Wakatoliki fundisheni watoto wenu - Askofu Chengula

Na Adolph Mwakyusa, Mbeya

WATOTO Wakatoliki popote pale walipo mashuleni, lazima wafundishwe dini, na waalimu wakatoliki, na siyo walimu wa madhehebu mengine.

Hayo yalisemwa na Askofu Evaristo Chengula wakati akizungumza na waumini wa parokia ya Mwanjelwa hivi karibuni.

Askofu Chengula alisema, mtoto kumlisha chakula kisichofaa ambacho baba yake amekataza asipewe ni kosa.

Mtoto Mkatoliki, kufundishwa imani ya madhehebu mengine ni kuwapotosha imani ya Kanisa Katoliki, ambayo wazazi walilishwa toka utoto wao.

"Kwa hiyo walei popote mlipo, msikubali mazoeya ya mwalimu asiye Mkatoliki kutufundisha watoto wetu dini shuleni," alisema Askofu Chengula

Aidha aliwataka Wakatoliki kufuata imani ya Wamisionari ambao walifanya kazi ya utume bila woga,"Wakatoliki angalieni historia ya kanisa lenu wekeni mbele sala pia kusali Rozari ili kupatanishwa na Mungu, kuunda mfumo wa maisha, kutuunganisha Mungu na watu wengine ili kuepa mapokoe ya kwao na waliyoyakuta." alisisitiza

Viongozi watambue ushirikishwaji wa madaraka kunasaidia jamii, kutii sauti ya Mungu, ili maandiko matakatifu yawe na uhai ndani yao.

Akiwaasa mapadri na makatekista aliwataka wawe wakweli kwa mambo ya kanisa, na kuongeza kuwa wakifanya mambo ya hakika na ukweli wategemee upinzani hali ambayo huenda ikawa hawapendezwi nayo .

"Na kama katika kazi zenu hamna upinzani mjiulize kwa nini?" aliuliza.

Askofu Chengula ambaye alifika parokiani hapo kutoa kipaimara alitaka parokia zionekane kwa vitendo na sio semina. Alisisitiza kuwa ubatizo na kipaimara, yote hayo hayafai kitu bila imani.

Walei wapato 280 walipata kipaimara siku hiyo parokiani Mwanjelwa.

Parokia yatoa mchango wa Chakula kwa Seminari

Na. Faustin Mkaudo, Arusha

JUMLA ya magunia 29 ya mahindi pamoja na kilo 635 za mchele zimetolewa na waamini wa parokia ya Unga Ltd. kwa ajili ya seminari ya Jimbo Katoliki la Arusha iliyoko Oldonyo Sambo, Kilometa 40 toka mjini Arusha kando ya barabara iendayo Nairobi.

Akiongoza ujumbe maalum toka parokiani hapo kwenda kutembelea sminari hiyo, Paroko, Padsre Rochus Mkoba aliwataka waamini kuwa na moyo wa kuweza kuitegemeza seminari hiyo kwa hali na mali ili kupata mapadre bora na kuondokana na uendeshaji wa seminari kwa kutegemea ruzuku kutoka Vatican, ruzuku ambayo haina uhakika na kutokidhi uendeshaji wa seminari hiyo.

Pamoja na magunia 29 ya mahindi na kilo 635 za mchele, parokia hiyo ilitoa pia maharage , nyanya pamoja na mbuzi mmoja kwa ajili ya kuwapongeza mapadre na waalimu wanaofundisha hapo kama shukrani kwa juhudi zao za malezi bora na ufundishaji mzuri uliofanikisha seminari hiyo kushika nafasi ya tisa kitaifa kwa matokeo ya mitihani ya kidato cha sita. Mbali na mbuzi huyo, parokia ilitoa zawadi mbali mbali kuwapongeza waalimu na kuwatia moyo zaidi.

Akipokea mchango huo wa chakula, Mkuu wa Seminari, padre Simoni Tengesi alimshukuru sana padre Rochus Mkoba pamoja na waamini wa parokia ya unga kwa mchango huo ambao amesema unahitajika sana seminarini hapo.

Padre Tengesi alitoa wito na kuwaomba sana parokia nyingine jimboni Arusha kuiga mfano mzuri wa Parokia ya Unga Ltd, katika kuitembelea na kuitegemeza seminari hiyo kwa chakula na misaada mbali mbali ili kufanya shughuli za uendeshaji wa seminari hiyo kuwa nafuu.

Hii ni mara ya pili katika kipindi kisichozidi miezi sita kwa parokia hiyo ambayo inajenga kanisa kubwa lenye kugharimu mamilioni ya fedha, kutembelea seminari hiyo. Ilipotembelea kwa mara ya kwanza mnamo mwezi wa tano mwaka huu, parokia hiyo ilitoa mahindi, unga wa ngano, mafuta ya kupikia, chumvi, sukari pamoja na zawadi kwa mapadre na waalimu wanaofundisha hapo na fedha taslimu sh. 50,000 na kuahidi kutoka tena sh 50,000.

 

Yuda Tadei atimiza miaka miwili Mtoni

Na Peter Dominic

WAUMINI wa dini ya Kikristo wameombwa kutochukulia masihala na mzaha mambo ya dini na badala yake wajiunge na jumuiya za kidini na kusali mara kwa mara ili kuweza kuzilea familia zao katika misingi hiyo.

Haya walisemwa na mwenyekiti wa jumuiya ya Mt. (Yuda Tadei) katika sherehe za kuadhimisha kilele cha jumuiya hiyo ambayo imetimiza miaka miwili (2) toka ilipoanzishwa.

Katika hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Ndendeule Maeneo ya Mtoni Sabasaba, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Bw. John Joseph Shakani aliwaomba waumini wa dini, hiyo kutoka ushirikiano, upendo kwa majirani na wanajumuiya wote kwa ujumla ili kuweza kuishi katika imani Katoliki yenye kuisisitiza misingi hiyo.

Risala iliyosomwa katika hafla hiyo ilieleza mafanikio ya jumuiya hiyo ambayo ni pamoja na wanajumuiya kufahamiana, kusaidiana katika matatizo mbali mbali pamoja na mambo mengine ikiwa ni pamoja na waumini wapya 9 ambao wamejiunga na dini hiyo na kufundishwa imani Katoliki.

Pamoja na mafanikio hayo wanajumuiya wameelezea matatizo wanayokabiliana nayo ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanajumuia kutokuwa na uwezo na wengine ni vilema ambao wameonyesha uwezo wao na kushirikiana na jumuiya hiyo hivyo wamemuomba baba Paroko kama kuna uwezekano kupatiwa misaada ya mikopo na (mitumba) ili jumuiya iweze kujisaidia.

Jumuiya ya Mtakatifu Yuda Tadei imeanzishwa mwaka 1996 ikiwa na idadi ya wanajumuiya (13) wakiwemo Mwenyekiti wakati huo Bw. Richard Fayari na Mzee Peter Mnally.

Hivi sasa jumuiya hiyo ina idadi ya familia 133 chini ya Mwenyekiti John Joseph Shakani na makamu mwenyekiti Bw. Peter Mnally na ilianzishwa kwa dhumuni hasa la kutekeleza agizo la (Vatican) ambalo linataka hadi kufikia mwaka 2000 Kanisa Katoliki liwe na nguvu kuliko kundi lolote la kidini duniani

 

Mafrateli watakiwa kuishi kwa imani

Na. Frt. Thomas Mambo

BALOZI wa Papa Nchini Tanzania Mhashamu Askofu Mkuu Francisco Javier Lazano amewataka Mafrateri kuishi adhila ya Imani ambayo alisema ni kutii amri za Mungu.

Askofu huyo alisema hayo wakati wa ufunguzi wa mwaka wa masomo wa seminari Kuu wa Mt. Karoli Lwanga hivi karibuni.

Amesema kwamba kwa kufanya hivyo watakuwa wanatoa mifano bora na inayoishi kwa ulimwengu mzima na hivyo kumleta Kristo kwa watu na ulimwengu mzima.

Ufunguzi huo wa mwaka wa masomo 1998-1999 ulitanguliwa na uwekaji wa Jiwe la msingi katika jengo jipya la utawala lililopo seminarini hapo. Mara baada ya kuweka jiwe la msingi Askofu Mkuu Francisco Javier Lazano, mapafdre, masista, mafrateri na wageni waalikwa walielekea kanisani kwa maandamno.

Sambamba na rai hiyo, Askofu Mkuu Lazano, aliwaomba Mafrateri hao wawe daima wavumilivu, jasiri katika kuhubiri Neno la Mungu na hasa upendo ukiwa ndiyo msingi wa Imani yao. Aidha Askofu huyo Mkuu alisema padre ni mpatanishi wa Mungu na watu, daima lazima awekaribu na Yesu Kristo.

 

Wezi wavunja tena Kanisa na Kuiba

Na Adolph Mwakyusa, Mbeya

WATU wasiojulikana hivi karibuni, wamevamia kanisa Katoliki la Ruanda, Parokia ya Mwanjelwa na kuiba vitu kadhaa na kumjeruhu mlinzi wake.

Watu hao walivamia kanisa hilo usiku wa manane, wakiwa na nondo, na virungu, walivunja mlango mmojawapo na kumvamia mlinzi aliyekuwa ndani.

Mlinzi huyo aitwaye Jacksoni Mbella, alimwambia mwandishi wa habari hizi, alivamiwa pale alipojaribu kupiga filimbi ili kuomba msaada baada ya kuwaona watu wawili wamesimama nje ya mlango.

Watu wapato wanne waliingia kwa kasi kanisani na kuanza kumkimbiza mlinzi ambaye alikuwa akielekea mlango mkubwa ili atoke nje, ndipo alipokutwa na kupigwa teke na nondo ya mkono wa kushoto.

Alivutwa na watu hao wanne kuelekea kwenye ofisi ya Padri ambayo walivunja na kuingia na kuanza kupekua makadi, vitabu na mafaili yenye taarifa mbali mbali za Kigango kuvitupa hovyo hovyo sakafuni

. Ndugu Mbela alisema baada ya kukosa fedha ofisini humo walimrudia mlinzi na kuanza kumpiga mateke ili aonyeshe fedha.

Mmoja wapo alienda Altaleni, na kuvunja Tabenakro, na kukuta vikombe na sakramenti, hawakuchukua vikombe ila mifuniko ya vikombe wakaacha wazi na kuondoka sehemu hiyo.

Walipokuwa wakiondoka walibeba vioo vinne, baiskeli ya mlinzi, tochi, filimbi, waliondoka kanisani humo kupitia mlango wa mbele

Polisi wa kituo cha VETA hawakuwapo kituoni kuzungumzia suala hilo, kwani toka saa nne, mpaka saa 9.30 alasiri hawakuwapo kituoni hapo.

Hata hivyo walifika siku ya pili kuchunguza na kuondoka tena wakiwa wamefuatana na Paroko, Gabriel Mwakasita.

Habari toka ofisi ya paroko zinasema hiyo ni mara ya tatu kuvunjwa kwa kanisa hilo la Katoliki Ruanda. na mara zote kumekuwa kunachukuliwa vitu vya thamani kama vikombe, nguo za watumishi, vioo nk. Paroko wa Mwanjelwa alikuwa bado anafuatilia askari wa kituo cha VETA, ili waanze upelelezi mapema.

Viwawa Jimbo la Kigoma Wapata Viongozi

VIJANA Wakatoliki wafanya kazi (VIWAWA) Jimbo Katoliki la Kigoma, tarehe 13.10.98 walifanya kikao cha uchaguzi wa Viongozi wao gazi ya imbo. Uchaguzi huo ulitanguliwa na semina iliyo tayalishwa na Sista Genifa Mbekeze. Semina hiyo ilihusu mambo mawili, Ujana na Mahitaji ya Kijana.

Semina hiyo ilihudhuliwa na viongozi wa Viwawa toka katika Parokia za Jimbo, akiwa ni Mwenyekiti, Katibu, na Mhasibu wa Viwawa kila Parokia.

Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma lina Parokia 16 kati ya hizo zilihudhuria parokia 9 na parokia 7 hazikuweza kuhudhuria.

Katika semina hiyo Sista alieleza kuwa ujana ni muda ambao mtu anahesabiwa kuwa sio mtoto na wala sio mzee. Namaana halisi ya ujana inapatikana katika Biblia Takatifu Ikoritho 13:11.

Upande wa mahitaji ya vijana alieleza kuwa yapo mahitaji mengine ya vijana ambayo ni: kuwa na usalama, Kuwa na uhuru, kuwa na uhusianao na watu wengine, kutaka kupata heshima, kutaka kufahamu mambo yote, kuwa na utulivu moyoni. Na mambo hayo yote ni budi yaongozwe kwa kuzingatia matunzo mazuri kutoka mimba hadi kufikia ujana.

Baada ya semina hiyo ilifuata uchaguzi mkuu wa Viwawa Jimboni uliosimamiwa na Padre JulianoRubandanya Mkurugenzi wa Vijana Jimbo akisaidiana na Sista Jenifa Mbekeze.

Uchaguzi huo uliwachagua Nichlaus Zakaria - Mwenyekiti, Festo Ludovick- Katibu, Adelina Raphael - Mhasibu, Benward William - Mwenyekiti Msaidizi, Israel Manyulane - Katibu Msaidizi, Justin Lichard - Mhasibu Msaidizi, Daniel Baltazary - Mjumbe, Skolastika Lameki - Mjumbe.

Baada ya uchaguzi ilifuata misa maalumu ya kuwaapisha viongozi wapya

 

 

Askofu Mwela wa kanisa la Kianglikana aasa matumizi ya elimu

Na Adolf Mwakyusa,Mbeya

ELIMU ni Mungu, chanzo cha elimu ni Mungu anayetafuta elimu anamtafuta Mungu, Ukicheza na Elimu unamchezea Mungu, unapomchezea Mungu unacheza na Moto, kauli hiyo ilisemwa na Askofu John Mwela Kanisa Anglikana hivi karibuni katika mahafali ya sita shule ya sekondari ya Ivumwe .

Askofu Mwela alisema elimu ni wokovu, na usalama na uhakika wa maisha na kutaka wanafunzi wanaomaliza mafunzo kuwa wabunifu wa mambo mbali mbali ya kimazingira.

"Mlipokuwa shule, mliandaliwa mpambane na mambo matatu: ujinga, maradhi na umaskini, mambo hayo mpambane nayo sababu elimu mliyopata ni wokovu' alisema Askofu.

Aidha amewaasa kuacha matumizi ya madawa ya kulevya, ufuska na uzururaji na kujiimarisha katika kazi za kujitegemea.

Naye Mwalimu Mkuu Julias Ngala alisema mwaka 1990 shule ilikuwa katika hali mbaya lakini mpaka sasa shule ina maendeleo mazuri, imeweza kujenga vyumba 12 vya madarasa, makataba moja, maabara mbili.

Aidha alisema kuwa shule inatarajia kuongeza madarasa nmanne, nyumba mbili za walimu na ofisi mbili kwa mwaka huu na wa kesho.

 

Kanisa la Kianglikana Mount Kilimanjaro waandaa tamasha

Na Charles Masanyika, Arusha

KANISA la Kianglikana la Dayosisi ya Mount Kilimanjaro linatarajia kuandaa tamasha la vijana litakalofanyika Desemba 5-6, 1998 katika shule ya Sekondari ya Ufundi Moshi mwaka huu.

Tamasha hilo linatarajiwa kuwashirikisha zaidi ya washiriki 350 kutoka katika Dayosisi mbalimbali za Kanisa la Kianglikani hapa nchini. Miongoni mwa dayosisi hizo ni pamoja na Zanzibar na Tanga, Dar es Salaam, Morogoro, na Dayosisi ya Mount Kilimanjaro ambayo ni mwenyeji wa tamasha hilo.

Akizungumza na Kiongozi ofisini kwake, Mkurugenzi wa vijana na mjumbe wa elimu Mchungaji Andrew Kajembe alisema kuwa lengo la tamasha hilo ni kuwafundisha vijana mambo mbalimbali yahusuyo elimu ya jamii na Kikristu.

Akifafanua, alisema miongoni mwa mambo yatakayofundishwa katika tamasha hilo ni pamoja na kujiepusha na madawa ya kulevya, uasherati, kijinsia na ajira binafsi.

Mchungaji aliendelea kufafanua zaidi elimu ya jinsia ndani ya Kanisa hilo, alisema kuwa Kanisa halina budi kuwashirikisha vijana wa kike ambao ni sawa na wa kiume katika nyanja mbalimbali ndani ya kanisa. Alizitaja nyanja hizo kuwa ni elimu ya Mungu (Theology) na kushiriki katika ibada.

Aidha Mchungaji Kajembe alifafanua mfano mzuri unaoonyesha tofauti ya jinsia ndani ya Kanisa ambapo ni pale msichana anapopata mimba nje ndoa na badala yake kutengwa mara baada ya kujifungua inambidi arudishwe kundini ili aweze kukubalika kanisani.

"Ni kwa nini mvulana wa kiume aliyempa mimba asirudishwe kundini," alihoji mchungaji Kajembe.

 

Kilele cha Kongamano la Ekaristi Takatifu kuazimishwa leo

Na Dalphina Rubyema

LEO ni kilele cha maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu katika jimbo la Dar-es-salaam na hitimisho hili litafanyika kwenye Kanisa Katoliki la Msimbazi Senta jijini.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi hivi karibuni, Msemaji wa Askofu Kardinali Pengo,Pd.Stefano Kaombe alisema kuwa mada kuu ya kongamano itakuwa ni Ekaristi na Maadili na mada hii imechagulia kwa vile nyakati hizi kunaonekana wazi kwamba kuna mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Pd.Kaombe alisema kuwa maandalizi ya kuhitimisha kongamano yalianza siku nyingi ambapo kuanzia Juni hadi Novemba 13 mwaka huu kilikuwa ni kipindi cha sala: Na sala maalum ziliandaliwa ambapo kila kanisa mkoani Dar-es-salaam lilitoa siku mbili kwa kila wiki kwa ajili ya kusali na kuabudu.

Mbali na kuandaa sala ,mikutano ,semina na mafungo vilifanyika kwa vikundi mbalimbali.

Akitoa ufafanuzi zaidi juu ya adhimisho hili,Pd.Kaombe alisema kuwa maadhimisho yataanzia kwenye parokia ambapo kutakuwepo na semina kwenye parokia ya Mtakatifu Josef , Chang'ombe na Magomeni na Mada kwenye Parokia zote itakuwa ni moja ya Ekaristi na Maadili.

Aliongeza kuwa baada ya semina,kutakuwepo na maandalizi ya maandamano ambapo kila Parokia itaweka misa kwenye parokia yake na baada ya hapo ndipo mandamano ya kuelekea Msimbazi yatakapoanza ambapo Parokia zote zitakutana Msimbazi na baada ya parokia zote kuwasili Msimbazi ndipo Misa itakapoanza.

Alisema kwenye misa itakayofanyika Msimbazi,jumla ya watoto 300 watapokea komunio ya Kwanza na hawa watoto ni kutoka kwenye parokia zote za mkoa wa Dar-es-salaam.

 

Waumini watakiwa kuwalea mapadri

Na Mwandishi Wetu, Sumbawanga

ASKOFU wa Jimbo la Sumbawanga Damian Kyaruzi ametoa wito kwa waumini Jimboni kuwapatia mapadre wao huduma zote wanazohitaji kwa maendeleo ya kanisa mahali pao walipo.

Akihutubia umati wa waumini waliokuwa kwenye kanisa la Mpui, wakati wa kutoa daraja la upadre kwa shemasi Charles Lyela, Askofu alishangaa kuona ratiba ambayo haikuwa na nafasi ya kumpa padre mpya zawadi.

Alisema kuwa padre Charles atakapokuwa anatoka kijijini, waumini wahakikishe kumpatia mtumishi wao huyo mahitaji yake, kwani alisema hatakuwa na mtu mwingine wa kumpatia nje yao.