Vita na matatizo ni matokeo ya dhambi- Papa

Vatican city,

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Paulo Yohane II amewaambia vijana kuwa vita , chuki na matatizo yaliyoko duniani ni matokeo ya dhambi za wanadamu waishio juu ya uso wa dunia na kamwe Mungu asitwishwe furushi la lawama kufuatia matatizo hayo.

Akiongea na vijana katika kongamano la jioni linalofanyika Machi 25 ya kila mwaka mjini Vatican, kiongozi huyo wa kanisa alisema kuwa wakati wanadamu wanapopatwa na matatizo ya aina hiyo imekuwa ni kawaida yao kusema ''uko wapi upendo wa Mungu''.

Papa amehoji ni kwa nini watu kumlaumu Mungu ?.

''Uamuzi wa ni kitu gani wafanye ili wasifikwe na matatizo hayo umo mikononi mwao wenyewe Mungu hasthaili lawama kabisa,"alisema.

Akizungumza ni kwa jinsi gani wanadamu wanaweza kuishi kwa kutegemea upendo wa Mungu akilinganisha na hali iliyoko Yugoslavia sasa hivi alisema kuwa mambo hayo ambayo ni matokeo ya dhambi yanaweza kuepukwa iwapo wanadamu watakuwa waaminifu na kufuata kanuni za Mungu.

Aliongeza kuwa ushahidi unaothibitisha kuwa upendo wa Mungu bado unaweza kuokoa wanadamu kwenye matatizo kama hayo ni kitendo chake cha kumtuma mwanaye wa pekee Yesu aje kuwafia wanadamu. Aliwaambia vijana kuwa njia pekee wanayoweza kufuata ni kukua katika upendo wa baba ambao umefunuliwa kwetu kupitia kwa mwanaye wa pekee Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu amewaambia vijana kuwa mtu kubadilika inakuwa vigumu sababu ya majaribu ya mwovu, lakini wanapaswa kuutazama upendo wa Mungu ambao utaweza kuwajaza msukumo wa mabadiliko.

 Wanafunzi wa Kiislamu wawazuia wenzao wa Kikristo kuingia Chuo Kikuu

Ujungpandang, Indonesia,

Wanafunzi wa Kikristo huko Ujongpandang, mji mkuu wa jimbo la kusini mwa Indonesia la Sulawesi wamewalalamikia wanafunzi wenzao wa Kiislamu kwa kuwazuia kuingia kwenye eneo la chuo kikuu cha Hassanuddin wanakosoma.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la Kanisa Katoliki CNS, wanafunzi wa Kiislamu walikuja juu dhidi wa wenzao wa Kikristo kufuatia kile walichokiita "Wakristo kuwachuja Waislamu" katika jimbo la Ambon Maluku nchini humo.

Sakata hilo la wanafunzi wa Kiislamu kuwazuia wenzao wa Kikristo kuingia kwenye eneo la chuo hicho lilianza mapema mwezi Machi ambapo waliweka kituo cha kukagulia vitambulisho penye lango la chuo hicho huku wale ambao vitambulisho vyao vilionyesha kuwa ni Wakristo wakizuiliwa katakata kutia mguu chuoni hapo.

Wanafunzi kadhaa wa Kikiristo wameliambia Shirika la habari la kikristo la Asia UCA lililoko Thailand kuwa wanafunzi wote walishurutishwa kuonyesha vitambulisho vyao ambapo waliogundulika kuwa Wakristo kuzuiliwa kuingia chuoni hapo na pia walipigwa.

Hapo awali sakata hilo lilipoanza wanafunzi wa Kiislamu walikuwa wakikagua vitambulisho vya wanafunzi toka jimbo la Ambon peke yake kwa sababu ndipo walipodai kuwa Wakristo wamechinja Waislamu, lakini baadaye waligeuza kibao ambapo wanafunzi wote pasipo kujali wanatoka jimbo lipi walitakiwa kuonyesha vitambulisho kwenye lango la chuo.

''Mpaka sasa bado nimechanganyikiwa kufuatia kitendo cha makusudi cha wanafunzi wa Kiislamu kukagua vitambulisho vya wanafunzi wa Kikristo penye lango la kuingilia hapo chuoni"alisikika akilalamika Herlina Lopang, Mwanafunzi wa kike wa Chuo kikuu kutoka jimbo lenye Wakristo wengi nchini Indonesia la Tana Toraja, ambalo liko umbali wa maili 200 kaskazini mwa Ujunpandang.

Wanafunzi wengine Waislamu katika mabweni ya chuo hicho nao pia waliwageuka wenzao wa Kikristo na kuwaamuru kuondoka chuoni hapo haraka. wanafunzi kutoka jimbo lenye Wakristo wengi la Tana Toraja lililo kusini mwa jimbo la Sulawesi wao waliamua kurejea nyumbani kabla ya Machi 28 , siku ambayo ndiyo iliwekwa na wanafunzi wa Kiislamu kuwa ikifika hawajaandoka chuoni hapo wangetangaza 'Jihad' kushinikiza mapigano kati ya Wakristo na Waislamu katika jimbo la Ambon yasitishwe.

Hali ya amani katika katika jimbo la Ambon ilirejea kuwa shwari katikati mwa mwezi Machi baada wanajeshi wa kutuliza ghasia kuwasili huko kutoka Java mji mkuu wa Indonesia, mapambano kati wa Waislamu na Wakristo ambayo yalianza Januari 19 katika jimbo la Maluku yaliacha watu wapatao zaidi ya 200 wakiwa wamepoteza maisha huku Waislamu wapatao 60,000 wakiwa wameyakimbilia makazi yao wengi wao wakiwa ni wa kutoka jimbo la kusini la Sulawesi.

Wakati huo huo, idadi kubwa ya wanafunzi wa Kikristo kutoka jimbo la kaskazini mwa nchi hiyo la Irian Jaya wameondoka mjini Ujungpandang kurejea kwenye jimbo hilo kwa ajili ya usalama wao.

Hata hivyo msaidizi wa Gavana wa jimbo la Irian Jaya , Bw. Abraham Ataruri amesema kuwa ilikuwa ni mapema mno kwa wanafunzi hao kuukimbia mji wa Unjungpandang kurejea nyumbani.

'Kwa ajili ya usalama wenu mngejikusanya mahali, hata hotelini kisha mkawaalika wakufunzi wenu waendelee kuwafundisha" Ataruri, ambaye ni Mkristo alisikika akiwaambia wanafunzi hao.

 

Wimbi jipya la wakimbizi toka Kosovo wafurika Macedonia

Associated Press, Mecedonia,

Wimbi kubwa la wakimbizi wa Kinta kutoka Kosovo wameanza kuingia kwa wingi kwa makundi ya maelfu huko Macedonia wengi wao wakiwa ni wenye asili ya Albania.

Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa wakimbizi hao wanaozidi kumiminika Macedonia wanatumia usafiri wa treni, kutembea kwa miguu na hata usafiri wa magari .

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Macedonia amesema kuwa wanatarajia idadi kubwa zaidi ya wakimbizi hao kufurika nchini mwake wakitokea Kosovo na ameilezea hali hiyo kuwa ni mwanzo tu.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi UNHCR limesema kuwa wanatarajia kuwa idadi nyingine ya wakimbizi wapatao 50,000 kutoka Kosovo kuingia Macedonia katika siku chache zijazo.

Habari zaidi zimeeleza kuwa pamoja na wimbi hilo la wakimbizi kuelekea huko, lakini Macedonia imesema haina nafasi tena ya kupokea wakimbizi hao na imeiomba nchi jirani ya Albania kuisaidia kubeba mzigo huo.

 

Bintiye Tony Blair anusurika kwenye ajali ya ndege

Colin Adamson, London

Binti wa Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair ni miongoni mwa abiria 235 na wafanyakazi wapatao 18 walionusurika kwenye ajali ya ndege aina ya Boing 747 iliyokumbwa na msukosuko wa dhoruba ikiwa angani.

Kathryn Blair alikuwa akisafiri kutoka likizo huko Australia ndani ya ndege hiyo mali ya Shirika la Ndege la Uingereza wakati wa msukosuko m ulipowakumba wakiwa angani.

Binti huyo wa Waziri Mkuu wa Uingereza pamoja na rafiki yake mwingine mdogo walikuwa wakisafiri kati ya jiji la Brisbane, Australia na Singapore wakati ndege yao ilipopatwa na misukosuko wakikaribia kutua Singapore. Hata hivyo walisalimika na hawakujeruhiwa kwenye ajali hiyo.

Vyanzo vya habari vimesema katika likizo hiyo ya Australia Catheryn alienda pasipo kusindikizwa na ulinzi wowote ambapo alikuwa apitie Singapore kuchukua ndege nyingine ambayo ingemleta London.

Baada ya ndege hiyo kutua salama Singapore ambapo majeruhi wachache walichukuliwa na gari la wagonjwa kupelekwa hospitalini, abiria waliosalia wakiwemo Catheryn Blair waliendelea na safari yao kutoka Singapore ambapo walitua salama penye uwanja wa ndege wa Heathrow mjini London.

Catheryn aliwasili London na ndege ya awali ya asubuhi ambapo alitengwa na abiria wengine wa kawaida na kupokelewa kwa mapokezi ya kipekee kwenye chumba cha kupokelea wageni wa heshima .

Kwenye uwanja wa ndege wa Heathrow , abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo namba BA 016 waliwaelezea waandishi wa habari jinsi ambavyo ndege hiyo iligonga kifuko cha hewa umbali wa futi 35,000.

Walieleza kuwa baada ya tukio hilo la ghafla kutukia, ndege hiyo ilitikisika mfululizo kwa takribani dakika 30, hali iliyopelekea abiria mmoja wa kiume kunaswa kwenye vishikizo vilivyoko nyuma ya kiti chake ndegeni.

Abiria watano walibakia Singapore wakitibiwa, ambapo wengine waliosalia waliruhusiwa kuendelea na safari yao mpaka Heathrow Jijini London.

Abiria Tony Newton mwenye umri wa miaka 55 mkazi wa Tiverton Uingereza alisema ilikuwa ni mara yake ya kwanza kukumbukwa na msukosuko akisafiri na ndege.

'Mawazo yangu yote yalikuwa kwa wanangu wawili; Hoshua mwenye umri wa miaka kumi na Lucy miaka tisa. Lakini mawazo yangu yalirejea kuwa katika hali ya kawaida baada ya hali kuwa shwari ndani ya ndege na kugundua wako salama.

Abiria waliosafiri ndani ya ndege hiyo wakiwemo binti yake Waziri Mkuu Blair walitoa pongezi kwa rubani wa ndege hiyo ya British Airways ambaye alikuwa Bill Mullins pamoja na wafanyakazi wenzake ndani ya ndege kwa namna walivyojitahidi kuhakikisha maisha ya abiria yanakuwa salama .