AMECEA yalaani mauaji ya kinyama, uvunjaji wa haki za binadamu Sudan

lYashauri Umoja wa Mataifa uwe makini zaidi

Umoja wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Mashariki mwa Afrika (AMECEA)unaozishirikisha nchi nane umeelezea kusikitishwa kwake na mauaji ya kinyama nchini Sudan ambayo yamekuwa yakitokea kwa miaka 16 sasa.

Taarifa ya AMECEA iliyotolewa wiki hii ambayo imeelekezwa kwa makao makuu ya Umoja wa Mataifa imesema uvunjaji wa hali za binadamu unaoendelea nchini Sudan ikiwa ni pamoja na mauaji, kunyimwa uhuru wa kubudu hususan kwa wasio Waislamu

na mateso mengine kwa raia wasio na hatia ni mambo yasiyostahili kutazamwa yakiendelea.

"Tumebaini kuwa vita hivi vimesababisha vifo vya watu wapatao milioni mbili wasio na hatia. Imesababisha ukosefu wa makazi kwa watu zaidi ya milioni nne, wengi wao wakiwa ni wakimbizi katika nchi za ukanda wa AMECEA," imesema taarifa hiyo na kuongeza kuwa hali ya kulegalega kwa serikali ya Sudan nayo imeziathiri nchi jirani.

Baadhi ya mateso ambayo yameshamiri nchi Sudan kwa mujibu wa taarifa hiyo ni pamoja na baadhi ya raia kufanywa watumwa, kuteswa vibaya kwa wanaowekwa kizuizini, adhabu zinazovuka mipaka ya sheria na adhabu ya kifo, kutoweka kwa watu, kukosekana kwa haki ya kujieleza na kuwabagua wasio Waarabu au wasio Waislamu.

Mengine ni upendeleo au matumizi mabaya ya vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikiwapendelea Waislamu na Waarabu na kuwatenga wasio Waislamu.

Kadhalika AMECEA imesikitishwa na mtindo unaotumika wa kuwaadhibu kwa kutowapa mgao wa chakula wale wasiounga mkono itikadi za kiislamu na kirarabu huku wakifa njaa katika maeneo ya mapigano.

AMECEA ambayo Mwenyekiti wake ni Askofu Mkuu Josaphat Lebulu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha imesushauri Umoja wa Mataifa kuchukua hatua zifuatazo ili kurejesha hali ya amani nchini Sudan;

Moja; Kuchukua kila hatua iwezekanayo kukomesha vita nchini Sudan. Pili; Kuunga mkono kikamilifu jitihada zinazofanywa na IGAD kurejesha amani nchini Sudan kwa njia ya mazungumzo. Tatu; kuwalinda raia wasio na hatia kutokana na mashambulio mbali mbali ya silaha na Nne; kutoa msaada wa chakula usio na masharti kwa raia wanaokufa njaa iwe njaa hiyo inatokana na vita au ni ya asili.

Ushauri mwingine uliotolewa ni kuvidhibiti vikundi vya wanamgambo vinavyoungwa mkono ba Serikali, na kwa nguvu zote kung’oa vitendo vinavyofanywa vya kuwafanya akina mama na watoto kuwa watumwa.

Vatican yawa mwanachama shirikisho la michezo duniani

Vatican City,

Kwa mara ya kwanza katika historia, Vatican imesajiliwa kuwa mwanachama wa Shirikisho la Michezo Duniani "World Athletics Federation".

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana katika michezo ya dunia ya Olimpiiki upande wa riadha inayoendelea huko Seville, Uhispania, Vatican imesajiliwa na shirikisho hilo kama mwanachama namba 211 ndani ya shirikisho hilo.

Hii haimaanishi kuwa wakati wa michezo ya Olimpiki, mapadri, maaskofu na makardinali watazimika kushiriki katika riadha kuwania medali mbali mbali, bali jukumu lao litakuwa kuhudhuria michezo hiyo kama wawakilishi wa Vatican na kuwasaidia wanamichezo kuwa na maadili mema.

Wakati huo huo kamati ya maadhimisho ya Jubilee ya mwaka 2000 inaandaa maadhimisho ya mwaka huo wa jubilee kuwa wa kimichezo Duniani kote pia. Kamati hiyo pia inaandaa mashindano ya mbio ndefu za Marathon ambayo yataanza na kumalizikia St. Peter’s Square mjini Roma. Maadhimisho ya jubilee ya michezo yatafanyikia uwanja wa Olimpiki mjini Roma.

 

Maadhimisho ya Jubilee 2000 huko Wales na Uingereza kushirikisha dini mbalimbali

London, Uingereza

Maashimisho ya jubilee ya mwaka 2000 huko Wales na Uingereza yatashirikisha makanisa na madhehebu tofauti, imefahamika mjini hapa.

Ndani ya waraka wa Papa Paulo Yohane II "Tertio millennio Adveniente" ulioutumwa sehemu mbalimbali duniani ni kama maandalizi ya maadhimisho hayo umeonyesha kupokelewa kwa mikono miwili na madhehebu tofauti hapa Uingereza na Wales.

Uongozi wa sehemu mbalimbali za kazi katika mashirka na hata makampuni hapa Wales na Uingereza nao pia wameonyesha kila dalili ya kuunga mkono jubilee hiyo na kukaidi kushiriki.

Maadhalizi ya jubilee 2000 hapa Uingereza ni makubwa ambapo Mai 23, 2000 kunapangwa kusherehekewa sikukuu ya kidini ya "Pentekost" na dayosisi nyingi hapa zimeonyesha kila hali ya kuhimiza maandalizi ya maadhimisho hayo.

Muda mfupi tu kabla ya kifo chake hivi karibuni Cardinal George Basil Hume, ambaye alikuwa Askofu mkuu wa Westminster aliwahimiza vijana wawashawishi wazazi wao kurejea kanisani kwa ajili ya tukio la jubilee 2000.

Katika miaka ya hivi karibuni idadi kubwa ya watu huko Wales na Uingereza ameonyesha hali ya kuzembea kuhudhuria makanisani tofauti na miaka ya nyuma.

Baadhi ya mapendekezo ya Papa aliyoyatoa kwenye barua yake ya kitume ya Novemba 10 1994 nayo pia yameanza kufunyiwa kazi mwaka 2000 ukianza kubisha hodi.

Mapendekezo hayo yalikuwa ni pamoja na nchi maskini kusamehewa madeni . CAFOD (Catholic overseas Charity and Christian Aid) shirika la kanisa katoliki la kutoa misaada ya kikristo, kwa kushikikiana na shirika la kanisa Anglicana la "Christian Aid" kwa pamoja zikikuta CAFOD, zinaendesha kampeni nzito ya kushinikiza nchi maskini zisamehewa madeni na nchi tajiri amazipunguziwe.

CAFOD tayari imewasilisha mada hiyo kwenye mkutano mkuu wa nchi tajiri zenye viwanda duniani ambapo kampeni yao mpaka sasa imeonyesha kila dalili za kuzaa matunda.

 

Wakristo 38 watiwa mbaroni China

Beijing, China

Serikali ya China imewatia mbaroni Wakristo zaidi ya thelathini na

wanane katika nchini China kwa kukiuka amri ya serikali ya kuwa na vikundi vya kidini visivyo na udhibiti wa serikali.

Kulingana na kituo kimoja cha kutoa habari na kutetea haki za binadamu chenye makao yake makuu huko Hong Kong, msemaji wao ameeleza hapa Beijing kuwa polisi wa China wamewakamata Viongozi wa dini wanaoendesha Makanisa ya Kikristo kisiri siri nchini humo wakati walipokuwa katika mkutano nyumbani kwa mmoja wao.

Kwa mujibu wa wasemaji wa kituo hicho polisi wapatao 20 walijitoma ndani ya nyumba hiyo na kuwaweka chini ya ulinzi wachungaji hao kisha wakaipekua nyumba nzima na kuchukua pesa na Biblia zote walizowakuta nazo.

Wasemaji wa kituo hicho cha haki za binadamu wameeleza kuwa wachungaji hao sasa wanashikiliwa kwenye vituo vya kufanyishwa kazi ngumu (Labour camps) kwa kuendesha mikutano ya injili pasipo ruhusa.

Mwezi mmoja tu uliopita serikali ya Uchina ilikipiga marufuku kikundi cha kidini cha "Falum Gong". China ambayo ni nchi ya Kikomunisti imekuwa ikiruhusu tu vikundi vya kidini ambavyo vinaongozwa na Serikali na hata Kanisa Katoliki nchini humo haliruhusiwi kuwa na mahusiano yoyote na Vatican. Inasadikiwa kuwa kuna Wakristo wa kisirisiri wapatao kati ya milioni 50 na 80, wakati Wakristo walio chini ya uongozi wa serikali ni milioni 10.

 

Walutheri wakaza uzi kudhibiti mashoga

Denver, Colorado USA

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la huko Marekani Jumamosi iliyopita lilipiga kura na kuamua liendelee kupiga marufuku mashoga ndani ya kanisa hilo kupewa utumishi au uchungaji.

Kura hiyo ilifanyika kufuatia mkutano wa wiki nzima mfululizo ambao pamoja na ajenda ya mashoga pia ilijadili ikiwa utoaji mimba uhalalishwe ama uendelee kupigwa marufuku.

Baraza kuu la kinisa hilo katika jimbo la Colorado, iliwapiga marufuku rasmi Mashoga kuwa Wachungaji kunako mwaka 1990.

Lakini baraza la kutunga sheria la Kanisa hilo lilijulikana kama "Church wide Assembly" halikupiga kura kuunga mkono uamuzi huo.

Kwa mujibu wa gazeti moja la jimboni Colorado matokea ya kura hiyo yalikuwa ni 820 kuwa 159. Ambapo wajumbe 820 walioshinda walipinga Walutheri mashoga wasiruhusiwe kuwa Wachungaji ndani ya kanisa hilo.