Twayakaribisha mashindano ya Usafi

Hivi karibuni serikali imetamka kuwa kuanzia hapo mwakani kutakuwa na mashindano ya usafi katika Mikoa yetu hapa nchini.

Tamko hilo ni zuri sana hasa tukizingatia hali ya usafi ilivyo katika nchi yetu. Karibu kila mahali tumezungukwa na uchafu. Ni jambo la kusikitisha sana na tena ni jambo la aibu sana kuona sisi Watanzania licha ya sifa mbalimbali tulizo nazo kimataifa, lakini tuko wachafu sana.

Serikali imechukua uamuzi huo baada ya kuona kwamba kumekuweko na jitihada nyingi ambazo hazikuzaa matunda ya usafi.

TUKUMBUKE kuwa kulikuwa na msemo kuwa Mtu ni afya.Msemo huo ulikuwa kwa ajili ya kuwahimiza wananchi wawe wasafi ili waweze kuwa na afya bora. Lakini kwa bahati mbaya msemo huo haukuzingatiwa na wananchi wengi na matokeo yake mambo yamezidi kuwa mabaya siku baada ya siku.

Tunaambiwa kuwa usafi ni tabia ya mtu. Kwa hiyo tunapoamua kujenga hali ya usafi katika taifa letu tujue kuwa tunataka kujenga tabia ya watu kuwa wasafi. Tunavyofahamu ujenzi wa tabia hauji kwa siku moja, bali ni kutokana na mazoea ya matendo hayo ya usafi kwa kipindi kirefu.

Kuna matendo mengi sana ya usafi katika maisha ya binadamu.Kuna usafi wa mwili wake binadamu, kuna usafi wa nguo zake anazozivaa, kuna usafi wa vyombo vyake anavyovitumia kila siku, kuna usafi wa mahali anapolala au kujipumzisha. Pia kuna usafi unaodaiwa katika mazingira yale ambayo binadamu anashughulika na kufanya kazi kile siku.

Tungeweza kusema kuwa usafi ni kitu ambacho humzunguka binadamu kila mahli na kila wakati. Kwa maneno mengi tunaweza kusema kuwa usafi ni kitu kilicho sehemu ya binadamu katika maisha yake. Ni kitu ambacho hawezi akaacha nacho atake asitake, ili mradi tu anataka kuishi maisha mazuri.

Tumesema kuwa usafi ni kama maumbile ya binadamu, isingetakiwa apewe amri na mtu iliaweze kuwa msafi. Pia isingetakiwa kabisa kushawishiwa na mtu mwingine ili awe na usafi. Lakini mambo yalivyo binadamu wengi hawapendi kabisa kuwa wasafi wao wenyewe binafsi, katika mazingira wanamoishi na kadhalika.

Kwa vile uchafu ni kitu kinachowaudhi waungwana wengi, basi zipo kila sababu za sisi kuipongeza ahtua hiyo ya serikali ya kuleta mashindano ya usafi katika taifa letu.

Watanzania wengi wamepoteza maisha yao kwa sababu ya magonjwa yanayotokana na uchafu kama vile kipindupindu, malaria, kuhara, safura, nk.Kwa upande mwingine maisha ya binadamu wenzetu hao yangeweza kunusurika kama hali ya usafi ingezingatiwa.

Kuna baadhi ya wananchi ambao tabia ya kuwa wasafi imewapiga chenga kabisa. Hivyo wanaweza kuishi siku nyingi bila kuoga. Pia kwao kusafisha mazingira ya nyumba yao huona kuwa hilo si jambo la lazima. Kuna wengine wanaweza kuvaa nguo moja , shati au suruali kwa muda wa wiki nzima, achia mbali zile nguo zao za ndani. Wako wengine ambao huona kuwa shughuli ya kusafisha meno yao walao kila asubuhi siyo kitu kwao. Hivyo wanakuwa na vinywa vinavyonuka mbele ya watu wengine. Wako wengine ambao licha ya wao wenyewe kuwa wachafu hawaoni kuwa ni jambo lisilopendeza kutupatupa takatka ovyo ovyo. Hiyo ni tabia mbaya na kweli haipendezi kamwe.

Licha ya jitihada mbalimbali za serikali katika jambo hilo la kudumisha usafi, kinachotakiwa kwa kila mwananchi ni kujenga tabia ya kuwa msafi katika mazingira yo yote yale anamoishi. Kwa hiyo jambo linalotakiwa kwetu sisi Watanzania ni kujenga ile tabia ya kupenda usafi.

Tunapaswa kuwa wasafi kwa sababu mtu msafi hupendeza na pia kuvutia. Tunasema kuwa ingawa ni jambo la aibu kufanya mashindano ya usafi, baada ya miaka hiyo 37 ya UHURU, kwa kuwa hakuna jinsi nyingine ya kuwahimiza wananchi wawe na tabia ya usafi, basi tunaipongeza serikali yetu tukufu kwa kubuni njia hiyo ya mashindano ya usafi.

Tunaamini kuwa hilo halitakuwa ni jambo la mpito, bali litakuwa ni la kudumu daima.