Kanisa libadilishe sheria ya Ndoa

Na Mwandishi Wetu

 WANAWAKE wa kanisa katoliki wamedaiwa kutoziheshimu ndoa zao kwa kutambua kuwa kanisa haliruhusu talaka.

Kufuatia hali hiyo inayodaiwa wanawake kuwanyanyasa wanaume ili kuweka haki sawa katika ndoa za kikristo kanisa limeombwa kubadilisha sheria ili talaka ziweze kutolewa. Waumini kadhaa wa kanisa katoliki mjini Mbeya waliohojiwa wamedai kuwa wanawake wengi waliolewa hujingiza katika utovu wa nidhamu na kutoheshimu ndoa.

Mwenyekiti wa vijana wa parokia ya Mwanjelwa Grasiano Nziku ameeleza kuwa wanawake wengi hujivunia sheria ya ndoa ya kanisa ambayo hairuhusu talaka.

Akifafanua alisema ingelifaa kanisa lifikirie mabadiliko ya sheria ili kuruhusu talaka pale kanisa litakapothibitisha kuwa kuendelea kwa ndoa kunaweza kuhatarisha usalama mume na mke.

Alisema kuwa sheria ya sasa imewafanya wanandoa kutengana bila kibali cha kanisa na kudumu katika maisha nje ya ndoa kwa muda mrefu pasipo sababu.

 Seminari ya Mt. Maria, Malikia wa Mitume Sengerema, yatimiza miaka minne

Na Padre Revocatus Makonge, Geita

 KATIKA mazingira yaliyotawaliwa na shamra shamra mbali mbali, seminari ya Mt. Maria Malkia wa Mitume iliadhimisha umri wa miaka minne ya uwepo wake, pale wanafunzi 26, walipokabidhiwa rasmi vyeti vyao vya kuhitimu kidato cha nne hapo tarehe 21.11.98.

Seminari hiyo, ilianza rasmi Februari, 1995 ambapo wanafunzi wapato 38 walipokelewa rasmi kufungua shule hiyo inayomilikiwa na Jimbo Katoliki la Geita. Kwa kufuatia historia ya uhusiano wa majimbo ya kanda ya ziwa seminari hiyo ilipokea wanafunzi kutoka majimbo ya Geita, Mwanza, Musoma na Shinyanga. Majimbo hayo ndio huunda umoja unaojulikana kama SMMG

Wazo la ujenzi wa seminari hiyo lilianza sambamba na kusimikwa kwa Askofu Aloysius Balina ambaye ndiye askofu, na mwanzilishi wa jimbo la Geita, kabla ya kuhamishiwa jimboni Shinyanga .

Jiwe la msingi la seminari hiyo lilibarikiwa na Baba Mtakatifu, Papa Yohanne Paulo II alipokuwa katika ziara yake ya kichungaji katika kilima cha Kawekamo Mwanza, Septemba 1990.

Kazi ya ujenzi wa seminari hiyo ulianza mara moja kwa kuunganisha nguvu za waumini wote Jimboni na misaada toka kwa wafadhili walioko ndani na nje ya Jimbo. Waumini wote Jimboni walichangia fedha, mazao na nguvu zao, jambo ambalo liliifanya kazi ya ujenzi kuwenda kwa kasi; na kupelekea ufunguzi wa shule hiyo kufanyika mwaka 1994, ambapo sasa kuna vidato vinne vyenye jumla ya wanafunzi (97) tisini na saba.

Mkuu wa seminari hiyo, Padre Nicodemus Duba, amesema kazi ya kuwapata walimu wazuri wa shule hiyo siyo rahisi kwani inahitaji uchunguzi wa kina wa tabia na mwendendo wa walimu hao ambao licha ya kuwa na uwezo wa taaluma zao hufanya pia kazi ya malezi ya vijana hao ambao wanajiandaa kuwa viongozi bora wa kanisa hapo baadaye. Seminari hiyo inajumla ya walimu kumi na moja, kati yao wawili ni mapadre.

Wanafunzi wa seminari hii huweka bidii sana katika kusali na masomo bila kusahau kujishughulisha na kilimo cha kisasa. Asilimia 5 ya mahitaji yao ya chakula huzalishwa shuleni hapo, ambapo Parokia zote jimboni huchangia asilimia 65 ya chakula chote, na asilimia 30 iliyobaki hutolewa na jimbo.

Askofu, Aloysius Balina, wa Jimbo la Shinyanga na msimamizi wa kitume wa Jimbo la Geita alikuwa ni miongoni mwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, ya kwanza shuleni hapo, ambapo alikabidhi vyeti kwa wahitimu.

Wanafunzi hao watafanya mitihani yao mwezi Januari 1999 kufuatia kufutwa kwa mitihani ya Taifa kulikofanywa na Wizara ya Elimu na Utamaduni kuliko zikumba shule zote nchini kufuatia kuvuja kwa mitihani hiyo

Padri McCue afariki dunia

Na Mwandishi wetu

 PADRI Philip McCue (Pichani) alifariki dunia mnamo Oktoba 20 mwaka jana (1998) katika kituo cha afya cha Boston akiwa na umri wa miaka 70 na alifanya kazi za kichungaji kwa muda wa miaka 40.

Philipo ambaye ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya Bw.John na Bibi Isabel Kaarney McCue, alizaliwa Desemba 29 mwaka 1927 katika eneo la Dorchester, Massachusetts na alikuwa na kaka watatu na dada mmoja.Alipata Elimu yake katika shule ya St.Margaret iliyopo Dorchester na Elimu ya juu aliipata katika chuo cha Boston kilichopo Boston,Massachusetts.

Baada ya kuhitimu alifanya kazi kwenye Ubaharia wa Umoja wa Mataifa kwa muda wa mika mitatu.Baada ya hapo,Januari 29 mwaka 1949 Padri Mccue aliiangia Maryknoll kwenye seminari yaVenard iliyopo Clarks Summit,Pennsylvania na alimaliza masomo yake mnamo Juni 14 mwaka 1958.

Baada ya hapo Padri McCue alipangiwa kufanya kazi katika Jimbo la Shinyanga lililopo Afrika Mashariki nchni Tanzania (Tanganyika) na Januari 1959 baada ya kujifunza lugha ya Kisukama alianza kufanya kazi na watu wa kabila hilo ambapo alikuwa akifanya kazi katika parokia nne ambazo ni Wira,Malili,Kilulu na Sayusayu kwa kipindi cha miaka 15.

Mwaka 1973 padri McCue alijiunga na kozi kwenye chuo cha Maryknoll kilichopo New York,Marekani na baada ya hapo alirudi tena Afrika Mashariki ambapo mara hii alipangiwa kufanya kazi kwenye misheni ya Maryknoll iliyopo nchini Kenya na akiwa nchini humo alifanya kazi yake baada ya kujifunza lugha ya Kiswahili.

Padri MaCue alifanyakaki kwenye Miinuko ya Eldoret iliyopo kwenye Msitu wa Burnt na baadaye alipangiwa kufanya kazi sehemu za Pwani kwenye Parokia ya Kilifi kwenye Bahari ya Indi.

Mwaka 1990 ,Padri McCue alipangiwa kufanya kazi kwenye Parokia ya Umoja ,parokia ambayo ipo Nairobi Mjini,Kenya.

Kazi hii ilikuwa tofauti na hizo kazi alizokuwa amezoea kuzifanya.Baada kukaa kwenye parokia ya Umoja kwa kipindi cha miaka saba alirudi tena kwenye Jimbo.ambapo alisaidia kuendeleza vigango kwenye misheni ya Maryknoll.Baada ya kukaa Afrika Mashariki kwa kipindi cha miaka 30,Julai 1997 alihamishiwa kwenye Jumuiya ya Wastaafu na aliwahudumia wakazi kwa kusaidiana na dada yake, Kathleen,kwenye eneo la Dorchester,Massachusetts pamoja na kaka yake Francis X.

Heshima za mwisho zilitolewa mnamo Oktoba 23 mwaka 1998 saa 7.30 mchana kwenye kanisa la Malkia wa Mitume lililopo Marryknoll ambapoPadri Stephen Schroeppel na Padri Geogre Egan walitoa mahubiri na misa ya mazishi ilifanyika kwenye kanisa hilo mnamo Oktoba 24 saa 11.00 asubuhi ambapo mazishi yalifanyika kwenye kituo cha Marykoll.

Kila Padri wa Maryknoll aliombwa kuweka misa moja kwa ajili ya maombi ya Padri McCue na kila Muumini aliombwa kmwombea kwa sala Padri huyo katika kazi zake za kiofisi na za kibinafsi alizofanya wakati wa uhai wake.

Askofu Mkude awataka Mashemasi kuachana na 'matawi'

Na Sr. G. Shirima

 ASKOFU Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro, amewataka vijana aliowapatia Ushemasi kuwa tayari kuachilia mambo ya ulimwengu ili waambatane na Yesu badala ya kuendelea kung'ang'ania mambo ya awali.

Askofu Mkude aliyasema hayo wakati akitoa Daraja la Ushemasi kwa vijana 10 wa Mashirika ya Mtakatifu Francis na Damu Takatifu Azizi ya Yesu ambapo kila moja lilikuwa na vijana watano, katika Seminari ya Salvatorian Kola Morogoro.

Hata hivyo Askofu Mkude alikiri kuwa katika miaka 11 ya Uaskofu wake, hajawahi kutoa Ushemasi kwa vijana wengi kwa mara moja kama alivyofanya hivi karibuni. Hivyo alihimiza uaminifu katika maisha yao ya wakfu kama watawa na kama Mashemasi ambao kazi yao ni kutoa huduma.

Akisisitiza wito wake kwa vijana hao, Askofu Mkude alifafanua umuhimu wa kujitoa kwa kazi za Bwana kwa kusema kwamba, siku moja Yesu alipokuwa akitembea kando ya bahari, alikutana na kijana mmoja ambaye alikuwa anakumbwa na mawimbi ya bahari. Akawa anashikilia matawi yaliyoning'ingia baharini. Alipomuona Yesu alimwomba msaada, Yesu alimtaka aachilie yale matawi ili amshike mkono wake, yule kijana alishindwa kuachilia matawi akawa ameyang'ang'ania tu.

Askofu Mkude kwa kauli hiyo, aliwauliza Mashemasi hao kwa pamoja na watawa wote waliojumuika kusherehekea tukio hilo kama wako tayari kuachilia mambo ya ulimwengu ili wambatane na Yesu au wazidi kung'ang'ania majani yaani mambo yao ya awali. Misa hiyo aliongoza kwa kushirikiana na mapadre kutoka seminari zote za Kola na kuhudhuriwa na watu kutoka sehemu mbali mbali.

Alisema kuwa wakiendelea kung'ang'ania matawi, hawataweza kusaidiwa na Yesu, mpaka waachilie yote na ndipo Yesu atakuwa na nafasi ya kuwasaidia na ndipo utume wao utakuwa na nguvu.

 

Kardinali asisitiza mipira ya kiume kutokuwa kinga ya ukimwi

Na Burton Brown

 MWADHAMA Kardinali Polycarp Pengo amesema mipira ya kiume na ya kike kondom si kinga madhubuti ya kujiepusha kuambukizwa ungonjwa wa ukimwi na badala yake ameshauri watanzania wote kuacha kabisa zinaa.

Akizungumza ofisini kwake jijini hivi karibuni kardinal Pengo alisema ni jambo la busara ikiwa watu wataoa au kuolewa na kuheshimu ndoa zao na kuaminiana, na wale ambao hawajaoa waachene kabisa na zinaa kwa vile kondomu si kinga halali ya kuzuia ukimwi.

Alisema kuruhusu matumizi ya kondom ni sawa na kuhalalisha watu waendeleze ufuska ama zinaa jambo ambalo litachochea kuongezeka kwa ukimwi duniani.

"Hivi kweli kama mume anamwamini na kumheshimu mke wake anaweza kuthubutu kumwambia atumie kondom, hii ni dalili ya kuwa hawaaminiani, jambo ambalo ni hatari katika maisha yao alihoji" kwa wawili wapendanao kuhiji matumizi ya kondomu ni dalili au ishara kuwa hawaaminiani.

Alisema Mungu ameumba watu kupendana na kuheshimiana lakini sio kutoaminiana na kuanza kutumia vifaa kondomu ambazo ni kinyume na kanisa.

"Ningependa kuwaomba watu waachane na zinaa hata kama ni mapadre inabidi waachene na zinaa, wake kando" alisema.

Kuhusu matumizi ya madawa ya kulevya kwa vijana Pengo alisema inatokana na tabia ya watu wachezhe kutaka utajiri wa haraka haraka na kusahau kumweka Mungu katika nafasi ya kwanza.

"Utumiaji wa madawa ya kulevya hauwezi kukomeshwa ikiwa watu katika jamii, watatupiana majukumu ya kuwakemea vijana kuacha kutumia madaya ya kulevya" alisisitiza.

 

TUNAJIFUNZA NINI KATIKA BIBLIA

 

Yohana: Ni Nabii bila kifani

"Basi, mlikwenda kuona nini? Nabii? Naam, hakika nizaidi ya nabil. (Mt.11:9) Yohane Mbatizaji alikuwa nabii. Lakini alikuwa zaidi ya nabii. Ni Mtangulizi wa Masiya. alikamilisha mstari wa manabii wa Agano la Kale. Huko Palestina kwa muda wa miaka 200 hapakuwepo na nabii. Baadaye alikuja Yohane Mbatizaji ambaye Baba yako Zakaria alitabiri baada ya kujazwa na roho Mtakatifu:

"Nawe, mwanangu

Utaitwa nabii wa Mungu mkuu,

Utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake:

Kuwatangaziea watu kwamba

Wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao" Lk.1:76-77)

Nabii Malaki alitabiri juu ya Yohane: "Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu" (Malaki 3:1). Yohane Mbatizaji alikuwa zaidi ya nabii, alikuwa mtengenezaji njia. Alivaa vazi maalumu la kimapokeo la manabii kama alivyokuwa nabii Eliya. "Alikuwa amevaa vazi la manyoya, tena amejifunga shuka ya ngozi kiunoni mwake. Naye akasema, ndiye yule Eliya Mtishbi" (2 Wafalme 1:8). Kwa karne nyingi watu waliheshimu vazi la namna hiyo alama ya nabii, lakini manabii wa uongo walisababisha vazi hili lisheshimike, kulivaa ilikuwa ni kukaribisha dhihaka kuwa aliyelivaa ni nabii wa uongo. "Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba manabii, kila mmoja wao, atayaonea haya maono yake atoapo unabii; wala hawatavaa joho ya nywele ili kudanganya watu" (Zakaria 13:4).

Wengine walifikiri Yohane Mbatizaji alienda jangwani kutanua. Wengine walifikiri ni Eliya: "Angalieni, nitawapelekea eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya BWANA, iliyo kuu na kuogofya. Naye ataigeuza mioyo ya baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana "Malaki 4: 5-6.

"Wayahudi walingoja kurudi kwake eliya kwa shauku wakakutazamia kurudi kwake kama alama ya kuwajulisha kwamba wakati wa Masiya ni karibu. Yesu amesema kwamba Eliya amekwisha fika. Ni Yohana Mbatizaji (Mt. 17: 10-13; Mk. 9:2-13; Mt.11:7-13)". Yohane alitokea kama sauti iliayo nyikani:

lMAISHA

Tunatayarisha njia ya Bwana tunapokuwa sauti inayosikika. Na sio sauti inayonongona au iliyo haisikiki. Tunatayarisha njia ya Bwana Yohane Mbatizaji tunapolipeleka neno la Mungu kwa watu. Kwa ubatizo sisi ni "manabii". Hatuna budi kutoa neno la Mungu, pia na kulisoma. Shetani haogopi biblia yenye vumbi. Tunapoondoa mambo na vitu vinavyoziba njia, tunakuwa watayarishaji wa njia hasa kipindi hiki cha majilio. Vilema vinalvyoziba njia ni uchoyo, wizi wa mitiahani, majivuno, rushwa, chuki, ukabila, kutaja machache. Tunanyosha njia na vijia kama nabii Yohane Mbatizaji kwa kuondoa hayo.

Katika mapokeo ya Kanisa Yohane Mbatizaji ni Mhubiri ni nabii anayetuelekeza kwa Yesu Kristu. Kila mhubiri wa injili anakuwa Yohane Mbatizaji mwingine ambaye analishuhudia neno la kinabii la Mungu.