Kanisa lashutumu serikali kwa kuchangisha pasipowezekana

Na Dalphina Rubyema

 SERIKALI imeshutumiwa kwa kuweka gharama za kuchangia katika mambo ambayo ni lazima kwa binadamu wa kawaida ili hali ikitambua kuwa wengi wao ni wale ambao hawajimudu hata katika mambo madogo ya kawaida.

Hayo yalisemwa hivi karibu na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania Padri Methodi Kilaini wakati akitoa mada kwenye semina ya kujadili Uchumi iliyoandaliwa na Kikundi cha Mazungumzo ya Madheehebu ya Makanisa ya Kikristu Tanzania, The Tanzania Ecumenical Dialogue Group (TEDG) semina iliyofanyika katika Kwenye ukumbi wa Baraza la Maskofu- uliopo Kurasini.

Pd.Kilaini alisema kuwa serikali inapotoa tamko la kuchangia gharama kwa huduma muhimu wanaoathilika si serikali yenyewe bali ni wale watu wenye kipato cha chini ambao wanatoa pesa kuchangia gharama za matibabu,elimu pamoja na chakula.

Alisema serikali pamoja na kutoa tamko hilo la kuchangia huduma hizo lakini haitoi mishahara mizuri kwa Wafanyakzi wake hali inayowafanya wazidi kuona uchumi wa Tanzania ni mbaya.

"Watu hawana pesa,wanafanya kazi nyingi sana lakini mshahara wanaopata ni mdogo hii haiwapi moyo na badala yake wanaona uchumi wa nchi hii unayumba na wanategemea kupata kitu kidogo ukilinganisha na kazi wanazozifanya"alisema katibu huyo.

Alisema kanisa kama taasisi nyingine zilizopo nchini inalo jukumu la kutafuta usawa katika jamii hivyo kanisa linajukumu la kuiuliza serikali pindi inapopandisha matumizi ili ifahamu sababu za kufanya hivyo.

Pd.Kilaini alisema kuwa ili kujenga mshikamano uliokamili ni lazima serikali kuangalia upya mipango yake na itoe mapendekezo ambayo hayatawaathiri wananchi.

Semina hiyo ilimalizika jana kwa kutolewa wito wa ushirikishwaji wa umma katika maandalizi ya sera za nchi ikiwa pamoja na maendeleo ya kiuchumi.

 Askofu awasifu wanawake

MHASHAMU Askofu Severine Niwemugizi wa jimbo Katoliki la Rulenge akifunga rasmi warsha ya wiki moja ya wanawake viongozi wa shughuli za maendeleo jimboni Rulenge iliyofanyika Mwoleka Seminar Centre katika makao makuu ya Jimboi alisifu juhudi za wanawake wanazozifanya kwa lengo la kujikomboa na kubadili hali ya jamii kuwa na maisha bora zaidi.

Akiwahutubia aliwataka washiriki wa warsha hiyo kuzingatia mambo matatu yakiwemo ushiriki wa wanawake katika maendeleo, nafasi ya elimu katika maendeleo, na wanawake na miradi ya uchumi.

Kuhusu ushiriki wa wanawake katika maendeleo alisema washiriki wa warsha wanao wajibu mkubwa wa kuwahamasisha wenzao ili akina mama wengi zaidi wajihusishe na shughuli za kuiendeleza jamii.

Akizungumzia nafasi ya elimu, Askofu alisema kuwa elimu ni msingi wa maendeleo na hivyo wanawake hawana budi kutafuta nafasi za kujielimisha ili kuweza kupambana ipasavyo na mazingira.

Askofu aliwaonya akina mama kuwa macho dhidi ya dhana potofu za maendeleo. Alisema kuwa nyakati hizi yako mafundisho na mielekeo mbali mbali ambayo yasipoangaliwa vema ni hatari kwa jamii yetu. Alitoa mfano wa mielekeo inayotenga maendeleo ya kimwili na yale ya kiroho na ile inayotenga maendeleo ya mama na yale ya mtoto kama mielekeo isiyofaa kwa jamii yetu.

Katika warsha hiyo ya wiki moja, iliyoendeshwa kwa hiari ya kitengo cha maendleeo ya akina mama (WIDP) cha Idara ya Caritas ya Jimbo, washiriki walipata nafasi ya kujifunza mambo mbali mbali kuhusu wanawake maendeleo na uhifadhi wa mazingira.

 

Waumini watakiwa kuacha tabia za kung'ang'ania waganga wa kienyeji

Na Sr. Maria Gaspara

 PADRE Attilio Myenyelwa wa Jimbo Katoliki Dodoma ameonya watu kuacha tabia ya kung'ang'ania waganga wa kienyeji na badala yake waishi katika ukweli, kufuata utaalamu wa waganga wenye ujuzi na wanaofuata teknolojia ya kisasa.

Akizungumza katika Misa ya mazishi ya Sr. Maria Alberta wa Shirika la Masisita wa Moyo Safi wa Maria Mgolole Morogoro wiki hii, Padre Attilio alisema kuwa tabia ya mwanadamu imejaa wasi wasi na haitaki kutafuta ukweli inapenda zaidi kuelekea kwenye udanganyifu. Ndiyo maana utakuta mtu anapougua, huenda kwa daktari na papo hapo huchangnya miguu, kwenda kwa mganga wa kienyeji.

Padre huyo amesema ni vizuri kutafakari juu ya kifo na kujiuliza mara kwa mara, Mungu atakapokuja atakukuta katika hali gani? Amefananisha maisha ya mwanadamu na mshale unaoanza na kuishia katika mauti akisema ndivyo mwanadamu anapoanza na kuishia mautini.

Padre huyo ambaye alikuwa akitoa mafungo ya roho kwa Mapadre 54 wa Jimbo la Morogoro huko Bigwa UNITAS wakati wa tukio hilo la kifo, amesema kuwa dunia ya sasa imejaa dhuluma na maovu ya kila namna ndio maana mtoto anapozaliwa hujificha katika tumbo la mama kwa ajili ya kukataa kuonana na maovu hayo.

Alisema mtoto anapokuwa tumboni mwa mama ni mithili ya kuwa mbinguni. Ndiyo maana anakataa kutoka. Aliendelea kusema kuwa anapotoka analia mara moja tu, ishara kwamba anangonjea wengine waje kumlilia siku ya kifo. Aliomba Hayati Sr. Alberta aliliwe kwa kumwombea ili Mungu ampokee mbinguni.

Misa hiyo iliongozwa na Mhashamu Askofu Telesphor Mkude akishirikiana na mapadre zaidi ya 54 watawa na waumini waliotoka ndani na nje ya Jimbo.

Sr. Alberta 57 alizaliwa Parokia ya Mango kibosho Moshi 1941 na baada ya masomo ya shule ya msingi 1963 alijiunga na shirika la Masisita wa Moyo safi wa Maria Mgolole Morogoro. Alifunga nadhiri za kwanza mwaka 1968 na kutoa huduma kama sista katika parokia za Tchenzeama 1968 hadi 1973, St. Peter Seminari 1974 hadi 1975 na St Joseph Dar es Salama 1976 hadi 1987. Parokia nyingine alizohudumia marehemu katika uhai wake ni pamoja na Gairo mwaka 1988 hadi 1992, Lumbiji 1994 hadi 1995 na Mgeta 1996. Baada ya hapo alianza kuugua ugonjwa wa kansa na kurudi Mgolole nyumba ya asili hadi alipofariki Novemba 2, 1998. Alizikwa Novemba 5, 1998 katika makaburu Mgolole Convent.

Apumzike kwa Amani.