Waisraeli wamnyima Papa mtumbwi

lUmegunduliwa Bahari ya Galilaya ukiwa umedumu tangu zama za Yesu

lVatican ilitaka utumike kuadhimisha miaka 200 ya Injili

JERUSALEM, ISRAEL

WAKATI makala ya mambo ya kale ya Israel ilikubaliwa kuyapatia makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani (Vatican) mtumbwi wenye umri wa miaka 2000 ili utimike kuadhimisha miaka 2000 tangu Yesu aanzishe kanisa duniani Mkurugenzi wa Makumbusho ya Galilaya na maafisa kadhaa wa serikali wamepinga hatua hiyo.

Habari kutoka Israel zimeeleza kuwa hivi karibuni, Mkurugenzi huyo pamoja na maafisa wengine wa serikali ya Israel wamepinga mtumbwi huo uliogunduliwa katika Bahari ya Galilaya Januari mwaka 1986 usipelekwe Vatican kwa madai kuwa utaharibika na kuadhiri sekta ya utalii ya nchi hiyo.

Kuvumbuliwa kwa mtumbwi huo ambao hakuna ajuaye kama ni mmoja kati ya ile iliyotumiwa na mitume au Bwana Yesu au la, kulitokana na ukame wa miaka miwili uliotokea katika maeneo ya Israel na kuufanya utokeze ufukoni mwa Bahari ya Galilaya.

Mtumbwi au Mashua hiyo ilichimbuliwa na Mamlaka ya mambo ya kale na wanancchi wengine waliojitolea kutoka eneo la mashambani la Kibutz Ginogar na hivi sasa umehifadhiwa katika chumba maalum chenye udhibiti wa joto ukiwa ndani ya vioo.

Hata hivyo uchunguzi ulifanywa na timu ya wataalamu wa kimataifa ulieleza kwamba hakuna uharibifu wowote unaoweza kutokea endapo mtumbwi huo utahamishwa kwa uangalifu kwenda Vatican.

Maafisa wa Wizara ya Elimu ya Israel na mbunge wa upinzani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utalii Bw. Avi Yehezkel, wameitaka Mamlaka ya Mambo ya kale ya Israel isithubutu kuupeleka "mtumbwi" huo Vatican.

"Ni jambo la ajabu na uamuzi mbovu", Yehezkel alikaririwa akisema kupitia Radio ya Israel.

"Utaumiza utalii katika Israel, na kuiharibu ‘boti’ yenyewe".

Bibi ayala Zussman wa Mamlaka ya Mambo ya kale alisema chombo hicho kingetumika katika maonyesho ya Vatican mwanzoni mwa mwaka 2000 kwa muda usiozidi miezi mitatu na kisha kurejeshwa Israel kuwahi misimu ya utalii katika Israel ya kuchipua na kangazi.

Habari hizi ni kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kanisa Katoliki (Catholic News Service).

Kwa mara ya kwanza Rais wa Iran amtembelea Papa

lUhusiano wa Waislamu na Wakristo waongelewa

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Ulimwengu ,Rais wa Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran amemtembelea kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani,Papa Yohane Paulo ll katika makao yake makuu mjini Vatican.

Rais wa sasa wa Iran Bw. Mohammad Khatami ndiye aliyeweka historia hiyo ya pekee wiki iliyopita baada ya kutembelea makao ya Papa na baada ya maongezi ya kina yaliyohusisha uhusiano kati ya Waislamu na Wakristo, kiongozi huyo wa jamhuri ya Kiislamu alisema anarejea Iran akiwa na matumaini mapya ya siku zijazo.

Kwa upande wake Papa Yohane Paulo ll alimshukuru Rais Khatami kwa ziara yake ya mafanikio.

Rais Khatami pia alikutana na Waziri wa nchi wa Vatican Kadinali Abgelo Sodano ambapo walizungumzia pia suala la mgogoro wa Mashariki ya Kati na mazungumzo kati ya Waislamu na Wakristo juu ya masuala ya kiutamaduni.

Masuala ya haki za binadamu na jamii ya Kikristo nchini Iran nayo pia yalizungumziwa.