Make your own free website on Tripod.com

MIAKA 20 YA PAPA YOHANE PAULO WA PILI: PAPA WA 11 ALIYEONGOZA KWA KIPINDI KIREFU

Amesafiri umbali upatao zaidi ya mara 3 ya ule kati ya dunia na mwezi

Saa 10:45 Alasiri ya Oktoba 14, 1978, siku kumi baada ya mazishi ya Papa Yohane Paulo wa Kwanza, Makardinali 110 wenye haki ya kupiga kura wakisaidiwa na watu wengine 88 waliingia kwenye conclave iliyokuwa haina mawasiliano na ulimwengu wa nje kumchagua mrithi wake.

Saa 12.18 jioni, Oktoba 16, moshi mweupe ulionekana kwenye bomba dogo la kutolea moshi wa kikanisa cha Sistine, ukiashiria kwamba Makardinali wamemchagua Papa mpya.

Dakika 27 baadaye, Kardinali Pericle alitokeza kwenye loggia ya Basilika ya Mt. Petro na kutangaza kuchaguliwa kwa Papa Yohane Paulo wa Pili kuwa halifa wa Mtume Petro kwa maneno haya: "Annuntio vobis gaudium magnum Habemus Papam Carolum Wojtyla, qui sibi nomen imposuit Ioannem Paulum II."

Saa 1.15 Jioni Papa mpya, akiwa amevalia joho jeupe la kipapa, alitokeza na kuzungumza kwa lugha ya Kitaliano maneno ambayo hivi sasa yanajulikana mamilioni ya watu: "Asifiwe Yesu Kristu!"

"Wapendwa ndugu zangu," aliendelea, "sote bado tumesikitishwa na kifo cha mpendwa wetu Papa Yohane Paulo wa Kwanza. Na sasa Waadhama Makardinali wamemwita Askofu mpya wa Roma. Wamemwita kutoka nchi ya mbali, ..., lakini daima karibu katika ushirika wa imani na mapokeo ya Kikristu. Niliogopa kupokea uteuzi huu, lakini nilifanya hivyo kwa moyo wa utii kwa Bwana wetu na uaminifu mkubwa kwa Mama yake aliye Mtakatifu.

"Sijui kama nitaweza kujieleza vizuri katika lugha yenu - lugha yetu- ya Kiitaliano. Lakini kama nitakosea, mtanisahihisha. Na pia ninajitambulisha kwenu, kukiri imani yetu pamoja, tumaini letu, uaminifu wetu kwa Mama wa Kristu na kwa Kanisa, na pia kwa kuanza tena katika njia ya Historia na ya kanisa kwa msaada wa Mungu na wa binadamu wenzetu.

Papa Yohane Paulo wa Pili, Kardinali Karol Wojtyla, Askofu Mkuu wa Cracow, alichaguliwa kuwa Papa wa 264 katika walipopiga kura kwa mara ya pili kwenye siku ya pili ya Conclave ya 1978, baada tu ya miezi mitano tangu aadhimishe miaka 58 ya kuzaliwa. Siku sita baadaye, Oktoba 22, 1978 shughuli zake za kichungaji zilizinduliwa. Leo Oktoba 17 anafikisha siku 7,304 za upapa wake.

Ni Papa wa 11 kutumikia kwa kipindi kirefu katika historia ya mapapa. Aliyetumikia kwa muda mrefu zaidi alikuwa Papa Pius IX (1846-78: miaka 31, miezi 7 na siku 17) wa pili alikuwa mrithi wake Papa Leo XIII (1878-1903: miaka 25, miezi 4 na siku 17).

Mapapa wengine wanane kufuata vipindi vyao vya utawala ni kama ifuatavyo: Pius VI (1775-99, miaka 24, miezi 6); Pius VII (1800-23, miaka 23, miezi 5); Alexander III (1159-81, miaka 21, miezi 11, na siku 10); Mt. Sylvester I (314-335), miaka 21, miezi 11); Leo I (440-461, miaka 21, mwezi 1 na siku 2); Urban VIII (1623-44, miaka 20, miezi 10); Leo III (795-816, miaka 20, miezi 5); Clement XI (1700-21, miaka 20, na miezi 4).

Katika miaka 20 akiwa Papa, amekuwa na Consistory saba ambapo amewateua Makardinali 157. Consistory ya mwisho ni ile ya Februari 21, 1998 ambapo aliwapa ukardinali makardinali 20 (akiwa ameacha majina mawili "in pectore"). Hadi hivi leo kuna Makardinali 157 ambapo 128 wanateuliwa na Yohane Paulo wa Pili.

Kati ya Makardinali 157, makardinali 115 wako chini ya miaka 80 na hivyo wanaweza kuingia kwenye uchaguzi wa Papa mpya. Kati ya hawa 115, makardinali 110 walipewa ukardinali na Papa Yohane Paulo wa Pili.

Toka alipoanza kazi yake ya Upapa, Baba Mtakatifu ameteua zaidi ya maaskofu 2,650 kati ya karibu Maaskofu 4,200 ulimwenguni. Amekutana na karibu kila mmoja wao hasa wanapokuwa na hija ya kichungaji "ad limina Apostolorum."

Ameandika nyaraka 13 ya mwisho ni ile iliyochapwa Jumatano wiki hii Oktoba 15, 1998; barua nyingi za kitume na ujumbe mwingi. Katika matayarisho ya Jubilee Kuu 2000, Papa Yphane Paulo wa Pili ameandika waraka "Tertio Millennio Adveniente," Novemba 10, 1994 na ukachapwa siku nne baadaye. Pia ameunda kamati ya Jubilee Kuu 2000.

Papa huyu mwenye miaka 78 am,eongoza Sinodi za Maaskofu 12: tano zikiwa za kawaida (1980, 1983, 1987, 1990, 1995), moja ya dharura (1985) na sita Sinodi maalum (1980, 1991, 1994, 1995, 1997, 1998).

Sinodi zingine tatu ziko kwenye mpango wake Oceania Novemba 22 - Desemba 12, 1998; na mbili za Ulaya 1999.

Katika miaka hiyo amekuwa na ziara za kichungaji 84 nje ya Italia, wa karibuni ukiwa ule Oktoba 2-4 huko Croatia ambapo alimtangaza mwenye heri Kardinali Alojzije Stepinac. Amekuwa na ziara 134 nchini Italia na karibu ziara 700 katika mji na Jimbo la Roma ikiwa ni pamoja na ziara 274 katika parokia 325 za Jimbo lake pamoja taasisi za kidini, vyuo vikuu, seminari, hospitali, nyumba za wazee, magereza na shule.

Mwaka huu amefanya ziara nne za kichungaji nje ya Roma: Cuba Januari 21-26; Nigeria Machi 21-23; Austria Juni 19-21 na Croatia Oktoba 2-4.

Pamoja na ziara zake 218 za nje na ndani ya Italia Papa Yohane Paulo amefikia kilomita 1,118,130 sawa na maili 670,878 ambayo ni zaidi ya mara 27 ya mzunguko wa dunia au mara 2.8 ya umbali kati ya dunia na mwezi. Ametoa hotuba 3,078 katika siku 720 ambapo amesafiri asilimia 9 ya upapa wake.

Akiwa Roma Papa amekuwa akikaribisha wastani wa watu milioni moja ikiwa ni pamoja na kati ya 400 - 500,000 waliokuwa wakihudhuria mazungumzo yake ya kila wiki pia alipokea kadiri ya watu 150-180,000 ya watu kila mwaka kutoka vikundi maalum, wakuu wa nchi na serikali..

Katika kipindi chake, uhusiano wa kidiplomasia kwa ngazi ya apostolic nunciature na ubalozi ulianzishwa kwa mara ya kwanza nchi 64 zilirejesha uhusiano na Vatican. Vatican sasa ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 170.

Katika miaka 20 iliyopita amewatangaza watakatifu 798 katika maadhimisho 109 na amewatangaza wenye heri 280 kwenye maadhimisho 35 ikiwa ni pamoja la hivi karibuni la kutangazwa mwenye heri Teresa Benedict wa Msalaba (Edith Stein).

Karol Jozef Wojtyla, akijulikana hivi sasa kama Yohane Paulo II tangu achaguliwe miaka 20 iliyopita alizaliwa huko Wadowice, mji mdogo uliopo kilomita 50 kutoka Cracow, Mei 18, 1920. Alikuwa ni mtoto wa pili kati ya watoto wawili wa Karol Wojtyla na Emilia Kaczorowska. Mama yake alifariki alipokuwa akijifungua mtoto wa tatu mwaka 1929. Kaka yake mkubwa Edmund, Daktari alifariki mwaka 1932 na Baba yake aliyekuwa afisa wa jeshi alifariki mwaka 1941.

Alipokea komunyo ya kwanza akiwa na umri wa miaka 9 na aliimarishwa alipokuwa na umri wa miaka 17. Wakati wa kufuzu masomo yake kwenye shule Martin Wadowita high school huko Wadowice, alienda kwenye chuo kikuu cha Cracow's Jagiellonian mwaka 1938 na pia alikuwa kwenye kikundi cha kuigiza.

 

WAWATA yapata viongozi wapya

Na Fr Anthony Chilumba

MKUTANO mkuu wa 26 wa wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) uliokuwa ukifanyika katika kituo cha mafunzo ya kiroho Mbagala jijini kuanzia Oktoba 12 hadi 14 umemalizika kwa kuwachagua viongozi wa Taifa watakaoongoza umoja huo kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Kwenye uchaguzi huo viongozi wote walioongoza umoja huo tangu mwaka 1995 walichaguliwa tena isipokuwa mwenyekiti mama Sarah Kessy.

Mama Oliver Luana wa Dar es Salaam amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa wakati mama Josepha Michese wa Rukwa alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti.

Nafasi ya katibu mkuu ilichukuliwa na mama Betty Mweluhi wa Dar es salaam wakati mama Domina Fungo wa iringa alichaguliwa amerudia kiti chake cha ukatibi msaidizi.

Zoezi la uchaguzi lilihitimishwa kwa kumchagua mama Elizabeth Imisa kuwa mweka hazina

.Akiongea mara baada ya uchaguzi huo msimamizi mkuu wa uchaguzi huo Mhashamu Askofu Magnus Mwalunyungu wa jimbo Katoliki la Tunduma Masazi aliwapongeza viongozi hao kwa kuchaguliwa kushika nafasi za uongozi katika umoja huo.

Askofu Mwalunyungu alisema aliwataka viongozi hao kuubeba umoja huo mabegani badala ya kuuburuza .

Shirika la Misaada la KFS la Austria kwa kushirikiana na Vijana katoliki katika nchi hiyo Serikali ya Austria na Jumuhiya ya Uchumi wa Ulaya wametoa vifaa vya ofisi vyenye thamani ya shilingi milioni 9.5 kwa Umoja wa Wanawake Katoliki Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu.

Hato yalisemwa na mwenyekiti wa WAWATA Taifa Mama Olie Luena wakati wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya umoja huo katika kipindi cha miaka mitatu kwenye mkutano wa uchaguzi wa WAWATA uliofanyika Mbagala Setural Centre.

Aidha zimetolewa habari kuwa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) wanategemea kukusanya jumla ya shilingi milioni 139,034,000 katika kipindi cha mwaka ujao kutokana na vyanzo mbalimbali vya fedha vya umoja huo.

Akitoa taarifa ya mapato na matumizi ya umoja huo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita mtunza hazina wa jumuiya hiyo ya Kanisa mama Elizabeth Twisa alisema baadhi ya mapato yatatokana na riba za mikopo na Benki pango la nyumba , marejesho ya mikopo pamoja na misaada ya wafadhili.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo umoja huo umepanga kutumia shingi milioni 128,564,860 katika shughuli za uendeshashaji mafunzo , malipo ya ada za benki pamoja na ukaguzi wa mahesabu.