Mahakama za Ndoa za Majimbo zisaidie watu kuimarisha ndoa

BABA Mtakatifu amekumbusha haja ya mahakama za ndoa za Kanisa kutumika kusaidia wakristu kuishi pamoja kwa upendo na wala sio kutengana.

Kauli ya kiongozi huyo wa Kanisa ameitoa wakati alipokutana na Maaskofu wa Marekani wakati walipomtembelea katika ziara za kawaida za kila mwaka za kichungaji mjini Roma.

Papa amesema kwamba ndoa za Kikatoliki hazivunjiki kiholela wala kimpango kwa kuwa kauli ya kutovunjwa kwa ndoa ipo katika Biblia na ilitolewa na Kristu mwenyewe.

Amesema ni vyema maaskofu wakahakikisha kuwa mahakama hizo (Mabaraza) yanatumika katika kuondoa kasoro za kwenye ndoa na hivyo kufanya wenye ndoa kuishi vyema kwa karama za mwenyezi Mungu. "Mabaraza haya yanatakiwa kusaidia wenye ndoa kukabiliana ipasavyo na matatizo yao, kuyatatua na kuishi vyema kwa mujibu wa Biblia" alisema kiongozi huyo.

Amesema ni vyema mabaraza yakatumika kuhifadhi haki sheria na amani katika ukweli na upendo wa Kristu kwa manufaa ya kanisa na waumini wake.

Aidha amesisistiza kuwa mabaraza yasitumike kutoa muhuri wa kuachana au kutengana bali viwe vyombo madhubuti vya kushughulikia kwa hekima matatizo ya watu wenye ndoa kwa kuwa kila mmoja anastahili kusikilizwa na kusaidiwa.

Amesema hata hivyo kupeleka suala la ndoa katika mahakama lazima liwe ni jambo la mwisho kabisa.

Amesisitiza kuwa uangalifu mkubwa unastahili kuchukuliwa wakati wa kueleza moja ya maamuzi magumu kabisa kwa wenye ndoa, maamuzi yakutenganisha ndoa na kwamba waumini hao wasifikirie kwamba kitendo hicho kitakuwa ni talaka.

Aidha ametaka mabaraza hayo ya majimbo yanatengenezwa au kuundwa kutokana na watu ambao kweli wanafaa na wanaweza kutekeleza sheria za kanisa kwa kuzisoma na kuzitambua vyema.

Amesema hata uendeshaji wenyewe lazima ufanywe na watu ambao angalau wamejifunza sheria za Kanisa na pia wahusika lazima wapatiwe maelezo namna kesi yao itakavyoshughulikiwa, wajibu wao katika shauri hilo na pia haki yake katika kuita mashahidi na namna gani hukumu hiyo inavyoweza kupokelewa.

Aidha waelezwe wanavyoweza kukata rufaa kwa mahakama ya Roma. Amesema ni vyema kuzingatia sheria za Kanisa kwa kuwa ndizo ambazo zinaweza kutumiwa kuendeleza upendo wa Kristo kwa kuwa hazipo kwa ajili ya kukomoa bali kumuopoa mtu.Wamisionari waeneza upendo kwa kukabili matatizo ya sasa - Papa

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani Papa John Paul wa Pili amewataka wamisionari kuangalia njia mpya ya kueneza upendo wa Kristo kwa kushughulikia matatizo ya sasa ya dunia yakiwemo ufinyu wa uhuru wa kuabudu, uharibifu wa mazingira na amani.

Papa huyo alisema hayo wakati akizungumza na masista wa Comboni waliomtembelea wakati wa mkutano wao mkuu mjni Roma.

Amesema kwamba dunia kwa sasa ina majaribu mengi na wamisionari wanawajibu wa kuwaweka binadamu katika upendo na moyo wa Kristo.

Aliwapongeza wamisionari hao kwa kufanya kazi katika maeneo ya vita na yenye haja kubwa ya kusambaza upendo kama Kusini mwa Sudan na Congo.

Aliwataka wamisionari hao wasikate tamaa wala kulegeza nia yao ya kusambaza upendo wa Kristo.

Pia alimpongeza Mkuu Mpya wa Wamisionari hao ambaye alichaguliwa kuongoza Shirika hilo, Sista Adele Brambilla. Alimwombea Sista huyo kuwa na moyo mkubwa wa kusambaza upendo wa Kristo.

Alisema shughuli zao za kueneza Injili zinaonekana dhahiri katika mipango yao ya afya, elimu na maendeleo ya jamii na kuwahimiza kuendelea hivyo pamoja na Mungu.

 

Croatia, Vatican watia saini kurejeshwa mali za Kanisa

MWEZI uliopita Vatican na Croatia walitiliana saini mkataba ambapo Serikali ya Croatia itarejesha mali za Kanisa zinazoweza kurejeshwa na zile ambazo hazitarejeshwa kulipwa fidia.

Mkataba huo ulitiwa saini na Askofu Mkuu Giulio Einaudi ambaye ni Balozi wa Vatican nchini Croatia kwa niaba ya Papa na Naibu Waziri Mkuu anayeshughulikia maendeleo wa Croatia Bw. Jure Radic.

Utiaji saini huo pia ulishuhudiwa na Kardinali Frnajo Kuharioc na Rais wa Baraza la Maaskofu la Croatia Askofu Mkuu Ante Juric.

Wengine ni Waziri Mkuu wa Croatia Dr. Zlatko Matesa na viongozi wengine wa Serikali.

Mkataba huo wenye vipengele 15 unaruhusu kurejeshwa kwa mali ya Kanisa iliyotwaliwa wakati wa utawala wa kikomunisti na ile ambayo hawezi kurejeshwa angalau kulipwa fidia.

Aidha Croatia imekubali kutoa fedha za Serikali kuingizwa katika Baraza la Maaskofu la Croatia kwa ajili ya shughuli mbali mbali za kijamii na malipo kwa wafanyakazi wa Baraza hilo.Papa apewa tuzo na FAO

PAPA John Paul wa Pili amepokea tuzo ya kimataifa ya Agricola iliyotolewa kwake na Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa ,FAO, na kulishukuru kwa kusaidia kukabiliana na njaa duniani.

Akipokea zawadi hiyo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa FAO, Dk. Jacques Diouf, Papa amesema kuwa FAO kwa takribani miaka 53 imefanya kazi ya kusaidia kukabiliana na matishio ya njaa na hivyo kuifanya dunia kuwa eneo bora la kuishi.

Aliwataka viongozi wa FAO na wafanyakazi wengine kutokata tamaa katika kazi yao ambayo inachangia katika kuboresha maisha ya viumbe wa Mungu hapa duniani.

FAO wamempatia tuzo hiyo Baba Mtakatifu kwa kutambua mchango wake na wa Kanisa katika kukabiliana na njaa na kuboresha maisha ya binadamu. Aidha kiongozi huyo wa Wakatoliki duniani ameishukuru FAO kwa kumpatia zawadi hiyo kubwa na kusema ni heshima kubwa kwa uongozi wa kanisa na kanisa lenyewe.