Make your own free website on Tripod.com

KWANI TUSIZINGATIE RATIBA?

 

Kwa kawaida kila inapofanyika shughuli ya watu wengi na hata pengine ya mtu mmoja hatukosi kuwa na ratiba. katika ratiba huandikwa au kupangwa ni jambo gani litatendekea wakati gani na kwa muda gani ili kufanikisha shughuli hiyo.

Tukienda huko mashuleni tunakuta kuna ratiba za masomo. Ratiba hizo hutuelezea masomo huanza saa ngapi hadi saa ngapi. Ratiba hutuonyesha pia muda wa mapumziko na muda halisi wa masomo. Wale wanaozipanga hizo ratiba huzipanga kulinga na masomo yanayotakiwa kufundishwa kwa siku, kwa wiki, kwa mhula na hata kwa mwaka. Walimu na wanafunzi sharti wafuate ratiba hizo ili kulifikia lengo la elimu kwa muda huo au mwaka huo.

Mambo huwa hivyo hivyo hata kwa wale wanafanya semina, kozi na warsha mbalimbali. Nao lazima wawe na ratiba ya shughuli hizo. Pia ni lazima wawe waaminifu kwa ratiba zao wakitaka kufaidika na shughuli hizo. Bila kufuata ratiba itakuwa ni vigumu sana kuweza kufikia malengo ya hizo shughuli wanazotaka kuzifanya.

Kuna pia ratiba katika shguhuli za ibada hasa huko makanisani. Uongozi wa kanisa hupanga ni saa gani ibada ianze na hata ikiwezekana imalizike saa gani. Bila kufanya hivyo mambo yanaweza kuwa magumu na hata kuleta fujo.

Katika kila nchi, serikali imeweka ratiba maalumu ya watu kufanya kazi. Wafanyakazi wanaambia waanze kazi saa gani na wamalize lini. Hapo inatakiwa wakati mtu anapotakiwa awe kazini sherti awe kazini. Kutofanya hivyo kwaweza kuleta hasara katika taifa. tunaambiwa saa za kazi ni saa za kazi, labda kuwe na dharura nyingine.

Licha ya hizo ratiba za kazi kuna pia ratiba za vyombo vya usafiri kama vile ndege ulaya, mabasi, magari moshi, na hata meli. Kila msafiri hupenda kufahamu lini anaondoka na lini kuanza safari yake na ikiwezekana lini atafika kule aendako kama mambo yanakwenda vizuri bila ajali au shida nyingine.

kwa kifupi tunaweza kusema kuwa ratiba ni mwongozo unao tuwezesha tufanikiwe katika shughuli zetu. Lakini swali la kujiuliza ni hili: Je, sisi sote tunazifuata ratiba zetu za shughuli mbali mbali? Wako wale ambao kusema kweli ni waaminifu sana kwa ratiba zao. Lakini kuwa wengi wetu ambao hatuko waaminifu kwa ratiba na mapato yake hujionyesha hapa na pale.

Pamoja na hizo ratiba za watu wengi, mtu binafsi naye anapaswa kuwa na ratiba yake. Ni lazima mtu ajipangie ni saa ngapi aende kulala na saa ngapi aamke na kufanya shughuli za binafsi. tunapaswa kuwa na muda wa kupumzika kwa wakati wake.

Wengi wetu huwa tunazama katika shughuli na hivyo tukawa na muda mfupi mno wa kupumzika. Hapo tukumbuke miili yetu huhitaji sana kupumzishwa hasa baana ya kazi nzito ziwe za mikono au za kiakili. Pia tunapaswa kukumbuka kuwa usingizi ni dawa kubwa sana kwa afya zetu. Wako wale ambao pengine ni kutokana na shughuli nyingi au pengine kutokana na starehe fulani fulani husamehe usingizi. Hapo huishi bila ratiba na mapato yake huonekana wanapozidi katika umri.

Katika hoja yetu hii tunapenda kuwakumbusha wale ambao hawahsiki ratiba katika maisha yao wafanye hivyo. Bila kufuata ratiba ni vigumu kufikia yale malengo tunayonuia kuyafikia. Ni jambo la ustaaarabu mtu kushika na kufuata ratiba. Maisha au shughuli bila kufuata ratiba ni maisha ya fujo yasiyo na mafanikio.

Ni jambo la kufurahisha na kupendeza ikiwa watu wanashika ratiba. Wale wanaofuata ratiba hawatachelewa pale wanapotakiwa kuwepo. Lakini ikitokea watu hawafuati ratiba hapo kunakuwa na ucheleweshaji. Ni vibaya sana mtu kuchelewa kufika pale unapohitaji.

Wale wamisionari Wabenediktine walitulea wakati tukiwa wadogo walitufundisha kuwahi na kufika mahali unapotakiwa. Walitufunza kuwahi au kufika wakati wake kuanisani au mahali pa ibada, kufika mezani kwa chakula na pia kufika wakati unaotakiwa kuanza kazi. Lilikuwa ni jambo lisilopendeza kwa mtu kuchelewa kufika kanisani, kufika mezani na hata kuanza kazi. Wale wanaoishi katika jumuiya hata ile ya familia natumaini wanakubaliana na jambo hilo. Kuchelewa mahali ni kuvunja ratiba. na kuvunja ratiba ni kuharibu utendaji wa shughuli.

Ni jambo tunalodaiwa na kutenda kila kitu kwa wakati wake. Tulipokuwa shuleni tulikuwa tukionyana kuhusu mambo yale yanayoendelea bila mwisho. tulisema tusifuate kunoga au vionjo vya moyo. Muda ukisha hata kama kitu hicho ni kuziri tunapaswa kukiacha na kuendelea na ratiba nyingine. Tukifuata ratiba tunaweza kufanya mambo mengi sana katika maisha yetu mafupi ya hapa duniani.

Mtu mwenye kushika ratiba tunasema ni mtu mwenye nidhamu. na mtu mwenye kuwa na nidhamu tunaweza pia kumwita ni mtu mwenye kujitawala maonjo yake bali utashi na akili ndiyo hasa vinavyotawala utendaji wake.

Inasikitisha hasa tunaposhuhudia watu wakubwa au viongozi hawafuati ratiba. Kuna wananchi wengi wamepoteza muda wao wa kazi kwa sababu ya kuwasubiri wakubwa ambao hawataki kufuata ratiba.

Kuna masaa mengi ya kazi ambayo hupote bure kila siku kwa sababu ya wale wanaohusika kutofuata ratiba au mpango uliowekwa. Haipendezi kumsubiri mtu kwa muda usiojulikana na hata kwa sababu zisizojulikana kwa wengine labda kwake yeye mwenyewe tu.

Daima tunapaswa kukumbuka kuwa wakati ni mali. Muda ukishapotea huwarudi tena na hubakia hasara tu katika kitabu cha maisha. Pia tukumbukue yale maneno ambayo mtu mmoja aliambiwa wakati akiomba radhi kwa sababu ya kuchelewa. Watu walisema "samahani si dawa". Neno la kuomba radhi haliwezi kulipa hasara ambayo imepatikana kwa kuchelewa.

Pengine hutokea kuwa watu ambao hawafuati ratiba huwa na usumbufu mwingi. Kwa mfano wamechelewa kufika kwenye mkutano hapo watakuwa wamesikia mambo nusu tu na mengine hawakusikia. Watu wa namna hiyo ni wa hatari kwani wana taarifa zilizo nusunusu tu. Kama ni kuhusu utekelezaji hapo hatuwezi kuitegemea kuwa wataweza kufanikisha zoezi hilo.

TUNASEMA kuwa tunapaswa kutenda kila kitu kwa wakati wake, kila kitu kwa kiasi chake, na kila kitu mahali pake, hakuna zaidi wala pungufu. Tutafanikiwa katika shughuli zetu ikiwa tunafuata ratiba na mipango tuliyojiwekea. Binadamu kiumbe chenye akili na utashi huishi na kutenda kwa mipango na ratiba aliyojiwekea.