Mahujaji wa Poland waungana na Papa

Mahujaji 20,000 kutoka Poland waliungana na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili Oktoba 16 kwenye viwanja vya Basilika ya Mt. Petro kusherehekea miaka 20 ya Upapa wake.

Mwanzo wa hotuba yake Baba Mtakatifu alisema kwamba tukio hilo linamkumbusha wakati baada kuchaguliwa kwake kuwa Papa ambapo aliulizwa kama atakubali.

"Mbele ya macho yangu nina picha ya Mtumishi wa Mungu Stefan Wyszynski. Wakati tukiwa kwenye conclave ... alikuja kwangu na kuniambia 'kama watakuchagua, usikatae.' Nilimjibu 'Asante sana na Mungu awe mwema kwako Kardinali'."

"Leo ninapokumbuka miaka niliyotumia katika huduma zangu kwa ajili ya makao makuu ya Kanisa, Ninamshukuru Mungu kwa kunipa neema ya kutangaza habari njema ya wokovu kwa watu wengi na kwa mataifa mengi katika mabara yote ikiwemo pia Poland."

Baadaye Baba Mtakatifu alikumbusha maneno aliyoyasema mwanzoni mwa utawalala wake wa kipapa "Fungueni milango kwa Kristu! Leo tuko karibu na millenia ya tatu na maneno haya yana muhimu wa pekee. Ninawaambia tena ninyi wananchi wenzangu ikiwa ni matashi yangu makubwa kwenu."

"Kufungua milango kwa Kristu," aliendelea, "ina maana kujifunua kwake na kwa mafundisho yake. ... Bila kuwa na uhusiano na Kristu kila kitu kinapoteza maana yake na kunakuwa na ukungu kati ya mazuri na mabaya. Nchini Poland hivi sasa, kuna umuhimu kwa watu wenye imani thabiti na dhamira bora kluongozwa na injili na mafundisho ya Kanisa. ... Kuna umuhimu wa kuwa na Wakristu wasiokata tamaa na wenye kuwajibika wanaoingia katika sekta zote za kijamii na nchi kwa ujumla, wasiogopa vikwazo vyovyote.

Papa alimalizia kwa kusema, "Leo Oktoba 16, Ninawaomba tena kuniombea ili niweze kumaliza vizuri hadi mwisho, kazi ambayo Mungu amenikabidhi kwa ajili ya utukufu wake na kwa ajili ya huduma ya Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla.

Wakati huo huo jioni siku hiyo Baba Mtakatifu kutoka kwenye dirisha la chumba chake cha kujisomea alitoa baraka kwa waumini waliofurika kwenye viwanja vya Mt. Petro kwa ajili ya kuadhimisha miaka 20 ya upapa wake.

Aidha alishukuru matangazo ya moja kwa moja ya televisheni yaliyoiunganisha Vartican na Poland na hivyo hata kumwezesha kuzisikia kengele za Kanisa la Cracow zikipigwa wakati huo huo.

Maelfu ya watu walikusanyika jioni kwa ajili ya kusikiliza muziki uliokuwa umeandaliwa mahsusi kwa ajili ya sherehe hizo.

"Baada ya miaka 20," alisema Baba Mtakatifu kutoka kwenye dirisha lake, "Ninapenda kumshukuru Mungu kwa wema wake. Pia napenda kuwashukuru nyote mliokusanyika hapa kwa ajili ya sala kwa tukio hili ambalo ni muhimu kwa ajili ya maisha ya Kanisa la Roma, Kanisa zima na pia kwa maisha yangu ya kawaida."

 

Papa atoa changamoto kwa Jumapili ya Misioni duniani

Kabla ya sala ya Malaika wa Bwana kwenye viwanja vya Basilika ya Mt. Petro Jumapili asubuhi, Baba Mtakatifu aliwazungumzia Waumini wapatao 75,000 waliokuwepo kuadhimisha Jumapili ya Misioni na juu ya waraka wake alioutoa Oktoba 15.

"Leo," alianza, "tunasherehekea Jumapili ya Misioni Ulimwenguni. Ilikuwa hivi hivi miaka 20 iliyopita nilipoanza utume wangu kama Halifa wa Petro. Hii kwangu naiona kama bahati ya pekee hasa ninapofikiria juu ya moyo wa umisionari ambao ndio umechochea utume wangu, ambao pia unajieleza katika ziara zangu ambazo nimekuwa nikizifanya katika kupiga kelele katika kila upande wa dunia: 'fungueni milango kwa Kristu'".

Baadaye alisema waraka wake Imani na Fikara "Encyclical 'Fides et Ratio,' uliotolewa alhamisi iliyopita, pia una moyo wa kimisionari. ... ndani yake, kama inavyofahamika ninakutana ana tatizo la uhusiano kati ya falsafa na teolojia, ukitilia maanani kuwa imani na fikara havipingani, bali vinasaidiana kwani matawi haya mawili ambapo moyo wa kiutu unaelekezwa kwenye ukamilifu wa ukweli. Huzuni ya utu inapoteza maana ya ukweli, jitihada za kuutafuta na imani ya kuupata. Siyo tu imani inaweza kukamilishwa na hili bali pia maana ya maisha.

 

 

Mapadre wasaidiwe kutambua sifa na utakatifu wa huduma zao

Baba Mtakatifu amewakumbusha mapadre wajibu wao kuwaangalia na kuwatunza watu waliokabidhiwa kuwachunga.

Hayo alisema wakati akiongea na washiriki wa Mkutano wa Idara ya Makleri uliofanyika mwishoni mwa wiki jana huko Vatican.

Mkutano huo ulikuwa ukijadili dhamira ya 'Padre, Mwangalizi wa jumuiya, Mwalimu wa Neno na Sakramenti katika mtazamo wa uinjilishaji mpya.

Alisema muundo wa Kanisa unapita ule wa kidemokrasia au utawala wa mtu mmojam kwa sababu lenyewe limepatikana kwa Baba kumtuma mwanaye na kukabidhi mapaji ya Roho Mtakatifu kwa mitume 12 na mahalifa wao.

Aliongeza kuwa Padre kwa ushirika na Askofu wake ni mwalimu wa Bneno na mhudumu was Saklramenti.

Alitoas mwito wa kuwasaidia mapadre kutambua sifa za msingi za utakatifu wa huduma zao katika kuelekea kwenye mlango Mtakatifu.

Pia kuwasaidia ili waweze kujitambua kuwa ni watu muhimu na wamechaguliwa na Kristu Kichwa na Mchungaji mkuu kwa sakramenti ya daraja Takatifu.

 

 

Kanisa linawajali wanawake - Papa

Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili mwishoni mwa wiki iliyopita alituma ujumbe wake kupitia kwa waziri wa nchi wa Vatican Kardinali Angelo Sodano kwa Mkurugenzi wa Shirika la Chakula Dunia(FAO, Bwana Jacques Diouf, katika kuadhimisha siku ya Chakula Duniani.

Katika ujumbe wake Baba Mtakatifu alisema kuwa dhamira ya mwaka huu ya siku hiyo "Wanawake wanalisha Ulimwengu" unafanya mtazamo wa FAO kuelekea kwenye mapambano ya kiutu dhidi ya njaa na utapiamlo.

"Kanisa linaheshimu na kujali wanawake katika hali zake zote na linatambua michango madhubuti inayotolewa na wanawake hasa wa vijijini ambapo ni mihimili ya maisha ya familia na maisha ya jumuiya. Hii ina maana kuwa huwezi kutenganisha maisha ya wanawake katika familia kama wake na mama na kazi zao katika jamii kama wafanyakazi na mihimi ya uchumi. Kinachojitokeza katika pande zote mbilio ni utashi wao halali wa kufanya kazi kwa ajili ya manufaa ya wote na hasa kwa ajili ya usawa."

Alisema kuwa anatumaini siku hii ya chakula duniani itafanya dunia iwatambue wanawake siyo tu wanaopaswa kulisha ulimwengu bali kama wanaoleta amani na tuni za kiutu."

 

 

CAFOD kuendelea kuisaidia Tanzania

Na Dalphina Rubyema

SHIRIKA la CAFOD kutoka nchini Uingereza (Caritas ya Uingereza) kupitia serikali ya nchi hiyo, itaendelea kuipatia Tanzania misaada ya chakula ili kukabili upungufu mkubwa wa chakula unaotarajiwa kutokea katika maeneo kadha ya Tanzania kuanzia Novemba mwaka huu hadi Machi Mwakani..

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni,Katibu Mtendaji wa Caritas hapa nchi Bw.Clement Rwelamila alisema kuwa Shirika hilo litakuwa linafanya mwendelezo wa kutoa misaada kama hiyo kwani mwaka jana lilitoa lilitoa misaada ya shilingi milioni 300 kutokana na uhaba wa chakula uliosababishwa na mvua za El-nino.

Katibu huyo aliyerejea kutoka kwenye Mkutano wa nchi zenye maziwa Makuu Barani Afrika,mkutano uliofanyika Dublin nchini Ireland, alisema kuwa tayari amesha zungumza na uongozi wa CAFOD na wamekubali kutoa misaada yao ya hali na mali.

Alisema mbali na CAFOD kutoa misaada yake,Bw.Rwelamila alisema nchi nyingine za Ulaya katika mkutano huo uliozijumusha nchi za Rwanda,Burundi,Congo pamoja na nchi zote za Ulaya zilizoendelea,zimefikia muhafaka kuwa zitatoa misaada kwa ajili ya Wakimbizi waliongia nchi Tanzania na hii misaada itapelekwa kwenye Caritas ya Kigoma kwani ndiyo yenye wakimbizi wengi.

Mbali na kuudhulia mkutano wa Dubrin,Bw.Rwelamila pia aliudhulia mkutano wa Mashirika ya Caritas Afrika nzima(Pan-African Caritas) ,mkutano uliofanyika nchini Mauritius na kuhudhuriwa na zaidi ya nchi 50 ambapo madhumuni ya mkutano huo ilikuwa ni kupanga mikakati ya Caritas ya afrika kwa kipindi cha miaka minne.