KATIKA HARAKATI ZA KUUKABILI UKIMWI

Askofu Balina ashauri wafunga ndoa watarajiwa kupimwa

Na Charles Hililla, Shinyanga

 Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki la Shinyanga ameshauri wanaotarajiwa kufunga ndoa kupimwa ukimwi kama njia ya kukabiliana na uwezekano wa kuambukizwa ugonjwa huo.

Askofu alisema kwamba njia hiyo ni salama zaidi kuliko matangazo ya kutumia kondom ambayo amesema kwamba si kinga ya kurejesha nyuma ukimwi.

Aidha alisema kwamba kondom hizo zina athari kubwa kwa watumiaji na zimetengenezwa kwa ajili ya biashara na siyo salama ya kujikinga na ukimwi.

Amesema kwamba licha ya kupima kwa wanandoa watarajiwa , wanandoa hao wasianze kujishughulisha na tendo la ndoa bila kupimwa na kupata baraka za kanisa.

Askofu Balina alisema kuwa njia ya kujikinga isiyokuwa na mashaka ni kuwa mwaminifu katika ndoa.

Kiongozi huyo wa dini aliyasema hayo siku ya ufunguzi wa warsha ya siku ya ukimwi, inayohusu ushirikishwaji wa jamii katika uendeshaji wa mpango wa kuthibiti ukimwi, Februari 2 mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano wa hosteli ya Jimbo hilo iliyopo Ngokolo mjini hapa.

Kwa upande wa malezi, Askofu huyo alishauri kuwa watoto yatima ni vizuri walelewe kwenye familia ili wapate maadili na utamaduni wa kifamilia badala ya kulelewa kambini, mahali ambapo alisema kuwa watoto wanakua na kulelewa kwa mila na tamaduni za kigeni.

Aidha jukumu la kupiga vita ugonjwa huo siyo la sekta ya afya peke yake bali ni la jamii nzima kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali naviongozi wa ngazi zote. Kwa ushirikiano huo tunaweza kupunguza kuenea kwa ugonjwa huo, alisema Askofu Balina.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 1997 taarifa zilizoripotiwa kitaifa zinaonyesha kuwa watu 103,185 walikuwa wameugua ugonjwa wa ukimwi tangu ugonjwa huo uingie hapa nchini mwaka 1983.

Idadi halisi inakisiwa kuwa watu 520,000 au zaidi hadi hivi sasa ni wagonjwa. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa kuna watoto yatima wapatao 720,000 hadi hivi sasa.

Mkufunzi wa warsha hiyo Ndugu George Kanga kutoka Idara ya Afya, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kitengo cha Ukimwi alitaja kuwa Umaskini ni chimbuko kubwa la kuenea kwa ukimwi katika maeneo mengi.

Ndugu Kanga aliziomba jamii zielimishwe na zikubali kuwasaidia wagonjwa wa ukimwi kama wago-njwa wengine kufuatana na msukumo wa Injili: "Nilikuwa mgonjwa mkaja kunitazama." [Mat.25:35].

Kwa upande wa Yatima Ndugu Kanga alishauri kuwa watoto wana haki ya kupata huduma za msingi kama Elimu na Afya. Njia hiyo inawezekana tu pale jamii itakapokubali kubadili tabia na kuwaona wagonjwa na mayatima wana haki sawa kama wagonjwa wengine.

Warsha hiyo iliyoandaliwa na Idara ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, imewakutanisha jumla ya washiriki 12 kutoka Majimbo ya Kanda ya Ziwa na Jimbo jirani la Kahama. Shirika la maendeleo la Kanisa Katoliki nchini Uingereza CAFOD ndio wafadhili wa warsha hiyo.

Lengo la warsha hiyo ni kupata watendaji kutoka majimbo yanayoshisriki ili wawe wakufunzi wa baadaye wa mbinu za ushirikishaji wa jamii katika kupambana na ukimwi katika sehemu zao.

Dini yaweza kuchanganywa na siasa-Pengo

Na Dalphina Rubyema, Arusha

MWADHAMA Polycarp Kardinali Pengo amesema kuwa haoni sababu ya dini kutochanganywa na masuala ya siasa kwa kile alichoamini kuwa viongozi wa dini wakiwafundisha waumini wao masuala ya kisiasa wanakuwa wamewasaidia kufahamu zaidi juu ya siasa yao, uchumi wao na uhuru wao.

"Kiongozi wa dini ni lazima awafundishe waumini wake masuala ya kiroho na jinsi ya kuishi katika nchi yake,kiongozi wa dini akizembea analeta maafa si kidini tu bali hata kijamii" alisistiza Kardinali Pengo

Akitoa nasaha zake katika sherehe za kusimikwa rasmi Askofu wa Jimbo la Arusha Josaphat Luis Lebulu,sherehe zilizofanyika hivi karibuni kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abed uliopo mjini Arusha,Kardinali Pengo alitoa wito kwa Askofu Lebulu kuwajibika kuwaongoza Waumini wa Arusha kiroho na kujamii ila alisisitiza kuwa Askofu huyo asiingilie kwa undanimasuala ya siasa kiasi cha kuwaingilia viongozi wa serikali.

"Sikwambii umwingilie Mkuu wa Mkoa na viongozi wa serikali,wewe shirikiana vizuri na waumini wako nao waumini wakutii wewe na hiyo kazi ya viongozi wa serikali waachie wenyewe wanajua jinsi ya kuifanya"alisema Kardinali Pengo.

Pengo ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Saalam alisema kuwa Askofu Josaphat Lebulu ni lazima ajihesabu kama mmoja wa wazaliwa wa mkoa wa Arusha na siyo mzaliwa wa Same tena ambapo alisema kuwa mchungaji mwema ni lazima ajihesabu mmojawapo wa kondoo anaowachunga.

"Wewe umezaliwa Upare lakini sasa umeletwa Arusha hivyo tangia leo unajihesabu kama mzaliwa wa Arusha tena Wamasai wamefurahi sana maana wao hawakuiti tena Lebulu na badala yake wanakuita Lobulu ambapo ukiitwa Lobulu unaonekana wewe ni Mmasai,huna tena pakupaita kwako bali kwako ni Arusha"alisema Kardinali Pengo.

Sherehe hizo pia zilihudhuliwa na Rais wa Jamuhuri Ya Muungano wa Tanzania ,Benjamin Mkapa,mkewe mama Anna Mkapa,Maaskofu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchini akiwemo Askofu Mkuu wa Jimbo la Nairobi,Raphael Mwananseki na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Afrika Mashariki na Kati(AMECEA),Padri Peter Lwaminda na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu katoliki nchini (TEC),Padri Method Kilaini.

Kabla ya kuhamishiwa Jimbo la Arusha,Askofu Josephat Lebulu alikuwa ni Askofu wa Jimbo la Same ambapo aliongoza Jimbo hilo kwa kipindi cha miaka ishirini kabla ya kuhamishiwa Arusha kama msimamizi wa Kitume .

Askofu Lebulu anachukua nafasi ya aliyekuwa askofu wa Jimbo hilo,Fortunatus Lukanima ambaye amestaafu.

NCCR Dar waamua kumjadili Marando

Na Mwandishi Wetu

 HALMASHAURI Kuu ya NCCR - Mageuzi ya mkoa wa Dar es Salaam, inakutana leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu Manzese Argentina mjini Dares Salaam ili pamoja na mambo mengine, kumjadili Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Mabere Nyaucho Marando kutokana na kile kilichoelezwa kuendeleza vurugu baada ya kurejeshwa madarakani na Mahakama Kuu ya Tanzania wiki iliyopita.

Habari zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya maofisa wakuu, zimethibitisha kuwepo kwa kikao hicho ambacho kitaongozwa na Mwenyekiti wa NCCR - Mageuzi wa mkoa huo, Bw. Hashim Seif Madongo na kimepangwa kufanyika kwa siku moja kuanzia saa nne kamili asubuhi leo.

Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa chama hicho mkoani humo, Bw. Charles Charles amesema kikao hicho cha dharura kimeitishwa maalum kwa ajili ya kuipitia hukumu nzima iliyotolewa na Mahakama Kuu kutokana na kesi iliyokuwa imefunguliwa na Bw. Marando dhidi ya Mwenyekiti wa Taifa, Bw. Augustine Lyatonga Mrema, kupinga kung'olewa kwake madarakani kulikofanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa Juni 21, mwaka juzi.

"Hili la kumjadili Marando mimi ndiyo kwanza nalisikia kwako. Ninachofahamu ni kwamba kikaohicho kinafanyika Jumamosi (leo) kwa ajili ya kuipitia hukumu nzima iliyotolewa na Jaji Laurean Kalegeya ili baadaye kitoe tamko la kichama kwa ngazi ya mkoa endapo itabidi", alisema.

Pamoja na hayo, habari za ndani zilizopatikana zimethibitisha kwamba Bw. Marando atajadiliwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa "vurugu" anazozifanya katika Makao Makuu ya chama hicho baada ya kurejea kwake kutoka "mafichoni" ya wiki iliyopita ambako alijichimbia kwa takribani miaka miwili tangu Mei 15, mwaka juzi.

Wakati huo huo, wanawake wote ambao ni wanachama wa NCCR - Mageuzi wanaoishi mjini Dar es Salaam na vitongoji vyake, wanakutana na Katibu Mwenezi wa chama hicho wa mkoa huo, Bw.Charles Charles katika Makao Makuu Manzese Argentina, leo asubuhi.

Mwenyekiti wa Kitengo cha Kina Mama wa NCCR - Mageuzi mkoani humo, Mama Rose Kuheka, aliliambia gazeti hili kuwa mkutano huo wa ndani utahutubiwa na Bw. Charles, lakini hakufafanua zaidi.

"Mimi sijui (Katibu Mwenezi) atazungumza nini, lakini ninachojua ni kwamba yupo kwenye ziara ndefu ya kutembelea majimbo yote saba ya mkoa huu pamoja na vitengo vyote vitatu vya chama", alisema, jambo ambalo pia limethibitishwa na Bw. Charles mwenyewe alipoulizwa juzi kwa simu kutoka ofisini kwake Mnazi Mmoja, Jijini.

Wapinzani wapanga kuchochea migomo

Na Seraph Kuandika

 Vyama vya siasa vya upinzani huenda vikaandaa migomo ya aina mbalimbali na maandamano nchi nzima iwapo serikali ya chama tawala cha CCM itaendelea na msimamo wake wa kutowakubalia juu ya haja ya kufanyika mkutano wa mabadiliko ya katiba ya nchi.

Aidha vyama hivyo vimesema kuwa mbali na kuandaa migomo na kufanya maandamano,pia watawasiliana na mataifa ya nje na kuyaomba yaishinikize Serikali juu ya kuwepo na umuhimu wa kufanyika mkutano huo wa katiba itakayoendana na matakwa ya wananchi .

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa vyama tisa vya siasa vya upinzani vinavyounda Kamati ya Mabadiliko ya Katiba (KAMAKA),Bw.Bob Makani,alipokuwa akizungumza na Kiongozi ofisini kwake jana kufuatia kauli ya Waziri Mkuu, Bw.Frederick Sumaye aliyoitoa Bungeni hivi karibuni kwamba uamuzi wa kuifanyia mabadiliko katiba umo mikononi mwa Bunge na sio vinginevyo.

Bw. Makani alisema kuwawapinzani hawatakubali kuona kuwa serikali inawaburuza kadri itakavyo, hivyo iwapo hali hiyo itaendelea hawatakuwa na namna nyingine ya kufanya isipokuwa kutafuta mbinu nyingine za kuishinikiza serikali ikubaliane na matakwa yao.

Alisema kuwa miongoni mwa mbinu hizo ni kuandaa migomo kwa wananchi na kufanya maandamano nchi nzima ikiwa ni pamoja na kuomba msaada kwa mataifa ya nje yaingilie kati suala hilo.

"Iwapo Serikali itakataa ombi letu la kufanyika kwa mkutano wa katiba, tutatafuta namna nyingine ya kuishinikiza serikali juu ya umuhimu wa kuwepo kwa suala hilo,"alisema.

Aliongeza kusema kuwa pamoja na serikali kupitisha waraka wake maalum "Whitepaper"na kuwataka wananchi kutoa maoni yao juu ya mabadiliko ya katiba kupitia waraka huo, hata hivyo alidai kuwa wananchi hawakubaliani na maoni ya serikali yaliyoko kwenye waraka huo.

Hata hivyo alisema kuwa iwapo juhidi zao hizo hazitazaa matunda, hawatasusa kushiriki uchaguzi mkuu ujao na badala yake watashiriki na wakishinda katika uchaguzi huo, watahakikisha kuwa katiba hiyo inabadilishwa.

Kamati hiyo ya mabadiliko ya katiba inatarajia kukutana mwishoni mwa mwezi huu na kwa mujibu wa Bw.Makani,l engo la kukutana huko ni kutaka kutathmini shughuli zake mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuona wamefikia wapi katika mpango wao wa kukusanya maoni kutoka kwa wananchi juu ya mabadiliko ya katiba.

 

Watatu wafa katika matukio tofauti Dar

Na Waandishi wetu

 WATU watatu wakazi wa Jijini wamekufa katika matukio tofauti yaliyotokea mwishoni mwa wiki hii .

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Dar es Saalam Bw, Alfred Gewe aliwataja waliokufa ni pamoja na mtoto mmoja wa Kihindi Kuship Ashan 12, ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Sharif Shamba ambaye aligongwa na gari aina ya Toyota Hiace yenye Namba za usajili TZC 8294 na kufa papo hapo katika barabara ya uhuru juzi majira ya jioni, ambapo dereva wa gari hilo amepatikana.

Aliendelea kusema kuwa katika barabara ya Mandela imeokotwa maiti ya mwanaume ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja akiwa uchi amekufa na walipochunguza katika mwili wake walikuta kidole chake cha mkono wa kushoto akiwa na jeraha ambalo alikuwa amefungwa na suruali yake na inasadikika kuwa alikuwa ni kibaka mzoefu katika maeneo hayo na bado haijafahamika aliyehusika na mauaji ya mtu huyo na mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa Muhimbili.

Kamanda Gewe alimtaja mtu mwingine aliyekufa kuwa ni Garus Gangwe (30), ambaye ni mkazi wa Segerea alikuwa katika machimbo ya mchanga yaliyopo Segerea

Kamanda Gewe aliongeza kusema kuwa mtu huyo alikutwa amekufa kwenye maeneo ya machimbo hayo, na pembeni yake walikuta Sululu, Jembe na mfuko wa kiloba na haikuweza kufahamika mara moja kifo chake kimesababishwa na nini. Mwili wa marehemu huyo umepelekwa Muhimbili kuhifadhiwa.

Mbegu za Tanseed hazishikiki

Na Said Mmanga, Morogoro

 Wilaya ya Morogoro bado haijapokea aina yoyote ya mbegu za nafaka kwa ajili ya kuwagawia wananchi wa wilaya hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi.Hawa Ngulume alitoa taarifa hiyo hivi karibuni alipokuwa akiongea na gazeti hili ofisini kwake kuhusiana na hali ya mbegu na upatikanaji wake wilayani humo.

Bi.Ngulume alisema wananchi hawana budi kujikimu na kununua mbegu kutoka kampuni ya mbegu Morogoro ingawa bei ya mbegu hasa ya mahindi katika ghala la kampuni hiyo hado ni kubwa, lakini hawana budi kununua hadi ofisi yake itakapofanikiwa kupata mbegu.

Hivi sasa bei ya mbegu katika ghala la Tanseed kwa ujazo wa kilo moja inauzwa hadi kufikia shilingi 850/= Kwa mbegu aina ya 'star' na shilingi 950/= kwa kilo ya mbegu za mahindi aina ya 'kito'.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema ofisi yake tayari imewasiliana na kampuni ya Tanseed ya Morogoro, ili iweke punguzo la bei kuwasaidia wananchi hasa katika kipindi hiki ambacho mkoa unakabiliwa na baa la njaa.

Wakati huo huo tani 25 za chakula cha msaada kutoka ofisi ya waziri mkuu kwa ajili ya watu wanaokabiliwa na njaa mkoani Morogoro kimeanza kusambazwa.

Chakula hicho cha msaada kinasambazwa katika wilaya za Morogoro vijijini, Kilosa, Ulanga, vijiji vya Ifakara na wilaya ya Kilombero, Wilaya ya Morogoro mjini imeondolewa kwenye mgao huo kutokana na kuwa na wananchi wengi wenye uwezo.

Awali Wilaya ya Morogoro vijijini ilipata tani 30 za chakula kutoka ofisi ya waziri mkuu kwa ajili ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa.

Wanakijiji watakiwa kushirikiana kusomesha watoto

Na Josephs Sabinus, Kisarawe

Wakazi wa kijiji cha Gumba katika kata ya Masaki tarafa ya Sungwi wilayani hapa, wametakiwa kushirikiana kuwasomesha watoto ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwapeleka shule badala ya kusadiana katika ngoma na mambo ya posa.

Wito huo ulitolewa na mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Bw. Mwinyimageli Goma alipokuwa akimkaribisha mkuu wa wilaya ya Kisarawe Kapteni James Yamungu katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika shule ya msingi Gumba Jumatano iliyopita.

Katika mkutano huo , Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi hao kushiriki kikamilifu katika mradi wa ujenzi wa vyumba sita vya madarasa ya kudumu shuleni hapo unaofadhiliwa na shirika la kimataifa la PLAN INTERNATIONAL ambalo linaaendesha ujenzi wa shule katika vijiji vya Kisanga, Gumba na Homboza ambapo wazazi wa maeneo hayo wanatakiwa kuchangia nguvu zao katika shughuli kama uchimbaji wa mchanga na ufyatuaji wa matofali.

Goma alisema wazazi hawana budi kutambua umuhimu wa elimu hasa katika kipindi hiki ambacho ulimwengu mzima unaingia kwa vishindo katika karne ya 21 ya sayansi na teknolojia. "Saidianeni ili watoto wa wazazi ambao hawana uwezo; wasome.

Aliongeza kuwaomba washirikiane katika mambo ya elimu na siyo katika kucheza ngoma za unyago na kusoma barua za posa tu."

Alisema kuwa elimu katika wilaya ya Kisarawe inashuka kwa kuwa bado wazazi hawajatambua umuhimu wake na kwamba bado wapo wenye imani potofu zilizopitwa na wakati.

"Hivi kweli unaacha kumwandikisha mtoto shule; eti kwa kuwa jina lake litakwenda kuuzwa Ulaya?"Alihoji kwa mshangao.

Mwenyekiti huyo aliwahimiza kufuata uzazi wa mpango ili waweze kumudu gharama za kuwahudumia watoto wao ipasavyo.

"Zaeni kwa malengo ili muwasomeshe watoto na kuwapa haki zao za msingi. Msiwe hodari wa kuzaa tuu hali mnashindwa kuwapa watoto wenu elimu", alikazia.

Awali katia risala ya serikali ya kijiji kwa mkuu wa wilaya iliyosomwa na afisa mtendaji wa kijiji hicho Bw. Abdalahakimu Salimu, serikali hiyo ilisema ni watoto 30 tu; kati ya 70 waliotarajiwa kuandikishwa kuanza darasa la kwanza mwaka huu.

Hata hivyo ni watoto 4 tu kati ya 255 wa shule hiyo waliokwishalipa mchango wa UPE ambao ni shilingi 2000/= kwa mwaka. Risala hiyo ilizidi kusema kuwa wazazi hao wanadai hawawezi kumudu gharama za shule ikiwa ni pamoja na mchango wa UMITASHUMTA shilingi 1000/= na ule wa madawati wa shilingi 1000/=

Mkuu wa wilaya alitoa agizo kwa wazazi ambao hawajaandikisha watoto wao wawe wamefanya hivyo ifikapo Februari 8 na wale ambao hawajalipia mchango wa UPE , wafanye hivyo hadi ifikapo mwisho wa mwezi huu vinginevyo watafikishwa mahakamani.

UDEA yaweka mikakati ya kuendeleza Uru

Na Gloria Tesha, Moshi

 Chama kisicho cha kiserikali (UDEA) Uru Development Association kimeweka mikakati ya kuimarisha maendeleo ya uchumi katika Kata za Uru Moshi Vijijini, Mkoani Kilimanjaro.

Akizungumzia mikakati hiyo pamoja na malengo haswa ya chama cha UDEA mwanzoni mwa wiki hii ,Mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kilimanjaro Internation Technology(K.I.T) Mkoani Kilimanjaro Bw. Onesmo Ngowi alisema kukua kwa maendeleo kutakuwepo kama umoja uliopo utadumishwa.

Alisema pamoja na malengo hayo ya kuendeleza Kata za Uru Kielimu, kilimo, matibabu na biashara pia kutakuwa na Tamasha maalumu litakalofanyika mwishoni mwa mwaka huu ili kukichambua kwa undani chama chao na kilipofikia.

Alisema Tamasha hilo pia l itawashirikisha Wana-Uru wote walioko nje ya Mkoa na nje ya nchi ili kujua maendeleo gani yamefanyika na yanayohitajika katika Kata zao.

Allisema uongozi uliopo Moshi hivi sasa umeteuliwa na Wanakamati wa Dar-es-Salaam kuwa wa muda ili kukidhi mahitaji na ikiwa ni pamoja na vikao muhimu vya hasa kwa Moshi ambapo ndipo kwa walengwa.

Bw.. Ngowi alisema UDEA ni chama kidogo tu cha kabila la Wachaga wa Uru na kimeanzishwa takribani miaka miwili iliyopita Mkoani Dar-es-Salaam na mwaka jana ndipo kilipoanzishwa Moshi.

Mwenyekiti huyo alisema mwezi huu tarehe 28 katika ofisi za K.I.T Moshi watakuwa na kikao na Kamati nzima ya Moshi pamoja na Makatibu Kata na Tarafa wa vijiji vya Uru ili kuichambua Katiba ya chama hicho.

Shule ya watoto walio na mtindio wa akili yaanzishwa Jijini

Na Neema Dawson

SHULE ya kulelea watoto walio na mtindio wa akili imeanzishwa katika shule ya Msingi Mbagala Kizuiani ,Temeke,Jijini ambayo inatarajia kuwa na watoto zaidi ya 30 kutoka maeneo mbalimbali,ndani na nje ya Mkoa wa Dar Es salaam.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Kurusumu Ngalawa, amesema kuwa hadi sasa majengo ya shule hiyo iliyofadhiliwa na Bw.George Ally wa TANCONCERT, yameishakamilika na wameaanza kuandikisha wanafunzi.

Mwalimu huyo alisema msaada uliotolewa na mfadhili huyo umefanikisha ujenzi wa vyumba vinne ,jiko,choo pamoja na chumba cha chakula.Hata hivyo alisema kuwa bado wanahitaji msaada zaidi kwa ajili ya kuweza kukidhi mahitaji ya wanafunzi shuleni hapo.

Alisema kuwa shule hiyo tayari imeshapata mwalimu mmoja kwa ajili kuwafundisha watoto hao walemavu.Hata hivyo alisema kuwa juhudi zinafanyika kutafuta walimu wengine .

"Msaada tulioupata kutoka kwa Bw, George ni mkubwa sana ingawa bado tunahitaji misaada mingi ili kuweza kuendeleza ujenzi wa majengo mengine zaidi kwani wanafunzi hao wanatakiwa wawe wanalala shuleni hapo na hii itakuwa ni njia mojawapo ya kuweza kuwasaidia watoto hao walemavu kwa kiasi kikubwa sana". alisema Mwalimu mkuu wa shule hiyo.

Akatwa vidole katika purukushani na mume wa 'mtalaka' wake

Na Dalphina Rubyema

 MKAZI mmoja wa Makondeko wilayani Kinondoni,Bw.John Msabaha (32) ameumizwa kwa kukatwa vidole viwili vya mkono wa kushoto na aliye mfanyia kitendo hicho ni mme mwenzake aliyemtaja kwa jina la Called Paulo.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi hivi karibuni nyumbani kwake,Bw.Msabaha alifanyiwa kitendo hicho baada ya kumfumania mke wake wa ndoa aliyemtaja kwa jina la Jane William akifanya ngono na Bw.Paulo ambapo baada ya kumuuliza mke wake anafanya nini ndipo Bw.Paulo aliposhika kisu na kumkata nacho.

"Mimi ni mke wangu wa ndoa nimemfumania akifanya tendo la ndoa na mwanamme mwingine na nilipomuuliza anafanya nini ndipo huyo mume mwenzangu aliposhika kisu na kunikata vidole vyangu"alisema Bw.Msabaha.

Hata hivyo Mwandishi wa habari hizi alipomuuliza Bibi Jane kuhusu tukio hilo,Bibi Jane alisema kuwa ni kweli kwamba Bw.Msabaha alikuwa mme wake wa ndoa lakini hivi sasa wameisha tengana tayari na siku ya tukio yeye (Msabaha) alimfuata nyumbani kwake na alipofika alimkuta mwanamke huyo akiwa na Bw.Paulo ndipo Msabaha alipoanza kufanya fujo.

"Mimi nilisha tengana naye,alinifuata nyumbani kwangu na kuanza kunifanyia fujo baada ya kunikuta na bwana mwingine"alisema Bibi Jane.

Hata hivyo tukio hilo lilifishwa kwenye Mahakama ya Mwanzo Magomeni ambapo Mlalamikaji wa Kwanza ni Jane ambapo anamshtaki Msabaha kwa kosa la kumshambulia na shitaka la pili Mshtakiwa ni Paulo ambapo akakabiliwa na shtaka la kumjeruhi Msabaha.

Kesi zote mbili zipo mbele ya hakimu wa Mahakama hiyo Bibi Marry Matoi na Msoma mshtaka ni Konstebo wa Polisi Thobias Anselemo ambapo ilidai kuwa Washtakiwa wote wawili walitenda makosa yao Januari 18 mwaka huu sa 4.00 usiku katika eneo la Makondeko.

Paulo yupo nje kwa dhamana na Msahaba alirudishwa rumande kwa kukosa mtu wa kumtolea dhamana ambapo kesi hiyo itatajwa tena Februari 15 mwaka huu.