Hospitali ya Serikali yamwacha mjamzito afe kwa kukosa pesa

lAweka redio yake rehani hospitalini na kutoa sh 3,000 lakini wapi, aambiwa havitoshi

lDaktari amwandikia barua apelekwe hospitali binafsi ambako pia akataliwa

lBaada ya kufa daktari aenda kumfanyia upasuaji nyumbani kwa shinikizo la polisi

Na Josephs Sabinus,Tarime

MJAMZITO Mariamu Nyangarya (20) amefariki katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime baada ya kukosa pesa za kulipia gharama za upasuaji na kisha mwili wa marehemu kuondolewa hospitalini usiku hali iliyomfanya mganga mmoja wa hospitali hiyo kufanya upasuaji nyumbani kwa marehemu baada ya siku mbili ili kumtenga marehemu na mtoto.

Mume wa marehemu Bw. Boniface Kemore (24) mkazi wa Mtaa wa Starehe na wifi wa marehemu Bi. Anastazia Ghati Kemore (34) makazi wa Magamaga mjini hapo, kwa pamoja walisema baada ya kumfikisha marehemu hospitalini hapo saa 4 asubuhi Julai 31 mwaka huu walilipia sh 500/= kwa mapokezi na kulazwa katika wadi ya wazazi (No.5).

Walisema marehemu Mariamu alitakiwa kuongezwa chupa mbili za damu zilizotolewa na mumewe na ndugu waliyemtaja kwa jina moja la Morris.

Wakizungumza kwa majonzi muda mfupi baada ya mazishi Agosti 2 mwaka huu, walisema licha ya kutoa damu, ndugu yao alinyimwa huduma hiyo baada ya kukosa sh 11,000/= walizodaiwa hadi walipolipa sh 3000/= na kuweka rehani redio kaseti ya Bw. Kemore kwa nesi mmoja aliyetajwa kwa jina la Sara katika chumba cha maabara.

Waliongeza kuwa licha ya hatua hiyo, bado walidaiwa sh. 12,000/= ili mgonjwa afanyiwe upasuaji na zilipokosekana waliomba kuweka rehani kamera. Hata hivyo Mganga aliyekuwa zamu aliwaandikia ya kumpeleka kwenye hospitali ya mtu binafsi, barua iliyoeleza kuwa hospitali yake imeshindwa kumhudumia mgonjwa kwa vile hakuweza kununua vifaa muhimu kwa ajili ya upasuaji (Nakala ya barua hiyo tunayo).

Baada ya hapo mganga huyo alitoa gari la hospitali ya wilaya aina ya Toyota Hilux Double Cabin, lililomhamisha mjamzito huyo kutoka hospitali hiyo ya serikali kwenda hospitali binafsi ya Dk.Winani saa 2:30 usiku.

Waliongeza kuwa huko pia hawakupokelewa kwa kukosa sh 15,000/= kwa ajili ya upasuaji hospitali hapo na badala yake wakakopeshwa vifaa ili warudi tena katika hospitali ya serikali ya Wilaya baada ya kuweka kamera rehani..

Bw. Kemore alisema usiku huo walirudi tena hospitali ya wilaya na kwamba hawakupata mapokezi hadi marehemu alipofia mlangoni majira ya saa 5 usiku.

Huku wakitoa machozi walisema Jumamosi hiyo usiku walishangazwa kuambiwa wamwondoe marehemu usiku huo huo kabla ya marehemu kufanyiwa upasuaji kuondoa kiumbe tumboni kwa ajili ya mazishi, hadi Jumatatu (Agosti 2) majira ya saa saba mchana mganga mmoja wa hospitali hiyo ya serikali aliyetambulika kwa jina moja la Chimwejo alipotumwa kufanya upasuaji huo nyumbani kwa marehemu baada ya ndugu hao kuomba msaada kwa Mkuu wa Polisi wilayani hapo.

Alipoulizwa na gazeti hili ni sababu gani zilizosababisha kifo hicho, mganga aliyekuwa zamu siku hiyo Dk.A.Kululetela alisema kilichosababisha kifo hicho ni ukosefu wa vifaa vya upasuaji kwa wakati muafaka.

"Hospitali haina vifaa muhimu vya upasuaji na kama ndugu zake wangeleta hizo materials(vifaa) mapema tungeweza kuokoa uhai wake. Kesho nenda kwa DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya) atakueleza zaidi"alisema Dk. Kululetela

Naye Mganga Mkuu wa hospitali hiyo,Dk.Philemon Hungiro alipofuatwa na mwandishi wa habari hizi Agosti 3, mazungumzo kati yao yalikuwa hivi:

Mwandishi: Kuna malalamiko kuwa Jumamosi (Julai 31) mjamzito Mariamu Nyangarya alifia hapa kwa kukosa pesa za matibabu; hivi taratibu za uchangiaji huduma za afya kwa wajawazito na watoto zikoje na kulikuwa na uzembe gani uliosababisha kifo hicho?

Mganga Mkuu : Mbona wagonjwa wanaokufa hapa ni wengi lakini hufuatilii; kwa huyu umegundua nini au kuna ‘skendo’?

Mwandishi : Nimelifuatilia kwa kuwa ndilo nililofahamu baada ya wafiwa kulalamika.

Mganga Mkuu: Unashangaza sana; kama kweli una uchungu, ulipaswa kuwa kwenye matanga. Yaani msiba bado mbichi, unawaacha wenzio kilioni, wewe unakimbilia kutafuta habari badala ya kushirikiana nao katika maombolezo? Hivi Kiafrika hicho ni kitendo cha utu! Huu sio uchu wa habari?

Mwandishi: Dokta, kifo hakimaanishi watu wasifanye kazi na ndiyo maana hata wewe umekuja kazini ingawa unajua wazi alifia hospitalini kwako. Na si hivyo tu, hata jana tulifanya kazi nyingine ya mazishi.

Mganga Mkuu: Aaa! Hiyo si ilikuwa kazi inayohusu msiba huo.

Mwandishi: Hata habari hizi pia zinahusu msiba huo huo.

Mganga Mkuu: Nakushauri uende kwenye matanga; uje baada ya siku tatu ukiwa na maswali kwa maandishi ili iwe kumbukumbu ya ofisi.

Agosti 6, mwaka huu mwandishi wetu alipopeleka maswali Dk. Hungiro alimjibu kwa barua yenye Kumb.Na.I.1/2/5: iliyosema hivi; "...Kwa sasa suala la mtu huyo ambaye ni marehemu linashughulikiwa na mamlaka inayohusika kisheria-Polisi. Hivyo ili kutokuvuruga uchunguzi, ni vema kuipatia nafasi polisi iendelee na uchunguzi ikisaidiwa na uongozi wa hospitali. Kwa hiyo naona siyo wakati muafaka kujibu maswali hayo kwa kuwa kufanya hivyo unaweza kukwamisha uchunguzi wa polisi."

Hata hivyo nesi huyo aliyedaiwa kupokea sh. 3000/= na redio rehani alipozungumza na ndugu wa marehemu nyumbani kwake katika nyumba za NHC bila kujua kuwa kuna mwandishi wa habari alisema, "Nilivipokea vitu hivyo ili marehemu apate huduma kwanza wakati fedha za upimaji wa damu zinatafutwa ili kuokoa maisha yake na mpaka sasa ninadaiwa sh. 8000/= na itabidi nizilipe mimi."

Kwa muda mrefu hospitali hiyo imekuwa ikilalamikiwa kutokana na ukosefu wa huduma kwa wagonjwa wasio na pesa.

Baadhi ya wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo walipohojiwa walisema hushangaa wanapoambiwa hakuna dawa na vifaa vingine lakini wanapotoa pesa vitu hivyo hupatikana mara moja hospitalini hapo.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliamuru kuwafukuza kazi wauguzi kadhaa waliodaiwa kuhusika na kifo cha mjamzito katika hospitali ya Mwananyamala, jijini baada ya mjamzito huyo kukosa pesa alizotakiwa atoe.

Maelezo ya kina ya ndugu wa marehemu kuhusu kisa hicho ukurasa wa sita.

 

Wakristo, Waislamu watakiwa kufaidi pamoja neema ya Mungu

Na Dalphina Rubyema

IMEELEZWA kuwa ili kujenga haki na amani katika Afrika Wakristo na Waislamu hawana budi kuungana katika masuala ya kufaidi neema na utukufu wa Mungu.

Hayo yalielezwa hivi karibuni na Padri Peter Smith wakati akitoa mada juu uhusiano baina ya Uislamu na Ukristo kwenye semina ya kimataifa ya jumuiya ya Kolping iliyofanyika kwenye ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC).

Alisema Waislamu na Wakristo hawana budi kutembea pamoja kwa kujenga ushirikiano mzuri kuanzia ngazi ya kitaifa hadi kimataifa.

Alifafanua kwa kusema kuwa ili suala hili litekelezwe, mambo matatu yanapasa kufanyika .

akiyataja kuwa ni mazungumzo baina ya dini hizi mbili ambapo alisema kuwa Wakristo na Waislamu hawana budi kuonyesha ujuzi na ufahamu wa kiteolojia.

Kitu kingine alichokitaja ni ubinadamu na haki ya kijamii akisisitiza kwa kusema usawa na haki za binadamu havina budi kusisitizwa katika kila sehemu duniani.

Padri Smith alitaja kitu kingine kuwa ni kusisitiza hali ya kuwepo na uhuru wa kueneza imani za dini katika kila kona bila kuwekewa mipaka ikiwa sheria hazivunjwi. .

Padri Smith alisema kuwa miaka 500 iliyopita asilimia 19 ya watu ulimwenguni walikuwa ni Wakristo kuondoa watu wa Ulaya ambapo asilimia mbili ilikuwa ni ya watu wenye uelekeo kidogo wa Ukristo na asilimia 79 iliyobaki ilikuwa ni ya wapagani.

Alisema hali hii imekuja kubadilika kwenye miaka ya 1990 ambapo wingi wa dini umeleta mabadiliko makubwa. .

Alisema kutokana na ongozeko la makanisa idadi ya Wakristu imeongezeka kutoka milioni 329 kwenye miaka 500 iliyopita na kufikia bilioni 1.2 kwa hivi sasa na kuongeza kuwa kila mwaka kuna ongezokeo watu milioni 146 wanaozaliwa ambapo kati yao milioni 45 ni Wakristo.

Jumuiya ya kimataifa ya Kolping ina matawi katika nchi 50 ulimwenguni ikiwemo Tanzania na kimataifa inafamilia 5000 zenye kiasi cha watu 50,000.

Uhaba wa vifaa kwa wajawazito huwaletea mauti - Mkunga

Peter Dominic na Dalphina Rubyema

UKOSEFU wa vifaa vya kutolea huduma kwa wajawazito kabla na baada ya kujifungua vinachangia sana kueneza magonjwa ya kuambukiza kwa akina mama hao ukiwemo ugonjwa hatari wa Ukimwi.

Maelezo hayo yalitolewa hivi karibuni na washiriki wa warsha ya mtandao wa utafiti wa wakunga Afrika tawi la Tanzania iliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) jijini Dar es Salaam.

Akisoma risala mbele ya msajili wa Baraza la Wauguzi nchini, mshiriki wa semina hiyo bibi Sebalda Lesambari alisema kuwa vifaa vya kutolea huduma kwa wajawazito ni vichache, hali inayosababisha kifaa kimoja kitumiwe na mtu zaidi ya mmoja.

Tunaomba tuangaliwe kwa kozi zinazoenda na wakati ili tuweze kuinua taaluma yetu"alisema bibi Lesambari katika taarifa yake baada ya kusema kuwa tatizo mojawapo walilo nalo wauguzi na wakunga ni kukosa elimu inayoenda na wakati.

Akifunga warsha hiyo bibi Sebagu alisema kuwa washiriki wa warsha hiyo hawana budi kuyazingatia yote waliijifunza kutoka kwa watoa mada mbalimbali .

Msajili huyo pia amewataka wauguzi na wakunga kufanya utafiti unahusiana na taaluma yao na kutumia matokeo ya utafiti huo katika kutoa huduma.

Semina hiyo ya siku tano ilihudhuriwa na wauguzi na wakunga wasajili wa mikoa mbali mbali na ilidhaminiwa na Kitengo cha Afya kwa Wanawake kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO).

 

Msitambe kuwa mmeokoka huku mnatenda maovu - Askofu

Na Fr. Joseph Hando na Festus Mangwangi, Arusha

VIJANA Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA) na vijana wa madhehebu mengine wameonywa kuacha kujifanya wamekata shauri kumfuata Yesu Kristu wakati mawazo, hisia, maneo na matendo yao ni potofu.

Onyo hilo limetolewa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha Josaphat Lebulu huko Sakila - katika Parokia ya Kakatiti kwenye adhimisho la kusherehekea kongamano la tisa la VIWAWA Jimboni humo.

Akiwahubiria VIWAWA wapatao 200 na watu wengine waliohudhuria sherehe hiyo, Askofu Mkuu Lebulu alisema kuna vijana wengi wanaojifanya wameokoka au kukata shauri kumfuata Yesu Kristu lakini kwa siri wanajihusisha na madawa ya kulevya, wizi wa kutumia silaha, ubakaji, utoaji mimba na ulaghai au utapeli.

"Ninaomba ninyi VIWAWA na vijana wengine wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kuutetea ukweli kwa kubainisha hadharani matendo hayo yote maovu yanayodhalilisha utu wetu", alisema Askofu Mkuu Josaphat Lebulu.

Aidha, aliwapongeza VIWAWA jimboni Arusha kwa jitihada zao za kupambana na mmomonyoko wa maadili na kuwataka wawe chachu kwa vijana wengine ili haki, amani na utulivu vizidi kuwepo nchini na hivyo kuufanya ulimwengu kuwa mahali pazuri pa kuishi.

Pia Askofu Mkuu Lebulu aliwaahidi VIWAWA kuwa angewapatia Padri mshauri kama walivyoomba kwenye risala yao iliyosomwa na Katibu wa VIWAWA Fausta Lyimo.

 

Watakiwa kuungana kudai serikali irudishe mabasi ya watoto

Na Mwandishi Wetu

WAZAZI kote nchini wametakiwa waungane kwa pamoja ili waweze kutoa kauli itakayoiwezesha serikali kurejesha mabasi ya watoto wa shule.

Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Kamati inayoshughulikia haki za watoto katika Mahakama ya Rufaa, Bi Mariam Shangali wakati akichangia hoja katika semina ya haki za watoto na uhuru wao.

Bi. Shangali amesema katika miaka ya 80 serikali ilianzisha usafiri wa magari ya wanafunzi, jambo lililowawezesha wanafunzi kuwa huru huku wakizingatia haki zao ambapo waliweza kurudi majumbani mapema lakini hivi sasa wanafunzi hao wamekuwa wakinyanyaswa kijinsia na daladala na wenye vyombo vya usafiri.

"Mtoto anaondoka asubuhi na mapema kwenda lakini akifika kituoni kusubiri gari,anapaona kama kituo cha polisi kwa sababu anaishindwa kuwa huru pale anapotaka kupanda gari na kizuiliwa na makonda wa daladala na hata kutumika kama vishawishi kuwanasia watoto wa kike" alisema Bi. Shangati.

Alisema, iwapo mtoto huyo atachelewa shule, mwalimu wa zamu siku hiyo humwadhibu bila kujali wala kutaka kujua sababu iliyopelekea kumuuliza ni nini kilichopelekea achelewe kufika jambo ambalo mtoto anaamua kujificha na kuwa majonzi kwa kuogopa kuchapwa viboko.

Aliiomba serikali irejeshe mabasi hayo ili kuondoa kero kwa wanafunzi na akasema hali hiyo itakuwa ni kutenda haki kwa watoto hao na akaiomba jamii nzima iungane kwa pamoja ili iweze kuiomba serikali irejeshe mabasi hayo.

WAWATA washangaa watoto kuomba kondomu za saizi zao

Na Mwandishi Wetu

Wanawake Wakatoliki katika Jimbo Kuu la Dar Es Salaam wamesema kitendo cha watoto wa shule za msingi kuomba watengenezewe kondomu za saizi yao kinaashiria namna jamii ilivyopuuza maadili na kuhalalisha uzinzi kwa kugawa kondomu kwa taasisi mbalimbali za elimu kama njia ya kudhibiti maambukizo ya ugonjwa hatari wa ukimwi na kuepuka mimba zisizo kusudiwa.

Hayo yalisemwa jijini hivi karibuni na Mratibu wa Shughuli za Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) jimboni hapa Bi. Perpetua Mashelle kufuatia gazeti hili kutaka kupata maoni ya WAWATA jimboni hapa juu ya ombi la wanafunzi wa shule za msingi huko Tanga kuomba watengenezewe kondomu za saizi zao

"Najua dini zote hazikubaliani na ombi hili la kubariki uzinzi kwa watoto wetu; hivi Watanzania kama tumewapa watoto wetu kondomu mpaka wamefikia hatua wanaomba watengenezewe zinazowatosha, tunakwenda wapi; Watanzania tutamwambia nini Mungu?

"Najua hata hao wanaozigawa wanajua wazi kuwa wanaua kwa makusudi na hata nafsi zao zinawasuta, maana wanajua kuwa asilimia kubwa ya kondomu hizo ni mbovu na ingawa sina data, zimechangia vifo kwa wengi waliozitegemea. Sio siri; zinapitisha viini vya ukimwi na mbegu za kiume," alisema.

Bi. Mashelle alisisitiza kuwa kitendo cha mashirika, taasisi na viongozi mbalimbali kuhimiza matumizi ya kondomu ni kuchochea vitendo vya zinaa katika jamii badala ya kushirikiana kukemea mmomonyoko huo wa maadili ya kidini na kijamii na akabainisha kuwa njia iliyo bora na ya pekee ni kuepuka vitendo vya kujamiiana kabla na nje ya ndoa.

"Uliona wapi mtoto aliyelelewa kimaadili akiomba hadharani apewe kondomu ili akafanye zinaa kama sio ushirikiano wa walimu na wafanya biashara hao wa kondomu kutumia udhaifu uliopo kuchangia upotofu huo kwa kuwahimiza watoto matumizi ya kondomu kwa ajili ya tamaa ya kujipatia fedha kuliko kujali utu na heshima ya uhai wa jamii?" alihoji .

Hivi karibuni vyombo vya habari vilili ripoti kutoka Tanga kuwa wanafunzi wa shule za msingi wilayani hapo wameomba watengenezewe kondomu za saizi zao kwani wanazotumia sasa ni kubwa na huwalazimu kuzifunga kwa mipira (RubberBand) wakati wanapofanya tendo la ndoa ili zisivulike ovyo.

 

Vijana Wakatoliki kuadhimisha Jubilei Kuu Nairobi

Na Leocardia Moswery, DSJ

VIJANA wapatao 120 wa Kikatoliki Tanzania (TYCS} wanatengemea kuondoka nchini kuanzia Septemba 5, mwaka huu kuelekea mjini Nairobi katika maadhimisho ya Jubilei Kuu ya mwaka 2000 yatakayofanyika mjini hapo.

Mmoja wa wanakamati wa Kamati ya Taifa ya TYCS Bw. Hilary Maximin amesema vijana watakaoshiriki kongamano hilo litakaloanza Septemba 6 - 19 ni Wakatoliki wa Afrika Mashariki kutoka mashuleni, vyuoni, makazini na walioko majumbani.

Alisema gharama za ushiriki wa kongamano hilo la maadhimisho ni sh.10,000/= fedha za Tanzania na kwamba nauli ya kwenda na kurudi ni sh. 24,000 kwa kila mshiriki.

Bw.Maximin alisema kuwa wasio na pasi za kusafiria watatafutiwa na kamati ya taifa ambapo watalipia kiasi kingine cha shilingi 10,000/= na kwamba jumla ya gharama zote kwa kila mshiriki ni sh. 44,000/= kwa wasio na pasi na sh.34,000/= kwa walio nazo.

Msafara huo utaongozwa na Fr.Lucas Mziwanda na kuwataka vijana kujitokeza kwa wingi ili kutimiza idadi inayotakiwa katika kongamano hilo.

 

Waziri Ntimizi kupokea maandamano kupinga utoaji mimba Sep.11

Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Afya Mhe.Tatu Musa Ntimizi (MB) anatarajiwa kupokea maandamano ya kimya kupinga vitendo vya utoaji mimba vinavyoongezeka nchini yanayoandaliwa na shirika la hiari linaloshughulika na utetezi wa uhai, utu, heshima ya binadamu na utakatifu wa ndoa (PRO -LIFE TANZANIA) Septemba 11mwaka huu..

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo iliyolifikia gazeti hili mwishoni mwa juma na kusainiwa na Mwenyekiti wa Pro-Life Tanzania, Emil Hagamu maandamano hayo yataanzia katika Viwanja Vya Mnazi Mmoja kupitia barabara za Uhuru na Samora hadi hadi Makao Makuu ya Wizara ya Afya jijini Dar Es Salaam.

Katika taarifa hiyo Bw. Hagamu amesema shirika lake limeamua kufanya maandamano hayo kwa vile linatambua kuwa vitendo vya utoaji mimba si tu kwamb ni vya kikatili na unyanyasaji dhidi ya binadamu wasioweza kujitetea na wasio na nguvu, bali pia vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotamka wazi dhamana na wajibu wa kila raia kulinda na kutetea uhai ambao ni haki ya kila mmoja. "Utoaji mimba ni kuua; na kuuua ni dhambi" inasema sehemu ya taarifa hiyo. Amewaomba Wakristo na mapadre wote kila mmoja kwa nafasi yake, kushiriki maandamano hayo yatakayoanza katika Viwanja vya Mnazi Mmoja kupitia barabara za Uhuru na Samora jijini Dar Es Salaam saa 3:00 asubuhi na kuwasisitiza mapadre kuvaa kanzu zao ili kuonesha mshikamano na heshima ya kichungaji.

 

Wananchi Kilwa wataka Serikali imalizie ujenzi wa soko

Na Mwandishi Wetu

WANANCHI Kilwa Masoko wameutaka uongozi wa wilaya hiyo uharakishe kuwajengea soko jipya ambalo limetelekezwa kwa muda mrefu sasa.

Akiongea na gazeti hili mwishoni mwa wiki hii, Katibu wa soko la zamani Bw. Ally Mikidadi Kidudu, alisema pamoja na soko jipya kuanza kujengwa mwaka 1998 halijakamilika mpaka leo kitendo ambacho kilidaiwa kuwa ni mbinu za kisiasa ili watu waone kuwa Serikali inawajali. Mwanzoni shughuli za ujenzi wa soko zilionekana kwenda haraka haraka na jengo hilo lilitarajiwa kuzinduliwa na mbio za mwenge mwaka 1998 lakini uongozi wa mkoa uliingilia kati na kuusimamisha ujenzi huo baada ya kuona kuwa kulikuwa na dalili za kukosekana utaalam wa kutosha"

Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kuhusiana na ujenzi wa soko hilo ambapo kutokana na ujenzi huo kusimamishwa wafanyabiashara wamekuwa wakilitegemea soko la zamani ambalo halina hadhi ya kuitwa soko la wilaya kutokana kuchakaa sana.

Hata hivyo katibu huyo alisema pamoja na ujenzi huo kusimamishwa hakuna juhudi zozote za haraka zinazofanywa japokuwa alisema tayari Shilingi milioni 20 zimekwishachangwa, serikali ikiwa imechanga sh. Milioni 10 na Halmashauri ya wilaya imechanga shilingi milioni10.

Soko la zamani la wilaya hiyo lilijengwa kwa nguvu za wanachi wenyewe kwa kila mfanyabiashara kutoa sh.1520/=.