za uanachama, sembuse kuchangia gharama za kuendesha chama!”
Makamu wa Mama Mkuu afariki
l Alizimia kwa miezi mitatu
Na Getruda
Kaninka, Sumbawanga
MAKAMU wa Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Maria
Mtakatifu Malkia wa Afrika, Sista Martha Ngua, amefariki
hivi karibuni, baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Sista Ngua alifariki kutokana na ugonjwa wa shinikizo la damu,
lililomsababishia kupooza na kisha kupoteza fahamu kwa muda wa miezi mitatu
kabla hajaaga dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya alikokuwa
amelazwa kwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa za shirika lake zilizolifikia Gazeti hili,
Marehemu Sista Ngua alianza kuugua mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka jana,
alipokuwa katika safari za kikazi katika Konventi ya Jimbo Katoliki la Mbeya.
Akihubiri wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya mazishi ya sista
huyo, Askofu wa Jimbo la Mpanda, Mhashamu Paskali Kikoti, alimwelezea Sista
Ngua kama mtu aliyejitoa kikamilifu na kwa moyo wote, kufanya kazi za utawa kwa
uadilifu, bidii na unyenyekevu mkubwa.
Mhashamu Kikoti alisema, marehemu atakumbukwa pia kwa jinsi
alivyokuwa mvumilivu hasa wakati wa magumu na kwa namna alivyojitolea
kuwahudumia watu mbalimbali kwa upendo, ukarimu na huruma bila ubaguzi.
Marehemu Sista Martha Ngua alizaliwa Januari 20,1937 katika
kijiji cha Matanga, Wilayani Sumbawanga katika Mkoa wa Rukwa, akiwa mtoto wa
kwanza kati ya watoto 11 wa mzee Alois Ngua na mama Marselina Nyika.
Baada ya masomo yake ya msingi, alijiunga na Shirika la Masista
wa Maria Mt. Malkia wa Afrika, Jimbo la Sumbawanga Desemba 8, 1954, akiwa kama
Mpostulanti. Miaka sita baadaye, aliweka nadhiri za kwanza, Novemba 21,1960.
Alipata kozi ya ualimu mwaka 1963, katika Chuo cha Ualimu cha
Ndala mkoani Tabora. Mwaka 1974 hadi 1977, alijiunga na shule ya sekondari
katika Seminari ya Kaengesa na kuhitimu vizuri.
Oktoba 25, 1970, Marehemu Sista Ngua, alijiweka wakfu kwa nadhiri
za daima. Alifanya kazi za kitume katika parokia mbalimbali kabla ya
kuchaguliwa kuwa Mama Mkuu wa Shirika tangu mwaka 1989 hadi 1995.
Aidha, alichaguliwa kuwa Makamu wa Mama Mkuu wa Shirika hilo
kuanzia mwaka 2001, na kushikilia nafasi hiyo hadi alipofariki Novemba 17,
mwaka jana. Mungu aiweke roho ya Marehemu Sista Martha Ngua mahali pema
peponi, AMINA