Afunga ndoa ya pili kwa siri kanisani

Mkazi mmoja wa Sinza jijini Dar es Salaam amefunga ndoa ya pili na mwanamke mwingine hivi karibuni katika Kanisa la Kianglikana Kibaha,mkoani Pwani, huku akiwa na ndoa halali aliyoifunga katika Kanisa Katoliki la Ilula mkani Iringa Septemba 23,1984.

Kwa mujibu wa habari ambazo Kiongozi imezipata na kuthibitishwa na Mchungaji wa kanisa hilo Canon M. Y. S. Machoyo, ndoa hiyo ilifungwa Desemba 12, mwaka jana maharusi hao kupewa cheti cha ndoa Nambari L.A.N. 020693.

Hata hivyo Mchungaji Machoya amesema alifungisha ndoa hiyo kwa kuamini maelezo toka kwa ndugu wa Bwana harusi kwamba hakuwa na mke wa ndoa wala watoto.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikina kutoka kanisani hapo, Mama mzazi wa Bwana harusi, na dada yake aitwaye (majina tunayahifadhi) ndio waliofanya njama na kumhadaa mchungaji wao wakishirikiana na watu wengine wawili.

Baada ya mbinu hizo za uwongo kufichuka Canon Machoya ameanza kuwachukulia hatua kali watu walioshiriki kumdanganya ikiwa ni pamoja na kuwanyima kushiriki Sakramenti Takatifu ya Meza ya Bwana.

Bwana harusi huyo Bw.Venance. Mtatifikolo imeelezwa alifunga ndoa na Bibi Stella Luhanga, katika Kanisa la Katoliki la Ilula mkoani Iringa, Septemba 23, 1984 na kupewa cheti cha usajili wa ndoa Nambari L.M. 291 Ilula, kulingana na kumbukumbu zilizopatikana.

Katika maelezo yake Canon Machoya alieleza kusikitishwa kwake na kitendo cha Bwana Mtatifikolo na ndugu zake cha kusema uwongo kisha kufunga ndoa mara ya pili na kusema kuwa huo ni uvunjaji wa maadaili ya kanisa lake pia kinyume kabisa na mapenzi ya Mungu.

Katika waraka wake aliomwandikia Mchungaji wa Kanisa la Anglikana, Paroko wa Parokia ya Ilula amesema ndugu huyo apewe onyo kali kutokana na vitendo hivyo ambavyo vinalidhalilisha kanisa la Mungu.

Bw. Mtalifikolo ambaye ni dereva katika kampuni binafsi ya uchakuzi ya (Igesa Line) ya jijini, alipofuatwa na mwandishi wa habari hizi alikataa kusema lolote kuhusiana na kisa hiki.

Watu waliokaribu na Bwana Mtalifikolo wamethibisha kuwa alifunga ndoa na Bi. Kihampa ambaye ni mfanyakazi wa Magereza jijini na kwamba kwa sasa Bibi Kihampa ni mwanfunzi wa mwaka wa pili katika chuo cha uhasibu (DSA), mkoani Mtwara.

Kwa mujibu wa Bibi Luhanga ambaye ni mke wa kwanza wa Bwana Mtalifikolo, mume wake huyo aliamua kufunga ndoa nyingine kufuatia kuvunjika kwa ndoa halali mwezi Aprili 1998. Kwa sasa Bibi Luhanaga naishi Iringa na watoto watatu ailozaa na Bwana Mtatifikolo.

Ang'olewa na polisi katikati ya ibada kwa kughushi hati

POLISI wilayani Karatu jumamosi iliyopita waliingia ndani ya Kanisa la moja la Wasabato wilayani humo wakati waumini wakiwa katikati ya ibada na kumtia mbaroni muumini, kisha wakaondoka naye. Afisa mmoja anayeshughulikia maadili ya polisi amesema sio sahihi kumkamata muumini akiwa ndania ya nyumba ya ibada, ila yafaa asubiriwe amalize ibada.

Kukamatwa kwa muumini huyo Bw. Christian Ani, kunafuatia kesi iliyofunguliwa mahakamani na Bw. Simon Hando, ambaye anadai aliikodisha shamba kampuni ya Safari Junction kwa shilingi laki nne kwa miaka saba, lakini kampuni hiyo ambayo Bw. Ani ni Meneja wake imeghushi hati ikidai imelinunua shamba hilo.

Kesi hiyo iliyokuwa imefunguliwa katika Mahakama ya Mwanzo Karatu, imehamishiwa katika Mahamaka ya Wilaya ya Karatu baada ya kampuni ya Safari Junction kuomba ihamishiwe huko.

Sambamba na tukio hilo pia Mwenyekiti wa Kijiji cha Jeykrum wilayani humo Bw. Raphael Slako amefutiwa mashtaka ya kutoroka chini ya ulinzi halali wa polisi yaliyokuwa yakimkabili katika Mahakama ya Mwanzo ya Karatu. Mwenyekiti huyo anadaiwa kushirikiana na kampuni ya Safari Junction kughushi hati za kumiliki ardhi.

Akisoma hukumu juu ya kesi hiyo Aprili 21, mwaka huu, Hakimu wa Makahama hiyo ya Mwanzo Patrick Maligama, alisema mazingira ya tukio hayatoi ushahidi wa kutosha kwamba Bw. Slako alitoroka chini ya ulinzi halali wa polisi.

Awali Msoma mashtaka wa polisi alisema Bw. Slako alijaribu kutoroka chini ya ulinzi halali wa polisi wakati alipokuwa akipelekwa mahabusu iliyoko nje ya Mahakama ya Mwanzo ya Karatu ambapo akiwa ameshafika umbali wa kama mita 200 polisi walipiga filimbi na kumfanya ageuke na kurudi.

Shule za Chekechea zisianzishwe 'kuganga njaa' - Pengo

MWADHAMA Polycarp Kardinali Pengo amelaani vikali mtindo wa baadhi ya watu na vikundi mbalimbali vikiwemo vya dini kuanzisha vituo vya kulelea watoto wadogo na kwa moyo wa tamaa kwani watoto wanaweza kuambukizwa tamaa na hivyo kujenga kizazi kijacho cha wenye tamaa na matapeli.

Akifungua rasmi kituo cha kulelea watoto cha Allamano Nursery School kilichopo maeneo ya Bugudadi Mbagala jijini Dar Es Salaam Jumamosi iliyopita,Kardinali Pengo alisema kwa siku za hivi karibuni umekuwapo mtindo wa watu kufungua vikundi vya kulelea watoto na kisha kuvitumia kwa malengo mengine ya kutaka kujineemesha badala ya kutoa huduma ya malezi bora kwa watoto.

Alisema wauminini,na walezi wote hawana budi kutambua kuwa watoto hujifunza hata bila kuambiwa na hivyo ipo hatari kubwa ya kujifunza moyo wa tamaa toka kwa walimu wenye tabia hiyo hivyo watu wenye nia hiyo hawana budi kuacha mara moja ili kulinusuru taifa.

"Endapo watoto watatambua kuwa walezi wao ni wenye moyo na tabia hiyo,na kwamba wanawatumia kama miradi ya kujinufaisha wao binafsi, vituo vyote hivi tunavyofungua vitakuwa balaa kwa jamii kwani watoto hao wataiga moyo huo wa ubinafsi toka kwa walimu hao hali ambayo itachangia kuongezeka kwa vitendo vya uharifu sambamba na ongezeko la magereza kwani najua kwa sasa hakuna gereza litakalo watosha."alisema.

Katika ufunguzi huo, Pengo alionya kuwa kituo hicho kilichopo chini ya parokia ya Mbagala kisiwe kama kitega uchumi kwa wahusika bali kiwe ni mahali ambapo Mungu anaongoza kila kinachofanyika , "Asiwepo mtu ambaye baadaye atasema kituo hiki kisinge kuwepo, angekufa kwa njaa."alisema.

Akifafanua kauli hiyo, Kardinali Pengo ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam alisema walimu ingawa wanalipwa, pale inapobidi hawana budi kujitoa mhanga ili kulitumikia Kanisa na kuwafanya watoto hao kuiga matendo mema toka kwao na hivyo kuondokana na moyo wa ubinafsi.

"... Pawe ni mahala pa kujitoa na siyo kutafuta faida ya kibinafsi ili baadae kanisa na taifa kwa ujumla vipate vijana wenye moyo na waadilifu,"alisema.

Akifafanua zaidi Pengo alisema jamii haina budi kujenga moyo wa kujitoa hali ambayo aliieleza kuwa inaumiza na kutoa jasho huku mhusika akiwa bado anaona ni jukumu lake kufanya hivyo tofauti na kujitolea ambapo hakuna mtu wala hali yoyote inayomlazimisha mtu.

Akihimiza umuhimu wa kutunza na kuendeleza vifaa vyote vilivyopo katika shule hiyo ya chekechea, Kardinali Pengo alionya dhidi ya tabia ya kutegemea misaada toka nje ya nchi. "Kwa muda mrefu Watanzania tumekuwa tukidhani kuwa maendeleo huletwa na watu wa nje na hali hiyo imetufanya tuchelewe kimaendeleo," alisema Pengo.

Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi katika ufunguzi huo kardinali Pengo, Mweka Hazina wa kituo hicho Bi. Magdalena Lyaruu alisema kituo hicho ambacho zamani kilijulikana kama Tumaini shule ya chekechea na baadaye kubadili jina kutokana na sababu za kiusajili, kiko chini ya uongozi wa Tumaini Mothers Group.

Hivi sasa kina jumla ya watoto 110 na walimu wanne. Kituo hiki kinawasaidia watoto 22 wa kutoka dini zote ambao wazazi wao wameshindwa kumudu gharama za masomo yao. Mwenyekiti wake ni Bw.Dionis Tarimo na Katibu ni Bi. Loyce Mitema.

Balozi wa Papa awataka Watanzania wailee amani yao

BALOZI wa Papa nchini anayehamia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Francisco Javier Lozano ametoa salamu zake za kuwaaga Watanzania kwa kumtaka kila Mtanzania mwenye mapenzi mema na nchi yake kuhakikisha ametoa mchango wake katika kudumisha hazina ya amani iliyoko nchini.

Balozi huyo alitoa salamu hizo katika barua yake rasmi aliyoitoa mwishoni mwa wiki na kusisitiza umuhimu wa kujali amani. Balozi huyo aliagwa katika tafrija fupi iliyofanyika jumatano iliyopita katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kurasini jijini.

Katika tafrija hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki ( TEC) nchini Mheshimiwa Askofu Justin Samba, Balazi Lozano alisema tangu zilipotolewa taarifa za kuteuliwa kwake na Baba Mtakatifu kwenda nchini Kongo mwezi uliopita amekuwa akipewa pole nyingi kwa vile anaondoka katika nchi ya amani na kwenda mahali ambapo pana vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hata hivyo alisema anafarijika kwenda huko kwani anawajibika kujitoa mhanga kuwahudhumia watu walio katika dhiki.

Akiongea katika tafrija hiyo Katibu Mkuu wa TEC, Dk. Method Kilaini, alisema ni jambo la huzuni kwamba Watanzania wanamuaga mtu aliyekuwa karibu sana na watu na aliyejitoa kwa dhati kushirikiana nao, lakini akasema kwa upendo hakuna budi kukubali aende kuwahudumia Wakongo kwani Afrika ni moja. Alimtaka aende huko akiwa amebeba "bendera" ya amani ya Kristo Mfufuka.

Naye Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki nchini Olive Luena, akiongea kwa utani alisema WAWATA waliposikia kwamba Balozi Lozano anakwenda iliyokuwa Zaire ambako kuna vita walifikiri ni vema wampe magwanda ya kijeshi, lakini walipotafakari zaidi wakaona vema wampe (kinadhanria) Njiwa wa amani ( A dove of peace) ili akatoe mchango wake kurejesha amani nchini Kongo.

Bibi Luena alimkabidhi balozi huyo zawadi iliyofungwa ambayo alimtaka asiifungue hadi atakapofika nyumbani, wakati Katibu Mkuu wa TEC Padri Kilaini pia alikabidhi zawadi kwa niaba ya Baraza la Maaskofu.

Tafrija hiyo ilihudhuriwa pia na Watendaji kadhaa wa Baraza la Maaskofu.

Kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano aliyokaa Tanzania ameshuhudia ukarimu mkubwa na moyo wa dhati wa kujitoa wa waumini wa Kanisa Katoliki.

Zanzibar hakuna chuki za kidini

IMEELEZWA kuwa pamoja visiwa vya Zanzibar kuwa na idadi kubwa sana ya waumini wa dini ya Kiislamu,lakini mji huo umekuwa hauna migogoro ya kidini baina ya waumini wa dini ya Kiislamu na Kikristo.

Hayo yalielezwa hivi karibuni na Askofu wa Jimbo la Zanzibar,Augustine Shao wakati akijibu maswali mbalimbali yaliyolenga kuonyesha hali ya kidini ilivyo kwenye Jimbo lake,maswali yaliyotoka kwa washiriki wa semina ya Mashirika ya Kipapa ya Uinjilishaji (PMS) iliyofanyika kwenye ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoriki nchini (TEC) kuanzia mwanzoni mwa wiki na kumalizika mwishoni mwa wiki.

Akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo,Askofu Shao ambaye ni Mwenyekiti wa Shirika hilo alisema kuwa kutokuwepo kwa migogoro baina ya dini hizi mbili inatokana na Waislamu wa mji huo kukomaa kiimani tofauti na baadhi ya Waislamu wa Bara.

"Ni lazima kujua kabisa Uislamu wa Zanzibar ni tofauti kabisa kabisa na Uislamu wa Bara; kwani Muislamu wa Zanzibar anaanza kufundishwa masuala ya dini tangu akiwa mtoto ambapo huku Bara baadhi ya watu wanakuja kuwa Waislamu wakiwa wameishakuwa watu wazima," alisema.

Alisema kuwa Asilimia 96.7 ya wakazi wa Zanzibar ni waumini wa dini ya Kiislamu ambapo idadi ya Wakiristo Wakatoliki kisiwani Pemba ni 478 tu na Unguja Wakristo ni kati ya 600-700.

Semina hiyo ya siku sita,ilijumuisha Wakurugenzi wa PMS kutoka majimbo yote ya Tanzania.

Watanzania mafundi kuandika michanganuo, si utekelezaji - TEC

Naibu Katibu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Padre Dk.Pius Rutechura amesema Watanzania wengi ni mafundi wa kuandika michanganuo ya miradi ya kuombea misaada ndani na nje ya nchi, lakini si watekelezaji wa michaganuo hiyo baada ya kupata misaada.

Padre Rutechura alisema hayo hivi karibuni alipokuwa akifungua rasmi Mkutano wa 24 wa Wakurugenzi wa Habari wa Majimbo wa Kanisa Katoliki nchini na vituo vya Redio vinavyomilikiwa na kanisa hilo. Mkutano huo ulifanyikia kwenye ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kurasini mjini Dar es Salaam.

Alisema jamii ya sasa inapaswa kugeuka na kuacha utamaduni huo hasa kwa vile hao wafadhili wenyewe nao huitoa misaada hiyo kwa kujinyima.

Kadhalika alisema wanaotegemea kuandika tu michanganuo na kupata misaada hawana budi watambue kuwa hali hiyo ina mwisho wake.

Naibu Katibu Mkuu pia alisema kanisa katika nafasi yake linatakiwa kukuza njia za mawasiliano miongoni mwa waumini ili kuliweka kwenye nafasi nzuri ya kuwafikishia waumini hao habari njema za upendo wa Yesu Kristo.

Ili kuboresha njia za mawasiliano katika Kanisa Katoliki, Dk.Rutechura ameishauri Idara ya Mawasiliano kuzishauri na kuzisaidia idara nyingine kujenga na kuimarisha mtandao wa mawasiliano katika idara hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Akizungumzia siku ya Mawasiliano Duniani ambayo huadhimishwa na Kanisa Katoliki kila Jumapili ya kwanza ya mwezi Agosti, Naibu Katibu Mkuu huyo alisema siku hiyo imekuwa haiadhimishwi ipasavyo katika majimbo, hivyo akawataka Wakurugenzi kutumia siku hiyo kwa ajili ya tathmini ya mafanikio ya mawasiliano katika majimbo yao. Alishauri pia kuielimisha jamii umuhimu wa mawasiliano.

Aidha Dk. Rutechura aliwapa changamoto wajumbe wa mkutano huo kutafuta mbinu mpya za kuboresha sekta ya mawasiliano, zitakazoliwezesha Kanisa Katoliki kujiandaa vema kuingia karne ya 21 ambayo ni ya sayansi na teknolojia.

Amesema mawasiliano ni muhimu sana katika Kanisa na jamii hasa ya Watanzania inayohitaji kushiriki na kufahamu upendo wa Bwana Yesu, Baba wa Mbinguni na Roho Mtakatifu.

Mkutano huo uliomalizika Jumamosi ulikuwa chini ya Mwenyekiti, Askofu Anthony Banzi wa Jimbo Katoliki la Tanga.

Tanzania ya pili kwa wamisionari nje

TANZANIAimeelezwa kuwa nchi ya pili barani Afrika kwa kutuma vijana wengi nje ya nchi kwenda kusomea umisionari ikifuatia Nigeria, imefahamika.

Akifungua semina ya siku nne ya juu ya ushirikiano katika kazi za kitume iliyoanza Jumanne iliyopita, Mwenyekiti wa Tume ya Umisionari katika Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania Askofu Augustine Shao alisema uchunguzi wake binafsi umebaini hali hiyo lakini akasema Tanzania iko nyuma katika kuchangia gharama za masomo ya vijana hao.

"Hebu kila mmoja ajiulize tangu aanze masomo yake mpaka sasa amechangia nini katika kuendeleza umisionari duniani,"alisema Askofu Shao na kuongeza kuwa wengi hawaelewi na hawana msukumo juu ya uelewa wa michango.

Aliongeza kuwa kama Watanzania wangehamasishwa zaidi na kuelewa umuhimu wa kuchangia masomo ya kimisionari ya vijana.

Alitaka pia vijana wengi wanaoshindwa kwenda kidato cha kwanza kutokana na uwezo duni wa wazazi wao wajiunge na kusaidiwa na vyama mbalimbali vya kitume

Alizitaja sababu zilizopelekea Tanzania kuwa na vijana wengi wanaokwenda nje kusomea umisionari kuwa ni pamoja na wazazi wao kuona matunda mema ya kiroho wanayokuja nayo pindi watokapo katika masomo yao.

Alisema tofauti na wengi wanavyodhani, maisha ya vijana hao yamekuwa na ya kupendeza na kuivutia jamii kimwili na kiroho na akatoa wito kwa vijana wengine kujitokeza na kujiunga ili kulieneza Neno la Mungu.

Mwenyekiti huyo aliwahimaza washiriki wa semina hiyo kushirikiana katika ngazi zote za utendaji na akataka zisiwepo tabaka miongoni mwa watumishi wa Mungu.

Epukeni matendo ya Sodoma na Gomora - Padri

Paroko Camilius Lwambano wa Kanisa la Familia Takatifu la Mburahati, ameonya jamii ya Watanzania kuacha vitendo vilivyosababisha watu wa Sodoma na Gomora kuangamizwa na Mungu kwa kuwaletea gharika kuu.

Padri Lwambano alisema Mungu alikasirishwa mno na vitendo hivyo ambavyo vimeibuka tena katika jamii ‘yetu’ kwa nguvu kubwa. Alisema inasikitisha kuona vitendo vya ubakaji na ulawiti vinaongezeka na kuwa sehemu ya maisha katika jamii.

Katika mahubiri aliyoyatoa Jumapili iliyopita, Padri Lwambano alisema kitendo cha kumbaka mtoto wa miaka mitatu au kulawiti ni unyama, na mtu anayetenda anaonyesha kuwa yeye ni sawa na mnyama au zaidi ya mnyama.

"Mbwa, mbuzi, ng’ombe ni wanyama, ni nani ameona mbwa amelawiti, ni nani ameona mbuzi amelawiti"? alihoji Paroko huyo na kuwataka waamini na jamii kwa ujumla kuacha vitendo hivyo viovu na vya kinyama ambavyo ni chukizo mbele za Mungu na wanadamu pia.

Aidha Padri Lwambano aliwaasa kina mama kutoruhusu miili yao kutumika vibaya kwa kufanyiwa vitendo kama hivyo kwa minajiri ya kupata fedha kwani kwa kufanya hivyo wanaudhalilisha utu wao.

Mbulu watakiwa kujiandaa kumpokea Askofu

WAKRISTO wa Jimbo la Mbulu la Kanisa Katoliki wametakiwa kujitoa kwa moyo wa dhati katika kufanikisha sherehe za kumpokea Askofu wao mpya Mteule Mheshimiwa Yuda Thadei Rwaiki Mei 16, mwaka huu.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki (WAWATA) jimboni humo Elizabeth Masinda alipoongea na gazeti hili juzi.

Mwenyekiti huyo amekuwa akizunguka katika Parokia zote za jimbo hilo ili kuwahamasisha waumini wajiandae vema kufanikisha sherehe hizo.

Aliwataka wanawake wajitokeze kwa wingi zaidi kwani nafasi yao kama walezi wa kwanza itatoa hamasa ya kipekee.

Hivi Karibuni Papa Yohane Paulo ll alitangaza Mbulu kuwa Jimbo na kumteua Askofu mteule Yuda Thadei Rwaiki kuwa Askofu wake.

Mwalimu aeleza sababu za kushuka kwa elimu

"TUNAPOSEMA elimu imeshuka tuna maana kwamba hakuna uwiano kati ya elimu inayotolewa na wale wanaopokea elimu hiyo iwe kwa kusoma au vitendo".

Mwalimu wa shule ya Msingi Lugalo Silas Mgeta ameeleza alipokuwa akitaja baadhi ya sababu ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa elimu hapa nchini.

"Chazo cha kushuka kwa elimu ni pale Serikali ilipoidhinisha mwenye elimu ya msingi kufundisha elimu ya msingi bila ya kupitia chuo chochote cha elimu" alisema wakati wa mahojiano na gazeti hili mwishini mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Aliongeza kwa kuhoji kuwa " hebu angalia kwa mfano mwalimu kamaliza darasa la saba, halafu aje amfundishe mwanafunzi ambaye anaingia darasa la saba; unafikiri atakuwa na jipya la kumfundisha?"

Vilevile alisema kwamba mazingira mabaya ya shule yanachangia kushuka kwa elimu. Alisema kwa mfano shule inapokuwa karibu na kumbi za disko au karibu na baa, mwanafunzi hukosa usikivu kwani husumbuliwa na sauti za walevi au muziki ulio katika sauti kubwa. Alishauri kuwa ni bora shule hizo zingekuwa na uzio ambao ungezuia wanafunzi hao kuwa na mawazo ya vitu ambavyo vinafanyika nje ya shule.

Vifaa vya ufundishaji pia kwa kiasi fulani alisema imechangia kushuka kwa kiwango cha elimu kwa sababu hapo awali kulikuwa vifaa vya kutosha ambavyo vilimrahishia mwalimu kazi yake tofauti na hivi sasa ambapo licha kutokuwepo vifaa, pia idadi ya wanafunzi katika darasa moja ni kubwa mno kuliko inavyotakiwa.