Make your own free website on Tripod.com

Mhubiri auawa kwenye mkutano wa Walokole

lWaumini waporwa pesa na hata Biblia kisha wakimbia

Mombasa, Kenya

MHUBIRI mmoja maarufu wa madhehebu ya kipentekoste (PEFA) ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi akihubiri katika mkutano wa Injili, ambapo mamia ya watu waliokuwa wakimsikiliza waliporwa vitu vyao vya thamani na hata Biblia.

Mwandishi wa Habari wa magazeti ya Nation nchini Kenya Francis Mwaka, ameliambia KIONGOZI kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki kutoka mjini Mombasa kuwa tukio hilo limetokea katika eneo la Kipini wilayani Tana River na hadi tunaingia mitambani hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa kuhusiana na mkasa huo.

Mhubiri huyo aliuawa majira ya saa 12 Ijumaa ya wiki iliyopita akiwa amepiga magoti kuwaombea Mungu awasamehe majambazi hao ambao baada ya kuvamia mkutano wakiwa na bunduki waliwaamuru watu wanyamaze kimya na kukabidhi kila kitu cha thamani walichokuwa nacho. Idadi ya majambazi hao haikuweza kufahamika mara moja.

Imeelezwa kuwa waumini hao ambao walishindwa kuamini macho yao kwa kilichokuwa kikiendelea waliamua kutimua mbio kunusuru maisha yao na kuiacha maiti ya mhubiri wao ikiwa imelala jukwaani.

Mchungaji Morris Ndung’u aliyeuawa ambaye ni mhubiri maarufu wa kipentekoste nchini Kenya amekuwa akifanya mikutani mingi nchini humo na amewahi kufanya mikutano kadhaa katika eneo alimouawa ambalo lina idadi ndogo ya Wakristo na idadi kubwa ya Waislamu.

Mkuu wa Wilaya ya Lamu Bw. Wilson Wanyanga alikaririwa na gazeti la Taifa Leo la Kenya akisema kuwa mauaji hayo hayahusishi tofauti za kidini bali ni ujmbazi wa kawaida na akasema polisi wanawasaka waliohusika na unyama huo.

Hatimaye Israeli yamwalika rasmi Papa Yohane II

PAPA Yohane Paulo II amepokea ujumbe wa Serikali ya Israeli hivi karibuni ukiwa na mwaliko wa kumtaka atembelee nchi hiyo takatifu mwakani .

Taarifa hizi zimekuja baada ya taarifa nyingine zisizo rasmi ambazo zilitolewa hivi karibuni.

Waliotembelea makazi ya Papa huko Vatican ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Israeli Bw. Ariel Sharon na mkewe. Mazungumzo kati ya Papa na Sharon yalihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Balozi wa Israeli huko Vatican.

Baada ya mazungumzo hayo Sharon, pia alifanya majadilianao na Kardinali Angelo Sodano, (Waziri wa Nchi wa Vatican na Askofu Mkuu Jean-Louis Tauran, anayeshughulikia masula ya Kidiplomasia ya Vatican.

Hata hivyo ziara hiyo ya kichungaji ya Papa huenda ikaingia dosari kwani mapema mwezi huu Israeli itafanya uchaguzi mkuu ambao unaweza kubadilisha Serikali na hivyo kuleta athari kwa hatua zilizokwishafikiwa.

Vatican imekuwa ikisema mara kwa mara kuwa Papa ataitembelea Israeli pamoja na Palestina, lakini iwapo tu hali ya kisiasa na kiusalama itaruhusu kwani lengo la ziara ni kuleta upatanisho na si mvutano zaidi.

Ziara ya Sharon pia ililenga katika kuifanya Vatican ipuuze mgogoro uliozuka kati ya Waisamu wenye itikadi kali walioazimia kujenga msikiti mkubwa mbele ya kanisa moja huko Nazareti kunyume na ushauri wa serikali hiyo inayotaka wajenge msikiti mdogo.

Waziri Mkuu huyo vile vile aliendelea kukazia msimamo wa Serikali yake kwamba kamwe hawataikaribisha Palestina ipate eneo la mji mkuu wa Yerusalemu kama ambavyo Vatican imekuwa ikishauri kwamba Wapalestina nao wapewe eneo la mji huo ili kuleta usawa.

 Mnara wa Babeli wavumbuliwa?

London, Uingereza

MTAFITI mmoja wa mambo ya kale Mwingereza amedai kugundua mahali ulipokuwa umejengwa mnara maarufu wa Babeli unaotajwa katika Biblia.

Mtaalamu huyo Bw. Michel Sanders, amesema amegundua kwamba mnara huo ulijengwa katika eneo la Pontus huko Kaskazini mwa Uturuki.

Watafiti wengi wa mambo ya kale huamini kwamba mnara wa Babeli ulikuwa katika eneo la magofu ya Mesopotamia kaskazini ya mji wa Baghdad nchini Irak.

Katika miaka ya hivi karibuni Rais Saddam Hussein akiamini kuwa mnara wa Babeli ulijengwa kaskazini ya Baghdadi alijaribu kuujenga upya kwa kujenga kuta zilizojengwa vibaya vibaya za matofali.

"Kuwepo kwa mnara huo huko Pontus kunaingia akilini zaidi hasa kulingana na maelezo ya Biblia" amesema Sanders hivi karibuni.

Sanders anaamini amelipata hasa eneo lenyewe ambalo laitwa ";Lango la Mungu" ambalo humaanisha Babeli.

Katika kitabu cha Mwanzo cha Biblia, watu wa zama za Nuhu walioongozwa na Nimrod mwana wa Kushi waliweka makao yao katika nchi ya Shinar na hapo wakabubaliana kujenga mnara mrefu ufike hadi mbinguni kwa Mungu. Hapo ndipo Mungu aliamua kuwaadhibu kwa kiburi chao na akawachafulia lugha zao ili wasielewane tena na hapo kazi hiyo haikuendelea. Huo ndio ukawa mwanzo wa lugha zote zilizoko duniani leo.

Habari hii ni kwa mujibu wa gazeti la Sunday Times la Uingereza.

 Papa kumtangaza Mwenyeheri Padre Pio leo

Vatican,

UMATI mkubwa wa watu ambao haujawahi kutokea katika historia ya Roma unatazamiwa kukusanyika leo mjini hapo katika sherehe za Papa Yohane Paulo ll kumtangaza Padre Pio wa Pietrelcina nchini Italia kuwa Mwenye Heri.

Mwenyeheri Padre Pio Mei 25, mwaka 1887 huko Pietrelcin katika nchi ya Italia. Alibatizwa Mei 26, mwaka 1887 na kupewa jina la Fransisco Maria Forione.

Alizaliwa katika familia ya ki- kristo na baba Grazio Maria Forgione na mama Maria Geuseppa di Nunzio. Alikuwa mtoto wa tano kati ya watoto wanane wa mzee Grazio. Wadogo zake watatu walikufa wakingali bado wadogo na kufanya familia hiyo kuwa ya watoto watano tu.

Wazazi wake walikuwa watu wa kawaida wanyofu na wakulima hodari. Alisomea nyumbani mpaka alipokuwa na umri wa miaka kumi na tano. Mnamo tarehe 6, Januari mwaka 1903 alijiunga na Shirika la ndugu Wafransisko Wakapuchini katika convent ya Morcone.

Aliweka nadhiri zake za kwanza Januari 22 mwaka 1903 ambapo Januari 22 mwaka 1907 aliweka nadhiri za maisha .

Agosti 10 mwaka 1910 alipata daraja la Upadre katika jimbo la Benevento kadiri ya masilimuzi. Mwenyeheri Padre Pio alikuwa akisumbuliwa na magonjwa ya mara kwa mara na mnamo Desemba 2 mwaka 1911 hadi Februari 25 mwaka 1915 alirudishwa nyumbani kwa ajili kuangalia hali ya afya yake.

Baadaye wakuu wa shirika waliamua arudi shirikani na ilikuwa Julai 25 mwaka 1916 ambapo alifahamishwa kukaa katika nyumba yao ya San Giovanni Rotondo ambapo aliishi hapo hadi Septemba 23,mwaka 1968.

Septemba 20,mwaka 1918 alionekana kuwa na madonda ya Bwana wetu Yesu Kristu mwilini mwake, yaliyomfanya kuwa Padri wa kwanza katika historia ya kanisa kupata "madonda matakatifu".

Juni 9, mwaka 1931 alitumwa mjumbe toka Roma kufanya upelelezi juu ya habari za madonda ya Padre Pio zilizokuwa zimeenea karibu kila kona ya mji wa Italia. Uchunguzi ulichukua miaka miwili na baada ya uchunguzi huo ujumbe ulitoka makao makuu ya Kanisa Katoliki Vatican kumzuia kutoka nje na kuonana na watu.

 Vatican yavaa njuga kusaidia Wakosovo

ZENIT,

BARAZA la Kipapa la Misaada ya Kichungaji kwa Wafanyakazi wa Afya linafanya uhamasishaji mkubwa kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wa Kosovo katika matatizo ya afya na madawa.

Askofu Mkuu wa Mexico ambaye pia ni Rais wa baraza hilo, Javier Lozano ameliambia Shirika la Habari la ZENIT kuwa tayari Vatican imeitisha mkutano wa dunia wa taasisi zinazoshughulika na uganga na madawa ili kuweka mkakati wa vitendo kuwasaidia wakimbizi hao.

Shirikisho moja la kimataifa liitwalo International Federation of Medical Associations liliitikia wito na hivi sasa limefungua kituo cha kutoa msaada wa madawa kwa wanawake wajawazito waliokimbia makazi yao kwa sababu ya vita.

Baraza la Kipapa pia limetoa wito kupitia Redio Vatican kwa Wafamasia na Wauguzi wa Kikatoliki kutoa kila msaada uwezekanao kuwasaidia wakimbizi hao.

Wakati huo huo, Askofu Mkuu Paul Josef Cordes amekwenda Macedonia kwa maagizo ya Papa Yohane Paulo ll kusoma hali halisi ilivyo huko kwa wakimbizi wa Kosovo na pia kufanya utaratibu mzuri wa jinsi misaada zaidi inavyoweza kutolewa na taasisi za Kikatoliki.

 Kipofu akamatwa akiendesha gari

Alikuwa akisaidiwa na bintiye wa miaka 13

Buenos Aires, Argentina,

POLISI nchini Argentina wiki iliyopita walimtia mbaroni mwanaume mmoja ambaye ni kipofu akiendesha gari, jambo ambalo lilikuwa hatari kwa maisha yake na ya watu wengine.

Shirkila la Habari la Argentian (Telam) liliripoti mwanzoni ma wiki kuwa mwanaume huyo alikuwa akisaidiwa na binti yake mdogo mwenye umri wa mika 13 na kwamba alifikishwa mahakamani nchini humo hivi karibuni kujibu shitaka la kufanya tendo la hatari.

"Alikuwa akiendesha vizuri sana barabaranii isipoluwa baadaye alifanya kosa dogo ambalo liliwashitua polisi na kuwafanya wavutike kumchunguza" Msemaji mmoja wa polisi alisema.

Polisi wamesema walishangaa jinsi jamaa huyo alivyokuwa akibadilisha gia kwa ustadi na kukanyaga mafuta na breki bila matatizo kwa msaada wa 'kibinti' chake hicho.