Vatican yaandaa Kongamano la maprofesa duniani

lMamia yao kukutana na Papa Sept 2000

Vatican City

MAPROFESA kutoka kona zote za dunia wanatarajia kukutana mjini Roma na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Yohane Paulo wa Pili ili kushiriki katika jubilee ya maprofesa wa vyuo vikuu ambayo inalenga kuimarisha ushirikiano wa pamoja kama Wakristo katika nyanja za sayansi ubinadamu na sanaa.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la kanisa Katoliki tukio hilo linaandaliwa na Idara ya Elimu na utamaduni katika Baraza la Kipapa mjini Vatican. Maprofesa hao wanatarajiwa kukutana na Papa kuanzia Sept 4-10 mwaka 2000 ambapo pia watahitimisha kongamano lao kwa kusali misa maalumu na Papa.

Wiki za kongamano hilo zitakuwa zimegawanywa katika sehemu mbalimbali ambapo katika awamu ya kwanza ya kongamano itakayoanzia Sept 4-8 semina tofauti zitaendeshwa zitakazojadili mwelekeo wa vyuo vikuu vya Kikristo katika Uinjilisti.

katika awamu ya pili na ya mwisho ya kongamano hilo kuanzia sept 9-10 jubilee ya kidini itafanyika itakayoandamana na mkutano wa uso kwa uso na kiongozi wa Kanisa katoliki Duniani.

Habari zilizopatikana mjini Roma zimeeleza kuwa kilele cha mkutano wa maprofesa hao na Papa kitakuwa ni Sept 8 ambapo pia maproesa hao watapata wasaa wa kutoa mada zao mbele ya Papa.

Alasiri ya Jumamosi hiyo misa kadhaa zitaendeshwa katika Kanisa Kuu la "Roman Basilicas"katika lugha mbalimbali na siku inayofuata ya Jumapili Papa atasherehekea misa maalum ya Jubilee katika kanisa la Mtakatifu Petro lililoko jijini Roma .

Waandaaji wa kongamano hilo wamesema kuwa maprofesa wa vyuo vikuu ni wale waanao tarajia kutunukiwa heshima ya Uprofesa

 

Chuo kikuu cha Bethlehem chabatiza kiti jina la Kardinali wa Uingereza

lNi hayati Kardinali Basili Hume

Bethlehem, Israel

Chuo Kikuu cha Bethlehem kimeamua kumwekea kumbukumbu Kardinali mmoja aliyefariki hivi karibuni kwa kubatiza jina lake kiti, kinachotumiwa na mkuu wa kitivo chake kimojawapo.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana mjini Bethlehem kupitia kwa Shirika la Habari la Kanisa Katoliki ZENIT", kiti hicho kitakachopewa jina la aliyekuwa Askofu mkuu wa Uingereza na Wales, hayati Kardinali Basil Hume, ni kile kinachotumiwa na Mkuu wa kitivo cha Elimu ya Kidini katika chuo hicho.

Hayati Kardinali Basil Hume, alifariki Mwezi Juni mwaka huu akiwa na umri wa Miaka 76 baada ya kuugua ugonjwa wa kansa kwa muda mrefu.

Brother Vincent Malham ambaye ni Rais wa Chuo Kikuu cha Bethlehem amesema kuwa toka awali hata kabla Kardinali Hume hajafa, tayari uongozi wa Chuo ulishaafikiana kukipa kiti hicho jina lake ikiwa kama kumbukumbu ya kulienzi jina lake kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kupigania haki na amani.

Chuo Kikuu cha Bethlehem kinaendeshwa na Wamisionari wa "De La Salle Brothers" na kilianzishwa rasmi na Papa Paulo wa sita kunako mwaka 1973, ili kusaidia kudumisha Ukristo kuwepo katika maeneo ya Mashariki ya Kati hususan Israel.

Chuo hiki kimepitia wakati mgumu, hasa vita vilipokuwa vikilipuka mara kwa mara huko Israel ambapo nyakati zingine ilibidi kifungwe kwa ajili ya usalama wa walimu na wanafunzi huku madarasa ya kisiri yakiendeshwa kwenye nyumba za Maprofesa wake.

Chuo kikuu cha Bethlehem kwa sasa kinavyo vitivo vipatavyo vitano na wanafunzi 2,000 Waarabu. Huku asilimia 68 ya wanafunzi chuoni hapo wakiwa ni Waislamu. Kiti hicho kilichopewa jina la Kardinali kitakuwa moja ya vitu vitakavyotunzwa chini ya uangalizi wa kitivo cha sanaa.

Kanisa kubwa la kihistoria lateketezwa na Moto Marekani

New York Marekani.

KANISA kubwa la kihistoria linalojulikana kama "Our Lady of Perpertual help church" lililoko Holyoke jimbo la Massachusetts Marekani yapata umbali wa maili 90 Magharibi mwa jiji la Boston limeteketezwa vibaya kutokana na ajali ya moto.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kanisa Katoliki (ZENIT) Kanisa hilo lililojengwa katika karne ya 19 lilishika moto mnamo siku ya Jumapili iliyopita huku mchungaji akishuhudia kwa macho yake.

Ilikuwa ni kana kwamba mchungaji huyo Fr. J. Lessard amefika katika kituo chake kipya cha kazi akiwa na mkosi kwani Jumapili hiyo ambayo kanisa hilo lilishika moto ndiyo alikuwa amewasili Holyoke akitoka Springfield alikokuwa amehamishiwa. Kulingana na taarifa za Shirika la Habari la Assiciated Press, Moto huo mkubwa ulizuka kunako majira ya saa moja usiku katika jengo moja kubwa lililoko mtaa wa Elm na ndipo ukawaka na kusambaa na kufikia jengo la kanisa kongwe la "Our Lady of Perpetual Help Church"

Amy Fitzgerald mfanyakazi wa zamani wa kanisa hilo ni mmoja wa watu walishuhudia kwa macho watu yao jengo hilo la Kihistoria likiteketea alikuwa na haya ya kusema .

"Its like a piece of history and it's gone"

"kilikuwa ni mithili ya kipande cha kihistoria na limetoweka". Msichana huyo aliliambia shirika la habari la AFP pale alipohojiwa kuhusu kuungua kwa kanisa hilo.