Make your own free website on Tripod.com

Vatican Yashauri Uvumilivu wa Kidini

GENEVA, Uswisi

 

VATICAN imesema aina mpya ya kutovumiliana kidini inaibuka ambayo inakiuka haki ya dini kueleza misingi na kanuni zake kwenye maisha ya hadharani.

Ushauri huo ulitolewa na mwakilishi wa Vatican katika mkutano wa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, Askofu Mkuu Silvano Tomasi mkutano ambao unamalizika Aprili 23 mjini Geneva.

“Hali ya kutovumiliana kidini inayoibuka kichinichini inapinga haki ya dini kueleza mambo yake waziwazi juu ya masuala ya aina za tabia ambazo zinapimwa kwa kufuata kanuni za maadili na misingi ya dini,” alisema.

“Wakati hali nzuri ya dola kutokuwa na dini rasmi inabidi iheshimiwe, wajibu wa waamini katika maisha ya umma unapaswa kutambuliwa,” alisema Tomasi.

“Hili linahusiana na haja ya kuwepo vyama vingi vya siasa na kuchangia kujenga demokrasi halisi, miongoni mwa mambo mengine. Dini haiwezi kusukumizwa katika pembe ya maisha binafsi na kwa njia hii kuhatarisha hali yake kijamii na huduma yake ya   wahitaji bila ubaguzi,” alisema mwakilishi huyo wa Vatican.

Askofu Mkuu Tomasi alirejea Tangazo la Haki za Binadamu namna linavyoeleza na kukuza uhuru wa dini, ambapo alinukuu ibara ya 18 ambayo inasema: “Kila mtu anayo haki ya kuwa na uhuru wa mawazo, dhamiri na dini; haki hii inahusisha uhuru wa kubadili dini au imani, na uhuru aidha wa mtu akiwa peke yake au katika jamii pamoja na watu wengine na katika maisha ya umma au ya binafsi, kuonesha dini au imani yake kwa kufundisha, kuishi, kuabudu na kuikiri.”

Aliongeza kusema kuwa “kwa bahati mbaya uhuru wa dini unaendelea kukiukwa katika sehemu mbalimbali. Siku hizi kuna hali nyingine ya makundi yasiyo ya dola ambayo hujichukulia hatua za kudhalilisha waamini wa dini za wachache, ambayo mara nyingi huwa hayachukuliwi hatua.”

“Sehemu za ibada pamoja na makaburi yanachomwa au kuharibiwa na kubomolewa; waamini wanatishiwa, kushambuliwa na hata kuuawa, na viongozi wao wanafanywa kuwa malengo maalumu ya vitendo vyao,” alisema na kuongeza “Uwezo wa mtu kuchagua dini yake, ikiwemo haki ya kuibadili unakumbana na vikwazo vikubwa katika baadhi ya mazingira ya kijamii, ukikaji wa moja kwa moja wa uhuru wa dhamiri.” Alisema

 

 

 

 

 

Papa apendekeza Pasaka ya pamoja kwa Wakristo wote

VATICAN CITY

 

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kwa mara nyingine amependekeza Wakristo wa Magharibi na Mashariki kuadhimisha Pasaka kwa siku  moja kila mwaka.

Papa alichukua fursa hiyo kutokana na “kugongana kwa bahati” mwaka huu kwamba, Pasaka iliadhimishwa siku moja kufuatana na kalenda za Ki-Gregorian (Magharibi) na Ki-Julian (Mashariki). Kiongozi huyo alirudia tena pendekezo hilo alilowahi kulitoa miaka kadhaa iliyopita.

Baada ya kutoa baraka zake kama ilivyo desturi na kueleza salamu zake katika lugha 62, Baba Mtakatifu alielekeza salamu maalumu kwa mapatriaki, maaskofu na waamini wa Makanisa ya Mashariki, wengi wao wakiwa ni Waorthodoksi.

“Ninaomba kwa Bwana Mfufuka kwamba, sisi sote tuliobatizwa muda mfupi ujao tutaweza kuadhimisha sikukuu hii ya msingi katika imani yetu siku moja kila mwaka,” alisema.

 Pasaka ambayo ni sikukuu muhimu sana katika kalenda ya Kikristo huwa inahamishika na huadhimishwa Jumapili ya Kwanza baada ya mwezi mpevu kati ya Machi 22 na Aprili 25.

Kwa sababu ya makosa yaliyokuwa katika kalenda ya Julian (iliyoanzishwa na Julius Caesar katika mwaka 46 KK), Baba Mtakatifu Gregori wa 13 (1582 BK) aliifanyia marekebisho kwa kuzingatia vigezo vipya vya kuhesabu siku ya Pasaka. Hata hivyo, Makanisa ya Mashariki hayakuafiki kufuata mabadiliko haya.

Faharasa (appendix) ya “Sacrosanctum Concilium,” katika katiba ya dogma juu ya liturujia takatifu, Kanisa Katoliki lilieleza nia yake ya kufikia makubaliano na makanisa ambayo yalijitenga na Roma kuhusiana na tarehe ya Pasaka.

Wakati huohuo, Katika Misa ya Mkesha, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alitoa Sakramenti ya Ubatizo kwa wakatekumeni saba (7) katika Kanisa Kuu la Mt. Petro

Wakatekumeni waliobatizwa walitoka nchi za Italia, Togo na Japan. Papa alisema kwamba, tofauti hii ya mahali wanapotoka “inadhihirisha ukubwa wa mwito kwenye wokovu na zawadi ya paji la imani.”

Wairaq Watakiwa Kuishi kwa Amani

BAGHDAD, Iraq

 

ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki madhebebu ya Syrian amesema kwamba Wairaq wa dini zote wanaweza kuishi pamoja kwa amani licha   ya nchi yao kutokuwa na serikali muda mrefu.

Askofu mkuu huyo wa Baghdad, Mhashamu Athanase Matti Shaba Mattoka aliliambia shirika la habari la Fides, mara baada ya ibada ya watoto wa jimbo la Baghdad kupata Komunyo ya kwanza na kusisitiza “Wairaq wa imani zote wanaweza kuishi pamoja kwa amani.”

“Tunawaomba Wakristo wote kuwaombea watu wa Iraq katika kipindi hiki kigumu,” Askofu Mkuu Athanase Matti Shaba Mattoka aliliambia Fides.

“Wakati wote Wakristo wa Iraq wanasali na kufanya kazi pamoja kuhakikisha kwamba wafuasi wa imani zote ambazo zimekuwepo kwa miaka 1,600 waweze kuendelea. Hapa kuna hofu kwamba kunaweza kuwepo na mashambulizi katika miji wa Najaf na Falluja. Natumaini mashambulizi hayo hayatatokea kwa sababu tunaamini kuwa mazungumzo ni njia pekee ya kuondokana na vurugu,” alisisiza kiongozi huyo.

Wakati wa Pasaka Askofu Mkuu Mattoka yeye binafsi alijihusisha katika kukusanya misaada ya kutuma kwa watu wa Falluja mahali ambapo kulikuwa na mapigano makali. Askofu huyo aliongea na Fides kabla ya kwenda kutembelea familia za watoto waliokuwa wanajiandaa kupokea Komunyo Takatifu.

“Ninakaribia kwenda kwenye mkutano nje pamoja na watoto wa Baghdad ambao watapokea Komunyo Takatifu. Hili ni tendo la amani na matumaini katika wakati ujao pamoja na kuwa njia ya kushirikishana furaha ya watoto na familia,” alisema.

“Leo (Aprili 16), watoto wa madhehebu   mbalimbali ya Kikatoliki katika Baghdad watapokea Komunyo ya kwanza. Huwa tunatoa sakramenti ya Komunyo takatifu siku za Ijumaa, kwa sababu Ijumaa ni siku ya mapumziko nchini Iraq. Familia zinaweza kukutana pamoja kwa ajili ya tukio hilo licha ya hali ya ukosefu wa usalama, familia nyingi zimeandaa tafrija kwa ajili ya tuki hilo,” alisema.

Aliongeza kusema kuwa, katika wakati huu wa muhimu katika sakramenti ya Ekaristi Bwana na Mkombozi wetu Yesu Kristo anakuja kwa hawa watoto wadogo ambao ni matarajio ya hali ya baadae ya nchi ya Iraq.

Ukweli kwamba kuishi pamoja kwa watu wa imani na dini mbalimbali kunawezekana nchini Iraq ulioneshwa katika mji wa kaskazini wa Mosul, ambapo katika mji huo katika Siku ya Pasaka, Aprili 11, Wakristo walipokea vitisho. Na mara moja suala hilo lilijulikana na gavana wa Mosul, ambaye ni Mwislamu yeye mwenyewe alikwenda kutembelea jumuia za Kikristo na kuzihakikishia amani kwamba hawakuwa na kitu cha kuogopa na alisubiri na kushiriki katika misa na sherehe hiyo.