NI AIBU KUWA NA NJAA

Hivi karibuni kulisikika kuwa wananchi wa Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga wanakabiliwa na tatizo la njaa kutokana hasa na vijana wao kutopenda kufanya kazi za kilimo na badala yake wanapenda kufanya biashara ndogondogo ambazo haziwezi kamwe kukithi mahitaji yao ya chakula.

Sote tunajua kwamba nchi yetu ni hasa nchi ya wakulima.

Tumeambiwa mara nyingi kuwa kilimo ni uti wa mgongo kwa maendeleo yetu.

Mafunzo na mbinu mbalimbali zimekuwa zikitumika ili kuwaelimisha wananchi katika shughuli hii ya kilimo..Tunaweza kusema kuwa viongozi wetu wa ngazi mbalimbali wengi wao wamefanya kila jitihada katika kuwaelimisha na kuwahimiza wananchi kuhusu kilimo, na siyo tu kilimo cha hivi hivi bali hasa kilimo kilicho bora.

Baba wa taifa, Mwalimu Nyerere alijitahidi sana katika kuwaelimisha wananchi kuhusu kilimo bora katika nchi yetu. Kama tungefuata maagizo na maelekezo yake, nadhani sisi Watanzania tusingekuwa na tatizo hili la njaa.

Pia tumesema kuwa vijana ndio hasa nguvu kazi kwa ajili ya taifa letu, kwani wao ndio hasa wenye ari na moto. Na hivyo ndivyo tunavyoshuhudia hapa na pale kwamba vijana wanajishughulisha na kazi hii tukufu ya kilimo.

Lakini habari tulizozipata kutoka huko Wilayani Handeni, ama kwa hakika hukatisha tamaa na pia na habari za aibu sana. Je, tutatarajia nini ikiwa vijana hawataki kufanya kazi ya kilimo ambacho kwa hakika ni uti wa mgongo wa uchumi na maendeleo yetu?

Tena kama ilivyoelezwa na kama tunavyofahamu, Wilaya ya Handeni ni katika ya sehemu ambazo ni nzuri sana kwa kilimo katika nchi yetu. Inashangaza sana kuona vijana hawataki kujishughulisha na kilimo, na mapato yake ni kwamba kuna uhaba wa chakula na kwa uwazi zaidi ni kwamba kuna njaa. Hayo ni mapato ya uvivu kwa vijana wetu. Na tunasema kuwa hilo ni jambo la aibu kabisa.

Lakini hatuwezi kusema ni vijana hao wa Handeni tu ambao hutoroka na kuchukia kazi ya kilimo, bali ni vijana wengi hapa nchini ambao hawataki kabisa kutumia nguvu zao katika kazi hii ya kilimo.

Siku hizi ukipita karibu katika miji yote ya nchi yetu hutakosa kuwaona hao vijana wanaoitwa "Wamachinga" wakiwa wamebeba bidhaa mikononi mwao na ambazo kusema kweli hazinunuliwi, na kama zinanunuliwa ni kwa kiasi kidogo sana.

Hao wote hupoteza kabisa ile nguvu kazi katika kilimo. Hapo tusishangae kama tunakabiliwa na njaa licha ya kujitetea kuwa ni kwa sababu ya hali mbaya ya hewa. Hilo ni kweli, lakini ni sababu ndogo mno. Sababu kubwa na ya msingi kwetu Watanzania katika kukabiliwa na balaa la njaa ni kutokana hasa na "UVIVU".

Dawa ya uvivu ni kufanya kazi kwa juhudi pamoja na maarifa. Kwa bahati mbaya wananchi wengi wamezoea kupata vitu kwa njia rahisi bila kutumia nguvu walizo nazo.

Tunasema kuwa ni jambo la aibu kuomba chakula wakati ukiwa na vijana wengi wenye nguvu sana, ukiwa na ardhi nzuri sana na hata pengine ukiwa na hali njema ya hewa.

Wazee wangu walinifundisha kuwa chakula la kuhemea hakishibishi kabisa. Na ndivyo ilivyo kwa hao wananchi wengi wanaotegemea chakula cha msaada. Kamwe hatutaweza kujenga afya zetu kutokana na chakula cha msaada.

Pia tukumbuke kuwa msaada ni msaada, kwani mara nyingi wale wanaotoa msaada hutoa kutokana au na ziada waliyo nayo, au ni kutokana na sifa ama shukrani watakayopewa. Lakini kwa nini turuhusu watu wajenge majina yao kutokana na uvivu wetu wa kutopenda kazi hasa hii ya kilimo? Papo hapo tunapenda kuwapongeza wale ndugu ambao wametambua kabisa umuhimu wa kilimo na wakawa tayari kuwalisha hao walio wavivu.

Kuna mikoa ambayo huitwa "The big four" ambayo imejulikana hasa kwa kuzalisha mahindi na vyakula vingine. Ukipita huko unaweza kuona ni kwa jinsi gani vijana walivyo mstari wa mbele katika kilimo. Hao vijana wamezingatia kilimo na hivyo wametulia huko makwao pamoja na wazazi wao.Kwao hakuna mpango wa kusafirisafiri huko na kule bali wanatumia muda wao na pia nguvu zao katika kilimo na shughuli nyingine za uzalishaji mali.