UNITA yateka miji muhimu

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

KUNDI la waasi wa Angola, UNITA, wameteka mji muhimu uliopo kilomita 500 kaskazini mwa mji mkuu wa Luanda.

Habari zilizokaririwa na IRIN zinasema kwamba mji wa M'banza Congo ulitekwa baada ya mapigano makali ya siku kadha.

Habari zilizokaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC kutoka kwa waziri wa ulinzi wa Angola Bw.Pedro Sebastiao zimesema kwamba mji huo ulitekwa katikati ya wiki.

Kutekwa kwa mji huo kutarahisisha majeshi ya UNITA kusonga mbele zaidi na kuwa katika nafasi ya kuteka maeneo yanayozalisha mafuta kwa wingi ya Soyo.

Akizungumza na Radio moja ya Ureno ambayo ndiyo iliyonaswa na BBC. Atena 1 radio waziri huyo amesema kwamba mji huo ambaop uko katika jimbo la Zaire ni njia ya kuelekea kwenye mji wa Soyo.

Msukumo wa sasa wa kivita ambao unakwenda sambamba na kauli ya serikali ya kusitisha makubaliano ya Lusaka na chama cha UNITA na badala yake kuendelea kuwa na uhusiano na kundi lililojitenga, kumesababisha pia Umoja wa Mataifa kutaka kujiondoa nchini humo.

UNITA imekuwa iklaumiwa kwa kuacha kutekeleza makubaliano ya Lusaka ambapo walitakiwa kuwanyang'anya askari wake silaha na pia kukabidhi miji iliyoteka kwa serikali.

Umoja wa Mataifa baada ya kuona vita vinasamba kwa kasi na ndege zake mbili kutunguliwa imepunguza jeshi lake kutoka maeneo ya kati na milimani na kuwarejesha Luanda kwa usalama wao.

Ingawa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka asakari wote na maafisa wengine wa Umoja wa Mataifa waondoke nchini Angola, Marekani Ureno na Russia wametaka kundi dogo libakishwe.

 

Kardinali apinga kutwaliwa kwa nguvu kwa watu wenye asili ya Kitutsi

KINSHASA, Congo

ASKOFU Mkuu wa Kinshasa amepinga kukamatwa kwa watu kadha waliokuwa wakihifadhiwa katika kituo cha Betania.

Askofu huyo amesema kwamba watu hao waliwekwa hapo kwa maombi ya serikali wakingoja kusafirishwa kurejeshwa Rwanda na amesitushwa na kitendo cha askari kuja kuwatwaa kwa nguvu na kuwapeleka katika kambi ya kijeshi ya Kokolo.

Zaidi ya watu 30 walikuwepo katika kituo hicho ambacho huhudumiwa na Kanisa.

Askofu Mkuu huyo Mhashamu Frederic Kardinali Etsou Nzabi Bamungwabi, licha ya kushutumu kukamatwa kwa watu hao ametaka fedha zilizoporwa kutoka katika kituo hicho zirejeshwe na pia madirisha na vifaa vingine vilivyoharibiwa wakati wa operesheni hiyo ya kijeshi vitengenezwe.

Shirika la kutetea msamaha kwa wafungwa Amnesty International limesema kwamba baadhi ya watu hao waliokamatwa walionyeshwa katika televisheni ya serikali Januari 17, mwaka huu.

Kamanda wa brigedi ya 50 ambaye ndiye aliyetoa agizo la kutwaliwa kwa watu hao amekanusha madai ya Kardinali na kudai kuwa wamisionari wa Kikatoliki walikuwa wanatumiwa na watu wa nje kwa ajili ya kuleta hali mbaya katika taifa hilo.

Kamanda huyo alisema hayo katika taarifa yake aliyoitoa kwa gazeti la kila siku la 'Le Palmares' .

OLF yadai yawauwa askari 62 wa Ethiopia

ADDIS ABABA, Ethiopia

Chama cha Oromo Liberation Front, OLF, kilisema kwamba mnamo usiku wa Ijumaa kiliwaua askari 62 wa Ethiopia, kikawajeruhi 20 na kuwateka nyara wengine 18 kwenye shambulio lililofanyika katika kambi za kijeshi za serikali zilizoko Tuqa na Hidi-lola katika eneo la Borana.

Taarifa ya OLF iliyopokelewa na IRIN ilisema kwamba majeshi yake pia yaliteka silaha na risasi. Taarifa hiyo iliongezea kusema: "Ghala mbili zilizokuwa zimejaa mahitaji ya misaada iliyokuwa isambazwe kwa wakaazi wa maeneo ya karibu, lakini yaliyonyakuliwa ili yatumiwe na jeshi la Watigray, zilitekwa na kugawiwa raia."

Wakati huo huo, serikali ya Kenya inashikilia msimamo wake kwamba kuna amani katika upande wa Kenya wa mpaka, kinyume na taarifa zilizotolewa na magazeti ya humo nchini kwamba majeshi ya Kenya yalipambana na majeshi ya Ethiopia kwenye mashambulizi makali.

Afisa polisi mmoja wa ngazi ya juu aliiambia IRIN: "Hakuna matatizo yoyote upande wa Kenya.

Hakuna askari wa Ethiopia waliovuka hadi Kenya na hatufichi chochote kwa yeyote. Naibu Kamishna wa Polisi wa ngazi ya juu, David Munuhe, alisema: "Ukweli ni kwamba mnamo siku ya Ijumaa, kulikuwa na mapigano huko Ethiopia katika maeneo ya Hidilola, Tuqa na Magado yaliyoko kati ya kilometa 15 - 18 kutoka mpaka wa Kenya.

Baada ya mapigano hayo wanamgambo sita wa OLF waliomba uhifadhi nchini Kenya kijijini Damballa Fanchana. Wanamgambo hao sita walishindwa kujitambulisha, wakarushiana risasi kwa muda mfupi na polisi-kanzu wa Kenya walioko kwenye eneo hilo."

Msemaji wa Ubalozi wa Ethiopia, Wondimu Asamnew, aliiambia IRIN hangeweza kutoa taarifa yoyote kwa sababu mawasiliano na Addis Ababa yalikuwa yamekatika.

Alisema: "Nina uhakika wizara zinazohusika zinashughulikia swala hilo na muda usio mrefu tutatoa taarifa rasmi."

Annan kumtuma Sahnoun kama mjumbe maalum

WASHINGTON, Marekani

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan alitangaza kwamba Mohamed Sahnoun, mjumbe wake maalum huku Afrika, atatumwa ili "kusaidia juhudi za kidiplomasia" zinazofanywa na Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU, na Marekani katika kusuluhisha mgogoro wa Ethiopia na Eritrea.

Sahnoun anatazamiwa kusafiri hadi eneo hilo hivi karibuni. Annan ameeleza kutoridhika kwake katika "uadui unazidi" kati ya nchi hizo mbili, ambao wamekuwa na mgogoro wa mpaka tangu Mei 1998.

 

ADF yawaua watano na kuwateka wengine sita

KAMPALA, Uganda

GAZETI linalomilikiwa na miongoni mwa wengine, serikali ya Uganda, 'New Vision', limewakariri wasemaji wa usalama wakisema kwamba watu watano waliuawa na wengine sita wakatekwa kwa nguvu na waasi wa Allied Democratic Forces, ADF, katika matukio tofauti huko magharibi mwa Uganda.

Mashambulizi hayo yalifanyika katika kipindi cha wiki mbili zilizopita katika wilaya za Kabarole na Bundibugyo. Waasi hao ambao wanaelezwa na majeshi ya serikali kama watu wanaoendesha shughuli zao katika vikundi vidogo na kwamba ni hohehahe na wenye njaa. Pia inasemekana walivunja maduka na kuiba chakula na mahitaji ya hospitali.

 

Mahakama yanuia kuharakisha kesi za mauaji ya kikatili

KIGALI ,Rwanda

Mahakama ya Kimataifa kwa Rwanda wiki hii ilitangaza kwamba itaanza kutekeleza hatua za kuharakisha kesi za watu waliotuhumiwa kushiriki katika mauaji ya kikatili ya 1994. Hatua zilizochukuliwa mwaka jana ni pamoja na uamuzi kwamba hukumu na kusomwa kwa hukumu kutafanyika mara moja na sio kwenye siku mbili tofauti.

Taratibu hizo mpya zitatekelezwa Jumatatu ijayo katika kesi ya Alfred Musema, aliyekuwa mkurugenzi wa kiwanda kimoja cha chai huko tarafani Kibuye.

Anashtakiwa kwa makosa saba ya mauaji ya kinyama, kupanga kisiri kuua kikatili, jinai dhidi ya ubinadamu na ukiukaji mbaya wa Kaida ya Geneva. Alipoonekana kwa mara ya kwanza mbele ya mahakama hiyo mwezi wa Novemba mwaka jana, alikanusha mashtaka hayo yote.

 

Zambia yaionya Angola

LUSAKA, Zambia

Gazeti la 'The Post' liliripoti mnamo siku ya Jumatano kwamba RaisFrederick Chiluba wa Zambia alionya kwamba nchi yake itajilinda iwapo Angola itaamua kuishambulia.

Akijibu madai ya serikali ya Angola kwamba Zambia inawasaidia waasi wa chama cha UNITA, Chiluba alilieleza dai hilo kama la "kusikitisha sana" kwa sababu Lusaka haina nia kisiasa wala fedha kujihusisha na mgogoro wa Angola.

Kulingana na Chiluba, wanaotoa madai hayo wanataka kuitatanisha nafasi ya Zambia kama mpatanishi wa mgogoro wa DRC.

 

Duru ya nne ya mazungumzo ya Burundi yaanza

ARUSHA, Tanzania

Duru ya nne ya mazungumzo ya amani ya Burundi ilifunguliwa huko Arusha huku mpatanishi Julius Nyerere akitoa mwito kwa washiriki "wasirefushe bure" jitihada hizo.

Alisema: "Hatuwezikumaliza karne hii bila kuwapatia watu wa Burundi matumaini," shirika la habari la kujitegemea la Hirondelle liliripoti.

Miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa katika mazungumzo hayo ni kuondolewa kwa vikwazo vya uchumi vilivyowekewa serikali ya Burundi, kukijumuisha kikundi cha CNDD-FDD katika juhudi za amani na kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa.

Nyerere alimpendekeza jenerali mmoja wa Afrika ya Kusini kuwa naibu wa Padre Matteo Zuppi wa jamii ya Italian San'Egidio katika tume ya amani na usalama.

Juhudi za Arusha za kuleta amani zimegharimu dola milioni 1.1 tangu mwezi Juni hadi Desemba 1998 na inatazamiwa kuongezeka hadi dola milioni sita ifikapo Juni 1999.

Nyerere alisisitiza kwamba wahisani hawatapenda kugharamia mazungumzo yasiyokuwa na mwisho.