NGUVU YA HOJA Fr. P. Haule...

Tutambue uwezo wetu

WATANZANIA wengi siku hizi wanapenda kufanya mambo mengi sana yaliyo makubwa kwa ajili ya faida yao binafsi na pia kwa ajili ya faida ya familia zao. Wako wale ambao wastani wanajitahidi kujiingiza katika shughuli za kibiashara. Wako wale ambao wanataka kushughulika na mambo ya ufundi, labda seremala au umekanika. Kuna watu ambao wanatafuta elimu ya juu yao binafsi au ya watoto wao. Kwa kifupi kuna kiu ya kutaka kufanikiwa zaidi kwa walio wengi, ingawaje si kwa kila mwananchi kuna hamu hiyo.

Katika kutafuta mambo hayo makubwa, tunaona pengine watu wanafanya mambo bila kuwa na utafiti sawasawa. Tumesema kwa mfano kuna wazazi ambao wanatafuta elimu ya juu kwa ajili ya watoto wao. Lakini pengine hutokea kuwa wanasahau kufanya utafiti kuhusu uwezo wa hao watoto wao. Tunavyoelewa kuna viwango tofauti vya akili kwa kila mtoto. Kuna watoto wenye akili kali sana, na kuna watoto ambao wana akili ya kawaida ya wastani na watoto ambao akili yao ni nzito kabisa. Mzazi akishatambua uwezo wa mtoto wake hapo atamshughulikia kwa kadiri ya uwezo huo alio nao bila kulazimisha. Hivyo hata mtu binafsi akitambua uwezo wake, atajitahidi kujiendeleza kufuatana na uwezo huo alio nao bila kulazimisha cho chote.

Kumbe mambo yanavyotokea ni kwamba kuna watu ambao hujilazimisha katika kutafuta elimu na papo hapo uwezo wao ukiwa ni wa chini kabisa. Pia kuna wazazi ambao wanalazimisha watoto wao wachukue mafunzo ya juu, hali hawana uwezo kabisa katika mafunzo hayo. Tunavyofahamu ni kwamba hakuna maana kabisa kumlazimisha mtu katika mambo ya elimu au kazi kwani katika kufanya vile kunaweza kusababisha hali ya kutowajibika na uzembe katika utendaji hapo baadaye.

Kuna mambo mawili tunayodaiwa ktika kila kazi tunayoamua kuifanya katika maisha yetu. Kwanza kabisa tunapaswa kuwa na elimu inayolingana na kazi hiyo. Elimu hiyo isiwe ya kununua bali ni hasa iliyotokana na juhudi zetu za kusoma. Jambo la pili tunapaswa tuipende hiyo kazi na hivyo tutaweza kuifanya vizuri na kwa ufanisi. Lakini mambo yalivyo kwa sasa hivi kwa watu wengi ni kwamba vijana wanaingizwa katika mafunzo ambayo hayalingana na uwezo wao.

Ni jambo la kawaida kabisa kwa wazazi walio wengi kutamani watoto wao wapate mafunzo ya juu ya vyuo vikuu, au hata waende wakasome katika vyuo vya Ulaya au Marekani, lakini kumbe uwezo wao kiakili ni mdogo.

Hao wazazi hufanya juu chini ili mradi mtoto wake amekwenda ng’ambo licha ya uwezo wake kuwa mdogo sana.Mapato yake yatakuwa au huyo kijana atashindwa masomo, au atafanya kazi ya ziada na hivyo kufaulu kwa shida. Baada ya "kuhitimu" utendaji wake akiwa kazini utakuwa ni wa wasiwasi sana. Jambo hilo hujionyesha hasa katika utendaji kwenye maofisi yetu na mahali pengine. Watu wengi hujiingiza katika kazi ambazo siyo wito wao, na mapato yake ni kutokuwa na ufanisi unaotakiwa.

Tunaweza kutambua kuwa mtu fulani anafanya kazi kulingana na wito wake, pale tunaposhuhudia anaifanya kazi hiyo hasa kwa njia ya kujituma, na siyo kutokana na pesa anayoipata au faida fulani, bali ni kutokana hasa na wito alio nao katika kuhudumia. Tunaweza kushuhudia jambo hilo hasa kwa wale waganga na walimu ambao wanafanya kazi kutokana na wito wao. Kwa waganga, tunaona jinsi wanavyomhangaikia mgonjwa bila kujali muda au gharama, wanachojali hasa ni uhai wa mgonjwa. Hivyo pia tunaona kwa upande wa walimu jinsi wanavyowahangaikia wanafunzi, wakitumia muda wao katika kuwafundisha na kuwaelimisha hao wanafunzi wao bila kujali muda. Wanakuwa na uvumilivu mkubwa sana katika kuwaelimisha wanafunzi. Tunasema hao wanafanya kazi zao kutokana na wito pamoja na elimu walio nayo, na hivyo wako kweli mahali pao.

Taifa letu huzidi kupata hasara licha ya kuwasomesha vijana na watu wengi kutokana na kutofanya utafiti wa kina kuhusu uwezo wao kimasomo.

Hivyo pia hutokea hata katika mambo ya binafsi. Siku hizi kuna watu wengi ambao wanaamua kufanya shughuli za biashara.

Mapato yake huonekana, waziwazi. Kwa wale ambao wana elimu na wito katika shughuli hizo za biashara, mambo yanakwenda vizuri, lakini kwa wale ambao wanabahatisha, mambo hayanyoki sawasawa. Waingereza husema kuwa kila mmoja anapaswa kushona nguo yake kulingana na kitambaa alicho nacho, vinginevyo kutakuwa na kasoro kubwa sana na yenye kuleta aibu mbele ya watu. Hivyo taifa letu linapata aibu kubwa sana kutokana na watu ambao wamepata kazi zisizolingana na uwezo wao. Kuna watu wanafanya kazi ili mradi ni kazi, kumbe mapato yake ni kuzidi kurudisha nyuma maendeleo ya taifa na hata yao wenyewe binafsi.

Natumaini wakati umefika wa kuwa wazazi na unyenyekevu ili kutambua uwezo wetu unakomea wapi na papo hapo kufanya shughuli zile tu ambazo tunaziweza na sio tu ili mradi tuna cho chote cha kufanya.

Daima tunapojiingiza katika zile shughuli ambazo hatuna ujuzi nazo au wito, basi tutakuwa tunafanya kwa mashaka na bila kujiamini. Utendaji wetu utakuwa na hali ya mashaka mashaka pamoja na wasiwasi.