Wanaoshabikia utoaji mimba wagonga mwamba - UM

New York, Marekani

VIKUNDI vya watu wanaotetea mauaji kwa njia ya utoaji mimba ambavyo vilitaka utoaji mimba utangazwe na Umoja wa Mataifa kuwa miongoni mwa haki za msingi za binadamu, katika mkutano wa umoja huo hivi karibuni vimegonga mwamba.

Habari zilizokaririwa na Shrika la Habari la ZENIT mapema juma hili zimesema katika mkutano huo unaojulikana kama Cairo+5, Afisa mmoja wa Shirikisho la kimataifa la haki za uhai kwa kila mtu (IRLF) Bw. Peter Smith, alisema suala la kuhalalisha au kutohalalisha utoaji mimba katika hali yoyote liko juu ya kila taifa kuamua peke yake na si Umoja wa Mataifa.

Pamoja na mashinikizo makali ya vikundi vinavyoshabikia kwamba utoaji mimba uhalalishwe kama haki mojawapo ya binadamu katika mkutano huo uliofanyika mjini New York, Marekani hivi karibuni Bw. Smith alisema; hivi sasa vikundi vinavyoshabikia utoaji mimba havipati mafanikio kama vilivyokuwa vikitarajia.

Kauli inayofanana na hiyo ilitolewa na Jeanne E. Head, mwakilishi wa shirikisho la IRLF katika Umoja wa Mataifa. Alisema kumekuwa na ukuzaji wa mambo kupita kiasi kulingana na maazimio ya mkutano wa Cairo+5 wa hivi karibuni.

Alipinga wazo la kuutaka Umoja wa Matifa utangaze utoaji mimba kuwa miongoni mwa haki za binadamu na akasema mkutano huo haukuwa na uwezo wa kufanya hivyo.

Mkutano wa Cairo+5 ulifanyika mjini Cairo, Misri miaka mitano iliyopita ambapo suala la haki ya utoaji mimba lilipigiwa debe kwa nguvu, na mashabiki wa utoaji mimba walitaka maazimio ya Mkutano huo yatumike kuushawishi Umoja wa Mataifa ukubaliane na ajenda hizo za mauaji.