ILI WAWEZE KUFANYA MAZOEZI

Jeshi lavurumisha raia

lMashamba na majumba yaachwa bila ulinzi

lMifugo ya sambaratika, mazao yaharibiwa

Na Mwandishi Wetu

WANAKIJIJI wa Ngobanya nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam wamejikuta wakiwa katika wakati mgumu baada ya mifugo na mazao yao kuharibiwa na wanyama wa pori, baada ya kutimuliwa kwa muda na askari jeshi waliotaka kufanya mazoezi ya kivita katika eneo karibu na kijiji hicho.

Mazoezi hayo yalifanyika kwa siku tano.

Habari zinasema kwamba raia walipewa amri ya saa kuhama ghafla katika eneo hilo muda wa saa 12. jioni amri ambayo ilidumu hadi asubuhi yake.

Amri hiyo ilishinikizwa utekelezaji wake na maafisa polisi wa jeshi ambao walizunguka na 'kuwashughulikia' watu wasiotii amri.

Katika mazoezi hayo risasi za moto na mizinga ilitumika .

Habari kutoka katika serikali ya kijiji zimesema kwamba kitendo cha askari hao kuwatimua wananchi na kushughulika na mazoezi yao, kulisababisha mifugo mingi ya wanavijiji kupotea au kuliwa na wanyama pori. Mifugo hiyo ni pamoja na kuku, mbuzi, ngo'ombe na bata.

Aidha amri hiyo ambayo inadaiwa inakwenda kinyume na taratibu zilizoidhinishwa na serikali kuhusiana na mazoezi ya kivita maeneo karibu na raia, na pia kauli ya Luteni Makamba kwamba wanajeshi wasiingie katika eneo hilo kwa mazoezi aidha wanyama waharibifu kama nguruwe na nyani walitamba katika mashamba kwa kukosekana ulinzi kwenye mashamba hayo.

Wakazi hao wakizungumza na kiongozi wamesema mazoezi hayo ya kivita yaliyofanywa na JWTZ yamewatia hasara kubwa wanavijiji wa eneo hilo hasa baada ya kulazimika kuondoka kwa ghafla katika eneo hilo.

Wakazi hao wamesema askari hao walitoa taarifa kwa makeke na maguvu na kuwatimua wakati wa eneo hilo huku wakidai kuwa wao wapo katika mazoezi na hivyo hawataki kuwaona watu karibu.

Eneo hilo ambalo kwa sasa linamilikiwa na wanakijiji wa kijaka ambao wanamifugo na mazao katika mashamba yao inasemekana awali karibu yao lilikuwa ni eno la mazoezi ya kijeshi kabla ya serikali ya mkoa kuruhusu wakazi kujisogeza zaidi.

Aidha wapo vijana ambao waliona nafasi na wakapatiwa eneo la kupiga kambi ambao wanajishughulisha na kilimo cha mihogo.

Mwenyekiti wa serikali Peter Kaboja alipohojiwa kuhusu amri hiyo ya kijeshi ambayo ililazimisha familia kadhaa kuondoka katika maeneo yao na kupata hifadhi kwa majirani zao, alisema kwamba yeye hana la kufanya kwa kuwa ni amri ya kijeshi na yeye hawezi kuiuliza.

Wanavijiji waliohojiwa walisema kwamba wanajeshi wanalo sehemu jingine mbali na kijiji hicho ambalo linaweza kutumiwa bila athari na wakashindwa kuelewa kwa nini walitumia eneo hilo la karibu na raia.

Eneo ambalo lilitajwa ni la Golani ambako ni mbali na maeneo ya mpaka na kijiji cha Ngobanya kilichopo katikati ya Kigamboni taraja ya Kimbiji.

Mazao ambayo yaliharibiwa ni pamoja na muhogo, viazi ndizi na miwa. Uharibifu huo umefanyika huku hali ya chakula ikionekana kutokuwa njema.

Aidha watu wengine waliporejea katika maeneo yao baada ya siku tano walikuta matanuri yao ya mkaa yamefunuliwa na mkaa kuibiwa.

Juhudi za kumpata msemaji wa jeshi kufuatilia manung'uniko ya wakazi hao, zilishindikana kwa kuwa msemaji mkuu yuko ughaibuni kikazi na msaidizi wake ingawa awali kwenye simu aliahidi kulifanyia kazi suala hilo na kutujibu hakuweza kufanya hivyo na haikuwezekana kufahamika mara moja ni kwa nini kila alipopigiwa siku alidaiwa kwamba hayupo ofisini.

'Vikongwe kuendelea kuuawa mpaka watakapoacha uchawi'

lRamli yadaiwa kuonyesha kuwa wao ni wachawi

NaSadick Mgonja

JUMLA ya wazee tisa huuawa kila mwezi mkoani Shinyanga, kutokana na imani za uchawi ambazo huchochewa na waganga wa jadi na vijana wanaohusika wamesisitiza kwamba vikongwe hao wataendelea kuuawa hadi hapo watakapoiacha tabia hiyo.

Taarifa iliyotolewa jana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Nchini (TAMWA), inaonyesha kuwa kila wanawake watatu mkoani humo mmoja anahukumiwa kifo na makundi ya vijana wanaojulikana kwa jina la 'panga panga', na wanaishi katika hali ya wasiwasi wakisubiri siku ya kufa .

Aidha taarifa hiyo inasema wazee mkoani humo wengine huuawa na watoto wao wenyewe kutokana na matokeo ya ramli za waganga wa jadi.

Asilimia 90 ya waliohojiwa wanasema kuwa wanaamini mauaji kwa akinamama wazee ni halali kwa kuwa wanahusika na mauaji mbalimbali yanayotokea mkoani humo.

"Kwa maana hiyo vijana mkoani Shinyanga wanahitimisha kuwa, wanawake wazee wanastahili kuuawa hadi watakapoacha vitendo vya uchawi na kuua watu wengine.

Na wanahoji kuwa, kama wanawake wazee sio wachawi kwa nini waonekane katika ramli kuwa ni wachawi?" inasema sehemu ya ripoti hiyo .

Takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani zinaonyesha kuwa ,kati ya mwaka 1994 hadi Septemba 1998 jumla ya matukio 5,138 yaliripotiwa na kati ya hayo 1,369 au asilimia 16.8 yalitokana na imani za uchawi.

Watu 100 mbaroni Dar

Na Neema Dawson

 POLISI Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wamefanikiwa kuwakamata wahalifu zaidi ya 100 katika sehemu mbali mbali hususani kwenye vituo vya mabasi ikiwa ni njia mojawapo ya kupambana na vitendo vya uhalifu.

Hayo yalisemwa jana ofisini kwake na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Bw. Buka Kibona kuwa hali ya wimbi la ujambazi na uporaji limekuwa ni tishio na hivyo polisi wameamua kufanya msako ili kuweza kupambana na wahalifu na kuwachukulia hatua za kisheria.

Bw. Kibona aliendelea kusema kuwa polisi walisambazwa katika vituo mbalimbali hususani vya mabasi na daladala ambapo katika wilaya za Kinondoni na Ilala, walifanikiwa kukamata wazururaji 105 ambao walikutwa wakiwa katika vituo mbalimbali bila kuwa na kazi muhimu, ambapo zoezi hilo limeendelea katika Wilaya ya Temeke maeneo ya Keko na Tandika wamekamatwa wazururaji 40.

Aliendelea kuelezea kuwa zoezi hilo litaendelea siku hadi siku ili kuweza kupunguza wimbi la ujambazi na uhalifu ambalo lilikuwa likikua siku hadi siku, mbali na hayo Bw. Kibona alisema kuwa katika zoezi hilo pia polisi walifanikiwa kukamata Lita 110 za gongo, bangi misokoto 50 pamoja na madawa ya kulevya kete 17 ambapo alisema kuwa watuhumiwa hao wote wanatakiwa kufikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka .

Alisema kuwa polisi watajitahidi kuweka masako mkali ili kupunguza msongamano wa watu hasa katika vituo vya mabasi ambao wanakuwa si wasafiri wala hawana shughuli maalumu wanazokuwa wanafanya zaidi ya kuwaibia na kuwapora wasafiri.

Serikali ifunze walimu wa shule za awali- Balozi

Na Neema Dawson

BALOZI wa Nchini Romani Bw. Ioan Buner ameitaka Serikali kwa ujumla kuwapa kipaumbele walimu wote wa shule za awali waliopo nchini ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo na semina mbalimbali ili wamudu kazi yao.

Balozi Ioan aliyasema hayo akiwa ni mgeni Rasmi katika mahafali ya watoto 17 wa shule ya awali Mombasa Nursery and day care Centre iliyopo kitongoji cha Mombasa Ukonga Jijini, ambao tayari umri wao umepita na wanatarajia kuanza darasa la kwanza Januari Mwakani.

Aidha balozi huyo alimpongeza Mwenyekiti wa shule hiyo Bibi , Rita Kabati na wazazi kwa ubunifu na uhodari kwa kuanzisha shule hiyo ya awali.

Balozi huyo aliahidi kushirikiana kikamilifu na kutoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kusomeshea na kuchezea.

Aidha alisema atahakikisha ubalozi wake unatoa basi jingine dogo kwa ajili ya kusafirisha walimu wa shule hiyo na wafanyakazi wangine kuwaleta shuleni na kuwarudisha nyumbani

Serikali yatakiwa kutoipuuza idara ya Kazi

Na Lucas Mlekeafike Ndanga, Mbeya

 SERIKALI imeombwa kutoipuuza idara ya kazi nchini na kuiacha kama vile haina mwenyewe kwa sababu ina muhimu wake katika kipindi hiki cha mpito kutoka ujamaa kwenda ubepari au ubinafsishaji.

Hayo yameelezwa na baadhi ya wafanyakazi wa Idara hiyo wa mkoani Mbeya katika mazungumzo kati yao na Waziri wa Kazi Mheshimiwa Paul Kimiti alipofanya ziara mkoani hapa kuona hali halisi inayowakabili wafanyakazi mkoani hapa

Baadhi ya wafanyakazi hao wameeleza kuwa kuna vitendo vya wazi vya kuipuuza idara hiyo kwa sababu imefutwa ngazi ya mkoa na kuwatelekeza maafisa wa kazi wa idara hiyo.

Wafanyakazi wamedai kuwa serikali isiposimama kidete kutoka ujamaa kwenda ubinafsishaji kuna hatari maslahi ya wafanyakazi yakadhoofishwa na nguvu za kibepari kwa vile kwa asili ubepari una sumu ya unyonyaji na ukandamizaji.

Mapema waziri Kimiti alipozungumza na wafanyakazi hao ameahidi kuziangalia upya sheria za kazi zilizopitwa na wakati.

Polisi Moro hutia mbaroni watu 150 kila siku

Na Said Mmanga, Morogoro

 WATU 150 hukamatwa na polisi kila siku mkoani Morogoro kutokana na makosa mbali mbali.

Akiongea na gazeti hili ofisini kwake kamanda wa Polisi mkoani hapa Bw. Christopher Shekiondo alisema watu hao hukamatwa katika kampeni kabambe ya kupambana na uhalifu inayoendeshwa na jeshi la polisi mkoani hapa.

Bw. Shekiondo alisema kampeni hiyo imepata nguvu zaidi baada ya wanamgambo waliomaliza mafunzo hayo kuungana na jeshi hilo katika kuendesha doria pamoja na kufanya msako katika maeneo yaliyokithiri kwa vitendo vya uhalifu.

Alisema kati ya watu hao ambao hukamatwa kila siku kati ya 40 au 50 hufikishwa mahakamani kujibu mashitaka mbali mbali yanayowakabili.

 

Ombaomba wa Dar wasema utawala wa Makamba heri wa kikoloni

Na Sadick Mgonja

 OMBAOMBA waliopo Jijini wamesema utawala wa mkuu wa Mkoa wa Dar Es salaam, Luten Yusuf Makamba hautofautiani na ule wakoloni walioitawala Tanzania kabla ya uhuru.

Akiongea naMwandishi wa habari hizi hivi karibuni anayejidai kuwa mwenyekiti wa jumuiya ya omnbaomba Mzee Nuhu Msirikali Mazengo, alisema kuwa ameshangazwa na kauli ya kinyama iliyotolewa na Mkuu huyo wa Mkoa ya kuagiza kukamatwa kwa watu wote wanaotoa fedha kuwasaidia .

Mzee Mazengo ambaye ana makao yake Mnazi mmoja jijini karibu na Benki ya NBC 97, alisema kuwa wao wanamuona Makamba kama kiongozi mnyama kuliko wote waliokaa madarakani tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanzania mwaka 1961.

"Kinachotushangaza sisi ni kuwa mkuu wa mkoa ambaye amepiga marufuku tusipate msaada wowote hajawahi kutuita kuongea na sisi hata kama anaamini kuwa sisi ni wahalifu,huu ni uvunjaji wa haki za binadamu na umma hawezi kuukubali" alisema mzee Mazengo.

Alisema kuwa amri ya kufungulia mashitaka mtu anayemsaidia mtu mwingine kwa hiari yake mwenyewe haikuwahi kutekelezwa hata enzi za utawala wa kikoloni hivyo Mkuu huyo wa mkoa atakuwa amefungua ukurasa mpya wa kihistoria

Mzee mazengo anasema alipata wadhifa wake wa uwenyekiti wa jumuhiya ya omba omba huko Dodoma tangu mwaka 1971, na alipohamia Dar Es salaam, mwaka huo huo aliendelea nao hadi leo na ndio unaompa uwezo wa kuwatetea wenzake zaidi ya 5000 waliopo hapa jijini .

Hata hivyo alisema kuwa yupo tayari kukutana na Mkuu wa Mkoa na kuzungumza naye kutafuta ufumbuzi wa wao kuwepo hapa mjini kwani wanafahamu kuwa wanaharibu mazingira , lakini wanalazimika kuwepo kwakuwa wanahitaji kuishi kama yeye Mkuu wa Mkoa anavyoishi na hawana njia nyingine ya kufanya.

KDCU yapanga mikakati kujinusuru

Na Mwandishi wetu,Karagwe

 UONGOZI wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilayani Karagwe - KDCU Ltd. hivi karibuni kimejiwekea mikakati ya kunusuru chama hicho kinachokabiliwa na hali mbaya ya biashara kutokana na ushindani mkubwa kati yake na Makampuni mengi ya ndani na nje ya nchi wakiwemo hata walanguzi wanaonunua kahawa kimagendo na kuisafirisha nchi jirani.

Hatua ya kwanza iliyochukuliwa na Halmashauri Tendaji ya KDCU ni kuchagua watendaji waandamizi wapya kuendesha chama hicho kilichoachwa katika hali mbaya sana kifedha na uongozi uliotimuliwa kazi mwaka uliopita.

Wataalamu na Watendaji wapya waliochaguliwa na Halmashauri mpya chini ya Mwenyekiti Bw. Nekemiah Kazimoto, ni Bw. Simeon Byamungu ambaye alipewa wadhifa wa Meneja Mkuu na Bw. Clement Nsherenguzi Afisa utumishi na Utawala.

Wengine ni Meneja Masoko Bw. Tobias Itegereize na Bw. William Kiiza anayeongoza timu ya Wakaguzi wa Ndani.

Mtendaji wa Zamani aliyebaki katika wadhifa wa juu katika KDCU Ltd. ni Bw. Onesmo Rushokana aliyekuwa ameshikilia kiti cha kaimu Meneja Mkuu baada ya wanachama kumwondoa Bw. Andrew Kakama na timu yake amepewa nafasi ya Mhasibu Mkuu.

Hatua ya pili ni KDCU kubana matumizi kwa kupunguza marupurupu ya Wana-Halmashauri na Wafanyakazi.

Kutokana na hatua hizo Chama cha KDCU Ltd. Kitaweza kupunguza matumizi yake kwa kiasi cha zaidi ya sh. milioni 60 kwa kipindi cha msimu wa 98/99.

Aidha KDCU Ltd. inapanga kujenga Wilayani Karagwe Kiwanda cha kukobolea kahawa ambacho kinaweza kupunguza gharama za kusafirisha kahawa kukobolewa Bukoba Mjini, wananchi watapata ajira, na kiwanda hicho kitaharakisha ukoboaji wa kahawa na pia kinaweza kuingiza mapato ya KDCU Ltd. kwa kukoboa kahawa ya Makampuni ya wanunuzi binafsi.