Papa kupanda juu ya mlima alikofia Musa

Vatican,

PAPA Yohane Paulo ll anatarajiwa kukutana na Mfalme wa Yordan Septemba 18 mwaka huu kufanya mazungumzo naye kabla ya ziara yake ya mwanzoni mwa mwaka 2000 ambapo atapanda mlima ambao Nabii Musa alisimama kuonyeshwa nchi takatifu na kisha akafa.

Japokuwa Balozi wa Vatican nchini Israeli amethibitisha kuwa Papa Yohane Paulo ll, ataitembelea Mashariki ya Kati mnamo Machi, mwaka 2000, Balozi wa Israeli huko Vatican amesema hadi sasa hakuna ajuaye tarehe rasmi ya ziara ya Papa nchini Israeli.

Mustakabali wa tarehe rasmi ya Papa utajulikana rasmi pengine baada ya kukutana kwake na Mfalme Abdullah wa Jordan huko Castel Gandalfo.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Papa kukutana na Mfalme huyo kijana aliyetwaa madaraka ya ufalme baada ya kifo cha baba yake Mfalme Hussein.

Katika ratiba ya Papa huko Mashariki ya kati mwakani atatembelea maeneo mbali mbali ya kihistoria ikiwa ni pamoja na mlima Nebo huko Yordan ambako Nabii Musa alisimama kuitazama nchi takatifu ya ahadi kabla ya kufia hapo mlimani.

Musa alikufa katika mlima huo akiwa kiongozi wa Wanaisraeli aliyewatoa utumwani Misri kuwapeleka kwenye nchi takatifu huko Palestina.

Pamoja na eneo hilo pia Papa anatarajiwa kutembelea maeneo matakatifu ya kihistoria ya Bethlehemu na maeneo mengine kadhaa.

Aingia Kanisani na kuua watu saba kwa risasi

Texas, Marekani

MTU mmoja mwenye itikadi kali ya kiislamu wiki hii amevamia Kanisa moja huko Texas Marekani na kuwaua kwa kuwapiga risasi watu saba kabla ya kujiua pia kwa kujipiga risasi.

Mtu huyo aitwaye Bw. Larry Gene Ashbrook (47)aliingia katika kanisa la Kibaptisti la Wedgewood huko Fort Worths Texas na kuwamiminia risasi waumini waliokuwa katika ibada ambapo pia pamoja na kuwaua watu saba aliwajeruhi wengine saba watatu kati yao vibaya sana.

wakati wa shambulio hilo zaidi ya vijana 150 walikuwa wamekusanyika kanisani hapo kwa ajili ya ibada.

Wapelelezi wamesema kuwa walipofika nyumani kwa muuaji huyo walimbaini kwamba alikuwa amechanganyikiwa kwa vile walikuta vyombo vyake mbalimbali vikiwa vimepinduliwa picha za familia zilikatwakatwa na kulikuwa na matundu katika kuta za nyumba yake.

Gavana wa jimbo la Texas Bw. George Bush ambaye ndio kwanza alikuwa amerejea kutoka katika kampeni za chama chake za kumteua mgombea Urais wa chama hicho cha Republican alipinga dhana kwamba tukio hilo linonyesha umuhimu wa kuwekwa sheria ya udhibiti zaidi wa silaha (Anti-Gun laws).

Hata hivyo Rais Bill Clinton wa Marekani alikaririwa na vyombo vya habari mwishoni mwa wiki akisema kuwa sasa ni wakati muafaka kwa serikali ya Marekani kudhibiti biashara holela ya bunduki.

 

Askofu atiwa mbaroni na Wakomunisti wa China

Stamford, CWNews

SERIKALI ya China imemtia mbaroni Askofu mmoja mwenye umri wa miaka 81 na maparoko wengine watatu kwa tuhuma za kuendesha shughuli za kikanisa kwa siri nchini humo, taasisi moja ya Kanisa Katoliki nchini Marekani imesema.

Taasisi hiyo ya Cardinal Kung Fuoundation imetaja Askofu huyo aliyekamatwa Septemba 7 mwaka huu katika jimbo la Zhejiang kuwa ni Lin Xili wa Wenhou.

Taarifa imesema kuwa Askofu huyo aliwahi kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kwa sababu ya uaminifu wake kwa kanisa. Nao mapadre Wang Chengzi na Shoa Amin wa dayosisi ya Askofu Lin walikamatwa kati ya Septemba 3 na 5.

Kuongezeka kwa vitendo vya kuwakamata Wakatoliki wa siri katika nchi hiyo ya Kikomunisti

kumetajwa kuwa ni kukiuka madai ya serikali hiyo kwamba inajali sheria za Umoja wa Mataifa na haki za binadamu juu ya uhuru wa kuabudu.

 

Sheria ya Kiislamu ya kuwakata mikono wezi yagonga mwamba Pakistan

Islamabad, Pakistan

VIONGOZI wa Kikristo na vyama vya upinzani nchini Pakisatan Alhamisi iliyopita walikishutumu kikundi kimoja cha kiislamu kufuatia kauli yake ya hivi karibuni ya vitisho dhidi ya wanachusika na uwekaji sheria nchini humo wanapaswa kuuawa kwa kuwa wanapinga sheria za Kiislamu zisitawale nchi hiyo. Maulana Ajmal Qadri wa chama cha wasomi wa kiislamu (Party of Islamic Clerics) alitangaza hukumu ya kifo (Fatwa) kwa watunga sheria hao ambao wanapinga hoja ya kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo ili iruhusu Pakistan itawaliwe na sheria za Kiislamu. Kikundi hicho kinataka sheria zote za nchi hiyo ziwekewe msingi wake katika kitabu kitukufu cha Waislamu Koran.

Sheria hizo ambazo kikundi hicho cha Waislamu kinataka ziwekwe ni pamoja na kuwakata mikono na miguu wezi, kuwaua kwa kuwapiga mawe wazinzi, kuwaua wauaji na kuwapiga wahalifu wa aina nyingine hadharani. Wanaopinga hoja hiyo wamesema kikundi hico cha Kiislamu kinataka kuifanya Pakistan iwe kama Afghanistan ambako sheria kali za kiislamu zinatumika.

Kiongozi wa kikundi cha Ukombozi cha Kikristo (Christian Liberation Front) Bw. Shahbaz Bhatti.

Bhatti, alisema endapo sharia hiyo itawekwa itakuwa ni tangazo la kuua waumini wa vikundi vidogo vya dini, wanawake, wapenda demokrasia na watu wenye upeo mkubwa wa kufikiri nchini humo.

Muswada wa mabadiliko hayo ulipitishwa katika Bunge dogo la nchi hiyo mapema mwaka huu, lakini umegonga mwamba katika Bunge kuu la Senate ambako vyama vya upinzani vina nguvu kubwa.

 

Askofu wa Rwanda asema ameshtakiwa ili kudhalilisha kanisa

Kigali, Rwanda

Askofu Mkuu Augustin Misago wa Rwanda aliyeshitakiwa akihusishwa na mauaji ya halaiki nchini Rwanda mwaka 1994 dhidi ya watu wa kabila la Watutsi, amesema waliomfungulia kesi hiyo wamelenga katika kulidhalilisha Kanisa Katoliki.

Akihojiwa na vyombo vya habari hivi karibuni mahala alikokuwa ameshikiliwa, Askofu Misago, alitupilia mbali madai kwamba yeye kwa aliwatia watoto wapatao 82 katika mikono ya wanamgambo wauaji.

Na akaongeza kuwa yeye amekuwa mbuzi wa sadaka katika vitendo vya kisasi ambavyo serikali ya Rwanda imepania kulifanyia Kanisa Katoliki.

"Sina hatia... lakini kupitia kwangu Serikali ya Rwanda inapambana na Kanisa Katoliki" alisema.

Gazeti moja mjini Vatican L’Osservatore Romano, limeielezea kesi hiyo kuwa ni kampeni za Serikali ya Rwanda kuutua mzigo wa mauaji ya zaidi ya watu milioni moja waliouawa mwaka 1994 katika mapigano ya kikabila kwa Kanisa Katoliki.

 

400 wauawa katika vita vya kikabila Uganda

lUkame na njaa nao wapanda moto

Kampala, Uganda

Idadi ya watu wapaao 400 wanaripotiwa kuwa wamekufa katika mapambano makali ya siku tatu mfululizo Mashariki mwa Uganda.

Kwa mujibu wa Mashirika ya habari na wafanyakazi wa Mashirika ya kutoa misaada walioko huko mapambano hayo ni kati ya kabila la Bokora na Matheniko ambao wote hao wanatoka kwenye jamii ya Wakaramajong.

Vita hiyo ya aina yake ilizuka baada ya wabokora kuwa vamia kabila la wafugaji la Matheniko katik akijiji chao cha Moru Ariwon.

Zaidi ya watu 200 waliuawa papo hapo wakati wa mapambano hayo ambapo mifuo yao pia ilitekwa nyara.

Katika harakati za Majeshi ya Serikali ya Uganda kutuliza mapambano hayo ya kikabila, Helikopta ya jeshi hilo ilifyatua risasi katika eneo la Kalosarich siku ya Ijumaa na kuua idadi isiyojulikana ya mashujaa wa vita hivyo vya kikabila. Lakini yafikiriwa waliokufa ni toka kabila la Bokora.

Shirika la kutoa misaada la kanisa la Kulutheri lililo chini ya shirikisho la kanisa hilo LWF 'Lutheran World Federation' siku ya Jumamosi iliwasafirisha majeruhi kadhaa wa vita mpaka hospitali ya Morotho.

Mwakilishi wa jumuiya ya ulaya EC, Mjini Kampala Bw. Bernard Ryelandt ambaye alilitembelea eneo la vita siku ya Jumatatu amesema kuwa makundi mbalimbali ya kijamii, viongozi wa jadi, wabunge wa maeneo hayo na vyama vya kiserikali tayari vimeketi pamoja mezani kujadili nini kufanyike kufikia muafaka wa amani.

Bw, Ryelandt, amesema kuwa jumuiya ya ulaya ipo tayari kutoa msaada wa hali na mali katika kusaidia kuleta amani kwa makabila yaliyoko mashariki mwa Uganda.

Wachambuzi wa mambo nao pia wamesema kuwa kitendo cha Wabokora kuwavamia Wamatheriko hivi karibuni bila ya shaka ilikuwa ni kulipiza kisasi kufuatia uvamizi uliofanywa na Matheniko mwishoni mwa mwezi Julai katika kijiji cha Wabokora kiitwacho Turutuko.

Nazo taarifa zingine kutoka maeneo hayo ukame na njaa iliyokumba imechangia jamii ya makabila hayo ya Karamajong kuhamahama na kuzusha mtafaruku miongini mwao.

Mwingiliano wa utamaduni wa sasa ambao umepelekea wakaramajong kuacha kutumia silaha zao za jadi za zamani kama mikuki, pinde na mishale na kutuulia Bunduki za Kisasa imezidisha wasiwasi mkubwa.

Wakaramajong pia mara nyingine huvuka mpaka na kuingia nchini jirani ya Kenya kuvamia kabila la Waturkana.