Make your own free website on Tripod.com

NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule...

Shughuli za biashara zataka utafiti wa kina

WATANZANIA wengi siku hizi wanajishughulisha sana na mambo ya biashara za vitu mbalimbali. Wako wafanyabiashara ya maduka vya nguo za kutoka viwandani moja kwa moja na zile tunazoziita nguo za mitumba ambazo zimeshatumiaka huko ng’ambo; wako wafanyabiashara wanaojishughulisha hasa na vitu mbalimbali kama vile vyombo vya nyumbani; kuna wafanya biashara ambao shughuli yao ni kuuza labda vipodozi na vitu vingine kama vile sabuni, marashi nk. Hivyo kuna maduka mengi yenye kuuza vitu mbalimbali vya ujenzi, au vitu vyenye kuhusika na secta za ufundi, vyombo na pembejeo za kilimo nk.

Nao akina mama hawako nyuma katika suala hili la biashara hasa ile ya vyakula. Tunao akina mama wanaojulikana kama "mama ntilie". Hao hujishughulisha na biashara ya vyakula vilivyopikwa. Huandaa vyakula hivyo sehemu zile ambako kuna wateja wao kama vile pale ambapo kunafanyika shughuli za ujenzi , pengine karibu na viwanda na hata kwenye maofisi, na mahali pengine ilimradi tu kuna wateja.

Kuna biashara nyingine ambazo zinahusika na vinywaji, na hivyo kuna mahoteli mengi na mabaa mengi sana yanayojishughulisha na uuzaji wa vinywaji vikali na baridi. Inavyoonekana shughuli au biashara ya kuuza pombe na viywaji baridi imeshamiri sana katika nchi yetu. Biashara hiyo inatawala sana katika miji na hata huko vijijini. Hapa na pale siku hizi mtu hawezi kukosa vinywaji baridi kama vile soda za kila aina na pia bia hupatikana karibu katika kila kona ya nchi yetu. Wahusika na wasambazaji wanafanya jitihada kubwa sana kuwafikia wateja wao kila mahali panapowezekana licha ya ugumu pengine wa usafirishaji wa hizo bidhaa. Hata hivyo tunapenda kusifu juhudi za hao ndugu wenye kusambaza biashara mbalimbali hadi kule vijiji kwenye matatizo makubwa ya barabara zetu.

Ni kweli kuwa shughuli ya biashara kwa wengine huonekana kuwa ni rahisi na yenye faida ya haraka. Lakini kwa kadiri mambo yalivyo inaonekana kuwa siku ya leo shughuli hiyo ya biashara inazidi kuwa ngumu sana. Kwanza kabisa ni kwa sababu wengi hujiingiza katika shughuli hizo za biashara bila kufanya utafiti wa kina. Shughuli yo yote ile na hasa ya biashara inatakiwa ifanyiwe utafiti wa kina kabisa kabla ya kuianza. Katika kufanya huo utafiti, kuna maswali mengi ya kujiuliza. Kwa mfano swali la kwanza, ni je, unataka kufanya biashara ya aina gani? Swali la pili, je, biashara hiyo unataka kuifanyia wapi? Je, mahali hapo unapotaka kufanyia kuna mazingira mazuri ya biashara kweli? Una uhakika gani wa kupata wateja hapo ambapo umekusudia kufanyia biashara?

Licha ya maswali hayo na mengineyo ni lazima pia kufahamu kama utawezaje kuushinda ushindani, kwani inasemakana kuwa "biashara ni ushindaji". Hapo lazima kukiri kuwa siyo kila mmoja ana kipaji cha biashara au ile tabia ya kuwavutia watu kibiashara. Mara kwa mara tunaona jinsi wafanya biashara wengi wanavyopanda na kushuka kutokana na uendeshaji mbaya wa hizo biashara zao. Pengine hutokana hasa na kauli mbaya kwa wateja,na pengine ni kutokana na mahali ambapo biashara hiyo ipo. Ni jambo la kushangaza sana kuona jinsi wafanyabiashara wanavyojikusanya pamoja na hivyo kuvutania wateja. Jambo linalotakiwa hasa siyo kuvutana kwa nguvu bali lazima kuwa na kile kinachoitwa kivutio cha biashara, yaani mazingira yote yenye kupelekea wateja waikimbilie biashara hiyo kwa sababu inawavutia na pia iko katika mazingira ya kuvutia.

Ni jambo la kusikitisha sana tunapoona wafanya biashara wanafukuzwa hapa na pale kwa sababu wameweka biashara zao mahali ambapo si halali. Tunapenda sana kusikitika na hao wafanyabiashara kwa usumbufu huo wanaoupata. Yawezekana kuwa pengine ni kwa sababu ya makosa yao ya kutofanya utafiti sawasawa hasa wa mahali hapo wanapotaka kufanyia biashara hizo.Tunashuhudia jinsi vibanda vingi vya biashara vinavyobomolewa na Tume ya Jiji au Halmashauri za Miji.Hapo tunajiuliza ni kwa nini mtu alikubali kuanza shughuli ya biashara mahali ambapo si halali, kwa mfano kuweka gocery ya pombe karibu na barabara kuu. Labda hapo mambo yaliangaliwa kwa upande mmoja tu wa kuwapata wateja, na kule jambo la usalama wa wateja halikuangaliwa. Pengine kumekuwa na mazingira ambayo yanahatarisha usalama wa afya za wateja na majirani. Hayo tunasema ni mambo makubwa ambayo yalitakiwa kuangaliwa.

Pia inawezekana kuwa kukawa na makosa kwa hao wenye kutoa liseni au viwanja vya kufanyia biashara. Kuna watu ambao wameruhusiwa kufanya biashara mahali ambapo si halali kufanyia hizo biashara. Hutokea kwamba wakati biashara hiyo imeshamiri biashara, hapo mkono wa sheria unapita na hivyo kurudisha nyuma hiyo biashara. Hapo hutokea kilio na malalamiko mengi sana. Lawama nyingi huwaendea hao ambao walitoa hizo liseni za biashara na viwanja. Mambo hayo huweza kutokea kwa sababu ya urafiki, udugu au hata au kwa sababu ya watu wengine kutoa chochote ili kuweza kupata liseni ya biashara mahali fulani wanapotaka licha ya sehemu hiyo kutokuwa halali kwa kufanyia biashara.

Tumesema kuwa biashara ni shughuli yenye ushindaji hasa siku hizi.

Mtu aliyeamua kufanya biashara hana budi kufanya kila jitihada ya kuushinda ushindani kwa namna fulani. Kuna ule msemo usemao kuwa mteja ni mfalme, na ni kweli kwa upande fulani na hasa kwa siku ya leo. Kila mwenye biashara anapaswa kutambua jambo hilo kwani vitu vya biashara ni vingi na wafanya biashara nao ni wengi. Tunapenda kuwapongeza wale wenye biashara za usafiri wa magari ya abiria.

Hao tunaona kuwa wanatambua kweli kuwa mteja ni mfalme kwa jinsi wanavyombeleleza na kumvutavuta (ingawaje pengine huleta pia usumbufu) kwa mteja. Tunahitaji sana lugha tamu kutoka kwa kila mfanyabiashara siku ya leo. Angalia ni kwa jinsi gani wale wanywaji wa pombe wanavyomiminika katika baa fulani na wakaacha kwenda kwenye baa nyingine iliyo karibu yake. Tunasema kuna vivutio kadhaa vyenye kuwavutia hao wanywaji au wateja.

Tunapenda kumalizia Hoja yetu kwa kushauri kwamba wale ambao wameamuwa kufanya shughuli ya biashara wanapaswa kuifanya kwa uhakika wakiwa wamefanya utafiti yakinifu wa hiyo biashara. Biashara za ubabaishaji hazifai kwa siku ya leo tunapokuwa na ushindani mkubwa wa shughuli hizo. Kwa hiyo hao ndugu wafanya biashara wanapaswa kuzifanya kikweli kweli ili kuendana na huo ushindani wakitaka kweli kuleta mafanikio katika biashara zao. Pia tunapenda kuwashauri hao wafanya biashara kwamba inawapasa mara kwa mara kuomba ushauri na hata kujifunza kwa wale ambao wamebobea katika shughuli hizo za biashara.

Tunatambua kuwa kila shughuli ina ugumu wake, lakini katika kutafuta misaada mambo huweza kuwa rahisi zaidi na yenye manufaa zaidi.