Make your own free website on Tripod.com

Japo tunasaidiana kama ndugu, tujitegemee

SIKU moja nilikuwa nimesoma maneno yaliyoandikwa nyuma ya gari moja yasemayo: "Mjini taabu". Lakini jambo la ajabu ni kwamba licha ya maneno hayo yaliyoandikwa kwenye gari, na pamoja na mazungumzo ya watu kila siku kuhusu maisha ya mjini, jambo tunaloshuhudia kila siku ni kwamba watu wengi wanazidi kuingia mijini. Hivyo tunajiuliza ni kwa nini basi watu hao wanafurika kuja mijini ambako maisha ni ya taabu?.

Watu wengi hasa kule vijijini wana fikra potofu kuhusu maisha ya mjini. Wengi wanafikiri kuwa huku mijini ndiko kwenye pesa sana na hivyo ni rahisi kuzipata hizo pesa na kuweza kuishi maisha mazuri na ya starehe. Lakini kumbe mambo ni kinyume kabisa. Watu wengi mijini na hasa katika miji mikubwa kama vile Dar Es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Tanga, na mingineyo, huishi katika dhiki kubwa sana. Upitapo katika mitaa ya miji hiyo hutakosa kuona watu wengi sana wakiwa hawana kazi yo yote ile bali wanakaa siku nzima wakipiga domo. Na kwa kuwa hakuna mtu ambaye anaweza kupata pesa bila kufanya kazi basi hali na maisha ya wengi hasa vijana ni mbaya sana.

Hakuna mwananchi hivi leo asiyetambua kuwa maisha ni magumu kiuchumi. Kuna vijana na hata watu wazima ambao huja mijini kwa ajili ya kutafuta kazi, ambazo ni shida kuzipta. Wanaposhindwa kupata kazi basi hapo huwa ni mzigo mkubwa sana kwa wenyeji wao.

Hivyo unaweza kuona jinsi watu wanavyojirundika katika nyumba moja wakimtegemea mtu mmoja ambaye ana kazi , lakini huwa ni vigumu sana kuwategemeza hao ndugu. Sote tunatambua kuwa maisha ya mjini, ni maisha ya pesa, na kama mtu hana kazi si rahisi kupata pesa. Kwa kuwa mtu anahitaji kuishi hutafuta kila njia ya kupata pesa.

Kwa sababu hiyo tunashuhudia mambo mengi ya ajabu huku mijini kama vile ujambazi, kuuza madawa ya kulevya, wizi wa kila aina na hata mauaji. Hayo ni baadhi tu ya mambo yanayotendeka katika miji kwa sababu watu wengi wasio na kazi wameingia mjini na hawataki kabisa kurudi kule vijijini.

Hapo maneno yale ambayo nilisema kuwa naliyasoma kwenye gari kwamba mjini taabu, huwa ni kweli kabisa. Kwa wale ambao hawajaishi mijini wana fikra kwamba maisha ya mijini ni mazuri sana, lakini wanapofika na kuishi huku mijini hushuhudia jinsi mambo yalivyo kinyume kabisa. Ni kweli kuwa mjini ni taabu na maisha ya wasiwasi kila siku. Kwa hiyo iwe ni kwa wale ambao hawana cho chote, lakini pia ni kwa wale ambapo wana chochote, nao maisha yao huwa daima katika hatari kwani hushambuliwa daima na hao ambao hawana chochote. Kwa hiyo mjini ni taabu kwa wote wanaoishi humo siku ya leo. Yule aliye na cho chote huishi maisha ya wasiwasi kwa vile huweza kushambuliwa na kunyang'anywa mali yake wakati wowote ule. Hali hiyo ya kutisha huzidi kuongezeka siku hadi siku kwani umaskini nao unazidi kuongezeka pamoja na mlolonngo wa watu kufika huku mijini kutafuta nafuu ya maisha ambayo hawaipati kwa ujumla.

Kwa upande mwingine tena hata hao vijana ambao wanafanya ujambazi huko mijini maisha yao yanakuwa katika hatari kubwa sana kwani mara kwa mara wakishikwa hutendewa vibaya sana na hata kuuawa. Hilo ni jambo la fedheha kubwa sana kwa wazazi ndugu na jamaa wa vijana hao.

Licha ya hao wenye kutumia nguvu katika kutafuta nafuu ya maisha yao, kuna kundi jingine la watu ambalo nalo lina mbinu zake katika kujitafutia mahitaji yake kwa njia ya kuombaomba. Kundi hilo nalo linaleta usumbufu mkubwa sana katika miji yetu hivi leo. Kuna watu wazima pamoja na watoto ambao husimama katika barabara za miji yetu na kuomba, hasa katika mji wa Dar Es Salaam. Maisha yao ni ya kutisha mno kwani wanalala kwenye pembe za nyumba na wanashinda kwenye makutano ya barabara ili kuomba wakitumia mbinu ya kuonekana kweli wana shida kubwa sana. Tunasema kuwa jambo hilo linasikitisha sana na hivyo linaleta kero kwa wananchi wengine.

Tunasema tena kuwa maisha hayo ni ya taabu mno. Ni jambo la fedheha kubwa sana kushuhudia watu wazima wakiwa ombaomba na kulala kila mahali. Je, hali kama hiyo itadumu hata lini katika nchi yetu?

Ni kweli kwamba hatuwezi kamwe kuwafifisha ombaomba wote katika miji yetu, lakini ingewezekana walao kuwapunguza kwa namna fulani. Lakini tena waende wapi ambapo watapata uhakika wa maisha yao?

Sote tunaliona tatizo hilo la watu kukimbilia mijini, lakini tunajiuliza tufanye nini ili kuliondoa au kupunguza tatizo hilo. Wengi wanafikiri kwamba njia ya kuboresha maisha ya kule vijijni itasaida kuwavuta hao vijana wanaotaka kukimbilia mjini wavutike na kubakia kule vijijini.

Kwa hiyo ni sherti kuwa hali nzuri ya kupatikana pesa kule vijijini na hivyo vijana au wananchi kwa ujumla waweze kujipatia mahitaji yao ya kila siku.

Pia wale wanaishi mijini wajaribu kuwaelekeza wale ndugu zao namna ya kujitegemea kule vijini. Wafike mijini na kupata misaada au ushauri, lakini wasiwaendekeze wala kuwaonea aibu katika kuwapa msimamo na mwelekeo wa maisha yao, na hivyo kuwafanya waweze kujitegemea wenyewe hapo baadaye.

Yaonekana kuwa kutokana na utamaduni pamoja na mila zetu ambazo zimepitwa na wakati, kuna wengi wetu ambao hatupendi kuwaambia ndugu zetu ukweli wa hali halisi na hivyo tunaumia na kuteseka kimyakimya.

Ni jambo ambalo linaumiza mno mtu mmoja kwa mshahara mdogo kabisa aweze kuwatunza na kuwalisha kundi kubwa sana la ndugu na jamaa.

Kwetu sisi Watanzani si jambo jipya kuambiana kuwa inatakiwa kila mmoja wetu ajitegemee au yampasa kutoa mchango katika jumuiya ili aweze kuisihi na kuendeleza hali ya maisha yake popote pale alipo.