Na tuzingatia maana halisi ya utumishi na Mtumishi

Katika maisha ya kawaida huwa tunatumia sana neno hili la "MTUMISHI".

Huwa tunasikia kuwa fulani ni mtumishi wa serikali, au fulani ni mtumishi wa nyumbani.

Lakini mara nyingi neno hili "mtumishi" huwa na maana mbaya. Wengi wanaposikia neno "mtumishi" huelewa kuwa ni mtu ambaye hali yake ni duni, au ni mtu wa chini kabisa. Lakini kumbe sivyo.Neno "mtumishi" kusema kweli halina maana mbaya kama wengi wetu tunavyoelewa.

Tungeweza kusema kuwa mtumishi ni mtendaji mkuu katika kila jamii kwa ajili ya wanajumuia wengine.

Tusomapo Maandiko Matakatifu hasa katika Chuo cha Nabii Isaya tunasikia kuwa Masiha, yaani Bwana Yesu Kristu ni Mtumishi wa Bwana.

Waumini tunasadiki kwamba Kristo amekuwa ni mtendaji mkuu katika kazi ya ukombozi wa binadamu. Sisi binadamu tunamhitaji sana kama mtendaji mkuu katika kutupatanisha na kutuunganisha na Baba wa milele.Pia wale Mababa watakatifu, ambao ni viongozi wetu wa kanisa huitwa ni watumishi wakuu wa kanisa kama alivyo kiongozi wetu Bwana Yesu.

Katika utaratibu wa utendaji katika kila serikali tunasema kuwa tunao watumishi wa serikali. Hao ni watendaji wetu wakuu katika serikali. Kwa hiyo neno hili mtumishi ni la kawaida na tena ni lenye maana kubwa katika maisha yetu.

Kila mtu anapofanya kazi au kutoa huduma kwa ajili ya watu wengine huitwa ni mtumishi. Kwa hiyo mtumishi ni yule mwenye kuhangaikia maslahi ya watu wengine, walio karibu yake na ambao kwa namna fulani amekabidhiwa na uongozi au utawala.

Tukumbuke kuwa mtumishi siyo mtumwa. Mtumishi hufanya kazi zake kwa uhuru na pia kwa kuridhika pamoja na upendo. Lakini mtumwa mara nyingi hufanya kazi kwa kulazimishwa na Bwana wake na kwa hiyo mara nyingi kazi zake hazina ladha nzuri kwa mara nyingi huweza kulipualipua.

Watumishi ni watu wa muhimu sana katika kila jamii.

Wafanyakazi katika Idara mbalimbali za serikali ni watumishi na hivyo wanapaswa kufanya kazi zao kwa uaminifu, kwa upendo na kwa hiari.

Mtumishi kama mtumishi hufanya kazi yake kwa uhuru na kwa furaha. Mtumishi wa kweli hufanya kazi yake bila kusimamiwa na mkubwa yeyote yule.

Mtumishi hufanya kazi yake vizuri ili aweze kuiletea sifa idara yake au ofisi yake. Mtumishi ni mtu ambaye hufanya kazi kama mali yake na hata mapato ya kazi yake humfurahisha kwa sababu huwa ni kama ya kwake.

Hivyo ndivyo walivyo na wanavyotakiwa kuwa hata wale watumishi wa nyumbani. Ni sherti wajione kuwa wao ni sehemu ya nyumba ile wamohudumia. Hivyo watafanya kazi zao kwa uaminifu, kwa furaha, kwa bidii na upendo.

Tungeweza kusema kwa maneno mengine kuwa kazi ya utumishi ni kazi ya uzalendo kweli kweli. Watumishi wengi wa serikali na hata watumishi wa nyumbani huwa wanakosa uzalendo na hivyo kuleta utumishi mbaya.

Mambo mengi hukwamishwa na watumishi au watendaji wasio na uzalendo.Wako watumishi wengi ambao hawana uaminifu na hivyo wanafanya kazi zao bila maadili , wakidokoa dokoa mali ya umma.

Wako watumishi wengi ambao hawana uzalendo na ambao hufanya kazi zao bila uangalifu wakilupualipua na pia wakitaka wawe na wasimizi kama vile wangekuwa ni watumwa kumbe ni watumishi.