TUNAJIFUNZA NINI KATIKA BIBLIA

 

Bwana, utufundishe na sisi kusali

ZIPO silaha mbalimbali za kiroho alizovaa Yohane Mbatizaji nazo ni Sala, kufunga na sadaka. Kwa leo tutafakari silaha ya kwanza: Sala.

Tumeitwa na Kirsto. Tumeitika wito wake. Hivyo, tunafanya kazi yake. Yeye alikuwa mtu wa sala. Aliwafundisha watu namna ya kusali kwa mafundisho yake na tendo halisi la kusali. Sisi kama wafuasi wake na tulioitika mwito wake wa kuwa viongozi wa taifa lake, tuige mfano wake. Katika tafakari hiyo, tusaidiwe na Yesu wa Mwinjili Luka. Mwinjil Luka, anatilia mkazo mkubwa katika umuhimu wa sala. Kwa yakini, umuhimu huo unaonekana bayana. Kwanza jinsi Yesu aliivyosali mara nyingi. Pili, alivyowahimiza watu wasali. Tatu, jinsi alivyota mifano bora ya kusali.

Injili ya Luka inaonesha dhahiri kuwa kabla ya kuchukua hatua kubwa na muhimu, yesu anaanza kwa sala. Tuzitazame fasuli zifuatazo:

 

l1. Ubatizo wa Yesu (Lk 3:21-22)

Katika nafasi ya kubatizwa kwa Yesu, Luka anasema kuwa watu wote walipokuwa wamebatizwa, naye Yesu alibatizwa. Na alipokuwa anasali, mbingu zilifunguka, na Roho Mtakatifu alimshukia akiwa katika umbo la njiwa. Sauti ikasikika kutoka mbinguni: "Wewe ndiwe Mwanangu, nimependezwa nawe".

Hatua hiyo ya kubatizwa ilikuwa ya maana sana. yesu alithibitishwa kuwa Mwana tena mpenzi wa Mungu. Alijiunga na foleni ya wadhambi ili apokee ubatizo wa toba, toba iletaya ondoleo la dhambi. Lakini yeye hakuwa na dhambi. Alihakikishiwa kuwa njia aliyochukua yaani utume wake ilikuwa sahihi, na kwa kweli yalikuwa mapenzi ya Mungu.

 

l2. Yesu anawateua mitume kumi na wawili (Lk 6:12-16).

Tendo lilitanguliwa na sala. Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akisali. Kesho yake aliwaita wanafunzi wake, miongoni mwao akawachagua kumi na wawili ambao aliwaita mitume. Alijitenga na watu ili awe karibu na Mungu baba yake. Kwa hiyo, uteuzi wa mitume uliongozwa na Baba. Hatua hiyo ilibeba umuhimu mkubwa sana - kuwateua viongozi wanaofaa. tunasoma pia uteuzi wa mitume ukitanguliwa na sala katika Mdo 13:1-3. Katika kanisa la Antiokia kulikuwepo na watu wengine waliokuwa manabii na walimu. Walipokuwa wanafanya ibada yao kwa Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu alisema: :Niteulieni Barnaba na Saulo kwa ajili ya kazi niliyowaitia." Basi, baada ya kusali na kufunga zaidi, wakawekea mikono, wakawaacha waende zao.

l3. Petro anamkiri Yesu Kristo (Lk 9:!8-20) Yesu alikuwa akisali peke yake na wanafunzi wake walikuwa karibu kabla hajaanza kuwauliza: :Eti, watu wanasema mimi ni nani?" Baada ya kutoa majibu mbali mbali, Yesu anawauliza wanafunzi wenyewe: "Ninyi je, mwasema mimi ni nani?" Petro kwa niaba ya wanafunzi wenzake alitoa jibu sahihi: "Wewe ndiwe kristo wa Mungu." Hiyo ilikuwa hatua kubwa, yaani azma ya Yesu kujua kama watu na wanafunzi wake wanamfahamu: Yeye ni nani na utume wake ni upi. Kumfahamu ni sharti muhimu ili utume wake uzae matunda.

Itaendelea toleo lijalo

 

 Vijana Wakatoliki Manzese wataka uzingativu wa maadili

Na Mwandishi Wetu

 

Vijana wa dhehebu la kikatoliki nchini wametakiwa kuzingatia maadili mema yanayoendana na imani yao ili kuwawezesha kuwa watumishi wema wa kazi za mungu kwa siku za usoni.

Wito huo umetolewa na Mlezi wa kikundi cha vijana wa chama cha watumishi Kanisani,cha Manzese, jijini,Bibi.Lucy Kassanga, wakati wa sherehe za vijana hao zilizofanyika hivi karibuni.

Mlezi huyo alisema kuwa vijana wanaofanya shughuli hiyo hawana budi kuwa wasafi wakati wote kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanajijengea mazingira mazuri ya utumishi wa kazi za mungu hapo baadae.

Alisema kuwa mara nyingi wito wa kuwa mtumishi wa mungu huanzia katika utumishi huo,hivyo wanapaswa kuheshimu kazi yao ambayo huenda ikapelekea baadhi yao kuwa mapadri na mabruda wazuri. Alitoa wito pia kwa wazazi kuwaruhusu vijana wao kujiunga na vikundi kama hivyo ili waweze kuepukana na makundi mabaya.

Naye Mwenyekiti wa chama hicho Parokia ya Manzese,Bw.Antony Beatus,akizungumza katika sherehe hiyo,alisema kuwa watumishi wote wanapaswa kuwa na umoja na vikundi vingine,hali itakayopelekea umoja wa vijana wa Manzese kuwa na nguvu.

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na watumishi wa parokia nyingine ambazo ni Makunburi,Mburahati,Kigango cha Tandale na kwamba viongozi mbalimbali wa vyama vya vijana na vyama vingine vya kitume walialikwa kuhudhuria.

Waaumini watakiwa kupokea kifo kwa furaha

Na Padri Ben Rwegoshora

 Baba Askofu Severini Niwemugizi amewataka waumini wa Jimbo Katoliki la Rulenge kupokea kifo kwa furaha kama njia ya kuingia uzima mpya usio na mwisho, badala ya kuhuzunika sana na kukata tamaa.

Askofu Niwemugizi aliyasema hayo Parokiani rulenge tarere 15.1.99 wakati wa mazishi ya Padri Alfred Buholera aliyeaaga dunia parokiani Biharamulo, siku ya Jumatano tarehe 13.1.1999.

"Uchungu wetu uwe wa kibinadamu tu, lakini sisi kama Wakristu hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kupenda kuchukua kwake kiumbe chake Padri Alfred," alisema Askofu Niwemugizi.

Hayati Padri Alfred Buhorera ni mtoto wa kwanza wa Marehemu Cosma Buhorera Kananura na Mama Sara Mukabagorora Tihabyona. Alizaliwa Nyaishozi (Karagwe) mwaka 1954 na kubatizwa mwaka 1957 katika Kanisa la Nyaishozi.

Alisoma shule ya msingi Kyanyamisa darasa la kwanza hadi la saba na kumaliza masomo hayo katika shule ya msingi Nyaishozi. Baada ya masomo hayo alijiunga na Seminari ya katoke mwaka 1968 hadi mwaka 1970. Mwaka 1971 alijiunga na seminari ya Rubya na kumaliza masomo yake ya Sekondari mwaka 1972.

Alijiunga na seminari kuu ya Ntungamo mwaka 1973 na kumaliza masomo ya falsafa mwaka 1974. Mwaka 1975 alijiunga na seminari kuu ya Kipalapala na kumaliza masomo ya Teologia mwaka 1979. Alipewa daraja la Ushemasi trehe 1.7.1979 katika Kanisa la Bugene. Tarehe 16.12.1979 alitunukiwa daraja la Upadrisho na Baba Askofu Christopher Mwoleka Parokiani Nyaishozi.

Marhemu Padri Alfred Buhorera atakumbukwa kwa karama mbali mbali alizoonyesha katika uchungaji wake. karama hizi ni pamoja na upendo kwa watu, huruna, ukarimu na bidii ya kazi. Apumzike kwa Amani.

Askofu Banzi afungisha ndoa 130 kwa mpigo Muheza

Na Pd. E. Ndunguru,Tanga

 

MHASHAMU Askofu Antony Banzi hivi karibuni alifungisha ndoa 130 kwa mopigo katika moja ya mlolongo wa shughuli za kumbukumbu ya kupoewa kwake Upadre miaka 25 iliyopita.

Kazi hiyo ya kutoa sakramenti ya ndoa ilifanyika katika parokia katoliki ya Muheza.

Aidha Jubilei hiyo ya Mhashamu Askofu Anthony Banzi ilisherehekewa kwa maadhimsho ya Sakramenti za Ubatizo, Upatanisho, Ndoa, Mpako wa Wagonjwa na Komunyo ya kwanza na Sakramenti ya Kipaimara .

Akimkaribisha Askofu Banzi kwenye ibada ya kuadhimisha sakramenti hizo, Paroko Nyandwi alimweleza Askofu kuwa, Waamini wa parokia yake walikuwa wamejiandaa kwa namna ya pekee kusherehekea Jubieli yake ya Miaka 25 ya Upadre kwa kuboresha maisha yao ya roho kwa kujitayarisha kupokea sakramenti mbali mbali na hasa sakramenti ya Ndoa.

"Baadhi ya waamini wa Muheza, leo watapokea kutoka kwako Baba Askofu Sakramenti ya Ubatizo, Mpako wa Wagonjwa, Komunyo ya kwanza, Aidha utafungisha ndoa na kesho utahitimisha sherehe hizo kwa kutoa Sakramenti ya Kipaimara," alisema Paroko Nyandwi, na Kanisa zima la Muhezi lilijaa kelele za shangwe ya makofi na vigelegele.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza katika historia ya Jimbo katoliki la Tanga watu 130 kufunga ndoa. Muda wote wa ibada ya ndoa iliyochukua saa mbili maharusi walishangiliwa kwa nyimbo, hoi hoi na vifijo.

Katika mahubiri yake, pamoja na mambo mengine, Baba Askofu alimshukuru sana Baba Paroko Nyandwi, viongozi wa parokia na wale wote walioshiriki katika maandalizi ya sherehe hizo zilizolenga hasa katika kuboresha maisha yao ya roho.

Wakati huo huo waamini wa Parokia Katoliki ya Muheza wameahidi kwa Askofu Anthony Banzi mchango wao wa shilingi laki sita kujenga jengo la Kichungaji, Mjini Tanga.

Wakizungumza katika hafla ya kumpongeza Askofu Banzi kwa kutimiza miaka 25 ya Upadre waamini hao walisema kuwa wanaitikia ombi la Askofu Banzi kuchangia jengo hilo la kichungaji baada ya kuwaeleza kuwa jengo hilo litakapomalizika, litakuwa linatoa huduma za kijamii kwa watu wote bila ubaguzi, ndani na nje Mkoani Tanga, ndani na nje Tanzania.

Baba Askofu aliwaambia waamini kuwa kazi ya ujenzi wa jengo hilo ambalo kazi ya msingi ilikuwa imekwisha kukamilika ilikuwa imesimama kutokana na ukosefu wa fedha.

"Ilikuwa ni vigumu sana kupata msaada kutoka Ulaya kwa ajili ya kuendelezea ujenzi wa jengo hilo. Kwa vile waamini wa jimbo katoliki la Tanga mmechangia tayari shilingi milioni sita miaka 8 iliyopita, kiasi ambacho kimetumika kwa kazi ya msingi, basi nawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendela kuchangia ujenzi wa jengo hilo," alisema baba Askofu.

Katika hafla hiyo waamini mbali mbali wa parokia ya Muheza na Parokia nyingine za jimbo la Tanga na hata nje ya jimbo, watu binafsi akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Muheza, na viongozi na waamini wa madhehebu mengine Wilayani Muheza walitoa ahadi ya kuchangia fedha taslimu na vifaa vya ujenzi

Pamoja na mchango huo waamini waliopokea Sakramenti ya Ndoa, Komunyo ya kwanza, Ubatizo, Kipaimara nao walitoa michango yao ya pekee kama vile ya fedha na vitu mbali mbali. walichanga fedha taslimu shilingi 144,130 na vitu vyenye thamani ya shiling 150,000

Akimshukuru Paroko wa Muheza,. Mheshimiwa . padre Leopold Nyandwi, Uongozi wa Parokia ya Muheza, Waamini na Wananchi wa Muheza kwa mchango huo askofu alisema kwamba, alikuwa ametiwa sana moyo na hivyo alikuwa na matumaini makubwa parokia nyingine 26 za Jimbo la Tanga zitaiga mfano wa Muheza.

Aidha, Askofu aliwahakikishia waamini hao kuwa vitu vyote hivyo vitabadilishwa na fedha zitakazopatikana kutumika kwa ajili ya kuendelezea ujenzi wa jengo la Kichungaji.

Askofu Msarakie kubariki nyumba ya masista

Na Grolia Tesha, Moshi

 Askofu Mkuu wa Jimbo la Moshi Mhashamu Askofu Amedeusi Msarikie mwishoni mwa mwezi huu anatarajiwa kubariki na kufungua rasmi nyumba ya Masista katika Kanisa la Mt.Fransisko Xsaveri (Mkombole), Moshi vijijini Mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza na gazeti hili Padri Urbanusi Ngowi alisema, ujenzi wa nyumba hiyo yenye vyumba sita vya kulala iligharimu zaidi ya Sh milioni 30.

Paroko huyo alisema nyumba hiyo imejengwa kwa zaidi ya miaka kumi na miwili ikiwa ni pamoja na jiko kubwa lililogharimu sh. Milioni 1.8.

Alisema Masista wanaotarajiwa kuja kulea na kuikuza Parokia hiyo ni wa shirika la masista la Huruma Mkoani Kilimanjaro.

"Unajua Parokia yeyote yenye masista inakuwa na maendeleo makubwa sana kwanza inakuwa na utulivu na maombezi mazito kupitia kwa Bikira Maria," alisema Paroko huyo kwa furaha.

Alisema tarehe rasmi ya kuifungua na kuibariki nyumba hiyo haijafahamika ila Askofu ndiye anayesubiriwa kutaja siku aliyoipanga yeye ili asivuruge ratiba nyingine.

Pamoja na mafanikio hayo pia Padri Ngowi alisema ameahidiwa kupata msaada wa rangi za kupaka kanisa zilizotoka Ujerumani zilizogharimu T.sh 1,746,000.

Alisema pindi msaada huo utakapowasilishwa kazi ya kukarabati kanisa hilo la Parokia ya Mkombole Kibosho utaanza