Walutheri kujitenga na serikali mwakani

STOCKHOLM, Sweden

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kilutheri wa Uppsala, nchini Sweden, K.G. Hammar amesema kuanzia mwaka kesho kanisa lake halitakuwa tena taasisi ya Serikali kama lilivyo sasa.

Askofu Hammar amekaririwa na Shirika la habari la ZENIT hivi karibuni akisema kuwa hatua hiyo ni ya muhimu kwa mataifa ya magharibi kwani hali ya sasa ya kanisa na serikali kuwa kitu kimoja pia imekuwa ikileta matatizo.

Mfumo wa kanisa kuwa taasisi ya kiserikali nchini Sweden ulianza katika karne ya 17 ambapo maaskofu na mashemasi wote huteuliwa na serikali.

"Yote hayo yatafikia kikomo mwaka kesho wakati kanisa litakapoanza kuteua viongozi wake lenyewe na kujiwekea taratibu zake," imesema taarifa ya shirika la ZENIT.

Hata hivyo hali hiyo haitaathiri hali ya kifedha ya kanisa la Kilutheri ambalo ndilo lililoungana na serikali kwani bado serikali itakuwa na jukumu la kuwakata wananchi wake kodi kwa ajili ya shughuli za kanisa. Badiliko dogo litakalokuwepo ni kwamba tofauti na ilivyo hivi sasa, wale wasio Walutheri hawatakatwa tena kodi kwa ajili ya shughuli za kanisa.

Askofu huyo Mkuu amesema awali kulikuwa na upinzani kutoka kwa Walutheri ambao hawakutaka kupoteza hadhi yao ya kiserikali na nguvu za kidola, lakini hivi sasa asilimia 95 ya Walutheri wa nchi hiyo wamekubali mabadiliko hayo.

Upinzani huo uliondolewa kutokana na ahadi ya serikali kwamba vikundi vya Kilutheri vitatambuliwa kisheria kama "jumuia rasmi" kwa maana kwamba japo hawatakuwa tena taasisi za serikali watakuwa na hadhi ya juu kuliko taasisi nyingine zote nchini humo.

Askofu huyo amesema kwamba hatua hiyo pia ni ya muhimu katika mpango wa Kiekumene wa kuleta umoja wa kanisa duniani.

Kichwa cha msichana chakatwa na kufanywa mpira wa miguu

WAKATI vikundi vya haki za binadamu duniani kote vikipinga matumizi ya watoto wadogo katika jeshi, taarifa ya kusikitisha iliyotolewa na kikundi kimoja kinachopinga ukatili huo nchini Uswisi imesema, kundi la wauaji la vijana wa kati ya miaka12 na 17, lilimvamia na kumkata kichwa msichana katika kijiji kimoja nchini Algeria na kisha kutumia kichwa chake kama mpira wa miguu.

Kwa mujibu wa taarifa inayorejea Shirika la habari la Vatican "Fides," zaidi ya watoto 120 wa chini ya umri wa miaka 18 wamekuwa wAakipewa mafunzo ya kijeshi barani Afrika ambapo baadhi yao ni wa umri wa miaka 7.

Habari zinasema nchi zinazojihusisha zaidi na matumizi ya watoto vitani ni Algeria, Angola, Burundi, Congo-Brazzaville, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Watu wa Congo, Liberia, Rwanda, Sierra Leone, Sudan na Uganda.

Taarifa zaidi zinasema kuwa nchini Burundi pamoja na kutoa mafunzo hayo ya kijeshi kwa watoto kikundi cha Watutsi kimeunda doria ya vijana na watoto wenye umri wa kati ya 12 na 25 kwa ruhusa ya mamlaka zinazohusika.

Habari hizo zinaongeza kuwa kikundi cha wapinzani cha Wahutu pia kimewafunza watoto wa chini ya miaka 15 wakati Sierra Leone imewafunza kijeshi watoto wa miaka 7.

Nchini Uganda kikundi cha Jeshi la Lord’s Restance Army (LRA),kinachoipinga serikali ya Rais Yoweri Museveni, linahusika na matukio ya kuwabaka watoto wa shule na wa majumbani na habari zaidi zinasema watoto wanaofanya jaribio la kutoroka au kujificha wanauawa kikatili kama wanavyofanyiwa wanaokataa kujiunga na jeshi.

Mnamo Januari mwaka huu, jeshi la Serikali ya Uganda nalo liliwaua kikatili vijana watano wa kati ya miaka 14 na 17 wakidhaniwa kuwa wafuasi wa upinzani.

Katika nchi nyingi za Kiafrika umri wa watu wanaotakiwa kujiunga na jeshi kwa kujitolea ni kuanzia miaka 18; isipokuwa Angola ambayo imepunguza umri huo hadi kufikia miaka 17 ambapo Uganda katika mazingira kadhaa imepunguza hadi kufikia miaka 13.

Nchini Afrika Kusini umri wa miaka 17 umekubaliwa kwa kujitolea wakati ikifikiri uwezekano wa kuongeza umri huo hadi miaka 18.

Hali hii inawahusisha pia wasichana ambao pia wamekuwa wakipewa mafunzo hayo ya kuunga mkono juhudi za kijeshi.

Radio Vatican kutangazia wakimbizi wa Kosovo

lItasaidia kutafuta ndugu waliopoteana

VATCAN CITY

KUANZIA Mei 3 mwaka huu Radio Vatican imeanza kurusha hewani vipindi maalumu huko Albania ambavyo vitasikika katika kambi za wakimbizi katika mpaka wa Kosovo.

Habari kutoka Vatican City zinasema kila siku kati ya saa 3:00 hadi saa 4:00 usiku kituo cha kurushia matangazo cha Holy See’s kitatumia muda wa robo saa katika masafa ya kati kwa kipindi cha habari kwa Waitalia na Waalbania.

Zinasema dakika 45 zinazosalia zitatumika kutolea maoni moja kwa moja toka makambini kama njia ya uhakika ya kusaidia utafutaji na upatikanaji wa ndugu waliopoteana.

Radio Vatcan itatoa huduma hii ya habari kufuatia maombi ya mashirika ya kibinadamu ya Kikatoliki na vyombo vingine visivyo vya kimadhehebu vya Kiitalia vinavyoshughulikia athari zinazowakumba wakimbizi.

Shirika la habari za kidini la VID limepokea taarifa toka katika vikundi mbalimbali vya dini vinavyoshughulikia wakimbizi wa Kosovo vikisisitiza kuwepo kwa taarifa zinahusiana na wakatoliki. Habari zaidi zinasema kila kambi ya wakimbizi itawekewa vituo vya simu kwa ajili ya kurahisisha kupata mawasiliano ya moja kwa moja kupitia radio hiyo pale itakapobidi.