Mugana wamuaga paroko F. Mutagwaba

BUKOBA:Septemba 2,1998, ilikuwa siku ya hudhuni na masikitiko makubwa kwa Wakristu wa Mugana kwa ajili ya kuondoka kwa mchungaji wao mpendwa sana Paroko Padre aliyetajwa hapo juu. Waumini walimiminika kimya kimya tangia asubuhi kuelekea parokiani kwa nia ya kuonyesha heshima shukrani na upendo mkubwa, waliokuwa nao wakati wa kumuaga mheshimwa Padre Francis anaandika Sista M.G. Kanyawera

Katika kipindi cha kukaribia miaka miwili aliyoishi Mugana, padre Mutagwaba amefungisha ndoa 160 na kuzindua jumuiya ndogo ndogo nyingi.

Aidha amefufua mashine ya kusaga , akasimika na kinu cha kukoboa. Amejenga ukumbi wa Parokia ambao tayari unatumika. Amefufua mashamba ya parokia na kutoa masaada wa mbegu za mahindi, mbolea na madawa ya kuua wadugu waharibifu wa mimea kwa waumini.

Katika Wosia wake alisema atasikitika sana iwapo matunda yalityopatikana katika parokia hiyo ya Mugana yatapotea.

 

Kipaimara Shinyanga Sekondari

SHINYANGA:WAZAZI wametakiwa kusali pamoja na familia zao ili kujenga maadili ya sala na kutimiza wajibu wao wa malezi kwa watoto wao. Kwa njia hiyo itasaidia kujenga maadili mema ya kikanisa na kuepukana na mmomonyoko wa maadili ambao vijana wengi wanaiga tabia za kigeni pasipo kuelewa madhara yake anaandika Charles Hililla

Rai hiyo ilitolewa na Askofu Aloysius Balina, wakati wa misa ya kuwapatia sakramenti ya kipaimara vijana wapato 83 wa parokia ya Shinyanga sekondari Novemba 15, mwaka huu.

Aidha Askofu Balina aliwaambia waumini waliokuwa wamefurika kanisani hapo ambao asilimia kubwa ni wanafunzi kuwa na uchaji wa Mungu, na kumwogopa Mungu muumbaji kwa kuacha kiburi na anasa mbali mbali ambazo haiendeani na asili ya uumbaji wa Mungu. Na kuwa wakarimu kwa Mungu ili baadae kuwa viongozi safi wa Kanisa na serikali kwa ujumla.

Wakati huo huo waumini wa Parokia ya Kanisa Kuu la Jimbo la Shinyanga - Ngokolo mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu wametoa vifaa ya ujenzi vyenye thamani ya 1,023,000/- ikiwemo mifuko 112 ya saruji na mabati 54 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa seminari ya Jimbo inayoendelea kujengwa huko Maswa.

Mpaka sasa hivi jumla ya 2,634,500/- pamoja na vifaa mbalimbali vya ujenzi vimetolewa na waumini wa Jimbo la Shinyanga kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa seminari hiyo ambayo itakuwa ya kwanza Jimboni hapa.

Akiongea kwenye misa ya Kipaimara kwa vijana 370 wa Parokia ya Ngokolo na kupokea zaka ya mwaka 1998 kwa Parokia hiyo: Askofu Balina aliwashukuru wana Parokia hao kwa michango yao hiyo na kuongeza kuwa waendelee na moyo huo wa kulitegemeza na kulijengea Kanisa.

Wanaparokia hao waliwasilisha jumla ya Sh. 6,010,750/- kama shukrani yao kwa Mungu kulingana na walivyojaliwa kwa mwaka huu 1998. Hilo ni ongezeko la mara mbili; mwaka jana walitoa kiacha milioni tatu.

Aidha wanaparokia hao walitoa ufadhili kwa ajili ya Parokia zenye uwezo mdogo jumla ya Shs. Laki moja. Kiasi kingine kama hicho walitoa kwa ajili ya kusaidia Umoja wa Masista Jimboni.

Walitoa pia Laki moja nyingine kwa ajili ya mafuta ya gari la Askofu na zingine tena Laki moja kwa ajili ya chakula kwenye nyumba ya askofu. Zingine tena laki sita walimpatia Askofu kama asilimia 10% ya mapato ya parokia hiyo na kufanya jumla ya Tshs. milioni moja walizotoa kufadhili taasisi mbalimbali jimboni.

 

Wanandoa watoa ushuhuda wa mabadiliko katika kushirikiana

MBEYA:USHIRIKISHWAJI katika maamuzi na mipango ya familia ni moja ya mabadiliko ambayo yameanza kujionyesha kwa wanandoa 154 wa mjini Mbeya walioshiriki mafundisho yenye ndoa za ushirikiano yaliyoingizwa mjini hapa hivi karibuni na Padri wa dhehebu la Kikatoliki Pedro Fogue anaandika Lucas Mlekeafike Ndanga.

Wakitoa ushuhuda huo wa mabadiliko jana mjini hapa kwa niaba ya wenzao 154 wanandoa watano wameeleza kuwa tangu washiriki semina za maufndisho hayo wanafanya maamuzi na mipango yote ya maendeleo kwa kushirikisha familia nzima.

Jozi moja ya wanandoa waliotoa ushuhuda wa eneo la Simike Bwana na Bibi Michael na Emilline Sambwe wameeleza wenzao kuwa ingawa tendo la ndoa ni halali kwa waliofunga ndoa bado hata wanandoa waliokubuhu huogopana kuombana huduma hiyo takatifu lakini tangu wahudhurie mafundisho hayo wanahudumiana bila woga.

Jozi nyingine ya wanandoa ya Bwana na Bibi William na Veneranda Kulwa wamewadhihirishia wenzao kuwa wameyarekebisha mapungufu mengi sana kutokana na kuhudhuria semina hiyo yakiwemo ya kutoshitakiana kwa balozi wanapokosana na kuelezana kwa uwazi mambo ya familia kuliko ilivyokuwa awali.

Naye mkufunzi mkuu na mwanzilishi wa mafundisho haya maoni Mbeya Padri Fogue ameieleza gazeti hili katika mahojiano kuwa maeneo mengine ya mafanikio ya mpango huu wa mafundisho ya ndoa zenye ushirikiano ni kuongezeka kwa wanandoa walioshiriki mafundisho yenye ndoa za ushirikiano kutoka jozi 30 za wanandoa hadi 233 mwaka huu.

Sambamba na mabadiliko hayo, kumekuwepo mafanikio kadhaa yakiwemo ya kuundwa kwa matawi matatu ya chama cha wenye ndoa.

Wakati huo huo, katika maendeleo mengine, chama cha wenye ndoa kimejipatia Mwenyekiti katika ngazi ya parokia Bwana na Bibi Joseph Simbi.

Wamisionari wa Damu Azizi ya yesu wachagua uongozi

morogoro: Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu , vikarieti ya Tanzania hivi karibuni waliwachagua viongozi wao wa kwanza watakaoiongoza vikarieti hiyo kwa kipindi cha miaka minne ijayo anaripoti Fr. Chesco Msaga Cpps

Wamisionari hao walimchagua Padre Antonio Calabrese kuwa Mkuu wa Vikarieti ya Tanzania katika mkutano mkuu uliofanyika kwenye seminari kuu ya mtakatifu Gaspar mjini morogoro Chini ya uangalizi wa mkuu wa kanda ya Italia Padre Pietro Battista.

Aidha mkutano huo mkuu uliwachagua wajumbe wanne watakao unda Halmashauri kuu ya vikarieti. Padre Reginald Mrossso alichaguliwa kuwa mshauri wa kwanza wa mkuu wa vikarieti , naye Padre Chesso Peter Msaga alichaguliwa kuwa mshauri wa pili na katibu wa vikarieti.

Katika mkutano huo Padre Genes Mahedi alichaguliwa kuwa mshauri wa tatu na Padre Francis Bartoloni kuwa mtunza hazina wa vekarieti.

Mkutano huo ulianza na mafunzo ya kiroho kwa muda wa siku tatu ambayo yaliongoza na Padre Mario Brotini, ambaye ni Kaimu wa Shirika Kanda ya Italia, na Gombera wa Seminari kuu ya shirika iliyopo mjini Roma.