NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule...

Kazi sharti ziende na wito

NAKUMBUKA sana wakati viongozi wetu hapa awali walipotaka kutuhamasisha kuhusu ujenzi wa taifa letu na maendeleo kwa ujumla walisema kwamba taifa litajengwa na wenye moyo. Maneno hayo naona yana maana kubwa sana hadi hivi leo, na labda zaidi kuliko wakati ule.mwanzoni.

Katika taifa letu siku ya leo kuna watenda kazi wengi sana katika maofisi, katika viwanda na katika taasisi mbalimbali. Kuna ya umma na wengine hufanya kazi katika sekta za watu binafsi. Tunapoangalia na kulinganisha kati ya utendaji ule ulioko katika sekta za watu binafsi na zile za umma tunaona kwamba kuna tafauti kubwa sana ya ufanisi katika huo utendaji. Ufanisi huo hutokana hasa na utendaji ambao hutokana hasa na moyo.

Tunaposema kuwa utendaji hutokana na moyo ni kwamba mtu anafanya kazi yake kutokana na wito alio nao katika kazi hiyo. Kwa hiyo jambo kubwa sana tunalohitaji katika kufanya kazi kwa ufanisi ni kwamba inatupasa tufanye kazi zile ambazo tuna wito nazo.

Kuna watu wengi ambao wanafanya kazi siyo hasa kutokana na wito wao, bali kwa sababu tu wameajiriwa katika kufanya kazi hizo. Mtu yule ambaye hufanya kazi kwa sababu tu ameajiriwa kufanya kazi hiyo, bila kuwa na wito wa kazi hiyo mara nyingi ufanisi wake unakuwa ni mdogo sana.

Hutokea pia licha ya kutoleta mafanikio sawa sawa, mara nyingi kwamba watu wa namna hiyo hufanya kazi kwa wasiwasi na pamoja na manung’uniko. Kumekuwa na uzembe pamoja na uduni wa kazi katika sekta mbalimbali za huduma zetu. Hutokea kwamba mtu hana wito labda wa kazi ya uganga.

Kwa kuwa hakuna shughuli nyingine, basi huchukua mafunzo ya uganga na kuifanya kazi hiyo kwa shingo upande. Kitakachojitokeza katika utendaji wake ni kwamba huyo jamaa ataifanya kazi hiyo bila moyo wa kujituma.

Watu wenye kufanya kazi bila kuwa na moyo wa kazi, hasa kwa waganga hutenda kazi hizo pengine bila upendo na huruma. Mambo hayo tunayashuhudia sana siku hizi katika hospitali zetu nyingi na kwenye maofisi mbalimbali.

Wako wafanyakazi ambao wanadai kwanza rushwa au chochote kabla ya kutoa huduma wanazotakiwa kuzitoa kutokana na wajibu wao. Lakini hawafanyi hivyo kwa sababu ya kukosa moyo wa kazi au wito katika kazi hiyo. Tunavyojua ni kwamba mtu mwenye kufanya kazi kutokana na wito wake, haangalii muda, wala malipo, bali anachotaka ni ile faraja kwamba ameweza kumhudumia mwananchi mwenzake katika shida yake.

Hali hiyo inazidi kuwa ngumu sana siku ya leo ambao kuna watu wengi wamesomeshwa katika fani zile ambazo siyo wito wao. Kuna watu wamechukua sekta ya ualimu kwa sababu tu hapakuweko kazi nyingine.

Hivyo wanafundisha kama kazi, lakini siyo walezi au wenye wito katika kazi hiyo. Mapato yake ni kwamba hao walimu wanakuwa tayari kufanya shughuli nyingine zenye kipato kwa bidii zaidi kuliko hiyo ya ualimu.

Mambo huzidi kuwa magumu na mazito hasa pale ambapo hudaiwa kuwa walezi katika mashule yetu. Kazi hiyo inadai sana wito na moyo wa utendaji.

Tunalalamika sana kuhusu utendaji katika maofisi yetu siku ya leo. Watendaji wengi sana wanafanya kazi bila kuwa na moyo wa kujituma au kufanya kazi kwa kuipenda kazi hiyo.

Hivyo watu hao wenye kufanya kazi kutokana na moyo huifanya kazi yao kwa kujituma zaidi na pia hupenda zaidi kujenga majina yao kuliko kipato.

Hivyo ndivyo walivyo wale wenzetu ambao tunaamini kwamba wameendelea katika utendaji. Kwa wengi wetu kuna shida ya kufanya kazi kutokana na moyo wa kuipenda kazi na kuwapenda wale ambao wanawahudumia.

Mtu mwenye kufanya kazi kwa moyo na kujituma huwa ana kicheko na furaha pamoja na tabasamu usoni pake.

Lakini yule ambaye hufanya kazi kwa sababu tu ni kazi basi kunakuwa na manung’uniko pamoja na kulipualipua katika utendji wake.

Mwenye kutenda kutokana na wito au upendo wake kwa wale anaowahudumia hajali sana kuhusu muda, gharama na hata uhusiano wake na huyo anayemhudumia. Mambo hayo tunayashuhudia sana kwa wahudumu wengi.

Tunapenda kutoa rai kwa wale wote ambao wanawaandaa watoto au vijana kwa maisha ya baadae kuwa inawapasa kuwashauri hao vijana wachagua kazi za baadaye kutokana na wito walio nao katika kazi.

Hivyo wazazi na walezi wanapaswa kutambua sana wito wa watoto wao na hivyo kuweza kuwaanda vilivyo kutokana na maelekeo yao.

Ni jambo baya sana kwa wazazi au walezi kuwalazimisha watoto wao wachukue kazi fulani ambayo haiendani na wito wao. Kosa hilo tunalishuhudia sana siku kwa siku kwamba kuna watu ambao wakiaajiriwa huwa hawana moyo kabisa wa utendaji na hivyo hufanya kazi kama vile washurutishwa.

Ni jambo baya kwa mtu ambaye anapenda kutembea tembea kumweka ofisini mahali ambapo anapaswa kutulia na kuwahudumia watu.

Hivyo pia kumweka mtu anayependa kuzungumza na watu mahali ambapo katika mazingira ya kazi zinazohitaji ukimya. Kwa hiyo wahusika wanapaswa kuwapatia watu kazi kulingana na hali zao.

Ni kweli kuwa kuna ukosefu mkubwa sana wa ajira katika taifa letu, lakini tena hatuweze kulipuuzia jambo la wito katika kazi tukitaka kupata huduma nzuri. Linalotakiwa walau katika zile sehemu nyeti za utendaji kama vile ugangana ualimu. Kuna kazi zile ambazo huweza zikavumilika kwa kuwa hazihusu maisha ya watu moja kwa moja kama vile za biashara.

Kuna kazi katika jamii ambao ni za urithi katika familia. Karibu katika familia nyingi hutokea kuwa baadhi ya watoto hupenda kufanya kazi zile ambazo hufanywa na baba zao. Kuna wale wafanya biashara ambao huwa na watoto wenye wito wa biashara, na wazazi wao wawaelekeza kuhusu shughuli hiyo.

Wale wazazi ambao ni wakulima au wafugaji nao hupenda kuwaelekeza watoto wao kuhusu shughuli hiyo kutokana na ule mwito walio nao hao watoto kwa shughuli hizo.

Hao watoto wanapokuwa wakubwa kutokana na maelekezo ya wazazi na walezi wao pamoja na wito au vipaji walivyo navyo tunaamini kwamba watafanya kazi hizo vizuri sana.

Hapo tunapaswa kukumbuka kuwa siyo kila mtoto anakuwa na wito wa ile kazi anayoifanya baba yake. Wako baadhi ambao wanapenda kazi za baba zao na hivyo kuweza kuzirithi, na wako wengi wana wito wa kazi nyingine na hivyo inapaswa kuandaliwa kwa kazi zile ambazo wanazieelekea. Tusiwalazimishwe vijana au watoto kuchukua zile kazi ambazo hawazipendi au sisi tunataka wazifanye kwa kuwa hakuna kazi nyingine za kuzifanya.