Mchungaji ashinda kesi ya kumbaka muumini wake

lMwanamke asema mumewe alimlazimisha asingizie hivyo, vinginevyo angepigwa

Na Gabriel Mduma, DSJ

MCHUNGAJI wa Kanisa la Pentecoste Tanzania (KLPT) Kibaha Maili Moja, Fredrick Makulala (48) ameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwandamizi mkoani Pwani Bi. Pelegia Khodai, baada ya kuthibitika kuwa madai dhidi yake ya kumbaka Bi. Consolata Ngonyani (25) si ya kweli.

Katika hukumu iliyotolewa hivi karibuni katika mahakama hiyo, Hakimu Khodai, amesema kuwa ameridhishwa na vielelezo vyote villivyotolewa na daktari na mashahidi wa mlalamikiwa kuwa hapakuwa na ushahidi wowote wa kuthibitisha kuwa Bi. Consolata alikuwa amebakwa.

"Mahakama inakuachia huru baada ya kuthibitika kuwa madai (ya madai) hayakuwa na vielelezo (vya kutosha) kukutia hatiani kuwa umebaka". Hakimu Khodai ameandika katika taarifa ya hukumu yake.

Akisoma maelezo ya mlalamikaji, Hakimu Khodai alisema kuwa mnamo Desemba 4, 1997 saa 5.00 asubuhi huko nyumbani kwa Bi. Consolata Kibaha Maili Moja, Mchungaji alikuja kwa nia ya kusuluhisha ugomvi waliokuwa nao na mumewe Samwell Bandeke.

Taarifa ya Hakimu inaseama mshtakiwa alidai kuwa Mchungaji alipofika nyumbani kwa mlalalmikaji alimuulizia mumewe na alipojibiwa kuwa hakuwepo, waliongea naye mazungumzo ya kuwaida kuhusiana na ugomvi wao kwa muda, lakini baadaye alimvuta chumbani na kumbaka. Naye Mchungaji Makulala akitoa utetezi wake alisema yeye alifika nyumbani kwa mlalalmikaji akiwa pamoja na Mjumbe wa Shina Bw. Omari kwa ajili ya kusuluhisha ugomvi wao, ambao Bi. Consolata aliuleta kwake.

Taarifa ya hukumu inasema Bi. Consolata alileta ugomvi huo kwa Mchungaji kwa kuwa hao wanokorofishana ni waumini wake yaani Bi. Consolata na Bw. Samweli.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Bw. Omari aliitwa kutoa utetezi wake na yeye alikiri kuwa Mchungaji hakuwa amembaka kwa vile muda huo walifika wote nyumbani kwa mlalamikaji.

Shahidi wa pili wa Mchungaji alidai kuwa yeye aliwasikia watu waliokuwa na chuki na Mchungaji huyo wakipanga njama za kumdhalilisha.

Shahidi huyo alisema kuwa alimsikia Bw.Bandeke, akimshurutisha mkewe Bi. Consolata aende

polisi kushitaki kuwa Mchungaji amembaka, na asingefanya hivyo Bw. Bandeke angempiga vibaya.

Naye shahidi wa tatu na wa mwisho wa Mchungaji ambaye ni mkewe aliiambia mahakama kuwa Bi. Consolata, alifika nyumbani kwake na kumlalamikia kuwa mumewe ‘anamfosi’ aende polisi kushtaki kuwa mchungaji amembaka, na asingefanya hivyo angepigwa vibaya.

Bi. Consolata na mumewe Samwel ambao wana ugomvi wa muda mrefu unaosemekana kuwa unatokana na wivu, sasa hivi wametoroka na hawajulikani walipo, na mara baada ya kutoa ushahidi wao wakawa hawahudhurii mahakamani mpaka hukumu ilipotolewa.

Mwandishi wa habari hizi allipozungumza na mchungaji Makulala nyumbani kwake maili moja, kuwa ni kwa nini kuna kikundi cha waumini wanaompinga kanisani kwake, alisema waumini hao ni vibaraka tu wanaotumiwa na uongozi wa juu kumsakama.

Amesema mara baada ya taarifa za kuwa amebaka zilipofikishwa polisi viongozi wa juu wa kanisa hilo walifika kanisani hapo Desemba 7 mwaka 1997 toka Der Es Salaam.

Aliwataja viongozi hao kuwa ni makamu wa Askofu Nkhandda, katibu mkuu wa KLPT, Bw, Aron Mabondo na katibu mtendaji Bw,Shekihiyo.Anasema walipokuja aliwaeleza hali halisi ya mambo yalivyokuwa, wakati wanaendelea na kikao hicho ndipo alipokuja huyo jirani yake ambaye ndiye aliyekuwa shahidi wake wa jadi na kueleza mbele yao kuwa ‘’twendeni mukamuone bi. Consolata na mumewe pamoja na kikundi chao.

‘Asilimia 30 ya huduma za afya nchini hutolewa na Kanisa Katoliki’

Na Mwandishi Wetu

KANISA Katoliki peke yake limekuwa likitoa zaidi ya asilimia thelathini ya huduma zote za afya zinazotolewa kwa wananchi nchini, imeelezwa.

Takwimu hizo zimetolewa na Katibu Mtendaji wa Idara ya afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Nchini TEC Dk. Alban Hokororo ofisini kwake Jijini,wiki hii.

Dr, Hokororo amefafanua kuwa licha ya kanisa hilo kutoa kiasi cha asilimia 33.3 ya huduma zote za afya nchini, bado zipo hospitali na zahanati kadhaa za serikali ambazo kanisa hilo limekuwa likizisaidia.

Alisema Kanisa Katoliki hapa nchini lina majimbo yapatayo ishirini na tisa (29) na zaidi ya hospitali thelathini na tisa (39) ambazo zimo ndani ya majimbo hayo.

Alisema kutokana na umuhimu wa hospitali na zahanati hizo, Idara ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) inatarajia kufanya mkutano wa mwaka wa siku tatu mfululizo ambao unatarajiwa kuanza Septemba 6, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Dk. Hokororo, mkutano huo utafunguliwa na Mwenyekiti wa Idara ya Afya Mhashamu Askofu Aloysius Balina , ambaye ni Askofu wa Jimbo la Shinyanga na pia Msimamizi wa Kipapa wa Jimbo la Geita.

Mkutano huo utahudhuriwa na Makatibu wa afya wa majimbo yote 29 ya Kanisa Katoliki hapa Tanzania pamoja na Waganga Wakuu wa hospitali zipatazo 39 zilizo chini ya kanisa hilo.

Dr Hokororo ameeleza kuwa mkutano huo utahudhuriwa na watu zaidi ya sabini kutoka katika maeneo mbalimbali hapa Tanzania na utakuwa na lengo la kujadili mtazamo wa huduma za afya za hospitali zilizo chini ya Kanisa Katoliki Tanzania katika kuelekea karne ijayo, yaani milenia ya tatu.

Pia alisema kuwa kufufua vyama vya kitume vya madaktari na manesi wa Kikatoliki nalo ni moja ya mambo muhimu yatakayozungumziwa, hivyo Dr, Hokororo aliwaomba madaktari na manesi ambao wengi wao ni wakazi wa hapa hapa jijini ambao ni Wakatoliki kuhudhuria katika mkutano huo ambao utafanyika kuanzia Septemba 6, kuanzia saa 8 mchana katika ukumbi wa TEC uliopo Kurasini Jijini ili waweze kufufua vyama vyao vya kitume ambavyo vilikuwa vinalegalega kutokana na wengi wao kufariki na wengine kuhamia mikoa mingine.

 

Mashirika ya dini kushiriki mpango wa usingizi 'mororo' jijini

Na Neema Dawson

MPANGO wa kimataifa wa kuzuia na kupunguza uhalifu mijini uitwao Miji Salama (Safer Cities), tawi la jiji la Dare es Salaam, unafanya mawasiliano na taasisi za dini nchini ili kuona maeneo na jinsi ya kushirikiana kudhibiti uhalifu jijini na kuondoa hofu miongoni mwa wakazi.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana wiki hii kutoka ofisi za kitengo hicho kilichopo chini ya Tume ya Jiji la Dar es Salaam, zimesema kuwa tayari maafisa wa kitengo hicho wameanza kuwasiliana na madhehebu na taasisi mbali mbali za kidini ili kufanikisha mpango huo.

Baadhi ya madhehebu ya dini yatakayoshirikishwa katika mpango huo ni pamoja na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste nchini (PCT), Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania,(KKKT) Kanisa Katoliki nchini na kadhalika.

Nia ya mpango huo , kwa mujibu wa habari hizo ni kupunguza hofu miongoni mwa wakazi wa jiji kwani watu wamekuwa ‘wakikosa usingizi’ kwa kuhofia vitendo vya kihalifu kama vile ujambazi na vingine.

Habari zimesema, taasisi za dini zinahusishwa katika mpango huo kutokana na mvuto na ushawishi zilio nao kwa watu. Hata hivyo mpango wa Miji Salama ambao katika sera yake ni mpango unaoshirikisha jamii katika kupunguza uhalifu mijini umekuwa ukishirikiana na viongozi wa serikali wa ngazi mbali mbali wakiwemo maafisa watendaji wa kata na viongozi wengine wa ngazi mbali mbali serikalini.

Hadi sasa Mpango huo umekwishaendesha semina kwa viongozi wa serikali katika wilaya zote za Dar es Salaam, yaani Kinondoni, Temeke na Ilala.

Safer Cities iliingia nchini Agosti, mwaka 1998 ikiwa chini ya Shirika la Kimataifa

la Makazi Duniani (Habitat International).

Serikali kuwajengea walemavu kanisa na msikiti

Na Dalphina Rubyema

ILI kuonyesha kutenda haki kwa watoto wenye ulemavu, Tume ya Jiji imaemua kuifanyia ukarabati Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko pamoja na kujenga Kanisa na Msikiti kwenye eneo la shule hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa na Kamishna wa Elimu Tume ya Jiji, Bw.Joseph Mmbando, wakati wa ufunguzi wa Kituo cha watoto wenye ulemavu wa akili kwenye Shule ya Msingi Mbagala, jijini Dar es Salaam wiki hii.

Bw.Mmbando alisema kuwa Tume imeamua kujenga shule ya sekondari karibu na Shule ya Msingi Mchanganyiko, hivyo haitaleta picha nzuri kuona Shule ya sekondari ni nzuri na wakati ya Msingi imechakaa kwa hivyo nayo itawekwa katika hali ya kuridhisha.

"Unajua Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko ina wanafunzi walio na akili na viungo timamu na wengine wenye ulemavu wa viungo mbalimbali na ndio maana ikaitwa Uhuru Mchanganyiko. Tukiipendezesha Shule ya Sekondari ya Jiji tutaonekana kuwa na upendeleo, hivyo kutenda haki ni lazima tuipatie huduma muhimu shule hiyo ya Uhuru Mchanganyiko"alisema Bw.Mmbando.

Alisema kuwa watoto wenye ulemavu wa kutoona ambao wanalala shuleni hapo (Uhuru Mchanganyiko) hawana sehemu za kuabudia hivyo Tume imeamua kuwajengea kanisa na msikiti.

Hata hivyo Kamshna huyo hakutaja kiwango cha fedha kitakachotumia kukamilisha ujenzi wa majengo hayo.

Naye Waziri wa Elimu na Utamaduni ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika ufunguzi wa kituo hicho,Profesa Juma Kapuya alisema kuwa Tume ya Jiji imekuwa mstari wa mbele kuinua kiwango cha elimu ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu imeweza kujenga shule za sekondari nne.

"Tume ya Jiji naona imependelea sana Wizara yangu,kwa kipindi cha miaka mitatu imeweza kujenga shule za sekondari nne hivyo kuinua kiwango cha elimu mkoani Dar-Es-Salaam"alisema Profesa Kapuya.

Ujenzi wa kituo hicho kilicho gharimu jumla ya shilingi milioni 20,umefanywa na msamalia mwema wa jijini,Bw.George Haji Ally ambaye ni Mfanyabiashara.

Bw. Ally pia ameahidi kutoa shilingi milioni moja na nusu kwa ajiri ya ujenzi wa kisima cha maji shuleni hapo.

Kardinali afanya uhamisho wa maparoko Dar

Na Leocardia Moswery, DSJ

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam amefanya mabadiliko baadhi ya maparoko na wasaidizi wao katika makanisa mbalimbali yaliyopo hapa jijini.

Kardinali alitangaza mabadiliko hayo katika ibada ya upadirisho iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika Parokia ya Makuburi.

Katibu wa Kardinali Pengo Fr, Steven Kaombe, ameliambia KIONGOZI wiki hii kuwa, aliyekuwa Paroko wa kanisa la Mt. Boniface la Chang’ombe, Padri Ireneus Mbaulila, amehamishiwa Makuburi kuwa Paroko Msaidizi na aliyekuwa Paroko msaidizi wa Makuburi na Mkurungezi Mshauri wa Walei Padre Brian Mkude amehamishiwa kanisa la Mt. Joseph kuwa Paroko Msaidizi.

"Hayo ni mabadiliko ya kawaida yanayofanywa na taratibu za kanisa na tena ni kitu cha kawaida," alisema Fr. Kaombe alipoulizwa sababu za mabadiliko hayo.

Fr.Kaombe aliendelea kuwataja mapadri hao waoliobandilishwa kwenda parokia nyinyine kuwa ni Fr. Andrew Komba aliyekuwa paroko msaidizi wa Parokia ya Mt.Yosefu (St. Joseph) amepelekwa katika parokia ya Chang’ombe kuwa Paroko, wakati Padri Timotheo Yasuru anakuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Osterbay na Padri Sixtus Kimaro anakwenda Parokia ya Kibaha kuwa Paroko Msaidizi.

Alisema kuwa Padri Desiderius Rugemalila, anakuwa mwalimu wa Kiroho na padri Mathias Mabua anakuwa Mkuu wa Seminari ya Visiga wakati aliyekuwa mkuu wa seminari hiyo anakwenda kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Padri Kaombe kwa niaba ya Askofu Mkuu Jimbo Kuu la Dar es Salaam amewataka mapadri wote hao pamoja na waliopewa daraja hilo kujituma katika kazi ya kumtumikia Mungu bila kushurutishwa na kumwomba Kristu awatangulie katika kazi zao.

Wakati huo huo; Mapadri wametakiwa kutunza ahadi zao za utii walizoahidi mbele ya maaskofu wao wakati walipopata daraja la upadri.

Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati wa kutoa daraja la upadrisho kwa mashemasi Timotheo Yasuru, Sixtus Kimaro na Desiderius Rugemarila katika misa hiyo iliyofanyika katika parokia ya Makuburi katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Kardinali Pengo alisema kuwa mapadri wanatakiwa kushika ahadi zao za utii na siyo kwa maaskofu wao tu bali hata kwa waandamizi wao.

"Moja ya mambo mliyoahidi ni utii kwa Askofu na waandamizi wake wakati wote mtakapo kuwa hai na si kwa Pengo au waandamizi tu bali mtatakiwa kuwa watii pia kwa maaskofu wote,"

Kardinali Pengo pia amewataka waumini kuacha kujenga mawazo potofu kichwani mwao kwamba uwezo wa padre unatokana na elimu na ujuzi, hivyo kukataa kuwatii mapadri wao.

"Utamkuta mtu anasema, padre ananizidi nini, yote aliyoyasoma na mimi nimeyasoma na pengine hata kumpita. Huyo padri nilikuwa nikimpita darasani, sasa ataniambiaje niache jambo fulani na kufuata jambo jingine,"alikariri Kardinali Pengo na kuonya kwamba tabia hiyo sio nzuri.

Pia alisema Imani kama hii imefanya idadi ya mapadri kupungua katika nchi za magharibi na akaongeza kuwa hilo ni wazo potofu na ni kutozingatia ni nini maana ya sakramenti ya Upadre kwamba Uwezo anaopata mwanadamu ni ule unaotoka kwa Mungu.

TPDC kupunguza zaidi ya nusu ya wafanyakazi wake

Na Justin Mwereke

SHIRIKA la Maendeleo ya Mafuta nchini (TPDC) limeamua kupunguza tena zaidi ya nusu ya wafanyakazi wake katika kipindi cha miezi minne ijayo kutokana na kupunguzwa kwa shughuli zake.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Bw, Yonah Killagane, aliliambia gazeti hili mapema wiki hii kuwa hatua hiyo imetokana na uamuzi wa Serikali wa kujitoa katika uendeshaji wa mashirika ya umma na kuruhusu biashara ya mafuta ya petroli kuwa huria.

Bw.Killagane alisema uamuzi huo wa Serikali umesababisha baadhi ya shughuli za TPDC kufa na hivyo kuilazimu TPDC kupunguza wafanyakazi wake.

Shirika hilo liliishawahi kupunguza wafanyakazi wake wapatao 180 mwaka 1997 mara baada ya kuruhusiwa kwa soko huria la biashara ya mafuta.

Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema wafanyakazi wameshaelezwa juu ya kupunguzwa kwao kutakakofanyika kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Alisema TPDC ambayo ilikuwa shirika pekee lililopewa jukumu la kuagiza mafuta ghafi (crude oil) kutoka nje na kusafishwa hapa nchini kwenye kampuni ya kusafishia mafuta Tiper itabaki na shughuli za utafutaji na uzalishaji mafuta tu.

Alipoulizwa ni wafanyakazi wangapi watapunguzwa na kiasi gani cha fedha kitakachohitajika kwa ajili ya kulipa mafao yao, Bw. Killagane alisema ni vigumu kusema sasa kabla ya Uongozi wa shirika na Chama cha wafanyakazi wa viwandani (TUICO) kukaa kujadili na kufikia muafaka juu ya suala hilo. Alisema Uongozi utakutana na TUICO wakati wowote kuanzia sasa.

Hata hivyo habari za kuaminika kutoka ndani ya TPDC zinasema shirika linatazamia kubaki na wafanyakazi wapatao 50 tu kati ya wafanyakazi wapatao 180 waliopo hivi sasa. Pia habari hizo zimedokeza kuwa zoezi la kupunguza wafanyakazi hao litafanyika mwezi huu na mwezi Octoba mwaka huu.

Kuhusu namna gani TPDC imejiandaa kuepuka tabia ya kulipa mafao yao kwa awamu kama ilivyoishajitokeza katika mashirika mengi, Bw.Killagane alisema suala hilo linategemea upatikanaji wa fedha za kuwalipa mafao yao.

"Kama fedha zitapatikana hakuna sababu ya kuwalipa kwa awamu," alisema na kuongeza kuwa TPDC ingependa wafanyakazi wote watakaohusika katika zoezi hilo walipwe mafao yao kwa mkupuo mmoja.

Wakati huo huo wananchi wengi wameilalamikia serikali juu ya athari za uamuzi wake wa kuruhusu sekta ya mafuta inayogusa maeneo mbalimbali ya maisha ya wananchi kuwa huria kufuatia kupanda holela kwa bei ya mafuta nchini hivi karibuni.

Wananchi wanadai kupanda kwa bei ya mafuta kwa kiwango kikubwa kunatokana na serikali kujitoa kusimamia na kudhibiti bei ya mafuta wakati nishati hiyo ni muhimu mno katika uthabiti (stability) wa uchumi.

Hata hivyo Dr.Kigoda alisema Bungeni hivi karibuni kuwa serikali inaandaa taratibu za muda za kusimamia soko huria kuanzia mwezi huu (Agosti) ili kuiwezesha kudhibiti biashara ya mafuta na kukabili ongezeko la bei ya mafuta kwa kuhakikisha makampuni ya mafuta hayatozi bei kubwa kuliko inavyostahili.

Pia alisema serikali imeazimia kuweka sheria na kuunda chombo cha kuratibu biashara ya mafuta kabla ya Juni 2000. Alisema maandalizi ya kuundwa kwa chombo hicho yako katika hatua za mwisho.

Kusali Jumapili tu hakusaidii - Padre aonya

Na Sales Malula

PAROKO wa Mbagala Zakhem padre Leseus amewaambia waumini wapya waliobatizwa na kupokea kipaimara kuwa Tabia ya kuabudu jumapili tu haitawasaidia kujengeka kiroho.

Alisema wiki iliyopita kuwa watu wengi wamejenga tabia ya kusali jumapili tu badala ya kusali mara kwa mara na kusoma Neno la Mungu.

Alisema kama vile mwili unavyohitaji chakula kila wakati, roho ya mwanadamu nayo inahitaji chakula chake ambacho ni Neno la Mungu.

Padre Lesius ameyasema hayo huko Mbagala Charambe alipokuwa akifanya huduma ya ubatizo pamoja na kutoa kipaimara na Komunio ya kwanza watu kumi na mbili walibatizwa na kupokea komunio ya kwanza na watu watatu waliopokea kipaimara. Aliwasisitiza wakristo wapya kuhudhuria ibada mara kwa mara ili waweze kuimarika zaidi kiroho.

 Makamba asema yatima watapungua Ukimwi ukipungua

Na Getruder Madembwe.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Luteni Yusufu Makamba amesema kwamba tatizo la watoto

yatima litapungua endapo watu watazingatia maonyo ya wataalamu kuhusu kujihami na UKIMWI.

Makamba aliyasema hayo hivi karibuni alipotembelea kituo cha Kanisa Katoliki cha kulelea watoto yatima kilichopo Msimbazi jijini.

Alisema suala la UKIMWI ni lazima lisemwe kwa kila mtu na wala sio kwa vijana tu kwani

hata baadhi ya wazee nao huathirika kwa ugojwa huo.

Aliendelea kwa kusema kwamba idadi kubwa ya watoto yatima, wazazi wao wamekufa kwa ugonjwa huo wa Ukimwi ukilinganisha na wale ambao wazazi wao wamekufa kwa ajali, hivyo aliwataka Watanzania kwa ujumla kuangalia kwa undani suala hili la UKIMWI.