Ainuka kanisani na kumkemea Mchungaji

lAmtaka aache kuhubiri mambo yanayomgusa

WAUMINI wa Usharika wa Kifula wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheti Tanzania , Dayosisi ya Pare hivi karibuni walipigwa na butwaa baada ya muumini mmoja kuinuka katikati ya mahubiri na kumtaka Mchungaji aache mara moja kuhubiri mambo aliyodai yanamkera.

Tukio hilo la aina yake lilitokea huku kanisa hilo likiwa chini ya ulinzi wa polisi kufuatia taarifa zilizokuwepo kwamba siku ya tukio (yaani Jumatatu ya Pasaka) watu kadhaa walipanga kumzuia mchungaji wa kanisa hilo Elisamiah Mkaria asiendeshe ibada .

Watu waliosadikiwa kwamba wangefanya fujo kanisani hapo ni wale wanaodai Dayosisi ya Pare igawanywe ili Wilaya ya Mwanga iwe na Dayosisi yake, jambo ambalo limesababisha fujo na mgogoro uliopelekea watu kadhaa kupelekwa mahakamani. Kwa mujibu wa habari zilizothibitishwa na uongozi wa kanisa hilo, aliyemcharukia mchungaji katikati ya mahubiri yake ni Mzee Aseri Tuvuna.

Tukio hilo liliibuka pale Mchungaji Mkariah alipokuwa akihubiri juu ya Wakristo kutoyatukuza mambo ya kimwili kuliko kumtukuza Mungu kwani mambo ya mwilini huishia katika dunia hii tu, wakati mtu anayejiwekea hazina mbinguni atavuna mema baada ya kuondoka duniani. Mchungaji Mkariah akifafanua hoja hiyo alisema kuwa vyeo na mali ambavyo wanadamu wanavigombea hapa duniani vinaweza kuwaponza wasimuone Mungu wao. Ufafanuzi huo ndio uliotafsiriwa na Mzee Aseri kuwa umelenga kuwasimanga wale wanaodai Dayosisi ya Mwanga akiwemo yeye, jambo ambalo lilimfanya ainuke na kumtaka Mchungaji abadilishe mahubiri.

Tangu mwishoni mwa mwaka jana kumekuwa na mvutano mkali miongoni mwa Walutheri wa Dayosisi ya Pare kufuatia kikundi kimoja Wilayani Mwanga kutaka wilaya hiyo ijitenge na Dayosisi ya Pare ambayo inazihusisha wilaya za Same na Mwanga.

Baadhi ya waumini wanakabiliwa na kesi mahakamani kuhusiana na madai kwamba walimvamia mchungaji wao kanisani (sio Kifula) na kutaka kumvua joho.

 Serikali yawauzia wenye njaa chakula kilichotolewa bure

IMEFAHAMIKA kuwa chakula cha Misaada kwa watu wanakabiliwa na tatizo la njaa hapa nchini kilichotolewa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani ( WFP) kupitia Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki (Caritas Tanzania) ili kitolewe bure kwa Watanzania wanaoathirika na njaa kimekuwa kikiuzwa na Serikali.

Habari za kuaminika zilizotokana na tathmini iliyofanywa na baadhi ya wanawarsha iliyoandaliwa na Caritas tawi la Tanzania zinasema kuwa tatizo hilo limekuwa sugu katika Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza ambapo Shirika la Mpango wa Chakula Duniani lilituma chakula kupitia Caritas ili wananchi wapewe bure lakini Viongozi wa Serikali wakaamua kuwauzia 'wanaokufa' njaa.

Habari zinasema kuwa kabla Caritas haijaanza kugawa chakula hicho,Mkuu wa Wilaya hiyo aliwataka watendaji wake wakusanye pesa kutoka wa wananchi wa eneo hilo ambao wangehitaji chakula hicho ambapo kila aliyehitaji msaada huo alitakiwa kutoa shilingi 1,500 kwa debe moja la mahindi lenye kilo 18-20.

"Watu ambao walihitaji chakula kingi zaidi walitakiwa kulipa pesa nyingi na kutokana na hali halisi ya njaa ilivyokuwa,wananchi wengi walilipa kati ya shilingi 3,000 hadi 4,5000 kwa ajili ya kupata debe mbili au tatu za mahindi" inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Habari zaidi zinasema kuwa Ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo ilijipatia zaidi ya shilingi 450,000/=, pesa ambayo ilikusanywa kutoka katika kijiji kimoja tu cha wilaya hiyo kinachojulikana kwa jina la Usagara.

Habari zinasema siku watendaji wa Caritas wa jimbo la Mwanza walipofika katika eneo hilo kugawa chakula walishangaa kuona baadhi ya watu wanadai kuwa wanastahili kupata chakula zaidi kwa vile wamelipa pesa nyingi.

Taarifa zaidi za uchunguzi zinasema kuwa hali hiyo ilileta kero kubwa iliyosababisha baadhi ya watendaji wa serikali ya kijiji kujaribu kuiba chakula cha maafa kilichokuwa ndani ya lori, lakini kabla hawajafanya hivyo wafanyakazi wa Caritas walifanikiwa kukinusuru chakula hicho.

Kutokana na kero hizo zilizojitokeza,Caritas haikuweza kuendelea kugawa chakula katika eneo hilo, hali iliyosabaisha wahusika wazidi kuathirika.

Kutokana na tukio hilo ambalo kwa hivi sasa lina kipindi cha mwaka mmoja,kila kikundi yaani WFP,Caritas na serikali wanabaki kulaumiana juu ya tukio hilo la kusikitisha.

Gazeti la KIONGOZI limefanikiwa kuyapata majina ya waliogundua tatizo hilo kuwa ni Dk.B.S Mongula kutoka Chuo cha Mafunzo ya Maendeleo cha chuo Kikuu cha Dar es salaam (IDS),Dk E.Mwaigomole (IDS),Bibi Tertula Marandu, Mshiriki wa kujitegemea, Bw. Tungaraza kutoka Caritas ,Bw. Madulu (caritasi) na Bw. Kalemera (Caritas).

Wakati huohuo kiasi cha tani cha tani 18,289 za mahindi na tani 481.6 za maharage zimesambazwa na Caritas kote nchini na kufikia walengwa chakula kilichotolewa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP),serikali kupitia Kitengo cha Ofisi ya Waziri Mkuu.

Akifafanua zaidi juu ya takwimu hizo,Askofu wa Jimbo la Shinyanga na Makamu Mwenyekiti wa catitas Tanzania,Aloysius Balina alisema Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilitoa tani 7067 za mahindi na 412 za maharagwe na kwamba mwaka 1995/96 serikali kupitia kiengo cha maafa cha ofisi ya waziri mkuu ilitoa tani8558 za mahindi ambazo zilisambazwa na CARTAS Tanzania. Mwaka 1997mtandao wa CARTAS ulimwenguni ulitoa tani 1906za mahindi na tani70 za mbegu.ambapo mwaka huu mtandao wa wahisani wa CARTAS umetoa tani758 za mahindi kati ya tani3,804 zilizoombwa na CARTAS Tanzania.

Warsha hiyo ya siku nne iliyomaliza juzi,ilijumuisha zaidi ya watendaji 29 wa Caritas kutoka Majimboni na ilifunguliwa na Makamu mwenyekiti wa Caritas Tanzania ,Askofu Aloysius Balina na kufungwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoriki,Padri Method Kilaini.

 Walokole wapania kusali kwenye mabaa

lHadi sasa 'wamekamata' baa tano

KANISA la City Christian Fellowship la jijini, limebuni mtindo wa kufanyia ibada zake kwenye mabaa na hadi sasa limekwisha kamata baa tatu kwa Dar es Salaam na nyingine mbili katika mikoa ya Kilimanjaro na Singida.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na kuthibitishwa na Mchungaji wa kanisa hilo

Bw.Godfrey Malasy, unaonyesha kuwa baa zinazotumiwa na Kanisa hilo lenye makao yake jijini, ni FM-CLUB ya Kinondoni, IMASCO CLUB ya Sinza na CENTRE POINT ya Magomeni.

Huko mkoani Kilimanjaro baa moja iliyokuwa katika kijiji cha Kiruweni hivi sasa inajulikana kama Kanisa la Mwika na inatumiwa na waumini kwa ajili ya ibada,wakati mkoani Singida baa moja ambayo jina lake halikuweza kupatikana mara moja inatumiwa na waumini wa kanisa hilo kwa makusudi hayo hayo.

Aidha kiongozi limebaini kuwa tofauti na Centre Point ambako baa hiyo ilikuwa imefungwa tokea awali, baa za Kinondoni na Sinza hutumiwa siku za Jumapili kuanzia asubuhi hadi nyakati za mchana na mara baada ya ibada kumalizika uuzaji wa pombe huendelea kama kawaida.

Akizungumzia sababu ya kufanyia ibada katika maeneo hayo, Mchungaji Godfrey Malasy wa Kanisa la City Christian Fellowship alisema nia ni kuwafikishia injili watu ambao hawamjui Yesu ili wapate kubadilika katika maisha yao.

Mchungaji Malasy amesema wakati wa ibada hawalazimiki kufunika wala kung'oa mabango yanayotangaza pombe katika baa hizo kwa sababu hayana athari zozote kiroho wala hayawezi kuvuruga ibada zao.

Amefafanua kwamba pamoja na wao kuweka tangazo linaloonyesha kuwa ni wakati wa ibada, kibao kinachotangaza eneo hilo kuwa ni baa hubakia palepale na kuongeza kwamba kutokana na hali hiyo kufunika au kung'oa mabango kusingebadili lolote.

Mchungaji Malasy alisema ni katika baa ya Centre Point ya Magomeni pekee ambapo wameng'oa matangazo ya pombe kwa vile baa hiyo haitumiki tena kuuzia pombe.

Alisema katika kampeini yao hiyo i wengi wa wafanyakazi na wateja katika baa hizo wamekuwa wakionyesha shauku kubwa ya kumjua Mungu na wengine na tayari wamempokea Yesu kuwa Mwokozi wa maisha yao.

Mchungaji Malasy amesema nia yao siyo kugeuza sehemu hizo kuwa mahekalu bali ni kufikisha ujumbe wa maneno ya Mungu kwa watu ambao mara zote hawapati nafasi ya kuhudhuria ibada, mikutano wala semina kutokana na kusongwa na anasa za Dunia.

"Wengi wa watu wa aina hii wamekata tamaa na wamekuwa wakihisi kutengwa na jamii na kanisa, hivyo kuwepo kwetu katika maeneo hayo kunaonyesha kuwa tunawapenda na kuwathamini", alisema Mchungaji huyo na kuongeza kwamba wanafuata nyayo za Yesu Kristo aliyekuwa akishiriki na watu wenye dhambi.

Amesema kama kama wanavyofanya watu wengine kanisa lake lina mkataba maalum na wamiliki wa sehemu hizo na kwamba wanagharamia kuwepo kwao katika kumbi hizo kwa ajili ya ibada.

Malecela awataka Wakristo waishi kwa matendo, sio miaka

MAKAMU Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Tawala CCM Mheshimiwa John Malecela amesema Wakristo hawapaswi kujivunia idadi ya miaka wanayoishi duniani bali matendo mema waliyoyafanya.

Mheshimiwa Malecela alitoa changamoto hiyo katika mazishi ya Mchungaji Nicholaus Mwachusi ambaye alikuwa Msaidizi wa Askofu wa Jimbo la Iringa la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania. Marehemu Mwachusi alizikwa mjini Iringa Aprili 9, mwaka huu baada ya kufariki Aprili 6.

Changamoto ya Mheshimiwa Malecela ilitokana na maandiko matakatifu aliyoyasonma kutoka kitabu cha Biblia ambapo alinukuu Waraka wa Kwanza wa Paulo kwa Wakorinto 15:50-58.

"Sisi binadamu tunaishi kwa matendo na si kwa miaka hivyo kwa yeyote ambaye anaishi kwa kuwatumikia wanadamu kwa kazi ya Mungu; atakumbukwa daima tofauti na wale wanadamu ambao wanaishi kwa kutegemea mali, vyeo, na kupewa sifa kwa ajili ya mali nyingi walizo nazo,"alisema

Aliongeza kuwa damu na nyama haviwezi kuurithi Ufalme wa Mungu, Wakristo wanapaswa kuhakikisha wanatenda mema kwani yale wayatendayo wakiwa hai ndiyo yatakayowarithisha Ufalme huo. Malecela ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania alisema watu watendao mema hupata ujasiri hata wakati wa kukabiliana na kifo, wakati wale waliojaa matendo ya dhambi wamejaa pia hofu ya kifo kwa vile wanajua Jehanamu ya moto inawangoja.

Malecela ambaye alikuwa akiwasilisha salamu zake za rambirambi kwa niaba ya Chama Chama Mapinduzi katika mazishi hayo yaliyofanyika katika kanisa la KKKT Kihesa mjini Iringa, aliupongeza Umoja wa Makanisa mkoani Iringa na akawataka Wakristo kote nchini waimarishe mshikamano miongoni mwa madhehebu yao ya dini badala ya kubaguana na kuchukiana..

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Iringa Owdenburg Mdegela aliwashukuru maaskofu pamoja na wachungaji kutoka katika madhehebu mbalimbali ambao walishiriki kufanikisha mazishi ya mchungaji Mwachusi ambapo kanisa la Kianglikana, kanisa Katoliki, Moravian, Wasabato, AIC, Assemblies of God na Pentekoste kwa kuonyesha ushirikiano wao mkubwa.

Marehemu alikuwa anasumbuliwa na homa ya matumbo na ameacha mjane na watoto watano.

Padre akemea ndoa ‘zisizokomaa’

IMEELEZWA kuwa mila potofu za kuwaoza wasichana wakiwa na umri mdogo zinachangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.

Hayo yalisemwa na Katibu Mtendaji wa Idara ya Elimu ya baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Padre Elias Msemwa juzi alipokuwa akizungumza na gazeti hili ofisini kwake.

Msemwa alisema mila hizo zinazoendekezwa na baadhi ya makabila ya hapa nchini zimewafanya wasichana hao kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu na kwamba hata wale wanaonyanyaswa kwa kupewa wachumba huku wakiwa masomoni wamekuwa wakifeli mitihani yao kwani wakati wa masomo wanakuwa na mawazo mengine juu ya wachumba wao.

Aliyataja mambo mengine yanayozorotesha elimu nchini kuwa ni pamoja na ukosefu wa maadili kwa walezi wakiwamo viongozi mbalimbali wa dini, serikali na walimu ambao hudiriki kufanya mapenzi na watoto wa shule licha ya dhamana kubwa waliyopewa.

"Hivi mwalimu anadiriki kumfanya mwanafunzi wake mke? Au mchungaji mzima kweli?" alihoji kwa mshangao.

Alisema tatizo jingine ni hali ngumu ya maisha ambayo hupelekea baadhi ya wazazi kushindwa kumudu gharama za masomo yao.

Alisema imani kwamba watoto wanaosoma katika shule za kanisa wanalazimika kuwa watumishi wa Mungu, zimechangia pia kudorora kwa elimu. "Hakuna anayekulazimisha kuwa padre eti kwa kuwa umesoma shule ya kanisa; lengo la mashule ya kanisa ni kutoa elimu kwa vijana ili wanapomaliza wawe ni wenye maadili yanayokubalika na hivyo kuwa wa manufaa kwa taifa,"alisema.

Hivi sasa Kanisa Katoliki nchini linamiliki Chuo Kikuu kimoja cha Mtakatifu Augustino (SAUT) kilichopo Mwanza, seminari kuu sita ambazo ni Segerea ya jijini, Kipalapala ya Tabora na Peramiho iliyopo Songea. Nyingine ni Ntungamo ya Bukoba na Salvatorian Kolla ya Morogoro. Kanisa hilo pia linazo shule za sekondari 115 zikiwa ni pamoja na seminari ndogo pamoja na shule 10 za msingi.

Mkuu wa Wilaya aonya wasiodhibiti mifugo yao

KUFUATIA kampeni ya upandaji miti iliyozinduliwa rasmi kitaifa Aprili10, mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Temeke Kapteni John Chiligati amewataka wananchi wote kuhakikisha kuwa wanadhibiti mifugo wao badala ya kuwaachilia wakizurura ovyo na kusababisha uharibifu kwa miche iliyopandwa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Jumatano iliyopita, Mkuu huyo wa wilaya alisema tangu upandaji huo ulipoanza, mifugo wanaozurura ovyo wamekuwa wakiiharibu miche iliyopandwa kando mwa barabara na maeneo mengine mbalimbali hali aliyosema itarudisha nyuma juhudi za taifa za kutunza mazingira.

Alisema kwa mujibu wa sheria za Tume ya Jiji, mwenye mbuzi atakayekamatwa akizurura ovyo atatakiwa kulipa faini ya shilingi 5000/=kwa siku; kwa kila mbuzi mmoja wakati ambapo ng'ombe atakayekamatwa atalipiwa faini ya shilingi 10,000/= na kuongeza kuwa mifugo watakao kaa zaidi ya siku tano, watauzwa kwa njia ya mnada.

Chiligati alisema katika uzinduzi wa kampeni hiyo ya upandaji miche uliofanyika kiwilaya maeneo ya Yombo -Dovya katika kata ya Vituka, mgeni rasmi katika wilaya hiyo ambaye ni Waziri wa Ujenzi Anna Abdala aliwaagiza watendaji wa ngazi mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuweka mipaka katika eneo hilo na kuhakikisha kuwa wananchi waliotoka katika eneo hilo pamoja na wengine, hawarudi kuishi tena wala kuendesha shughuli zao katika bonde hilo..

Aidha , Kapteni Chiligati amewahimiza wananchi kuitunza miche hiyo kwa kuimwagilia maji ya kutosha, kuipalilia na kuipulizia dawa kila inapobidi.

Zoezi la upandaji wa miche wilayani hapo linaendelea ili kufikia lengo la miche laki tatu ifikapo Juni mwaka huu.

Mvua za El-Nino mwaka jana zilisababisha zaidi ya familia 34 kuondolewa katika bonde hilo ambalo lilijaa maji na kusababisha wakazi hao kupewa maeneo mengine ya kuishi.

Mtikila asema yuko tayari kuingia CCM mradi awanie urais

Mwenyekiti wa chama cha siasa kisicho na usajili- Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amesema yuko tayari hata kujiunga na Chama cha Mapinduzi ili mradi tu agombee kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu ujao utakaofanyika mwaka 2000.

Alisema Watanzania hawahitaji chama bali mtu atakayewakwamua kutokana na matatizo waliyo nayo, hivyo atapitia chama chochote kikimkubali endapo cha kwake hakitasajiliwa naye hataruhusiwa kugombea kama mgombea binafsi. "Hata CCM naweza kujiunga kama wanachotaka ni kuwa tu na kadi ya chama" alisema alipokuwa akiongea na Waandishi wa habari nyumbani kwake mwishoni mwa wiki.

Mtikila alidai chama chake hakijasajiliwa kwa kuwa kuna njama za baadhi ya viongozi wakuu wa serikali akiwemo Rais Benjamin Mkapa ambao wanamhofia kushika madaraka na akaongeza kusema;

"Chama changu hakijasajiliwa kwa sababu huwezi kufanya lolote kama haujamfurahisha mtu fulani... ninajua hata vyama vingi vya upinzani vimepandikizwa na serikali, ndiyo maana unaona hata hii migogoro katika vyama ni njama tu"alisema.

Mchungaji Mtikila amesema katika azma yake hiyo, hana shida na ruzuku kwani anajua wananchi wanaomtaka watamsaidia kwani wanamtaka mtu mwenye kuwapa matumaini na kujali haki za vizazi vyao.

Akitumia maneno mengi yanayolitaja na kulisifu jina la Mungu, Mtikila alisema, "Utaifa ni kiungo muhimu kwa mwanadamu ndiyo maana Mungu alimtuma Musa kwenda kulitoa utumwani taifa la Israel lililokuwa utumwani kwa zaidi ya miaka 400. Hata Msumbiji walipigania utaifa ndiyo maana Tanzania iliwasaidia katika kupata uhuru," alisema na kuongeza;

"Hata Maandiko yanasema msimtawaze mgeni,kuwa kiongozi wenu bali awe mmoja wenu atakayethamini nchi, ndugu, akiba na urithi kwa ajili ya vizazi vijavyo na siyo yule anayefuatwa na kuongozwa na mataifa mengine kwa faida yao maana huyo atawajali wageni kuliko raia," alisisitiza.

"Uliona wapi hati miliki ya nyumba anaimiliki house boy ? Watu wanahitaji ardhi kwa ajili ya ukombozi wao" alisisitiza.

 

Maaskofu waungana kupinga ‘mikakati’ ya UMATI

VIONGOZI wa madhehebu mabalimbali ya Kikristo wamepinga vikali hatua zinazokusudiwa kuchukuliwa na Chama cha Uzazi na Malezi bora Tanzania (UMATI) kuishinikiza Serikali kupitisha sheria itakayoruhusu utoaji wa mimba.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, viongozi hao wamesema Kanisa kamwe haliwezi kuingia katika mjadala wa kuhalalisha mauaji kinyume na maandiko na mapenzi ya Mungu.

Askofu Charles Salala wa Kanisa la African Inland Church (AIC), amesema kiumbe chochote hata kama bado kiko tumboni kina haki ya kuishi, hivyo si sahihi kabisa watu kuketi na kuanza kujadili uhalali wa maisha ya kiumbe hicho.

Askofu Salala amesema jukumu la uamuzi wa nani aishi na nani asiishi liko mikononi mwa Mungu na si mwanadamu awaye yote na kuongeza kwamba Kanisa lipo kwa ajili ya kutetea haki za viumbe wasiokuwa na uwezo wa kujitetea.

"Kama tutajadili mambo kama hayo ipo siku tutaketi kujadili uhalali wa kuishi kwa wazee wasio na uwezo wa kuzalisha chochote katika jamii", alibainisha Askofu huyo na kuongeza kwamba Kanisa litatumia nguvu zake zote kupinga hatua hiyo inayolenga kuhalalisha mauaji katika nchi yetu.

Naye Askofu Aloysius Balina wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga amesema kumekuwepo na msukumo wa kibiashara nyuma ya madai hayo ambayo yanatetea maslahi ya watu wachache.

Askofu Balina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, amesema madawa na vifaa ambavyo hutumika katika zoezi la utoaji wa mimba vinaleta athari kubwa kwa watumiaji kwani huharibu mfumo mzima wa uzazi.

"Njia ambazo zinatumika kwa ajili ya uzazi wa mpango si salama kwani vidonge na sindano vina madhara makubwa kwa watumiaji," alisema Askofu huyo na kuongeza kwamba njia za asili ni salama zaidi.

Hata hivyo Askofu Balina amesema ana imani kwamba serikali haitapitisha sheria hiyo ambayo inalenga kuuangamiza umma wa Watanzania na kuyataka makanisa kutumia nguvu zake kupinga sheria hiyo isipitishwe.

Amesema madai ya sheria hiyo ya utoaji mimba yanasababishwa na hofu ya kuongezeka kwa idadi ya watu hapa nchini, na kuonya kwamba kama uamuzi huo ukikubalika watanzania wataujutia siku zijazo kama ilivyo nchini Marekani na Ujerumani ambako sasa hivi kuna watu wachache sana wa asili ya huko.

Pamoja na kusisitiza mahubiri katika makanisa Askofu Balina amesema ni vizuri kama makanisa hayo yakatoa mafundisho kwa waumini wao juu ya uzazi wa mpango kwa kutumia njia za asili.

Naye Mchungaji Ajuaye King'homela wa Kanisa la Kilutheri Usharika wa Msasani amesema demokrasia katika Kanisa ni watu kufuata maandiko matakatifu na siyo vinginevyo.

Amesema kamwe Kanisa la Mungu haliwezi kuhusika kwa namna yoyote kujadili mauaji kwani mbali na kwamba ni kinyume cha haki za binadamu, pia Mungu hapendezwi kabisa na vitendo hivyo.

"Hatuwezi kuhalalisha utoaji wa mimba kwa sababu hata wenye madaraka katika jamii hivi leo wote walianzia huko huko. Sasa iweje leo hii tuketi kujadili uhalali wa maisha ya viumbe ambao tayari Mungu ameamua wawepo?" aliuliza Mchungaji huyo ambaye pia ni Mkuu wa Jimbo la Kinondoni la KKKT.

Mchungaji King'homela alisema kanisa la Kilutheri limewahi kumfukuza kazi mmoja wa madaktari katika Hosipitali linayoimiliki kutokana na tuhuma za kuhusishwa utoaji wa mimba. Hata hivyo hakutaja jina la daktari huyo na hosipitali husika.

Wiki iliyopita gazeti hili liliandika habari zilizokuwa zikieleza azma ya cahama cha Uzazi na Malezi bora Tanzania (UMATI) kuishinikiza serikali kuhalalisha utoaji wa mimba.

 

TEC yapoteza mtumishi muhimu

BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania wiki iliyopita lilimpoteza mtumishi wake muhimu Bw. Godfrey Kisakile (29) aliyekuwa na kipaji cha kipekee licha ya kuwa mlemavu wa miguu.

Akielezea jinsi alivyovutiwa na marehemu katika siku yake ya kwanza ya kukutana naye, Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Dk. Method Kilaini anasema;

"Alikuja hapa TEC kutafuta msaada wa mafuta kwa ajili ya pikipiki yake na hela kidogo kwa ajili ya kula na wala hakutuma maombi yoyote ya kazi; baada ya kuzungumza naye na kutazama vyeti vyake;nikaona anatufaa nikaamua kumpa kazi bila yeye kutarajia."

Dk. Kilaini aliyasema hayo wakati wa misa ya mazishi ya Kisakile iliyofanyika Aprili 12, mwaka huu katika kanisa dogo la TEC Kurasini, jijini.Mazishi yalifanyika katika makaburi ya Msimbazi.

"Hadi mwisho wake alikuwa ni tunu na ua ambalo kila mtu aliona ni la kwake, akalifurahia. Kila mtu alitaka kuwa karibu naye kwa ajili ya msaada wake wa mahesabu na mambo mengine mengi mazuri. Alikuwa ishara na ushuhuda ambao Mungu alitupa."aliongeza Katibu Mkuu huyo. Akielezea historia fupi ya marehemu; Padre Kilaini alisema Marehemu Godfrey Kisakile alizaliwa Masoko Tukuyu mkoani Mbeya mwaka 1970 na alisoma katika shule ya msingi Katumba huko Tukuyu. Mwaka 1985 hadi 1988 alisoma katika Shule ya Sekondari ya Rungwe na kisha akapata nafasi ya kujiunga na masomo ya Kidato cha Tano na Tita katika Shule ya Galanos mkoani Tanga tangu mwaka 1989 hadi 1991.

Juni 1991 alijiunga na JKT hadi 1992 huko Itende Mbeya. Mwaka 1993 mpaka 1996 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam ambapo alichukua Shahada ya Uchumi, na kuanzia Mei 1997 alijiunga na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) katika Idara ya Fedha. Alifariki dunia Aprili 10,na kuzikwa Aprili 12mwaka huu.

Mapema akitoa mahubiri katika ibada ya kuuaga mwili wa marehemu Katibu Mtendaji wa Idara ya Walei ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padre Nicholaus Segeja aliwataka Wakristo kote nchini kukomaa katika imani na kuwa wenye matumaini pindi wanapopata misiba ili kuwanusuru katika janga la kukata tamaa hali ambayo inaweza kuwafanya wanyakuliwe na mwovu Shetani.

Padre Segeja alisema wanadamu hawana budi kuwa wenye matumaini wanapofiwa na ndugu, jamaa au rafiki.

Wakati huohuo; Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania Padre Dk.Method Kilaini amesema amepokea salamu za rambirambi toka kwa maaskofu wa majimbo mbalimbali nchini akiwemo Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo na Askofu Justine Samba.