Mapadre na masista hawatakiwi kuondoka Kosovo

Kosovo,

Serikali ya Yugoslavia imesema kuwa mapadre na watawa wenye hati za kusafiria za Serbia wanaweza kuitwa wakati wowote na jeshi la nchi hiyo kutoa huduma wakati wa vita.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Zenit, mapadre na watawa hawaruhusiwi kuondoka nchini Yugoslavia wakati huu wa vita na majeshi ya NATO na wakifanya hivyo watachukuliwa kama wasaliti.

Shirika hilo limesema kuwa kwa wakati huu hawapewi ruhusa yoyote ya kuondoka nchini humo hata kama kuhudhuria mikutano waliyoalikwa.

Mikutano mingi hivi sasa ni ile ya kuratibu mipango ya kutoa misaada kwa walioathirika na vita.

Gazeti moja la kila siku la Italia limekaririwa likisema kuwa ujumbe wa Belgrade haukuwepo hata kwenye Mkutano Mkuu wa Caritas International uliofanyika huko Zagreb, Croatia.

"Niliomba ruhusa kwenda kwenye mji mkuu wa Croatia kwa siku chache, lakini sikupewa hata jibu", anasema Padre Antun Pecar.

Padre Pecar ni Mkurugenzi wa Caritas-Serbia na Paroko wa Parokia ya Nis nchini Yugoslavia.

Taarifa hiyo inasema kuwa mapadre na watawa wenye umri wa kufikia miaka 60 wanaweza kuitwa kwa ajili ya kutoa huduma

Amri hiyo haijali hata kama ni wa taifa jingine alimradi awe na hati ya kusafiria ya Yugoslavia.

Kati ya mapadre na watawa 200, ni Askofu Mkuu Franc Perco tu aliye zaidi ya miaka 60 na msaidizi wake wabaweza kusafiri.

Hata Askofu msaidizi Gasparovic wa Diakowo, kusini mwa Croatia, anafungwa na kizuizi kwani ana hati ya kusafiria ya Yugoslavia kutokana na kutoa huduma katika jimbo la Serbia linalojumuisha uwanja wa ndege wa Belgrade. Wakati wa Pasaka mamlaka yalijaribu kumzuia kurudi Diakowo na alipata shida ya kupata ruhusa ya kuondoka.

"Ingekuwa siyo vibaya sana kama wangeiruhusu ingawaje Caritas kushughulikia na kukusanya misaada," alisema Padre Antum na kuongeza "lakini kipingamizi chao dhidi ya shughuli za Cariotas kumeacha maghala tupu kwa wiki kadhaa na kibaya zaidi, hairuhusiwi hata kupokea misaada."

Misaada tunayotumiwa, ambayo ni mingi, hasa kutoka Italia, inakwenda moja kwa moja kwenye chama cha Msalaba Mwekundu, ambacho kinagawa bila hata kuwasiliana nasi. Mara nyingi tumeonyesha nia ya kushirikiana na kumsaidia kila mmoja, lakini tunapaswa kupewa uhuru wa kwenda kokote katika eneo hili," alimalizia.

Wakati huo huo, Kiongozi wa Kosovo mwenye siasa za wastani Bwana Ibrahim Rugova ametoa mwito wa kusali kwa ajili ya Mapadre walioko Kosovo na hasa Askofu Mark Sopi, ambaye ameamua kukaa na wale watakaokaa humo ili kuwapa nguvu.

Wito huo aliutoa mwishoni mwa vijilia ya kuomba amani kwa ajili ya Yugoslavia, iliyoandaliwa Basilika ya Santa Maria huko Trastevere.

Siku hiyo hiyo Bwana Rugova alimwambia Papa Yohane Paulo wa Pili kuwa Kosovo hivi sasa ni jangwa na Pristina ni jiji la mizuka. Hata hivyo Askofu Mark Sopi wa Kanisa Katoliki mwenye umri wa miaka 61, Askofu msaidizi wa waumini wa Kialbania huko Kosovo ameamua kubaki kwenye jangwa hilo.

Bwana Rugova aliliambia shirika la Habari la Vatican ‘Fides’ kuwa alipoandoka Yugoslavia kwenda Italia, Askofu Sopi alikuwa bado huko Prizren, pamoja na Padre Karrice, Gombera wa seminari na watawa kadhaa. Hizi ni habari za kwanza za Askofu huyo ambaye alikuwa hajulikani aliko kwa muda wa wiki tatu.

Wiki iliyopita, Askofu Farhat Edmond, Balozi wa Vatican katika nchi za Slovenia na Macedonia, alituma ujumbe huko Skopje (Macedonia) kupata habari za askofu huyo aliyebaki Kosovo.

Simu ya Askofu Sopi ilikuwa haifanyi kazi kwa wiki kadhaa, ikiwa ni matokeo ya mabomu ya NATO.

Mei 3 mamlaka ya Serbia yalimwambia Balozi huyo mjini Belgrade kuwa Askofu Sopi alikuwa salama katika nyumba yake.

Rugova ametoa mwito wa kumwombea Askofu Sopi ambaye ni rafiki yake na wanafanana katika mawazo ya kutafuta muafaka kwa mazungumzo hali ambayo Rugova amekuwa akiitetea wakati wote katika kampeni zake za kisiasa.

Rugova alithibitisha kuwa Askofu yuko Prizren na kwamba ameamua kubaki Kosovo ili kuwatia moyo wale wote walioamua kukaa kwenye nyumba zao.

Kabla ya vita kulikuwa na Wakatoliki 60,000 huko Kosovo wote wakiwa ni Waalbania isipokuwa Wacroatia 1,500. Kuna Parokia 23 na Mapadre 37.

Waabudu Shetani wanavyotazamwa nchini Zimbabwe

Harare, Zimbabwe,

"UNAMWONA mwanamke? Ni mtu wa kikundi cha Waabudu Shetani" kijana mmoja alimwambia nduguye huku akinyoosha kidole kwa mwanamke mmoja wa makamo aliyekuwa akipita katika mtaa wa First Street Mall, mjini Harare, Zimbabwe.

Kuwaita watu wengine wa kishetani sasa ni jambo la kawaida na lililozoeleka nchini Zimbabwe,lakini watu wengi hujiuliza kwanini hawa waabudu shetani wanaongelewa sana? Mengi yamesemwa kuhusu ibada ya za wazi za waabudu shetani, lakini yaonekana mazungumzo juu ya dini hiyo hayapoi labda kwa vile yanagusa sana hisia za wengi. Ibada za Waabudu Shetani zinadaiwa kuhusisha makafara kama vile kunywa damu za watu au hata kula nyama za watu.

Jumuiya ya Waabudu Shetani ni ya kimataifa inayoaminiwa kuwa na makao yake makuu huko Honolulu,nchini Marekani. Makao makuu katika bara la Afrika yanasadikiwa kuwa yako huko Burkina Faso, Afrika Magharibi. Watu wengi wamekuwa wakitoa wito kwa serikali mbali mbali duniani wakitaka dini au ibada za Waabudu Shetani zifuatiliwe na kupigwa marufuku. Nchini Zimbabwe Wizara ya Sheria na Masuala ya Bunge imesema serikali haina mpango wowote wa kufungua mashtaka wala kupiga marufuku Waabudu Shetani kwa vile hakuna kipengele cha sheria cha kusimamia ili kuchukua hatua hiyo.

Katiba ya Zimbabwe inalinda haki ya kila raia kuabudu akitakacho na atakavyo katika dini yoyote, ili mradi havunji sheria za kimsingi za nchi, hali ambayo inafanya kukosekane uwezekano wa kuhoji au kuyadadisi au kuyachukulia hatua makanisa au vikundi ambavyo vinatajwa kujihusisha na ibada hizo ziitwazo za Shetani.

Kuzuka kwa vikundi hivi vya "kishetani" ni moja ya dalili zinazoonyesha kuwa Bwana Yesu yu karibu kurejea, anasema Mwinjilisti Admire Kasingakore.

Badala ya Wakristo kuzipigia kelele Serikali zipige marufuku vikundi vua Waabudu Shetani wanapaswa kukaza uzi katika maombi na kujiandaa wao wenyewe kwa ajili ya ujio wa mara ya pili wa Bwana Yesu, ndivyo asemavyo Kasingakore.

Anasema dalili ziliztabiriwa za kurejea kwa Bwana Yesu nyingi zake tayari zimetimia na chache zilizosalia zinatimia hivi sasa. UKIMWI, anasema ni moja ya maradhi mabaya yaliyotabiriwa na hali za vita zilizopo siku hizi na zo pia zahimiza Wakristo wajiandae.

Katibu wa Idara ya Mawasiliano ya Jamii wa Baraza la Maaskofu Katoliki la Zimbabwe, Padre Oscar Wermter yeye anapinga kwamba kuwemo kwa vikundi vya kiajabu ajabu vya kidini ni dalili kwamba Yesu yuko mlangoni. Aanasema hayo ni madai ya kubahatisha tu.

"Miaka mingi iliyopita Mkorea mmoja alitangaza kwamba Yesu atarudi akasababisha watu wauze mali zao zote kujiandaa na hakuna lililotokea,"anasema Padre Wermter na kuongeza kwamba japo hapingi kuwepo kwa vikundi vya Ibada za kishetani anaamini watu wamekuwa wakipewa hamasa potofu kuhusiana na na uwepo wao na mwisho wa dunia.

Anasema vikundi hivyo ni sawa na vile vya waganga wa kienyeji ambao hutoa ahadi za kuwatajirisha wateja wao huku wakiwadai wafanye mambo yasiyofaa.

Naye Stanley Nherera, Mchungaji mwandamizi wa kanisa la "Utakaso wa Bwana" (Lord Sanctuary Church) yeye anasema ufumbuzi wa tatizo la kuwepo kwa waabudu Shetani unapaswa kuwa wa kiroho badala ya kuwa wa kimwili kama ule wa kuwapiga marufuku.

"Sio jukumu la Serikali kupiga marufuku dini ya Shetani bali ni juu ya Kanisa kwa sababu lina uwezo wa kiroho wa kupambana na Shetani" anasema na kuongeza kwa kupinga madai kwamba vikundi hivyo vimezeka nchini Zimbabwe kwa sababu ya mgawanyiko uliopo katika kanisa.

Naye msemaji wa Cahama cha Wganga wa Jadi wa Zimbabwe (Zinatha) Peter Sibanda anasema dini ya Waabudu Shetani ni ya zamani kama zilivyo nyingine na japo anaipinga anasema mradi tu nguvu za kichawi zingalipo duniani hakuna uwezekano wa kuitowesha hiyo.

Imetafsiriwa kutoka kijarida cha All Africa News Agency-AANA.