Wakatoliki, Walutheli, Wapentekoste wasali pamoja Dar

Mitindo ya salamu yasisimua

"BWANA asifiwe- Aamen!, Tumsifu Yesu Kristu-Milele Amina!, Uhuru wa Yesu- Ni wa milele!". Hizo ndizo salamu zilizotawala ndani ya kanisa Katoliki la Mtakatifu Yosefu, jijini Dar Es Salaam Jumatatu iliyopita wakati Wakristo wa madhehebu mbalimbali yapatayo 13 walipofanya ibada ya pamoja ya Pasaka.

Ibada hiyo ilikuwa ya kipekee kwani karibu kila kanisa lililokuwepo lilipewa nafasi ya kusimamia kipindi kimojawapo ambapo miongoni mwa waliopata nafasi hiyo ni Askofu Mstaafu Elinaza Sendoro wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzani (KKKT) aliyekuwa mhubiri mkuu na Askofu Philemon Tibanenason wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (KLPT).

Wengine walioshiriki katika uendeshaji wa ibada hiyo ni Askofu Mstaafu G. Chitemo wa kanisa la Kianglikana, Mchungaji A. Mwasandube, Bi. Lois Nhigula na Padre Juvenalis Muba ambaye ni paroko wa kanisa la Mtakatifu Yosefu.

Wengine zaidi ni Mchungaji Apollo Kingu na Padre Eria Mtokambali, Mchungaji Edward Mafuru, Mchungaji Josia Mganga.

Akitoa mahubiri katika ibada hiyo iliyoandaliwa na Kamati ya Umoja wa Makanisa mkoa wa Dar Es Salaam, Askofu Sendoro alisisitiza uwepo umoja wa kudumu wa makanisa. Akaongeza kusema kuwa baadhi ya watu wanaoamua kuanzisha vikundi na kujiita makanisa kwa lengo la kujinufaisha na misaada na michango mbalimbali hawataruhusiwa kujiunga na umoja huo kwani wengi wamechangia kwa kiasi kikubwa kuwepo na mivurugano miongoni mwa Wakristo.

"Baadhi ya vikundi vimeamua kujiita makanisa hali havina sifa za kuitwa makanisa."alisema.

Sendoro alisema hali hiyo ya baadhi ya viongozi kutokuwa makini katika kutumia jina la kanisa imekuwa kichocheo cha baadhi ya waumini kujihusisha na vitendo vya uvunjaji wa maadili ya Kikristo na akatoa wito kwa Wakristo kujihadhari na vikundi hivyo.

"Vitendo vya wasichana kutoa mimba na kutupa watoto vinaliabisha kanisa,"alisema na kuongeza kuwa inasikitisha sana kusikia kuwa miongoni mwa wahalifu wengi wanaofikishwa katika vyombo vya sheria na hatimaye kufungwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya ujambazi, mauaji, wizi, ubakaji na mengine; yamo majina ya Kikristo.

Alisisitiza kuwa Wakristo hawana budi kuwa mfano bora wa kuigwa na watu wengine. "Popote walipo, Wakristo hawana budi kushirikiana na kuishi kwa imani ya Mungu na kuonyesha kwa matendo kuwa Yesu alishinda mauti kwa fumbo la ufufuko ili wanadamu waokolewe na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu.

Sendoro alisema mtindo kama huo wa kufanya ibada za pamoja za makanisa unafanyika pia katika majimbo ya Moshi, Jimbo Kuu la Arusha na Mbeya na akasema hauna budi kuendelezwa zaidi.

 Kupinga Uungu wa Yesu ni dua la kuku kwa mwewe

WAKRISTO kote nchi wametakiwa wawapuuze watu wanaodai kuwa Yesu si Mwana wa Mungu, kwani upinzani wa namna hiyo ulianza tangu Kristo alipozikwa; ambapo walinzi wa kaburi walihongwa waseme hakufufuka, lakini alifufuka na kilio chao kikawa kama dua la kuku kwa mwewe, hadi leo.

"Kama ilishindikana kudanganya watu katika karne zile, haitawezekana leo tunapoingia Yubilei ya tatu ya Sayansi na teknolijia" amesema Padre Sergi Tarimo katika mahubiri yake ya hitimisho la Sikukuu ya Pasaka, jumatatu iliyopita kwenye Parokia ya Msimbazi, Dar es Salaam.

Aliwataka Wakristo kuelekeza nguvu zao katika kumhubiri Kristo kwa maandalizi ya Jubilei ya tatu, badala ya kuendekeza malumbano kwa vile wanaopinga watake wasitaka ukweli kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu unabaki pale pale milele.

Alisema anasikitika kuona baadhi ya watu wanapoteza muda wao na pesa nyingi kupinga ukweli usienee kwa kukashifu hali halisi.

Padre huyo alisema Wayahudi waliliwa pesa yao na bado ukweli ukabaki pale pale huku wao wakiaibika, hivyo, hata hawa wanaopiga debe kupinga ukweli leo hii wataambulia aibu tu wakati muafaka utakapofika.

"Wakati tulio nao ni wa kuvumbua mbinu mpya za kukoleza imani yetu juu ya Yesu aliyekufa na kufufuka ili kutukomboa na ni aibu kuwa kuona bado kuna waumini wenye mashaka juu ya ufufuko wake" alisisitiza.

Tunapoingia karne ya 21 kwetu sisi Wakristo ni wakati wa kuishi kwa amani, haki na upendo, tukiimarisha uelewano mzuri na watu wote; makabila yote, madhehebu yote na dini zote bila ubaguzi. Na ni nguvu ya Yesu mfufuka itakayotuwezesha kuyatenda hayo" alisema.

Alisema pesa ndiyo imekuwa kichocheo kikubwa cha malumbano yasiyo na manufaa.

Umati kuishinikiza serikali iruhusu utoaji mimba

WAKATI chama cha kutetea uhai wa binadamu kinachojulikana kama Pro-Life Tanzania kinakemea vikali masuala ya utoaji mimba ,Chama cha Uzazi wa Mpango nchini (UMATI) kinaendelea kukusanya maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi ili kuishawishi serikali iruhusu utoaji mimba.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi hivi karibuni ofisini kwake,Mkurugenzi wa UMATI Bibi Mary Mgaya alisema kuwa chama hicho kimeanza kukusanya maoni hayo tangu mwaka 1996 na hivi sasa kimepeleka mapendekezo kwa wanasheria.

"Tumepeleka mapendekezo kwa wanasheria ili waweze kuishauri Serikali iweze kutunga sheria inayoruhusu utoaji mimba"alisema Bibi Mgaya.

Habari za kuaminika kutoka kwenye vyanzo vyetu vya habari zinasema kuwa Shirika la Kimataifa linaloshughulika na kinachoitwa "Uzazi Salama wa Mpango na Masuala ya kujamiiana"au kwa kifupi IPPF lenye matawi 150 duniani,limepanga mkakati kufanya mambo makuu sita kabla haujafika mwaka 2000 katika mpango unajulikana kama 'Vision 2000'.

Miongoni mwa mambo hayo ni kuondoa vikwazo vyote vya kisiasa,kisheria na kiutawala vinavyozuia masuala ya kujamiiana na utoaji mimba ambapo IPPF imetoa nafasi kwa matawi yake kuwashawishi wanasheria ili wazishauri serikali za nchi mbali mbali ziruhusu sheria ya utoaji mimba.

Alisema suala hilo linalenga zaidi nchi ambazo sheria zake haziruhusu masuala ya utoaji mimba ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo.

Habari zaidi zinasema kuwa tayari IPPF imekwishatuma ujumbe huo kwenye matawi yake na Bibi Mgaya amekiri kupokea taarifa hizo na akasema shirika lake (UMATI) halikulazimishwa kutekeleza mipango hiyo ila kinachotakiwa ni kuchambua kipi kinaendana na jamii husika.

"Kila nchi inafuata utamaduni na sheria zake,na sisi ndio maana tunatafuta maoni kutoka kwa wananchi mbalimbali,"alisema Bibi Mary.

Habari zaidi toka kwa vyanzo vyetu vya habari zinasema kuwa tayari IPPF imewatumia UMATI gari lililoandikwa "Vision 2000" ili kufanyia kampeni ya kuruhusiwa kwa jambo hilo linalodaiwa na wengi hususan madhehebu mengi ya dini likiwemo kanisa Katoliki kuwa ovu. Hata hivyo Bi. Mgaya hakutaka kufafanua zaidi juu ya gari hilo.

Gazeti la Kiongozi lilipomwendea Mwenyekiti wa chama kinachotetea uhai nchini Pro-life Bw.Emil Hagamu ili kupata maoni yake kuhusu suala la Vision 2000, alisema nia na madhumuni ya IPPF kupitia tawi lake la UMATI, si kuelimisha bali ni kueneza zinaa katika jamii ya Kitanzania.

"Hivi UMATI inaposema kuwa inatafuta maoni kutoka kwa wananchi ili iweze kuwasilisha pendekezo serikalini kwa lengo la kutunga sheria ya kuruhusu utoaji mimba,haioni kuwa inataka kuhalalisha uzinzi?"alihoji Bw.Hagamu.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa mbali na sheria za nchi kukataza utoaji mimba, hata imani za kidini haziruhusu dhambi hiyo ambayo haitofautishwi na mauaji ya viumbe hai ambao hawajazaliwa.

Puuzeni uvumi kwambamwaka 2000 ni kiyama - Askofu

ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mashariki na Pwani Jerry Mngwamba, amewataka vijana nchini kupuuza uvumi ulioenea katika jamii kwamba mwaka 2000 ni mwisho wa dunia.

Askofu Mngwamba alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akifungua rasmi mkutano wa Ushirika wa Wanafunzi wa Kikristo Tanzania (UKWATA), uliofanyika katika Shule ya Sekondari ya Minaki iliyoko mkoani Pwani.

Askofu huyo alisema, hivi karibuni kumekuwepo na uvumi kwamba mwaka 2000 ni mwisho wa dunia hivyo kuwafanya vijana wengi kuacha shughuli za uzalishaji mali pamoja na shughuli nyingine za maendeleo wakihofia kuwa watapoteza muda wao kwani ifikapo mwaka 2000 dunia itaangamia.

Alisema hali hiyo ni hatari sana kwa Taifa kwani watu wanaweza kuvunjika moyo wa kufanya shughuli za uzalishaji mali pamoja na masomo (kwa walioko mashuleni) na kurudisha nyuma maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Mngwamba alibainisha kuwa msukumo wa watu kuamini kuwa mwaka 2000 ni mwisho wa dunia unatoka mataifa ya magharibi ambako tayari baadhi ya watu wameanza kutafuta makazi mapya kukwepa janga la mabadiliko ya kisayansi yanayotarajiwa kutukia.

Aidha alifafanua kwamba wanasayansi wanatabiri mabadiliko makubwa katika mfumo wa kompyuta ifikapo Januari mosi mwaka 2000,hali inayoweza kusababisha tukio baya duniani litakalodumu kwa zaidi ya saa sabini lakini hilo lisitangazwe kuwa ndio mwisho wa dunia.

Askofu huyo alisema kimaandiko katika Biblia takatifu hakuna andiko lolote linaoonyesha kuwa dunia itafikia mwisho mwaka 2000, hivyo aliwataka vijana wa Kikristo kuachana na nadharia hizo zisizo na mwelekeo wowote.

Aliyetaka kuuza msikiti kupelekwa mahakamani

WAISLAMU wa msikiti wa Masjid Mwinyi uliopo Ilala,wameamua kumfikisha mahakamani Bw.Daniel Zakaria anayetajwa kuwa mmiliki wa jengo la msikiti huo.

Hatua hiyo inakuja kufuatia tishio la kikundi cha haki za binadamu kinachoongozwa na Mchungaji Christopher Mtikila la kuwataka wampe Bw. Zakaria shilingi milioni 20 au wampe nyumba nyingine, vinginevyo wauhame msikiti wao ili uuzwe.

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na kubandikwa kwenye mlango wa msikiti huo ambao ni nyumba namba 66 plot Na.23 Block K, Waislamu wanaoswali kwenye msikiti huo wametakiwa kuchanga pesa kwa ajili ya kumpa Wakili ambaye atasimamia kesi hiyo ambapo jumla ya shilingi milioni moja inahitajika.

Katika barua hiyo yenye kichwa cha habari 'Maombi ya Mchango' imesisitizwa kuwa Waislamu hawezi kukubali kuona mali zao zinachukuliwa na watu wasio Waislamu wenzao.

"Tunahitaji ushirikiano wa hali ya juu kuhakikisha mali ya Waislamu inarudi mikononi mwa Waislamu kwa gharama zozote zile"inasema sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa msikiti huo Sheikh Abeid Maulid,inadai kuwa Zakaria hana undugu wowote na marehemu bali alikuwa ni mfanyakazi wake wa ndani na kuongeza kuwa mrithi huyo wakati anakula kiapo kwenye Mahakama ya Kisutu hakuwa na shahidi ambaye anaweza kuhakikisha kuwa yeye ndiye aliyekuwa msimamizi wa mirathi hiyo wala mrithi wa nyumba hiyo ambayo ilikuwa ya marehemu Bi.Hajati Aziza Binti Omar.

Kiasi cha fedha zinazohitajika kuendesha kesi hiyo ni shilingi milioni moja ambazo atapewa Wakili El-Maamry kwa mujibu wa barua hiyo.

Mvutano kati ya Waislamu na Bw. Zakaria ulianza mwezi mmoja uliopita baada ya Waislamu kuteka nyumba mojawapo aliyorithi kutoka kwa marehemu Aziza baada ya nyumba hiyop kutolewa kwa Kanisa la Full Salvation linaloongozwa na Mch. Christopher Mtikila ambaye alipeleka shauri hilo polisi na polisi wakaingilia kati na kumrejeshea nyumba hiyo ambayo hivi sasa Mtikila anaitumia kama kanisa. Hata hivyo Gazeti hili lilivyompigia simu wakiri huyo,halikufanikiwa kuongea naye baada ya yule aliyepokea simu hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Bw.Hemed kutoa taarifa kuwa Wakiri huyo yupo safarini Zanzibar na atarudi kesho.

Jengeni mahusiano na vyombo vya dola

VIJANA Wakatoliki Jimbo Kuu la Dar es saalam,wametakiwa kujenga mahusiano mazuri na vyombo vya dola ili kuondokana na dhana iliyojengeka na kuenea miongoni mwa wengi kuwa vyombo hivyo vinawaonea.

Rai hiyo ilitolewa na Mlezi wa Vijana Jimbo la Dar es salaam, Padri Winfried Hubber wakati wa ufunguzi wa tamasha la uzinduzi wa kampeini ya upandaji miti na uboreshaji wa mazingira, lililofanyika parokiani Manzese mwanzoni mwa juma lililopita.

"Hakuna chombo cha dola kinachowaonea vijana; ila vijana wenyewe ndio wamekuwa na utovu wa nidhamu kwa kufanya uharifu na wanapokamatwa, wanasema wanaonewe kumbe siyo kweli"alisema Padri Hubber.

Mlezi huyo amewataka vijana kuachana na vitendo vya uhalifu kama vile uvutaji bangi, ujambazi, ubakaji, wizi na matumizi ya madawa ya kulevya na badala yake wayaelekeze maisha yao katika kumtegemea Mungu kwa imani na matendo yao mema.

Akizungumzia suala la utunzaji wa mazingira, Padri Hubber aliwataka vijana hao kushirikiana bega kwa bega na serikali kuboresha mazingira. "Kuwa na mazingira mazuri na safi kunadhihirisha namna vijana walivyo na moyo safi,"alisema.

Maparokia yaliyoshiriki tamasha hilo ni Mwananyamala, Makuburi, Kisarawe, Ubungo, vijana wa kituo cha malezi kinachojulikana kwa jina la The Sun pamoja na wenyeji wa tamasha hilo Parokia ya Manzese.

Kitaifa Kampeni za upandaji miti ili kutunza mazingira zimeanza jana (Aprili 10) ili ifikapo mwaka 2000 Taifa liwe na miche mipya milioni 100.