NGUVU YA HOJA Na Padre Paul Haule

Kwa asili binadamu ni mcha Mungu

Binadamu ni kiumbe pekee ambacho aliyejaliwa kuwa na roho licha ya kuwa na mwili kama viumbe wengine. Kwa sababu hiyo binadamu pia ni kiumbe chenye akili na utashi, chenye kufikiri na kutoa maamuzi siyo kwa kufuata sirika. Kwa hiyo huweza kujijengea hoja mbalimbali katika maisha yake. Moja kati ya hoja ni ile ya kuweza kujiuliza kuhusu asili yake, yaani ametoka wapi na anaelekea wapi. Tunaweza kusema kwa maneno mengine kuwa binadamu ndiye anayeweza kutambua kwa akili yake kwamba kuna Mungu aliye Muumba wake.

Baada ya kutambua na kukiri kwamba kuna Mungu aliye Muumba, basi jambo linalofuata kwa huyo binadamu ni kwamba lazima atoe heshima kwa huyo Mungu kama Muumba wake, na Mfadhili wake. Hivyo binadamu kutoka awali kwa asili yake hutambua kwamba kuna Mmoja ambaye ni Mkuu kabisa, ambaye ni chanzo cha kila kiumbe kilicho hapa duniani na pia huko mbinguni. Jambo hilo laweza kufikika tu kwa kutumia na imani yake ambavyo amepewa na huyo Mwenyezi Mungu kwa upendeleo mkuu sana.

Binadamu hutoa heshima kwa Mwenyezi Mungu kwa njia mbalimbali. Hivyo binadamu anapaswa kuwa na kitu tunachokiita "DINI", yaani yale mahusiano yake na Mwenyezi Mungu. Kwa njia ya imani binadamu husadiki na kukiri juu ya uwepo wa Mungu na hivyo daima hupenda kujihusianisha na huyo Mwenyezi. Ni jambo la kawaida kwamba binadamu baada ya kukiri uwepo wa Mungu basi, humwabudu, humtukuza, humshukuru, hutubu makosa aliyoyafanya kinyume cha huyo Muumba wake. Pia binadamu akitambua unyonge wake daima hujiona kuwa sharti amtegemee huyo Mwenyezi kwa kumwomba wakati anapokuwa katika shida na mahangaiko ya maisha ya hapa duniani. Lakini hasa humwomba ili awe na maisha mazuri huko ahera baada ya kifo chake. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa binadamu daima anakuwa na mahusiano ya karibu kabisa na huyo Mwenyezi. Kwa hiyo huwa na muda maalum kwa ajili ya kuhusiana na huyo Mungu kwa njia ya sala na hata sadaka. Pia huwa na mahali maalum kwa ajili ya kumwabudu huyo Muumba wake. Kuna wale ambao wanamwabudu Mungu katika sehemu za kawaida kama vile majumbani, na wengi hujenga na kutengeneza mahali pa kuabudia kama vile makanisa, mahekalu, misikiti na kadhalika. Lakini pia huwa na watu maalum wenye kuongoza katika kumtukuza Mwenyezi Mungu. Hao watu wanajulikana kama wachungaji, maaskofu, mapadre, au mashehe na kadhalika.

Hivyo kwa kuwa hawa wachungaji au viongozi wa kidini hufanya kazi hiyo kwa ajili ya watu wanapaswa kutunzwa na hao watu wanaowahudumia kiroho na hata pengine kimwili. Na hivyo ndivyo Kristo alivyokuwa ameagiza kwa kusema "mtenda kazi anastahili posho lake" [Mathayo 11:10]. Kazi wanayoifanya hao wachungaji na viongozi wa kiroho ni nzito sana kwani wanawaandaa binadamu kwa maisha ya halafu na hakuna kitu bora zaidi kama kile cha kuwapeleka watu kwa Mwenyezi Mungu.

Shughuli nyingine zote huwa zinamalizika saa ile mtu anapokata roho, lakini huenda mbele ya Mwenyezi Mungu akiwa na roho safi pamoja na matendo mema. Na mtu mwenye kumwelekeza awe safi na pia mwenye matendo mema kwa kawaida ni kiongozi wake wa roho. Mpaka sasa kuna waumini wengi ambao hawaelewi au wanapuuzia wajibu wao huo. Kiongozi wa kiroho au wa kidini huwashughulikia watu wengi sana katika maisha yao ya kiroho. Ili aweze kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa anatakiwa awe katika hali njema kabisa ya afya. Kwa mfano mchungaji au padre huwahudumia watu wengi sana maelfu kwa maelfu, hivyo hupasika kutoa nguvu zake nyingi katika shughuli zake hizo. Lakini wengi kwa sababu ya kutokutambua jambo na pengine kutokana na uzembe huona kuwa kuwalisha na kuwatunza hao viongozi wa dini ni kazi ya hiari, kumbe sivyo.

Hapo tunapenda kuwaambia kuwa ni wajibu wa kila muamini anayepata huduma kutoka kwa kiongozi wa kiroho sherti amhudumie huyo kiongozi bila masharti mradi tu huyo kiongozi anatimiza wajibu wake. Waswahili husema "kula na kulipa", yaani kila anayekula huduma za wachungaji na viongozi wa kiroho ni sharti alipe kwa kuwatunza. Lakini linakuwa ni jambo la kusikitisha kuona jinsi waamini wengi wasivyotaka kutimiza wajibu wao wa kuwahudumia hao wachungaji na viongozi wao wa kiroho. Ni kweli kuwa mchungaji au kiongozi yo yote wa kiroho anapaswa kujitegemea kwa namna fulani.Kuna wachungaji, mapadre na hata mashehe ambao wameamua kufanya shughuli mbalimbali ili kujitegemea. Nadhani shughuli hizo zingekuwa ni za ziada, lakini kwanza inatakiwa wategemezwe kama malipo ya huduma wanazozitoa kwa ajili ya hao waumini.

Natumaini wakati umefika ambapo tunapaswa kuambiana ukweli kabisa ya kuwa kila mwenye kupokea huduma iwayo yote ile kutoka kwa kiongozi wake wa kiroho anapaswa kuilipa hiyo huduma kwa namna moja au nyingine. Ni wajibu wa kila mwamini wa kila dhehebu na dini kumtunza, kumlisha na kumhudumia kwa namna mbalimbali huyo kiongozi. Hivyo sadaka tunazozitoa huko makanisani na misikitini siyo tendo la huruma bali ni tendo la haki la wajibu, la lazima kabisa na pia ni takatifu mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa yule mwenyezi kuufahamu wajibu wake, hilo si tendo la kuomba kwa huyo mwenye kutoa kwani ni hake na vema kwamba huyo kiongozi anapaswa kutunzwa na kulishwa na hao kondoo anaowahudumia kiroho na kimwili. Kwa upande mwingine ni jambo la kufurahisha sana tunaposhuhudia jinsi waamini wengine walivyolielewa jambo hilo la kichamungu.

Hao waumini hutoa cho chote kwa ajili ya kuwalisha na kuwatunza viongozi wao wa kiroho, na hao viongozi baada ya kupata huduma hizo kutoka kwa waamini wao, hujikuta hawana jinsi nyingine isipokuwa kuwahudumia na kuwahangaikia hao waamini hasa katika mambo ya kiroho kwa ukamilifu zaidi. Jambo ambalo pia mahali pengine linaanza kueleweka ni kama usemavyo ule wimbo unaoimbwa wakati wa kutoa sadaka wakati wa ibada:toa ndugu, toa ndugu cho chote ulicho nacho...".Ni dhahiri kuwa siyo waumini wote wana pesa kila wanapotaka kwenda kwenye ibada takatifu, lakini wanaweza kutoa kitu fulani, na hata kutoa huduma fulani kwa ajili ya viongozi wao wa kiroho. Waumini wanapaswa kutoa cho chote kwa ajili ya huduma wanayopata licha ya vifaa vinavyotumika katika ibada.

Tunapenda kumalizia Hoja yetu hii kwa kusema wazi kwamba kila mwamini anapaswa kumhudumia mchungaji na kiongozi wake wa kiroho kwa kumlisha, kumtunza na kumpatia huduma anazostahili ili aweze kufanya kazi yake vizuri na asiwe mtu ambaye hutegemea watu wengine wenye huruma nje ya kituo chake cha kazi. Watu wale ambao anawahudumia sharti wamtunze, wamlishe na wahakikishe kuwa afya yake ni njema daima. Mwamini asione kuwa ni kitu cha hiari kumtunza na kumlisha kiongozi au mchungaji wake wa kiroho.