Papa kuitikisa Israel

Jerusalem, Israel

Wizara ya Utalii ya Israel imesema kuwa Waisraeli wanatamtarajia Papa Yohane Paulo ll kuitembelea nchi Machi, mwaka kesho, lakini mamlaka ya Kanisa Katoliki mjini Vatican, Italia bado haijathibitisha ziara hiyo.

Kwa mujibu wa kijarida cha Shirika la habari la kanisa Katoliki cha Machi 23, 1999, japo hakuna taarifa rasmi za kuthibitisha ziara ya Papa huko Mashariki ya Kati, vyanzo fulani vya habari vimesema kuna uwezekano mkubwa wa kutembelea huko wakati wa msimu wa kuchipua.

Waziri wa Utalii wa Israeli Moshe Katzav, na Kardinali Roger Etchegaray, ambaye anaongoza Kamati ya Vatican ya maandalizi ya Yubile Kuu ya mwaka 2000 Machi 22, walikutana kwa faragha mjini Yerusalemu, lakini hakuna hata mmoja wao aliyekuwa tayari kutoa taarifa rasmi baada ya mazungumzo hayo.

Hata hivyo kuna habari kwamba baadaye Katsav aliwanong'oneza Waandishi wa habari wachache kuwa Papa ataitembelea Israel Machi mwakani.

Baadaye Televisheni ya Israeli ilitangaza kuwa Papa atatembelea maeneo muhimu ya Yerusalemu, Bethlehem na Nazareti Machi 23 hadi 25 mwakani.

Kardinali Etchegaray, japo hakuwa tayari kutoa tarehe maalum ya ziara ya Papa alipoongea na waandishi wa habari baada ya mkutano wake wa faragha na Waziri wa Utalii wa Israeli, alisema ziara hiyo inaendela kuiva.

"Unapowazia kwamba Yubile Kuu ni sherehe za kuzaliwa Kristo (miaka 2000 iliyopita) na maisha yake katika ardhi hii, ni zaidi ya jambo la kawaida kwa Papa kutembelea hapa" alisema Kardinali huyo mjini Yerusalemu hivi karibuni.

Hivi karibuni kumekuwa na habari kwamba Israeli itashirikiana na Mamlaka ya Wapalestina kumpokea Papa katika ziara hiyo inayotarajiwa kuwa na uzito mkubwa katika masuala ya amani ya Mashariki ya Kati.

Katika maeneo mengi ambayo Papa Yohane Paulo ll ameyatembelea kumekuwa na mafanikio makubwa katika masuala yahusuyo amani. Hata hivyo, Kardinali Etchegaray hakutaka kuzungumzia hali ya kisiasa ya Mashariki ya Kati akisema sio kazi yake.

Kwa kupinga zinaa, wanawake Bangladesh waharibiwa sura zao kwa kumwagiwa tindikali

lWanaotoa mahari isiyotosha nao pia wapo hatarini

SIKU zote wanawake wakihesabiwa kuwa viumbe dhaifu wamekuwa wakishurutishwa na wanaume kuanguka kwenye dhambi ya zinaa hata kama dhamira zao haitaki. Katika hali isiyokuwa ya kawaida, hata kidogo wanaume huko Bangladesh wamezuka na tabia ya kuwaharibu sura wanawake kwa kutumia tindikali pale wanaposema hapana kwa dhambi ya zinaa. Ajabu ni kuwa hata wanawake maskini wanaoshindwa kuwalipa, wanaume mahari nyingi nao pia hutendewa ukatili huu, linaandika gazeti la Sunday Vision la Uganda la hivi karibuni.

Haiwagharimu fedha nyingi wanaume wa Bangladeshi kutekeleza azma yao ya kulipiza kisasi dhidi ya wanawake wanaowaambia "hapana" pale wanapotaka kuzini nao kwa nguvu. Chupa moja ya tindikali inagharimu senti zipatazo 60 tu.

Tindikali imekuwa ni silaha mpya madhubuti ya wanaume kuwashambulia wanawake na wasichana wamekuwa wakimwagiwa tindikali hiyo usoni kiasi cha sura zao kuchomwa vibaya lakini vyombo vya dola nchini humo hulipuuzia tatizo hilo kwa kutochukua hatua yoyote nzito ya kulikomesha.

Hivi karibuni polisi nchini Bangladesh baada ya kufanya tathmini yao walitoa taarifa zilizoonyesha kuwa katika mwaka uliopita wa 1998 peke yake. wanawake wapatao 180 nchini humo wamechomwa sura zao vibaya kwa kutumia tindikali aina ya "Hydrochloric" au "Surphuric"

Katika matukio kadhaa nchini humo wanawake kadhaa wakinyanyaswa, kisa wametoa mahari hafifu isiyoridhisha kuwaoa waume zao.

Akiwa ni mwansheria na mpiganiaji wa haki za binadamu nchini Bangladesh, Sigma Huda alilieleza Shirika la habari la REUTERS kuwa ni ukatili wa kusikitisha, kuhuzunisha na kutisha wanaotendewa wanawake nchini humo.

Akiwa na umri wa miaka 28 Peara Begum, mwanamke wa Kibangladesh anaelezea jinsi mkasa ulivympata binti yake ambaye ni mwanafunzi wa shule bado.

"Mwalimu wake wa kiume alimtaka kwa uhusiano wa kimapenzi. Alipokataa matokeo yake yalikuwa ni kumwagiwa tindikali usoni". Hali hii ya wanawake kuharibiwa sura kwa asidi huvunja matumaini yao ya baadaye kabisa. Wanawake na wasichana wengi wanasema kuwa ni nani huyo atakuwa tayari kumuoa mwanamke aliyeharibiwa sura? ndoto na matumaini yao ya baadaye hufifia kabisa.

Kwenye hospitali kubwa jijini Dhaka wamelela wasichana wawili ambao ni dada Hellen mwenye umri wa miaka 17 na Sufia mwenye umri wa miaka 15. Wasichana hawa wote wawili hawaugui ungojwa wowote tofauti bali ukizitazama sura zisizoweza kutambulika kwa jinsi walivyochomwa utang'amua kuwa ukatili kwa wanawake nchini humo umefikia kiwango gani.

Wasichana hawa wawili wanaeleza kuwa usiku wa Desemba mwaka 1998 mtu mmoja ambaye hawakuweza kumtambua lakini mwanaume, alikwea juu ya dari la chumba chao na kuwamiminia tindikali, kwa kweli waliungua kiasi cha sura zao kuharibiwa vibaya."Angeliogopa kufanya hivyo ningelikuwa ni mwanaume" Hellen anatamka kwa uchungu.

Katika jamii ya Bangladesh ukatili wanaotendewa wanawake unaonyesha hawathaminiwi kabisa. Sigma Huda, mwanasheria na mtetezi wa haki za binadamu nchini humo anamalizia kwa usema "Wanawake wanatendewa mambo hayo katika jamii yetu kwa sababu jamii haiwapi uzito wowote."

 

Shirika la Kikatoliki kuwasaidia waliokumbwa na maafa

MIAMI, Florida - Caritas, shirika la misaada la kimataifa la Kanisa Katoliki limetenga kiasi cha dola 500 milioni za Marekani kwa ajili ya kuzisaidia nchi za Amerika ya Kati katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Katika mkutano wa hivi karibuni uliofanyika Miami, wawakilishi wa Caritas walielezea umuhimu wa kuendeleza misaada ya muda mrefu kwa nchi za Honduras, El Salvador, Nicaragua na Gpuatemala ikiwa ni njia ya kuzijenga upya sekta za kijamii katika nchi hizo.

Nchi hizo ziliangamizwa na mvua kubwa ya kina cha inchi 24 iliyoambatana na kimbunga kiitwacho Hurricane Mitch mnamo Oktoba mwaka jana, ambapo kilisababisha mafuriko na maporomoko katika milima na kuwaacha maelfu ya watu wakiuawa na wengine wakipoteza makazi.

Katika maafa hayo shule, majengo ya serikali, barabara, madaraja na mashamba ya watu yaliharibiwa vibaya.

Kulingana na gazeti la "The Catholic News la Singapore linalomilikiwa na Kanisa Katoliki, katika mkutano huo uliofanyika Miami, Askofu Mkuu John C. Favalora alisema kuwa misaada zaidi inahitajika kwa ajili ya ujenzi mpya wa jamii za mataifa hayo.

Aidha alisema kuwa jitihada zinahitajika za kupatikana misaada kutoka kwa nchi mbali mbali kuwasaidia watu masikini waliokumbwa na maafa hayo na kuinua uchumi wa nchi hizo.

Shirika la kimataifa la Caritas ni shirikisho la vyama 146 vya Kikatoliki duniani na hutoa misaada kwa nchi zipatazo 194 duniani kote.

Shirika hili hutoa misaada ya kijamii kwa waliokumbwa na maafa kama vile vita, mafuriko na magonjwa.