Make your own free website on Tripod.com

NGUVU YA HOJA Na Fr. P. Haule

 Wachache tusijivunie elimu katikati ya wajinga, ni hatari

Kama kuna neno linalozungumzwa sana katika jamii yetu siku ya leo ni lile linalohusu ELIMU. Neno hilo kusema kweli ndilo linalotawala maisha yetu sisi binadamu, hasa siku hizi. Wataalam hutuambia kuwa Elimu ni ufunguo wa maisha. Binadamu wengi wanatambua kuwa bila elimu, hasa siku hizi maisha hayawezi kwenda vizuri. Kwa hiyo hufanya kila jitihada ili kujipatia elimu.

Sisi Watanzania, mara tu baada ya kupata uhuru wetu miaka mingi iliyopita tuliambiwa kwamba tulikuwa tukikabiliwa na maadui watatu: adui ujinga, adui maradhi na adui umaskini. Lakini tumekuwa tukiambiwa kuwa adui mbaya zaidi ni yule adui wa ujinga. Hao maadui wengine wawili, yaani maradhi na umskini huondolewa kwa njia ya elimu.Kwa maneno mengine, mtu huwa maskini kutokana hasa na ujinga, na pia mtu hupatwa na maradhi kwa kiasi kikubwa kutokana na ujinga alio nao. Kwa hiyo njia ya kwanza ya kushinda hao maadui ni kuwa na elimu.

Hivyo kutoka hapo mwanzo Serikali yetu ilijitahidi sana katika kuwaelimisha wananchi. Mashule mengi yakawa yamenzishwa kwa ule mpango wa UPE [Universal Primary School Education]. Kwa mpngo huo kulikuwa na shule nyingi hasa zile za Msingi na pia zile za Sekondari katika taifa letu. Watoto na vijana wengi waliweza kwenda shuleni na kusoma. Wananchi walihimizwa kujenga shule kila mahali. Mwito huo ulipokelewa kila mahali na kwa hali tofauti. Kuna sehemu zile ambako wananchi walijitolea kujenga majengo mazuri sana kwa ajili ya kusomea wanafunzi. Serikali pia ilichukua hatua ya kutaifisha mashule yale yya mashirika ili watoto na vijana wote waweze kujipatia elimu katika mashule mbalimbali.

Lakini pia kulikuwa na sehemu ambapo majengo ya shule yalikuwa alimradi tu. Majengo hayo kwa vikubwa hayakumalizika sawasawa. Unaweza ukashuhudia kasoro hizo mpaka siku ya leo ukipitapita hapa na pale hasa huko vijijini. Utanaona majengo ya shule mengine kuta hazikumalizika, hakuna milango, wala madirisha, hakuna madawati, ndani ni vumbi tu. Kwa kifupi ni majengo ambayo hayana kabisa hali ya kusomea. Vijana na wanafunzi wetu.

Licha ya uhafifu na hali duni za majengo, kumekuwa pia na ukosefu wa vifaa kama vile vitabu na mazingira machafu ya kusomea. Tunawashukuru na kuwapongeza wale viongozi ambao wametambua umuhimu wa elimu na wamekuwa wakiwahimiza wananchi katika kukamilisha majengo ya shule hapa na pale. Lakini kwa bahati mbaya hao wenye kufutatilia suala la elimu katika sehemu zao wamekuwa ekuwa ni viongozi wachache mno. Tunaloliona tukitembea huko na huko siku ya leo ni majengo ambayo hayajamalizika sawasawa. Kwa kifupi wanafanzi wetu wanasomea katika mazingira mabaya na hivyo hatuwezi kutegemea mafanikio mazuri kutokana na mazingira au hali hiyo ya kusomea. Kilio cha kuwa na madawati ya kusomea vijana wetu ni kikubwa sana. Hapa na pale kimesikiwa, lakini mahali pengi bado wanafunzi wetu wanasoma katika hali duni sana.

Pia tunapenda kuupongeza mpango ulioanzishwa, hasa katika Mkoa wa Dar Es Salaam wa kuzungushia uzio mashule yetu. Hapo walao tunaweza kutegemea kuwa vijana wetu wataweza kusoma katika mazingira mazuri na pia yenye usalama.

Linakuwa ni jambo la fedheha kuona watu wazima wakizunguka na biashara zao huko mashuleni na kuwafanya vijana wetu washindwe kusoma vizuri na kuzingatia masomo yao. Yatupasa kutambua kuwa haitoshi kuwa darasani, bali ni sherti kufahamu kile ambacho walimu wanawafundisha hao watoto na vijana wetu. Ili kuweza kufaidika na mafunzo wanayopewa na walimu, inawapasa wawe katika mazingira mazuri.

Kuna Watanzania wengi ambao wametambua kabisa umuhimu wa elimu kwao binafsi na pia kwa ajili ya watoto wao. Hivyo hufanya kila jitihada ya kuwapatia elimu watoto wao kwa hali na mali. Hao wazazi wametambua kuwa kwa njia ya elimu, mtu hujiwekea akina kwa maisha ya halafu. Tunashuhudia jinsi wazee ambao walibahatika kuwasomesha watoto wao wanavyofaidika katika uzee wao, hasa siku hizi wakipewa misaada ya hali na mali na hao watoto wao.

Lakini kinyume chake tunaona pia jinsi wale wazee ambao hawakuwasomesha watoto wao wanavyoishi maisha ya taabu, na wale watoto ambao hawakuwasomesha wanavyowaletea shida nyingi. Wengine wanakuwa majambazi, wevi na hata kuingia katika shida na matatizo mbalimbali ya maisha. Tunaweza kusema hao watoto wanakuwa siyo tatizo kwa wazazi wao tu bali ni kwa jamii nzima, maana wataalam husema kuwa mtu huvuna kile alichokipanda.

Tumesema kuwa elimu ni ufunguo wa maisha kwa kila binadamu.Watanzania tumeshindwa kwenda mbele katika maendeleo ya nchi yetu kutokana na ukosefu wa elimu. Wengi wetu hawakupata elimu, na wale walioipata elimu kwa bahati mbaya hawaitumii ipasavyo. Tunaambiwa kuwa elimu kama elimu inapaswa kumfanya mtu aishi maisha bora.

Elimu inapaswa kumsaidia mtu katika kuondokana na matatizo ya kimaisha. Kwa hiyo tuhapenda hapa kukazia mambo makuu mawili katika elimu.

Kwanza kabisa ni jukumu la kila mzazi na mlezi kuhakikisha kuwa mtoto wake anapata elimu yenye kumsaidia katika maisha yake ya hapo baadaye. Hivyo ni kosa kubwa sana kwa kila mzazi kutompatia mtoto wake elimu kama urithi kwa maisha yake ya halafu. Hakuna urithi ulio bora zaidi kuliko ule wa elimu. Ni wajibu wa wazazi kuhakikisha kuwa watoto wao wanasoma katika mazingira mazuri. Hivyo watafanya kila jithiada ya kuhakikisha kuwa watoto wanakuwa katika hali nzuri kimazingira, maana yake ni kwamba wanapata mahitaji yao ya lazima huko mashuleni kama vile sare za kuvaa, madaftari kalamu na vifaa vinginevyo vinavyotakiwa kwa ajili ya mwanafunzi kule shuleni na hata kule nyumbani.

Kwa watoto na wanafunzi kwa ujumla tunawasihi sana watumie muda wao wa masomo katika shughuli hizo za masomo. Ni vibaya sana kwa watoto kushika mambo mawili wakati wa masomo. Tunashangazwa kusikia kuwa kuna watoto wanaofanya mambo mabaya huko mashuleni, wanakuwa watovuwa nidhamu au wanashiriki hata katika mambo ya ulevi na ufuska wakiwa huko shuleni. Tunasema hao watoto wanatuaibisha , lakini zaidi wanakuwa ni hasara siyo tu kwa wazazi wao bali pia kwa jamii na taifa letu.

Tnapenda kuona kuwa watoto wetu baada ya kupewa misaada ya lazima kwa masomo yao, basi wazingatie masomo yao na siyo mambo mengine. Wazazi na pia marafiki hufurahishwa na kufaulu kwa watoto katika mitihani yao baada ya kuzingatia hayo masomo yao. Hapo natumainii hapatatokeo mtindo wa kuiba na kununua mitihani, jambo ambalo linatuletea fedheha kubwa sana katika taifa letu. Tumechoshwa na vitendo vya aibu vinavyofanywa na watoto wetu badala ya kuzingatia masomo yao.

Tunapenda kutoa rai kwa wazazi na watoto katika kuzingatia suala zima la elimu. Watanzania hatuwezi kamwe kuingia katika karne ya ishirini na moja ya sayansi na tekinolojia ikiwa hatutazingatia elimu. Pia hatutaweza kuwa watu wa maana katika ulimwengu huu bila kuwa watu wa kupenda elimu na kuitumia elimu yetu.

Mwalimu J.K. Nyerere alisema kuwa kwa kila Mtanzania, wakati ni huu wa kujipatia elimu hasa kwa watoto na vijana wetu. Tukumbuke kuwa tunapaswa kujielimisha sisi wenyewe, kuwaelemisha watoto wetu na pia kuielimisha jamii nzima. Haitoshi kujielimisha sisi peke yetu na tukazungukwa na wajinga. Hao watatukwamisha katika maendeleo yetu. Sote tunapaswa tuelimike na hivyo tutumie elimu yetu kuondokana na balaa kubwa la ujinga.