NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule...

Tuelimishane na tusadikishane katika maisha yetu

TAIFA letu kwa sasa hivi linakabiliwa na matatizo mengi sana. Kwa kuyataja baadhi ya hayo matatizo ni kama vile magonjwa na hasa ule ugonjwa wa ukimwi, tatatizo sugu la ajali za barabarani, shida ya ombaomba, ukosefu wa ajira nk.

Serikali na hata mashika ya dini na ya watu binafsi hufanya kila jitihada ili kuweza kukabiliana na matatizo hayo.

Kwa mfano kuhusu ugonjwa wa ukimwi kumekuwa na mbinu nyingi ambazo zimependekezwa kama vile watu kubadilisha mienendo yao na njia nyingine kadhaa.

Na hivi karibuni tena kumekuwa na jitihada ya kuwapeleka watu kule Uganda ili wakajifunze mbinu mbalimbali za kupambana na gonjwa hilo. Hatujui kwa uhakika kama kweli mbinu hizo zitafanikiwa .

Kuhusu tatizo la ombaomba kumekuwa pia na jitihda ya au kuwaondoa kwa nguvu hao wenzetu wenye kutegemea maisha ya kuombaomba na kujaribu kuwarudisha makwao.

Pia serikali iliwatuma watu waende kule Zambia wakajifunze jinsi ya kuwasaidia hao ombaomba.

Hata hivyo bado tuna mashaka kama kweli mbinu watakazotumia zitafanya kazi kikamilifu kabisa na kuleta suluhisho katika tatizo hilo.

Pia tunalo lile tatizo la ajira katika taifa letu.

Kuna vijana wengi ambao hawana ajira na hivyo wanazubaa zubaa tu mitaani bila kazi. Kumekuwa na mawazo au mapendekezo mbalimbali kuhusu tatizo hilo.

Wengi wanasema suluhisho lake ni kuwaambia vijana wajitahidi kujiajiri wenyewe katika fani mbalimbali.

Hata hivyo kumekuwa na shida hapa na pale hasa mijini.

Vijana wanazidi kumiminika mijini kutafuta kazi huku na kule.

Kwa kifupi tunaweza kusema kwamba suluhu mbalimbali za matatizo yetu ya kijamii huzidi kukwama na hivyo tunaendelea kuwa katika hali ngumu.

Katika Nguvu Yetu ya Hoja tungependa kutoa pia pendekezo kuhusu matatizo yetu na jinsi ya kuyatatua.

Sisi tunaona kuwa njia pekee na ya kwanza ni kuwaelimisha watu kuhusu matatizo hayo.

Baada ya kuwaelimisha, jambo linalofuta ni kuwasadikisha wahusika katika hatua zile zinazochukuliwa. Kwa mfano kuhusu tatizo la ugonjwa wa ukimwi, ni kama alivyosema Waziri Mkuu, Mheshimiwa Frederick Sumaye, mara baada ya kurudi kutoka kule Uganda.

Waziri Mkuu alisema kuwa jambo linalotakiwa ni kuambiana ukweli juu ya ugonjwa huo. Alisema kwamba hakuna sababu ya kuwaficha watu kuhusu ukweli kama mtu fulani amekufa kutokana na ugonjwa wa ukimwi.

Hapo haina maana ya kuwaogopesha watu, la hasha, bali ni kutoa ukweli kuhusu jambo hilo.

Ni lazima kabisa mtu aelewe na asadikishwe kuhusu hasara na ubaya wa ugonjwa huo.

Kwa hiyo tunasema kuwa jambo la msingi ni kuwapa wahusika usadikifu mkamilifu.

Kwa maneno mengine tunapaswa kujenga ndani ya akili za watu kuhusu ile hali mbaya iliyoko katika jamii au ndani ya mtu, na jambo la pili ni kumsadikisha kuwa ni lazima afuate njia hizo zilizopendekezwa au zilizotolewa ili kuondokana na tatizo hilo gumu.

Kazi kubwa inayotakiwa ifanyike ni kuelimisha na kusadikisha (to educate and to convince).

Kwa kuwa wengi wa wahusika na tatizo fulani hawana usadikifu (conviction), basi mambo yanaendelea kuwa mabaya siku hata siku.

Ni lazima kumwelisha yule mwananchi kuhusu ugonjwa wa ukimwi, na hivyo kumsadikisha kuwa asipofuata masharti na kanuni za maadili atapoteza maisha yake. Kwa hiyo ni lazima kabisa awe na usadikifu (conviction) kuhusu madhara ya ugonjwa wa ukimwi, na vile vile awe na usadikifu (conviction) kuhusu mbinu hizo za kujikinga na ugonjwa huo. Kwa yule ndugu yetu anayetegemea kuombaomba inatakiwa kumwelimisha kuhusu aibu au hasara ya kuombaomba kama binadamu.

Pia inatakiwa kabisa kumhakikishia kuhusu athari za kuombaomba kama binadamu ambaye ni mzima na anao uwezo wa kujitegemea.

Licha ya hayo inatakiwa kumsadisha kuwa kufanya kazi na kujipatia mahitaji kwa njia hiyo ya kufanya kazi ni uungwana zaidi kuliko kuombaomba mitaani.

Na hivyo pia kwa wale vijana ambao hawataki kujiari wenyewe, yaani kujipatia riziki yao kwa njia ya kufanya kazi za kujitegemea.

Hao ni lazima pia waelimishwe kwa undani kabisa, na pia wasadikishwe kuwa kuna kazi nyingi sana za kufanya na zenye kumletea riziki na kipato kila mmoja mwenye kuweka bidii katika kazi iwayo yote ile.

Hapo inafaa kabisa kuzungumza na mtu mmoja mmoja kuhusu tatizo hilo la ajira.

Tena inafaa kuwasadikisha vijana hao kwa kutoa mifano halisi inayowazunguka, kwani kuna watu wengi, hasa vijana ambao wanajitegemea na maisha yao yanazidi kuwa bora kutokana na jitihada wanazozifanya yafaa sana.

Kuwasadikisha kuhusu ubaya unaotokana na ile hali ya kutoweza kujitegemea na kufanya kazi, kwa kujituma.

Mambo mengi sana katika maisha ya binadamu huweza kufanyika hasa kutokana na ile hali ya kujituma mtu binafsi na siyo kwa kulazimishwa kwa nguvu. Na mtu hujituma pale ambapo ana usadikifu na kitu hicho. Bila kuwa na usadikifu (conviction) katika jambo liwalo lote lile si rahisi kwanza kulifanya, na zaidi ni vigumu sana kuweza kuleta mapato yanayotarajiwa.

Kwa hiyo sisi tunaona kuwa tukitaka kweli kufanikiwa katika miradi na mipango yetu mbalimbali kwanza lazima tuwaelimishe wahusika, na baada ya kuwaelimisha ni sharti tuwasadikishe kuhusu hali ilivyo kwa sasa hivi, na pia kuhusu ile hali njema ambayo itaweza kupatikana baada ya jitihada hizo zilizosadikishwa.

Tunapenda kusema kuwa katika kutekeleza mambo hayo inafaa kabisa kwenda pole pole. Binadamu huhitaji muda ili kuweza kuacha mazoea yake, au kuweza kulichuchumia jambo ambalo ni jipya, na hasa lile ambalo hudai utendaji. Kwa hiyo tunapenda kuwasihi wahusika wa kubadilisha mienendo ya jamii, sharti wawe na subira pamoja na uvumilivu katika kuwaelimisha waathiriwa. Yafaa kabisa kuwa na muda wa kuweza kukutana na waathiriwa ana kwa ana. Tunasema hakuna kisichowezekana kubadilika, lakini lazima kwenda pole pole pamoja na ule upendo kwa hao wenye shida.

Tukiwaelimisha kwa upendo na huruma, tunatumaini kwamba kutakuwa na mafanikio, lakini tukitumia nguvu hapo kuna mashaka kama kweli tutalifikia lengo hilo tunalotarajia.