Wakatoliki watoa aina mpya ya ibada ya kupunga mashetani

lAnayepunga lazima apate ruhusa ya Askofu

Na Mwandishi wetu

Idara ya Ibada Takatifu na Masakramenti imetoa rasmi aina mpya ya ibada ya kupunga pepo.

Ibada hiyo ilitolewa kwenye ofisi ya Habari na Mkuu wa Idara hiyo Kardinali Jorge Arturo Medina Estevez ikiwa imeingizwa kwenye kitabu cha ibada cha madhehebu ya Kirumi.

Akizindua ibada hiyo, Kardinali Medina alisema kuwa uwezo wa mtu kumkaribisha Mungu umeharibiwa na dhambi, na wakati dhambi inachukua nafasi ambayo Mungu anapaswa kukaa, kwa maana hiyo Kristo alikuja kumkomboa mwanadamu kutoka kwenye utawala wa maovu na dhambi.

Aliendelea kusema Kristo alifukuza mashetani na akamkomboa mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wabaya na kutayarisha nafasi yake kwa mtu huyo.

Alielezea kuwa kupunga mashetani ni mfumo wa sala wa tangu zamani ambao Kanisa linautumia dhidi ya nguvu za shetani.

Alisema Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 1673 inaeleza kuwa kupunga pepo kunaelekezwa katika kumfukuza shetani au ukombozi dhidi ya kupagawa na pepo na kupitia kwa mamlaka ya kiroho ambayo Kristo amelikabidhi Kanisa.

Kulingana na ibada ya kupunga mashetani, anaendelea Kardinali Medina, kuna vigezo kadhaa tunapaswa kuvifahamu kama tunashughulika na mtu aliyepagawa: kuzungumza maneno mengi kutoka kwenye lugha isiyoeleweka, kuwatambua, kujua vitu vilivyo mbali au vimejificha, kuwa na nguvu zaidi ya hali ya kawaida, na kumkufuru Mungu, Bikira Maria, Msalaba na Picha takatifu.

"Kuendesha ibada hiyo ya kupunga mashetani," anakazia, "lazima kuthibitishwe na kukubaliwa na Askofu wa Jimbo, ambako kunaweza kutolewa kwa tukio maalum, au kwa njia ya kudumu kwa Padre aliye na huduma ya kupunga mashetani Jimboni."

Kardinali Medina alisema Kitabu cha ibada za madhehebu ya Kirumi (The Roman Book of Rites) katika sura ya mwisho kina vidokezo na maelezo ya kiliturjia ya kupunga mashetani, lakini bado havijapitiwa tangu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano.

Alisema, baada ya miaka 10 ya kazi hiyo, maelezo hayo yamethi-bitishwa na Baba Mtakatifu.

Mara ibada hiyo itakapotafsiriwa katika lugha mbalimbali, zitawakilishwa kwenye Idara hiyo kwa ajili ya kutambuliwa rasmi 'recognitio'.

Katika kitabu cha sasa, kuna ibada yenyewe ya kupunga mashetani, na sala ambazo zinapaswa kusaliwa hadharani wakati ambapo kwa kutumia busara inaonekana kuna uelekeo wa kuwa na shetani mahali, katika vitu au kwa watu, kabla ya kufikia hatua ya kupagawa.

Kwa kuongezea kuna mfululizo wa sala ambazo waumini wanapaswa kusali binafsi wanapoamini kuwa wanakabiliwa na hali ya mashetani.

Hata hivyo alisisitiza kuwa ibada ya kupunga mashetani inalala katika imani ya Kanisa, ambamo shetani na pepo wabaya pia wamo.

Mafundisho ya Kanisa Katoliki yanatufundisha kuwa mashetani ni malaika walioanguka ikiwa ni matokea ya dhambi zao, na kwamba ni viumbe vilivyo na roho tu vikiwa na akili na nguvu kubwa.

Akikumbushia Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Kardinali Medina alisema kuwa nguvu za shetani hazidumu milele, lakini Mungu kuruhusu tujaribiwe ni fumbo kubwa.

Kwa kumalizia alisema kuwa kwa kawaida madhara ya shetani na nguvu za pepo waovu zinafanyika kwa kudanganya, uongo na kuchanganyikiwa.

Kama Yesu ni ukweli, shetani ni mwongo kupita waongo wote. Uongo ndio zana yake ya kwanza kabisa.

Akijibu swali kuhusiana na ibada ya zamani alisema kuwa ibada mpya ni mwendelezo wa ile ya zamani na hakuna mabadiliko makubwa. Imetumika lugha nzuri na ya upole.

Hata hivyo alikiri kuwa msisitizo wa imani katika nguvu ya Mungu ya kufukuza shetani inafanana na iliyomo kwenye ibada ya awali.

 

Shinyanga wakarabati barabara

 

Na Charles Hillila - Shinyanga

 

JIMBO la Shinyanga linakarabati barabara kwa gharama ya shs. 2,825,000/- yenye urefu wa kilomita 3 kutoka barabara itokayo Shinyanga kwenda wilayani Maswa kupitia Parokia ya Sayusayu.

Ukarabati wa barabara hiyo unatokama na kuharibika sana na kutopitika hasa kwa kipindi cha masika. Kukamilika kwa ukarabati wa barabara hiyo, kutawaondolea taabu na usumbufu wagonjwa na akina mama wajawazito waliokuwa wanapita kwenda kutibiwa kwenye zahanati ya Misheni Sayusayu.

Zahanati ya Sayusayu inahudumia zaidi ya vijiji 25 vinavyoizunguka Parokia hiyo.

Saba katika ya vijiji hivyo vinategemea sana barabara hiyo inayofanyiwa ukarabati. Vijiji hivyo ni Isulilo, Kidema na Masela, Vingine ni Njia Panda, Ganawa na Sayusayu.

Barabara hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu. Na wananchi wa Sayusayu wameonyesha moyo wa kushirki katika ujenzi wa barabara hiyo na wanseama wapo tayari kusaidia maendeleo watakapotakiwa.

Askofu Banzi aagiza wakristo kuacha desturi za giza

Na Lazaro Blassius

 

MHASHAMU Askofu Antony Banzi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga amewataka wakristo kuachana na desturi za giza na badala yake kukumbatia mwanga kwa jinsi walivyobatizwa.

Askofu huyo alitaja baadhi ya desturi hizo za giza kuwa ni mauaji, rushwa na ushirikina.

Amesema ingawa mambo mengi yanafanyika kwa kisingizio cha kupambana na ujinga, umaskini na maradhi, mwelekeo wa sasa ni tishio kwa amani ya roho na mwili.

Mhashamu Baba Banzi amesema kwamba tabia ya sasa ya wananchi ya kutoa mimba,kupokea na kutoa rushwa na matumizi mabaya ya raslimali zilizowekwa na Mungukwa manufaa ya binadamu ni uharibifu kwa mpango wa maisha ya Mungu.

Aidha amewataka wakristo wenye taaluma ya utabibu na viongozi wa kisiasa kulinda uhai wa wagonjwa, walemavu, vikongwe na watoto tegemezi ambao hawajazaliwa bado.

Askofu Banzi alikuwa akitoa mahubiri kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Antoni kwenye sherehe za Tokeo la Bwana ambapo pia alitoa salamu za mwaka Mpya 1999.

Aliwataka wakristo kuwa waadilifu na wanyenyekevu kushika amri za Mungu ili kuleta katika jamii upendo na kweli, umoja na amani ya kweli.

Amewaonya wakristo kutoshiriki mauaji kutokana na ubinafsi, majivuno na ukatili.

Amesema wakristu wanatakiwa kuacha desturi za giza, ramli, ushirikina ili kupata mali na vyeo vya kidunia. Aidha ameonya kuwa Mkristu anaezembea katika sala na Ibada za kanisa na kufuata tamaa za kidunia anaogopa mateso hivyo kupingana na agizo la Kristo.

"Dunia ya leo haitaki kusikia neno mateso" wapinga Kristo wamejaa tele, wanahubiri kuwa chochote kinachokuondolea raha yako ni kibaya lazima kiondolewe.. na kwa kutumia Teknolojia wanaangamiza uhai na maadili" amesema.

Hivi karibuni alipokuwa mjini Lushoto Askofu Banzi amekemea uharibifu wa mazingira na uchomaji moto misitu na mauaji ya makusudi yanayo endelea nchini. Alisema wanadamu wanapoangamiza misitu wanaleta athari na mauaji kwao wenyewe na viumbe wengine.

 

Shirika la Mt. Bernadetha lazidi kukomaa

Na Mwandishi Wetu Rulenge

 

SHIRIKA la Wafransisko la Mtakatifu Bernadetha na Jimbo zima la Rulenge katika sherehe ya Mama Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, walishuhudia masisita kumi wakiweka nadhiri zao za milele na wanne wakiadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya maisha ya wakfu

Masista wanane waliofunga nadhiri za milele ni wazaliwa wa jimbo hili la Rulenge na wawili waliobaki wanatokea katika majimbo ya Kigoma na Musoma. Wale wa Jubilei wawili ni wazaliwa wa jimbo hili wakati wawili waliobaki ni wazaliwa wa nchi jirani ya Rwanda.

Adhimisho la siku hiyo muhimu lilianza kwa ibada ya misa iliyofanyika katika Kanisa la Bwana wetu Yesu Kristu Mfalme, ambalo ni kanisa kuu la jimbo. Misa hii iliongozwa na Mhashamu Askofu Severine Niwemugizi akishirikiana na baadhi ya Mapadri Wanajimbo na Wamisionari.

Misa hiyo ilihudhuriwa na Watawa wa mashirika mbali mbali yanayofanya Utume jimboni humu na mamia ya Waumini toka ndani na nje ya jimbo hili.

Akiongea wakati wa mahubiri, Mhashamu Askofu Niwemugizi alianza kwa kuwatafakarisha waliohudhuria ibada juu ya chimbuko la kuadhimisha sherehe ya mama Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Mhashamu askofu aliongeza kusema kuwa kwa kuzingatia maana ya sikukuu hiyo aliwataka masisita kutafakari juu ya umusionari na kurudi kwenye lengo la kuwa kweli mitume na walimu wa kufundisha imani.

Shirika la watawa Wafransisko wa mtakatifu Bernadetha lilianzishwa tarehe 14. 9. 1958 likiwa n a masista wanne tu.. Likiwa sasa na umri wa takribani miaka 40 linaendelea kukua na kustawi . Masista ambao tayari wamefanya Jubilei ya miaka 25 ni 18 , ukimwondoa mmoja ambaye sasa ni marehemu.

Huyu ni Sista Prisca aliyefariki Julai 2 mwaka jana kwa ugonjwa wa ini. Wenye nadhiri ya milele ni 99 na wale wenye nadhili za muda ni 57.

Askofu Balina awataka walimu kuwa wabunifu

Na Charles Hillila - Shinyanga

 

Walimu wote wanaofundisha kwenye shule zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, wametakiwa kuwa wabunifu na kutatua matatizo yaliyo chini ya uwezo wao na siyo kumsubiri Askofu.

Agizo hilo lilitolewa na Askofu Aloysius Balina mwaka huu, kwenye mkutano na walimu wakuu wa shule za sekondari za jimbo huko Ngokolo.

Jimbo la Shinyanga linaendesha shule tatu za sekondari. Mbili kati ya hizo ni za bweni na zinaishia kidato cha nne. Nyingine ni ya kutwa na inaishia kidato cha sita, pia ina chuo cha ufundi stadi kinachofundisha vijana wa daraja la saba na sekondari.

Lengo kuu la mkutano huo ilikuwa ni kuweka mikakati ya uboreshaji wa elimu katika Jimbo la Shiyanga. Mojawapo ya mikakati iliyowekwa siku hiyo ni kudhibiti utoro, na kuelezwa kuwa mwanafunzi anayeshindwa kufika shuleni kwa kipindi cha siku 21 atakuwa amejifuta shule.

Upande wa maadili na malezi Askofu Balina alisema kuwa elimu ya dini machuleni ni muhimu sana na kutaka shukle za jimbo kuhakikisha kwamba uundishaji wa elimu ya maadili hasa kwa vijana unazingatiwa na kuboreshwa.

 

Askofu ahimiza Waamini kupiga vita umaskini

Na Clement Nsherenguzi, Karagwe

 

BABA Askofu Severin Niwemugizi wa Dayosisi ya Rulenge aliwataka Waumini kupiga vita umaskini na fikra za kuwa tegemezi na kwamba makanisa nchini humu yataendelea kupata misaada kutoka Ulaya, Marekani na nchi nyingine za Nje.

Askofu huyo aliwashauri waamini kujiunga katika vikundi vya jumuia kwa makusudi ya kuhimiza na kutekeleza harakazi za kumwendeleza mbele mwananchi katika mambo ya kiroho pamoja na uchumi.

Askofu huyo alitoa kauli hizo wakati akihubiri katika Kanisa la Parokia ya Bugene katika Wilaya ya Karagwe, Mkoani Kagera

Akitoa mfano, Baba Askofu huyo alidokeza: "Mapadre wa Zamani kutoka Ulaya waliojenga Makanisa na kutoa misaada kwa waafrika walikwisha ondoka na sasa Makanisa haya haya yanaongozwa na mapadre wanaotoka miongoni mwa jamii za Waamini walio maskini, hivyo ni lazima kupanga harakazi za kujikwamua kiuchumi, ili tuweze kuchangia katika ujenzi na kujitegemea kwa Makanisa, elimu ya Sayansi na teknologia na katika miradi ya Ustawi wa Jamii".

Vile vile, Askofu Niwemugizi aliwashauri Waumini wake kusimika Biblia katika Makanisa na Majumbani kujiandaa kuingia mwaka 2000. Kwa kumalizia mahubiri yake alisema: "Inatupasa kufanya hivyo kwa sababu tunahitaji Neno la Mungu katika maisha yetu".