Make your own free website on Tripod.com

HEADLINES

Askofu Butibubage afariki

Washangaa Balozi wa Papa kujua Kiswahili

Tuungame tuishi na kuitetea imani -Askofu Mtega

Jiji yafunga Kumbi tano za starehe

Utii uwe wa majadiliano - Askofu

 

Askofu Butibubage afariki

Askofu mstaafu wa Mwanza, Mhashamu Renatus Butibubage aliaga dunia jana jioni kwenye hospitali ya rufaa ya Bugando mjini Mwanza.

Askofu Butibubage alizaliwa mkoani Mwanza Aprili 3, 1918. Alipata daraja la upadre Agosti 22, 1948.

Aliteuliwa kuwa Askofu msaidizi (Auxiliary Bishop) wa Mwanza na kuweka wakfu Mei 8, 1960. Baadaye alimrithi Askofu Joseph Blomjous na kusimikwa Askofu wa Mwanza Mei 1, 1966.

Askofu Butibubage alistaafu Novemba 18, 1987 kutokana na hali mbaya ya kiafya.

Hali yake kiafya imeendelea kuwa mbaya hadi alipoaga dunia jana jioni.

Askofu Butibubage amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Kwa miaka sita alikuwa Mwenyekiti wa Idara ya Caritas.

Askofu Butibubage anatarajiwa kuzikwa Oktoba 8, 1998 kwenye Kanisa la Seminari ya Mt. Maria, Nyegezi.

 

Washangaa Balozi wa Papa kujua Kiswahili

Na Mwandishi Wetu, Muheza

BAADHI ya watu waliojitokeza barabara kuu ya kwenda Tanga eneo la Muheza kumpokea Balozi wa Vatican Nchini,Askofu Mkuu Franscisco Javier Lozano wakati akielekea kwenye sherehe za miaka 100 ya Ukatoliki mkoani humo

walimshangaa wapokuwa wakimsikia akiwabariki kwa Kiswahili.

Mwandishi wetu ambaye alikuwa kwenye msafara huo uliokuwa na jumla ya magari yapatayo 20 yaliyompokea eneo la Manga , mpaka wa mikoa ya Pwani na Tanga aliwasikia baadhi ya watu waliokuwa wakishuhudia jinsi Balozi huyo huyo alivyoshuka kwenye gari na kuwabariki akiongea Kiswahili.

"Kumbe anajua Kiswahili", waliulizana na kuonyesha tabasamu baada ya kusimama Muheza saa 9.05 jioni kuwasalimia na kuwabariki Wakatoliki waliokuwa barabarani kumpokea.

Hali hiyo pia ilianza kujitokeza eneo la Kabuku Handeni ambapo pia alisimama kuwabariki kwa Kiswahili.

Balozi huyo ambaye alikuwa anakwenda kwenye sherehe hizo akiwa na mwenyeji wake Askofu Anthony Banzi wa Jimbo hilo , alisimama vituo kadhaa kadi alipofika Tanga Mjini baada ya kusimama katika maeneo kama Hale , Korogwe, Mkanyageni ,Pongwe na Kange .

Katika maadhimisho hayo ya jubilei ya miaka 100 ya Ukatoliki Jimboni Tanga iliyofanyika Jumamosi na JumapiliSeptemba 27 mwaka huu , Balozi aliweza kutumia Kiswahili isipokuwa katika kutoa hotuba yake ndipo alipolazimika kuwa na mkalimani kazi iliyofanywa na Katibu Mkuu wa TEC Padri Method Kilaini.

Balozi wa huyo wa Papa nchini alisema mjini Tanga katika hutuba yake kuwa Mapadri ni mkono wa kulia na kushoto wa Askofu katika kujenga kanisa

Aidha Askofu Mkuu Francisco Javier Lozzano aliwataka kueneza Uinjilishaji hadi Tanga Vijijini.

Akiongea wakati wa Ibada ya Jumapili , Balozi huyo alisema kwamba kazi zinazoweza kufanywa na mikono yote miwili ya mapadri hao ndio iliyosaidia kulijenga jimbo hilo hadi likafikisha umri huo mkubwa.

"Askofu anahitaji hawa Mapadri waliozunguka hii Altare, waumini msaidie kuleta vijana hawa katika kutumikia Jimbo la Tanga", alieleza Balozi na kusisitiza tena kwa waumini kwamba njia pekee ya kuendesha na kuamsha wito huo wa upadri ni sala. Kwa kuwa kuna Masista wengi ambao ni moja ya tunu waliyonayo Wakatoliki wa Tanga, katika kusaidia kueneza Ukristo kwenye jimbo hilo.

Alisema kwamba miaka yote 100 ni historia tosha na kueleza kwamba ndio maana Baba Mtakatifu, Papa Yohanne Paul wa pili katika sherehe hizo amemtumia salamu Maaskofu, Mapadri, Walei na waumini kwa maadhimisho hayo hasa Maaskofu waliokuwepo.

Maakofu waliokuwepo katika sherehe hiz ni Askofu Mkuu Norbert Mtega wa songea,Askofu Telesphor Mkude wa Morogoro ,Askofu Evarist Chegula wa Mbeya,Askofu Agapiti Ndorobo wa Mahenge,Askfu Josephat Lebulu wa Same, Askofu Gabriel Mmole wa Mtwara na Askofu Augustino Shayo wa Zanzibar.

"Kama Askofu Banzi alivyosema ,mimi siko hapa kama binafsi bali kwa uwakilishi waPapa hapa Tanzania kama alivyokuja mwaka 1990".Alisema.

Alieleza kwamba ujio waPapa mwaka huo , ulikuwa wa kuimarisha imani ya kwamba wote ni kanisa moja la Katoliki duniani."Nilipomjulisha , alisisitiza kuwasisitizia upendo na baraka zake za Upapa na Kibaba".Alisema na kushangiliwa kwa vigelegele.

Alisema kwamba baraka hiyo ya papa ni kwa wavulana kwa wasichana watakaopokea Sakramenti ya Kipaimara Jumapili hiyo ya sherehe, ambayo ni ya ukomavu kwamba wao sasa watakuwa shahidi na kutoa ushuhuda popote pale watakapokuwa.

Tuungame tuishi na kuitetea imani -Askofu Mtega

Na Mwandishi Wetu, Tanga

 

ASKOFU Mkuu Norbert Mtega wa Jimbo Kuu la Songea amesema ni wajibu wa kila Mkristo kuungama na kuishi kwa kuitetea imani yake kwa kumsifu Mungu, badala ya kuendekeza imani zinazowapotosha.

Akihubiri wakati wa masifu ya jioni Jumamosi Septemba 26 mwaka huu kwenye Kanisa Kuu la Katoliki la Tanga ,wakati wa Jubilei ya miaka 100 ya jimbo hilo, Askofu Mtega alisema kwamba kutimiza miaka yote hiyo ni ishara tosha kwamba imani inatoka katika damu yao.

"Leo imani hii imetoka katika damu yetu sisi weusi , itapaliliwa na kuendelezwa na sisi weusi hadi kufikia miaka 100", alisema na kuuliza kwamba katika miaka hiyo wapo Wazungu wangapi? Alihesabu Kanisani na kuonekana yupo Padri mmoja na masista wawili.

"Nyie walei , nani kati yenu haendi kwa waganga wa kienyeji kutafuta mizizi na dawa ya michuzi?" Aliuliza Askofu Mkuu Mtega na kuuliza kama kuna Mlei ambaye hadi sasa bado hajachanjwa chale wala watoto wake kuvalishwa hirizi.

Wakati akianza mahubiri hayo, yaliyokuwa mwanzo wa kuadhimisha miaka 100 ya Ukatoliki Tanga, baada ya kuwasili kwa balozi ya Vatican nchini kwenye Kanisa hilo la Tanga, Mtega alisema kwamba watu wa mji huo kama wangekuwa ni Wakatoliki wanaotembea na imani za waganga kwamba wamerogwa, wasingefikia hapo. Maneno ambayo yaliwafanya waumini kuangua kicheko kwa furaha.

"Mimi damu yangu ya Kingoni ina mchanganyiko na Upagani, "alisema Mtega kwa kusisitiza, "pamoja na majoho yangu haya ya Uaskofu "huku akiyashika. Alieleza kwamba kutimiza miaka 100, ni zawadi ya kwamba waliwapatia imani katika Yesu Kristo katika miaka yote hiyo. Kutokana na kuwepo kwa mahudhurio mazuri ya Maaskofu, Mapadri, Masista, Maketekista na waumini kwa ujumla.

Askofu huyo alieleza kwamba, ripoti za miaka 100 ni matunda ya imani hiyo kwamba inaendelea kuzaa matunda zaidi kwa wale wasiokuwa wadini yao.

"Watu wa zamani walijaribu kutafuta tambiko la kweli, wasilipate," alieleza na kugusia masuala ya kufuata imani ya ushirikina kwamba wamerogwa."Walijaribu kupapasapasa , labda kwenye makaburi ya mababu zetu - hawakupata ...ni hii yetu ya baba, mwana na roho Mtakatifu. Hata ukitoa mkia wa Kondoo, bado imani ya Yesu Kristo ndio pekee inayotuongoza.

"Alisisitiza Askofu huyo alisema kwamba ni vema kuungama na kuishi kwa kuitetea imani hiyo, ili kueneza neno la Bwana kwa kuwa ndio mafanikio ya kutimiza miaka 100 kwa jimbo hilo la Tanga.

 

 

Utii uwe wa majadiliano - Askofu

Na Mwandishi Wetu

 

IMEPENDEKEZWA kuwa ili Kanisa libakie kuwa la Kimisionari ni lazima lirudi katika mizizi yake kwa kuonyesha imani ya kweli kwa Kristu.

Pendekezo hilo lilitolewa na Askofu Augustino Shao wa Jimbo Katoliki la Zanzibar wakati akitoa mada kwenye semina ya utume wa kimisionari iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania jijini juzi.

Alisema kanisa lazima liwe na mtiririko wa mara kwa mara wa kuchanganua na kufafanua mabadiliko ya nyakati na kufahamu mitindo inayohitaji kuinjilishwa.

Askofu Shao katika mada yake hiyo aliwaambia washiriki kuwa Kanisa la sasa linapaswa kuwa tayari kwa majadiliano na kuondoa hali ya utii kipofu.

"Wakati wa kwamba; mama mkuu amesema au baba mkuu amesema umekwisha. Utii uwe wa majadiliano," alisema Askofu Shao.

Alihoji hali ya kanisa la Tanzania kuwa la kimisionari kutokana na mapadri wa jimbo kutokukubali kufaidi karama na mila za mahali pengine nje ya majimbo yao.

Aliongeza kusema kuwa mapadre wengine hawako tayari kuwaona wamisionari katika majimbo yao na wanawaona wamisionari kama waanzilishi tu halafu wanapaswa kuwaachia shughuli baada ya kukamilisha uanzishaji.

Alisema dhana hiyo ni potofu kwani kila mmoja anapaswa kushiriki katika umisionari

Aidha alisema kuwa malezi ya wamisionari yanapaswa kuwa na mabadiliko makali ili yaendane na mahitaji ya ulimwengu.

"Malezi haya lazima kwanza yawakomboe wao, yawaimarishe, yawatie moyo na kuwawezesha kuwa wabinufu, washindani pamoja na kuwa makini kwa mambo yanayogusa jumuiya," alisema Askofu Shao.

Akizungumza suala la kuwakomboa wanawake, Askofu Shao alisema suala hilo haliwezi kufanikiwa bila kuwashirikisha wanaume.

"Ondoa kwanza dhamira mbovu ya wanaume juu ya nafasi ya mwanamke ndipo udai haki za wanawake.

Semina hiyo inayohudhuriwa na wajumbe kutoka karibu majimbo yote ya Tanzania ni matayrisho kwa dhamira ya mwaka 1999 Kanisa, familia ya kimisionari ikiwa ni matayarisho kuelekea jubilee kuu ya mwaka 2000.