Papa atunukiwa medali ya kupambana na njaa na utapiamlo

Mwandishi Wetu, Mashirika ya habari

Kiongozi wa kanisa Katoliki Duniani Papa Yohane Paulo wa pili ametunukiwa medali maalumu yenye picha yake kwa kushiriki kwenye harakati za kupambana na njaa na utapiamlo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi mkuu wa shirika la chakula na kilimo Duniani FAO bwana Jacques Diouf,Papa ametunukiwa medali hiyo na FAO baada ya shirika hilo kuridhishwa na juhudi zake za kushiriki katika kampeni za kupambana na njaa na utapiamlo kote duniani.

Bwana Diouf alimtunukia Papa nishani hiyo siku moja kabla ya kutimiza kwake mwaka wa 20 toka achaguliwe kuwa kiongozi wa kanisa Katoliki Duniani huku Dunia nayo pia ikiwa inaelekea kuadhimisha siku ya chakula Duniani hapo oktoba 16mwaka huu

Msemaji huyo wa shirika la kilimo na chakula duniani amesema kuwa medali kadhaa zenye picha ya papa zitauzwa na fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo yake zitaenda kushughulikia uboreshaji wa hali ya uzalishaji cha kula duniani na kudhibiti njaa na utapimlo katika nchi mbalimbali.

Medali hizo zitapatikana katika aina tatu,aina ya kwanza ikiwa ni ya dhahabu,moja ya fedha na nyingine ya shaba na zitatofautiana bei.

Wazo la kutengenezwa medali mbalimbali za kutunikiwa watu wanaotokea kufanya vizuri kwenye kampeni za kutokomeza njaa duniani na kuboresha uzalishaji wa cha kula lilibuniwa na FAO mnamo mwaka 1977.ambapo medali hiyo ilipewa jina la kilatini "Agricola"ambalo lina maana ya "Mkulima"

Toka wakati huo watu mbalimbali mashuhuri wameibuka kupata medali hizo,lakini ni kiongozi wa kanisa katoliki peke yake amebahatika kutunukiwa yenye picha yake.

 

Kardinali atupa hoja ya kuwapa wanawake upadre

Asema Papa ameshaweka msimamo wa Kanisa wazi, na hakuna wa kubadilisha

CWN, Canberra,

Kardinali Edward Clancy wa Canberra, Jumatano iliyopita alitupilia mbali mapendekezo ya kujadili uwezekano wa Kanisa Katoliki nchini Australia kuruhusu wanawake wapewe upadre kama ilivyo wanaume.

Kardinali Clancy, alisema tayari Papa Yohane Paulo II ameshaweka wazi msimamo wa kanisa juu ya jambo hilo hivyo haitarajii hata Papa mwingine ajaye abadili jambo hilo.

Maelezo ya Kardinali huyo yalikuja baada ya kutolewa kwa ripoti juu ya nafasi ya wanawake katika kanisa ambayo ilipewa jina "Mwanamke na Mwanaume; Wamoja katika Kristo Yesu," waraka ambao ulitolewa na maaskofu wa Australia.

Taarifa hiyo ilidai kuwa wanawake wengi wamekuwa wakifurahia wajibu na nafasi yao katika kanisa lakini wengine wanaona umuhimu wa kupata majukumu makubwa zaidi katika uongozi wa kanisa na kushiriki katika kutoa maamuzi.

Taarifa hiyo pia ilisema kwamba robo ya walioshiriki kutoa maoni yao wakati wa kuiandaa walionyesha kutokubaliana na mafundisho ya Kanisa Katoliki juu ya wanawake.

Mratibu wa mkakati huo wa kuwatetea wanawake wapate upadre Dr. Marie Macdonald alisema wanawake wanaona kwamba utamaduni wa Kanisa Katoliki na mwenendo wake haviendani na nafsi ya Kristo na mahusiano yake na wanawake.

Kardinali Clancy, hata hivyo aliwataka wahusika wajishughulishe na kuona ni vipi nafasi walizo nazo wanawake kwa sasa zitaimarishwa, badala ya kupoteza muda kwa jambo hilo.

"Napenda kusisitiza kwamba thamani ya wanawake katika kanisa leo hii, haiwezi kushushwa na suala la kupata upadrisho," alisema.

Akaongeza Kardinali Clancy kwa kusema kuwa haungi mkono mjadala juu ya upadrisho wa wanawake kwa vile baada ya miaka 30 ya mazungumzo na kushauriana, Baba Mtakatifu alitangaza kufungwa kwa mjadala huo.

Aliwataka maaskofu hao wanaopendelea wanawake wapewe upadre watumie njia zifaazo kulingana na utaratibu wa kanisa badala ya mbinu yao ya kuitisha mjadala kwa jambo ambalo Papa ameshalitolea maamuzi.

 

Tahadhari ya mafuriko ya mto

Sudan -

Ushirikiano wa Kimataifa wa Vyama vya Msalaba na Mwezi Mwekundu ulisema mafuriko mabaya huko Sudan yanayosababishwa na mvua kali isiyo ya kawaida yameharibu zaidi ya kaya 10,000 na kuwaacha watu 50,000 katika ‘uhitaji wa dharura wa msaada".

Katika taarifa iliyopokelewa na IRIN siku ya Jumatano, Ushirikiano huo ulisema viwango vya maji katika mito mikubwa vilikuwa juu wakati huu wa mwaka na, kwa sababu majira ya mvua yanatarajiwa kuanza, ‘kiwango cha janga litakalotokea kinatisha’. Chama cha Mwezi Mwekundu cha Sudan kimeanza operesheni ya kutoa msaada wa kupunguza watu mateso kikitegemea ‘uwezo mdogo uliopo nchini’, Shirikisho hilo lilisema, likaongezea kuwa uchunguzi wake wameonyesha kuwa kunahitajika msaada wa madawa ya hospitali kusaidia mpaka sasa watu 10,000.

 140 wauwawa

Uganda-

Shambulio la hivi majuzi dhidi ya ukoo wa Bokora wa kabila ya Karamajong huko Kaskazini-Mashariki mwa Uganda na watu wa ukoo wa Matheniko liliacha zaidi ya watu 140 wamekufa, gazeti linalomilikiwa miongoni mwa wengine na serikali ‘The New Vision’ lilitoa taarifa siku ya Jumatano. Walionusurika katika shambulio hilo wanakadiria idadi ya watot waliokufa kuwa 70.

Inasemekana walitupwa ndani ya moto baada ya washambuliaji kuziteketeza nyumba zao, gazeti hilo lilisema.